Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rombo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa fursa hii ya kuhitimisha hoja. Naanza kwa kuushukuru sana kwa uongozi wako kwa kipindi hiki cha bajeti yetu wewe na viongozi wengine wa Bunge letu na kuendelea kukupongeza kwa nafasi yako ya kuwa Rais wa Mabunge ya Dunia.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Wabunge wote kwa michango mizuri sana, maswali na hoja ambazo kwa kweli tunawajibika kuzitafakari vya kutosha na kuzifanyia kazi. Nyingi tunazibeba kama ushauri kwa ajili ya utekelezaji wa kazi iliyoko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shukurani za pekee kwa Kamati yetu chini ya uongozi wa Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Husna Sekiboko na Makamu wake, Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima kwa kazi nzuri sana ya kutusimamia na kutuongoza mpaka hapa tulipofika. Kwa kweli maoni yao kama yalivyowasilishwa katika Bunge lako hili Tukufu, tunayabeba kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukurani za pekee kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Omari Kipanga. Kwanza nampa pole kwa dhoruba iliyotokea kwenye Jimbo lake la Mafia, pia uongozi wake na usaidizi mkubwa sana anaotupatia katika Wizara yetu; Katibu wetu Mkuu Profesa Carolyne Nombo, Profesa James Mdoe, Naibu Katibu Mkuu; Dkt. Franklin Rwezimula, Naibu Katibu Mkuu; Dkt. Mutahabwa, Kamishna wa Elimu; Wakurugenzi, Wakuu wa Taasisi na Watumishi wote wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutuwezesha kufika hapa tulipofika.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru vilevile kwa nchi nzima walimu wote, wakufunzi na wahadhiri katika taasisi zote za umma na binafsi kwa kazi kubwa wanayoifanya kuendeleza elimu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda mbali, labda nimwelezee tu Mheshimiwa Rashid kuhusu suala la shule iliyopo Pemba, kwamba shule za Sekondari haziko kwenye Mfumo wa Muungano. Kwa hili jina zuri lililotukuka la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan linapaswa kuwekwa kule na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na tutawasiliana na Wizara ile tuhakikishe kwamba kweli jina linabadilishwa kama maelekezo yalivyokuwa yametolewa.
Mheshimiwa Spika, tulisikiliza vizuri sana maelezo ya Mheshimiwa Ally Kassinge kuhusu athari za mafuriko katika eneo lake. Tunampa pole na naungana na Naibu Waziri na Watanzania wote kutoa pole kwa wote walioathirika sana na dhoruba hii ya mafuriko na hali mbaya ya hewa.
Mheshimiwa Spika, sisi tumeona sekta ya elimu vilevile imeathirika. Nilipata fursa ya kutembelea Kibiti na Rufiji kujionea mwenyewe. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inafanya kazi na TAMISEMI imepeleka timu katika maeneo yote kufanya tathmini na kuhakikisha kwamba tunachukua hatua ili masomo yasiweze kuathirika.
Mheshimiwa Spika, ninamhakikishia Mheshimiwa Ally Kassinge kwamba hata kule Kilwa vilevile tunashirikiana na TAMISEMI kwamba hatuzuii masomo. Wizara imefanya jitihada ya kupeleka mahema, kuhamisha wanafunzi na kuhakikisha kwamba shule nyingine zinapokea wanafunzi ambao wameathirika, waingie pale waanze kusoma. Naomba tusubiri tuone tutafika wapi.
Mheshimiwa Spika, kwa ujumla tumepata maoni 62 kwa wachangiaji. Maoni 11 kwa maandishi na 51 yamechangiwa humu ndani. Nawashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu tutayabeba yote, kwani sitaweza kujibu kila hoja. Nawahakikishia kwamba tunayatilia maanani sana. Kila Mbunge aliyezungumza, kila mmoja amemshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mageuzi makubwa ya elimu ambayo ameyaahidi hapa Bungeni, na ameyasimamia. Kazi imeanza na inaendelea.
Mheshimiwa Spika, vilevile naungana na Wabunge wenzangu wote kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake haya makubwa na ujasiri wake wa kuhakikisha kwamba tunaanza na kazi hii. Ukiangalia Tume ya Rais ya Elimu ya Mwaka 1982, maarufu kama Tume ya Makweta, baadhi ya mambo mengi ambayo tunazungumza sasa hivi yalikuwepo mle mwaka 1982.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kutumia neno amali, mafunzo ya amali tunayoyazungumza sasa hivi yamo kwenye juzuu la kwanza la taarifa ile, lakini hayakutekelezwa. Nadhani kigugumizi labda kilitokana na hali ya uchumi ya wakati ule, japokuwa Mheshimiwa Makweta naye alikuja kuwa Waziri wa Elimu, lakini hali ya uchumi haikuruhusu.
Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 ambayo ilizinduliwa 2015, karibia mambo yote ya sera mpya hii yamo mle; miaka 10 ya elimu ya lazima, mafunzo ya amali na kadhalika; lakini baada ya kuzindua, hakuna chochote kilichofanyika katika maeneo hayo makubwa kwa sababu nadhani inahitaji sana rasilimali kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wameonyesha wasiwasi, kwamba ni suala kubwa sana linahitaji rasilimali watu, rasilimali fedha, kujipanga vizuri na usimamizi mzuri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Rais wetu kuamua kwamba tusonge mbele baada ya kufanya mapitio ya sera ile na kupata toleo la 2023 na anajua kwamba itagharimu fedha na kusema endeleeni na kazi hii, ni ujasiri mkubwa sana kwa Rais wetu. Kwa kweli maua yetu tunayatoa kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi yetu wasaidizi wake ni kuhakikisha kwamba hatumwangushi na kuhakikisha kwamba tunawaondoa hofu Watanzania wote kwamba kazi hii itafanyika vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mambo mawili makubwa katika mageuzi ya elimu ambayo lazima tuyakumbuke na kuyatilia maanani ni kwamba ikifika mwaka 2027 itakuwa ni lazima kwa kila mwanafunzi kukaa shuleni walau miaka 10 ukichanganya na elimu ya awali ni miaka 11. Hilo ni jambo kubwa na la kwanza na limezungumzwa hapa.
Mheshimiwa Spika, inatia hofu wakati mwingine kwamba tutawezaje? Wenzetu Zanzibar hawakuwahi kuondoka kwenye mfumo huo na elimu yao, walishaenda miaka 11, sasa hivi wanarudi tena miaka 10 na wanaendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kubadilisha mfumo wa elimu kuwa na mikondo miwili katika sekondari ya chini na sekondari ya juu, elimu jumla na elimu ya amali. Sitaweza kufafanua sana hili, tumeshazungumza sana, lakini niko tayari kutoa ufafanuzi kwa fursa nyingine. Hili nalo linahitaji rasilimali watu, rasilimali fedha nyingi na kuhakikisha kwamba tunatekeleza. Sababu yake ni kwamba tumeamua kuanza hatua ndogo ndogo kwenda mbele, kwa sababu tunataka kutafuna kile tunachoweza kukimudu.
Mheshimiwa Spika, kuna kauli ilitolewa hapa kwamba tunafanya piloting, siyo piloting kabisa. Tumeanza safari, hakuna gia kurudi nyuma. Hii kazi tuliamua kwamba kwa mfano, tungesema sasa hivi twende miaka 10, tunajua changamoto ingekuwa kubwa sana. Tumesubiri mpaka 2027 na nitaeleza rasilimali fedha tutazipata wapi kuhakikisha kwamba tunatekeleza hiki ambacho kimeahidiwa.
Mheshimiwa Spika, hata mafunzo ya amali, hata shule za Serikali nyingine ambazo zilitaka kuingia kwenye mkondo wa mafunzo ya amali, na shule binafsi zimefanyiwa tathmini na Kamishna wa Elimu, nyingi tumewaambia subiri, bado vigezo havijatimia. Shule za Serikali vigezo vimetimia kwa shule 28 peke yake, shule binafsi ni 68 peke yake. Tumesema tuko tayari kuanza kwa hatua ndogo ndogo.
Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Kaboyoka mtani wangu alizungumza hapa vizuri sana. Aliyazungumza hayo utadhani alikuwepo wakati sisi tunapanga namna ya kuweza kutekeleza. Kwa hiyo, haya ni mageuzi makubwa sana, lakini tumehakikisha kwamba tunaenda nayo kwa hatua ambazo tunazimudu. Kila hatua tunayoipiga tunaimudu kwa 100%. Kwa hiyo, haya mageuzi tunaenda nayo, muda ungekuwa unaruhusu ningejaribu kutoa ufafanuzi zaidi.
Mheshimiwa Spika, hebu tuangalie mitaala mipya tunaanza nayo vipi? Choice ingekuwa ni kusema kwamba tunafumua mitaala yote na kuanza upya kwa level zote na ziko nchi zimefanya hivyo, tumesema hapana, mitaala mipya itaanza elimu ya awali, ambapo imeanza mwaka huu. Darasa la kwanza imeanza mwaka huu, darasa la tatu imeanza mwaka huu na darasa la pili; darasa la nne, darasa la tano, darasa la sita na darasa la saba ni mitaala ya zamani.
