Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JANETH M. MASSABURI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa zawadi ya uhai. Nikushukuru wewe pia kwa kunipa fursa ya kwanza siku ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi hii. Amefanya kazi kubwa ya miradi, Mheshimiwa Waziri amesema, sina haja ya kurudia kwa sababu muda ni mchache. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Waziri Bashungwa, amekuwa ni kijana mtulivu, msikivu, mwenye nidhamu na unyenyekevu wa hali ya juu na ni mchapakazi asiyetiliwa shaka. Katika Wizara zote alizopita tumemuona uchapakazi wake. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kutokana na mpango wa kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa. Kwa kutekeleza mpango huu kutasaidia