Mheshimiwa Spika, watu wengine walishangaa lakini tulisema we bite what we can chew. Tunajaribu kuanza na kile ambacho tunaweza kukimudu. Rasilimali zitatosha, vitabu vitatosha. Kama alivyosema Mheshimiwa Kipanga, isingekuwa hali ya hewa, hapa vitabu vipo, vimepelekwa sehemu nyingi na hata vile ambavyo vimepelekwa kwa njia ya mtandao, Airtel tuna makubaliano nao, mwalimu hana haja ya kununua bundle. Akiwa na kadi ya Airtel ana-download, anavisoma lakini hardcopy ndiyo mwendo wenyewe; softcopy ni option. Tumefanya hivi maksudi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, upande wa sekondari kwa mwaka huu tumeanza Form One kwa wale wa mafunzo ya amali tu kwa mitaala mipya. Kwa hiyo, tumeanza kwa shule 28 za Serilkali na 68 za Serikali kwa form one. Tunaenda hivi kwa sababu tunataka kila hatua tunayokwenda tuhakikishe tumewekeza vya kutosha siyo piloting. Tunaangalia resource envelope ambazo kama nitakavyoeleza, kwa kweli zitafunguka na nadhani yajayo yanafurahisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaenda form five. Baada ya hapa sasa hivi kuchukua wanafunzi wa form five wataanza na mitaala mipya. Kwa hiyo, tunaenda hivi kwa sababu hatutaki hofu ambayo kila mmoja ameionesha ambayo ni ya haki kabisa kwamba, tusije tukakimbia sana wakati resources tumeziacha nyuma, halafu matokeo yake yatakuwa kama nchi moja ambayo siwezi kuitaja hapa, ambayo Waziri wake wa Elimu alinieleza kwamba, aliamua kufumua kila kitu wakaanza, wakaboronga, wakarudi tena nyuma, wanaanza tena upya sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, tumeenda kujifunza kwao, sasa hivi tumekuta wanajaribu tena kufanya kosa lile ambalo walifanya wakati ule, lakini sisi tunajifunza kwa waliofanikiwa na ambao kwa kweli hali haikwenda vizuri sana. Kwa hiyo, tunasema sasa hivi tunaanza na shule chache kwa mafunzo ya amali, lakini nina uhakika kwamba tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nimekisikia, nikiseme kutoa hofu walau Mheshimiwa Mbunge mmoja au wawili kuhusu wale wanaoenda mafunzo ya amali halafu wakishawapeleka kule hawaendi Chuo Kikuu, itakuwaje? Huu ni mfumo nyumbufu. Mafunzo ya amali yanayo mafunzo ya taaluma machache zaidi. More practical subjects, lakini wanaweza wakachukua yale machache kwenda high school kwenye masomo ya elimu jumla.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna high school za mafunzo ya amali ambazo itakuwa miaka mitatu. Unatoka na diploma na cheti cha form six, kama ilivyokuwa Mkwawa High School kwa wakati ule. Kwa hiyo, hilo tunakwenda nalo na hakuna sababu ya kuogopa kumpeleka mtoto kwenye mafunzo ya amali kwamba yeye hatakwenda mpaka chuo kikuu.
Mheshimiwa Spika, vyuo vikuu tunaanza streams of vocationalized university degrees kama nchi nyingine wanavyofanya. Kwa hiyo, unaweza ukaenda na degree yako mpaka Ph.D na tunaendelea ku-maintain unyumbufu kiasi kwamba unaweza ukarudi huku na kwenda kule bila kupoteza nafasi yako yoyote.
Mheshimiwa Spika, ukizungumza bajeti ya elimu ni muhimu kuzungumza bajeti ya sekta ya elimu, siyo bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia peke yake. Kwa mfano, mwaka huu unaoisha, sekta ya elimu imepewa jumla ya shilingi trilioni 5.95 zote hizi ziko kwenye elimu.
Mheshimiwa Spika, kama mnavyofahamu, hizi shule tunazozungumzia zinajengwa kupitia TAMISEMI. Nimesikia Mbunge mmoja amesema tunaona hapo mmepata fedha za kigeni, kwa nini haujaweka fedha za ndani? Nadhani ni Mheshimiwa Mnzava kama sikosei aliyeongelea hili kwamba, mbona hujaweka fedha za ndani?
Mheshimiwa Spika, hizo fedha za ndani utazikuta TAMISEMI, kwa sababu tukichukua BOOST hapa, tunapeleka TAMISEMI, wanachukua fedha za ndani, wanaendelea na kazi. Tukichukua SEQUIP zinatoka Hazina zinapitia katika Wizara yetu, zinakwenda TAMISEMI. TAMISEMI utakuta counter part funds za Wizara ya Ndani, hatuja-neglect nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, fedha kwa ujumla wake, kwa miaka miwili ijayo; 2024/2025 na 2025/2026 tuna takribani 1.5 trillion ambayo tutapeleka kwenye miundombinu tu. Tunayo BOOST, EP4R Awamu ya Pili, tuna SEQUIP, E-Stream, GPE na TSP, hizi ni fedha ambazo zipo assured kupitia Hazina. Tumeshaingia commitment ni kuzitumia. Tumeshakubaliana na wenzetu wa Hazina kwamba tuta-accelerate expenditure of the money ili tuhakikishe kwamba tunaandaa miundombinu mapema iwezekanavyo ili tutakapoanza kuchukua wanafunzi kwenda miaka 10 tutakuwa tayari. Ndiyo maana sasa hivi hatuna wasiwasi na suala hili la miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kazi ambayo tunaifanya, nimeona kuna wasiwasi, kati ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI mnaingiliana na nini. Kitabu hiki labda nitaomba wenzetu tuhakikishe kwamba kila Mbunge anakipata kwa softcopy. Kimeandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TAMISEMI, kina shule zote hapa Tanzania. Shule za Msingi katika maeneo ambayo yana watu wengi ambazo kuna eneo kubwa tutatumia BOOST kuongeza form one, form two, form three na form four utaikuta humu.
Mheshimiwa Spika, shule ya sekondari kwenye maeneo yenye watu wengi ambayo ina eneo kubwa tutatumia hela za SEQUIP kuongeza darasa la kwanza, la pili, la tatu, la nne, la tano na la sita. Kwa hiyo, kuna shule nyingi hapa sasa hivi zitaweza kuchukua mwanafunzi kuanzia elimu ya awali mpaka Form Four ili kuweza kutimiza azma yetu ikifika 2027.
Mheshimiwa Spika, shule zote; naweza nikakusomea shule moja hapa, mtu yeyote anayetaka atakipata lakini tutajitahidi kuweka kwenye softcopy ili Wabunge waone kwa sababu mimi na mwenzangu Mheshimiwa Mchengerwa tumekubaliana kwamba tutahakiki taarifa hizi na vizuri Waheshimiwa Wabunge wahakiki na kujua katika eneo lako kweli shule iliyowekwa huku iko sahihi ama vinginevyo? Tuko vizuri katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo, mnaona shule zinazojengwa sitataja idadi kupitia TAMISEMI kwa kila Kata na bajeti imewekwa, amezuingumza Mheshimiwa Mchengerwa hapa, kuna shule 100, hizi shule 100 siyo shule za amali tu, hili napenda nilielezee kwa sababu amali ni ufundi na ufundi stadi. Shule 100 ni technical secondary school ambayo ukimaliza Form Four your full technician, unapata cheti, unaweza ukaajiriwa ukaanza kazi. Tulikuwa nazo nadhani kama tisa tu sasa hivi ambazo nazo tunazi-revamp.
Mheshimiwa Spika, najua ukiangalia karakana unaona kidogo ziko outdated. Nilienda Tanga school, nimeiangalia tumewekeza fedha kuzi-revamp, tunajenga mpya 100. Tunajenga sehemu mbalimbali, mfano nimchukue Mbunge mmoja, Mheshimiwa Taletale nadhani yumo humu ndani, kwake hakupata VETA atapata shule ya ufundi. Wabunge ambao wako kwenye Wilaya yenye VETA, lakini yeye Jimbo lake kwenye Wilaya hiyo haikupata VETA, atapata technical secondary school kuhakikisha kwamba tuna-balance na list ipo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama unajua hukupata VETA unaweza ukaja ukahakiki. Fedha zipo, ujenzi unaanza sasa hivi na katika shule hizo 26 zitaanza kuchukua wanafunzi mwezi Januari.
Mheshimiwa Spika, changamoto ambayo kila mmoja anasema ni walimu. Tunajipanga kuhakikisha kwamba tutakapoanza tutakuwa na Walimu. Nawakumbusha tena Waheshimiwa Wabunge mtaona clip moja inazunguka nadhani CEO wa Apple or sikumbuki nani, alisema hawaendi kuwekeza China kwa sababu eti gharama ya nguvu kazi ni ndogo.
Mheshimiwa Spika, gharama ya nguvukazi China ni kubwa, hajui mnapozungumzia China ya gharama ndogo, mnazangumzia China gani? Wanazungumzia kule kwa sababu wana technicians wengi wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namna moja ya kuvutia uwekezaji hapa nchini ni kuhakikisha vijana wetu tunawa-train in high precision kwenye technical education. Hizi shule tutakazozijenga, hata tunavyozijua zilivyokuwa sijui Tanga school, Moshi school tunaenda kujifunza kwa wenzetu, tutaendelea kuzi-modernize kuhakikisha kwamba kweli zinatoa technicians ambao wanakidhi matakwa yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli naweza nikasema ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge yajayo kwa kweli yanafurahisha. Nadhani ujasiri wa Rais wetu wakati amekubali kupitisha mageuzi haya, tunaona yanazaa matunda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongeze tu, kwa mfano shule za wasichana 26 za mikoa nazo tunazigeuza, zitakuwa za sayansi vilevile na mafunzo ya amali. Vyuo vya kilimo, namshukuru sana Mheshimiwa Hussein Bashe, baada ya mazungumzo amesema atavitoa vile vyuo vitatumika kwenye mafunzo ya amali. Mazungumzo yanaendelea na Wizara nyingine sizitaji sasa hivi lakini kuna fursa ya kuongeza wigo mpana sana wa kuchukua wanafunzi katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano mtu anasoma diploma ya kilimo, atakuwa anasoma high school na diploma ya kilimo lakini it will be more practical. Anasoma kupata certificate, atapata cheti cha Form Four na certificate yake ya kilimo kwa sababu ni mafunzo ya amali kama tunavyotaka.
Mheshimiwa Spika, VETA za wilaya zote ambazo tunazijenga, tuna mpango wa kuhakikisha kwamba tunazi-modernize kwa kutumia mradi tuliuonao kuhakikisha kwamba kuna possibility ya kuchukua wanafunzi wa O’ Level na VETA za mkoa zichukue wanafunzi wa A’ Level. FDC vilevile kama ilivyopendekezwa hapa tutaangalia uwezekano wa kuzitumia vizuri. Tuna Chuo cha Ufundi Dodoma pengine Waheshimiwa Wabunge watapenda kukitembelea maana kinaenda vizuri sana.
Mheshimiwa Spika, campus zote zinazojengwa nje ya main campus ambazo zinajengwa, sasa hivi tumeziagiza, zitakuwa za mfumo wa mafunzo ya amali. Kwa mfano, huko Mtwara; narudia tena, Mtwara. Mtwara kawaida na Mtwara ufundi tunaunganisha chini ya chuo kimoja cha ufundi halafu watahakikisha kwamba wanafundisha mambo ya amali, mtu anaenda kusoma kule.
Mheshimiwa Spika, Lindi wapo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini kilimo atakachofundisha should not be academic, itakuwa ni mfumo wa mafunzo ya kilimo, mafunzo ya amali na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, muda ungeruhusu ningetoa details zaidi lakini kuna mambo mengine ni vizuri nikaeleza hapa. Tahasusi zimezusha taharuki, labda haifahamiki kwamba 2010 tulikuwa na tahasusi 80, lakini kuwa na tahasusi zilizoidhinishwa haimaanishi zinafundishwa. Mimi nilimaliza EGM high school. High school za Serikali zenye EGM ilikuwa ni Pugu, Tosamaganga na Shy Bush, tatu tu. Kwa hiyo, kuwa na ile tahasusi haina maana shule zote ziliweza kufundisha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kuongeza tahasusi kutoka 80 kwenda 88 haina maana zote zinaweza kufundisha bila kuwekeza vya kutosha. Kubwa zaidi kuwa na tahasusi nyingi zaidi za social sciences haina maana kwamba tutakuwa na wanafunzi wengi wa social sciences. Kama mwelekeo wa wanafunzi wengi inclination yao ni social sciences, ni option yao lakini sisi tumeweka kivutio maalum kwenda kusoma masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Samia Scholarship, ukitaka kwenda kusomeshwa na Serikali chuo kikuu, wewe kasome tahasusi ya science hizo ambazo unaziona ni chache, zinaweza zikatolewa na shule nyingi zaidi kuliko ambazo unaona tahasusi ni nyingi na zikatolewa na shule chache. Wingi wa tahasusi ni kutoa wigo tu wa choice. Unataka kusoma nini? Unataka kusoma Kifaransa, unataka kusoma Kichina, lugha nyingine kama Kiarabu na kadhalika, kuna fursa hiyo unaweza ukajisomea.
Mheshimiwa Spika, nchi nyingine zilizoendelea hazina tahasusi, zinakwambia tu utajichagulia wewe mwenyewe masomo matatu unayotaka kusoma au manne. Sisi kwa sababu hatuna rasilimali za kutosha tumepanga yale masomo kuku-limit kwa sababu tunajua ukienda kusoma Pugu ukajichagulia tahasusi ambayo haipo, huwezi kusoma.
Mheshimiwa Spika, wakati sisi tunamaliza Form Four, nakumbuka Mazengo hapa ilikuwa na tahasusi peke yake Tanzania nzima. Ilikuwa na tahasusi moja tu. Ipo kwenye list ya shule inayotoa ile tahasusi, ni moja tu.
Mheshimiwa Spika, sasa motisha ya Samia Scholarship imetusaidia. Tumeona wanafunzi wengi, ukitembea O’ Level wanakwambia nitajitahidi kusoma masomo ya sayansi, nikienda high school nitasomeshwa na Serikali, nitamwokolea mzazi wangu gharama ya kusoma.
Mheshimiwa Spika, nilizungumzie hili la scholarship, vigezo vipo wazi. Samia Scholarship is meritocratic scholarship. Tunataka the best brain zikasome science. Kwa hiyo, tunatoa kivutio, pamoja na kusomeshwa, una haki ya kusema mimi nilishinda Samia Scholarship. Hiyo yenyewe inaingia kwenye wasifu wako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nchi nyingine ukipata scholarship nzuri ukitamka unajua umefanikiwa. Hakuna sababu ya kusema hii ni kwa ajili ya Means Testing. Tunaweza tukaanzisha facility nyingine ya Means Testing, lakini tunataka daktari mzuri. Kama baba yako ana uwezo sana, unataka kwenda kusoma Law, jitangaze wewe mwenyewe umechukua Samia Scholarship, kasome udaktari uje ututibu kwa sababu uwezo wako ni mkubwa. Kwa hiyo, tunabakiza vigezo hivi tulivyovisema vipo wazi, hakuna mtu anaonewa.
Mheshimiwa Spika, ukipata point tatu kama ni masomo ya sayansi unaenda kusoma sayansi chuo kikuu, huachwi. Ukiachwa, njoo lalamika. Sasa point tatu umesoma masomo ya social sciences, hupati Samia Scholarship, haijalishi ndivyo vigezo vilivyo. Vipo wazi, lazima tuvikubali. Kama tunataka mfumo mwingine kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina scholarship ambazo ni Means Testing.
Mheshimiwa Spika, tunapambana kuongeza scholarship nyingine za Means Testing lakini hii ya meritocracy tuilinde, tuitetee kwa sababu ni kivutio kikubwa sana cha wanafunzi wenye uwezo mkubwa kwenda kusoma science, kwenda kusoma engineering na kwenda kusoma elimu tiba vyuo vikuu.
Mheshimiwa Spika, sasa kuhusu vyuo vikuu, yaliyosemwa hapa, kwanza nasema ni kweli lazima tukiri kwenye upungufu. Mheshimiwa Prof. Manya tulikuwa wote chuo kikuu, ni kati ya maprofesa, tumemzungumza Mheshimiwa Prof. Muhongo, hatujamzungumza Mheshimiwa Prof. Ndakidemi. Professors wazuri sana humu ndani ni internationally recognized. Pia Mheshimiwa Prof. Shukrani Manya ni Profesa mzuri sana, very young guy, very well recognized internationally. Alichosema, yote hapa tunabeba bila kupunguza hata kitu kimoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya yamerudiwa kwa namna moja ama nyingine na Mheshimiwa Prof. Ndakidemi, ndugu yangu Mheshimiwa Balozi Dkt. Bashiru, Mheshimiwa Prof. Muhongo na baadhi ya watu wengine hapa tunabeba. Tayari tumeshaanza kufanya baadhi ya kazi, congestion vyuo vikuu ni problem, hatuwezi kukaa hapa tukadanganya.
Mheshimiwa Spika, accommodation is a problem, we are not going to cheat anybody. Tunataka tuboreshe mazingira na maisha ya wanafunzi chuo kikuu. Tunataka walimu wawe na ofisi za kutosha, wakae kwa kujinafasi vizuri, waendelee kufundisha.
Mheshimiwa Spika, hapa katikati tulikuwa na presha kubwa ya kuongeza, lakini Serikali hii na hii ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan jamani ndiyo imevuta mradi wa Higher Education for Economic Transformation. Fedha takribani shilingi trilioni moja kuwekeza katika vyuo vikuu kwenye miundombinu na kufungua campus nyingine kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tuna-decongest hizi main campus tulizonazo.
Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Prof. Shukrani ungependa pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tujenge kila kitu pale, lakini wenzetu wengine wa Kigoma safari hii watakuwa na campus ya chuo kikuu na Lindi watakuwa na campus, lakini hizi tutazitumia sasa hivi ku-address baadhi ya hizo issue ulizosema kuwe na wahadhiri kule, kuwe na nafasi ya kutosha waweze kufanya vizuri.
Mheshimiwa Spika, suala la welfare kwenye mabweni na kadhalika tunalibeba na tuko serious, tunafikiria namna ya kulifanyia kazi. Kwa hiyo, hizi zote ni point well taken. Labda niseme kwa upande wa Tunduru kwa sababu Mtwara tumeshazungumza. Mheshimiwa, nisiposema hili maana yake Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru hili amekomaa nalo na ni Mjumbe wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tunduru kikwazo kikubwa kwanza ilikuwa ni ukubwa wa eneo. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Kingu, sasa tumepewa eneo kubwa zaidi. Sokoine University wanajaribu kumalizia compensation halafu baada ya hapo tutaanza kazi. Kwa hiyo, kile ambacho mmekivumilia muda mrefu natumaini baada ya muda kulingana na bajeti tutakavyopata kwa kadiri tutakavyopata bajeti, Mheshimiwa Kingu tutaona sasa kazi inaenda pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, umelisemea hili sana kila mara nikitoka hapa ni hilo hilo umenibana. Nadhani wananchi wa Tunduru wakuelewe, wakusikie, wakupige mitano tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namna ya kuhakikisha kwamba tunaongeza elimu ya juu ni kuunga mkono vyuo binafsi. Ndiyo maana hata kwenye mikopo ya wanafunzi tunahakikisha kwamba tunawapa fedha wanafunzi wajichagulie wanaenda kusoma wapi, ilimradi wakidhi vigezo na tunavisimamia vyuo hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndiyo tumekuwa tukichukua hatua, tunapoona hawajafikia vigezo. Sasa hivi wameniambia wamekuja Chuo Peramiho pale na Mbunge wa Peramiho namfahamu. Wamenifuata wenye Chuo chao pale kwamba sisi tumeanza kuwekeza, tutapata vigezo vinavyotakiwa, tutafungua tena Chuo Peramiho. Kwa hiyo, nadhani Ruvuma itakuwa siyo na chuo kikuu kimoja tu, pengine siyo viwili tu, lakini hiyo ni juhudi ya sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, sehemu zote sekta binafsi ikitetereka kidogo, hatupendi kufunga vyuo, hatupendi kabisa kufunga vyuo. Tunapenda kuvishika mkono viendelee, lakini na vyenyewe lazima vituelewe kwamba tunahitaji tusishuke kwenye standard. Lazima tujiulize maswali, sasa hivi mwanafunzi ni mtaji kwa chuo. Kwa hiyo, chuo ambacho source yake ya income ni mwanafunzi, mwanafunzi akifanya vibaya, akiwa discontinued ina maana unajinyima mapato kwa chuo binafsi.
Mheshimiwa Spika, lazima tuangalie mkakati, tutafanyaje ili hii incentive ya ku-retain mwanafunzi ambaye yeye mwenyewe sasa hataki tena kusoma ili kuwa na kipato aendelee kusoma kule? Hili ni muhimu tulifanye au kutoa marks kubwa ili wanafunzi waone tukienda huku tunapata GPA nzuri sana. Kwa hiyo, vyuo binafsi tutavisimamia, tutavishika, tutaendelea navyo.
Mheshimiwa Spika, naamini huenda Peramiho kikawa Chuo cha kwanza ambacho tutakifungua na hivi vingine ambavyo vimekwama, vimeyumba na vimepata matatizo, tutafanya navyo kazi kwa karibu, na TCU itafanya kwa karibu, na Mheshimiwa Mbunge wa Peramiho najua sasa tumemaliza hili suala ambalo nawe umekuwa ukilifuatilia sana.
Mheshimiwa Spika, hebu twende kidogo, na-pick randomly sasa hivi, kwenye VETA. Nadhani alikuwa Mheshimiwa Dennis Londo alisema sasa VETA iende TAMISEMI, ibaki Wizarani au iende wapi? VETA ni mamlaka na kama ambavyo vyuo vikuu na hatua zinachukuliwa. Sasa hivi kurudisha ule uhuru wa vyuo vikuu hatua mbalimbali zinachukuliwa, tumezianza lakini kuwa na mamlaka vile vile ina maana siyo idara ya Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ile inaweza ikafanya kazi vizuri. Tunachohitaji na ku-demand kutoka kwenye uongozi wa VETA ni kuwa umewa-robust kwa sababu VETA zitakuwa nyingi sana hapa nchini. Kuwe na usimamizi mzuri na kuhakikisha kwamba zinafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Shangazi alizungumza kitu ambacho ni muhimu sana. Alijaribu kuonyesha contradiction kati ya Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978 kama ambavyo imefanyiwa marekebisho kadhaa na Sera hii sasa hivi ya Elimu na Mafunzo Toleo la 2023. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna contradiction nyingi lakini kwa kweli sheria inatakiwa kuwa zao la sera. Sisi tulivyojua tunabadilisha sera tulisema tusikimbie kwenye sheria mpaka tujue makubaliano kwenye sera tunasema nini? Utaenda kwenye sheria kusema nini? Kwamba elimu ya lazima miaka 10!
Mheshimiwa Spika, hilo linaingia kwenye sheria endapo sera ndivyo ilivyoelekeza. Hapo mengine ya changamoto, tumesema re-entry program ambayo nitaizungumzia sasa hivi ambayo ukienda kwenye sheria utakuta ina ukakasi. Mwanafunzi hayuko shuleni siku 90, unamfukuza. Mwelekeo wetu sasa hivi ni kurudisha watoto wote wasome.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi baada ya sera kupita, tumeanza mchakato wa sheria. Mtasikia tu tunakusanya maoni kwa wadau ili twende kwa AG kumwuliza anaonaje yale ambayo tunadhani yafanyike, ni sheria mpya au ni marekebisho? Kwa hiyo, hilo tunalifahamu Mheshimiwa Shangazi na baadhi ambao wamezungumza hapa kwa sababu kwa sasa hivi kwa kweli sheria na sera zikikutana, zitagombana kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hebu tuzungumzie kuhusu re-entry kidogo ambayo tumezungumza hapa. Leo hapa wametambulishwa wageni wa Wizara ambao ni ma-researcher wanafanya kazi ya research aina mbili, moja nilieleza hapa. Moja ni kuhakikisha kwamba takwimu zote za kila Mtanzania zinaingia katika mfumo wa elimu wa BEST.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sasa hivi mfumo wa TCU utaunganishwa na NACTVET, tutaunganisha na Baraza la Mitihani. Wanafunzi hata wakienda kusoma shule ambazo zinatumia Cambridge Curriculum itabidi tuwajue, tuwa-track wanavyoendelea wakifika chuo kikuu tunataka tujue wanasoma program gani ili sasa hivi ukiulizwa wangapi wanasoma TEHAMA vyuo vikuu, degree? Uweze ku-click na kupata taarifa.
Mheshimiwa Spika, kazi inaendelea vizuri sana, inafanywa na wahadhiri wetu wa vyuo vikuu. Tumewakusanya tu, tunawalipa, wanafanya na support kidogo ya baadhi ya donor, lakini kazi inafanywa chini yetu ili tuweze ku-trace out. Maana yake baada ya kazi hii kukamilika ya kuunganisha na takwimu na kuwa tuna bench mark na census, tutajua kwa ukweli dropout ni kubwa kiasi gani kwa haraka haraka tunajua ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunaangalia tu wanafunzi walivyoingia darasa la kwanza halafu tunasubiri miaka saba, tukija tukiangalia ni wangapi wamemaliza shule. Hapa katikati kuna mgogoro mkubwa sana, lakini tunajaribu kufanya hiyo tuweze kuwa-trace. Lile swali ameuliza Mheshimiwa mmoja kwamba na wale wanaosoma wengine wameacha vyuo vikuu, wameacha kusoma pengine kwa sababu ya mikopo na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, katika mfumo huo ambao nadhani mwezi wa Sita mwishoni utakuwa umeshaunganishwa, utatusaidia sisi kujua haraka sana nani amejisajili? Ameenda Mzumbe na alisoma miaka mingapi? Ameondoka lini na pengine tutam-trace out kujua sababu ya kuondoka kwenda kusoma, lakini tutaenda kuangalia dropout kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna timu ndogo inafanya kazi, imepitia Tanga, imeenda Lindi, imeenda Mbeya, imeenda Njombe, iko Dodoma, itaenda Kigoma, itaenda sijui mkoa gani mwingine, imeenda Geita imeenda Mwanza kuwafuatilia wale mabinti ambao waliacha shule kwa sababu ya ujauzito, kuangalia waliorudi changamoto ni zipi na fursa zimekaaje, kuangalia maslahi ya vile vichanga, kuangalia wale ambao hawakurudi, ni kwa nini hawakurudi? Taarifa yenyewe tutaipata. Nadhani itatusaidia zaidi kuimarisha namna ya kuwarudisha hawa mabinti shuleni kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachoamini ni kwamba baada ya hapo itakuwa ni kazi kubwa itakayofanywa na timu hii ambayo wanaangalia re-entry program kwa teens pregnancy na dropout ya boys kwa ujumla wake kwa nchi nzima kwa sababu kwa kweli ni tatizo kubwa ambalo wanasema ni elephant in the room, nobody talks about it, lakini ni time ya kuli-adress hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa heshima na taadhima naomba kutoa hoja. (Makofi)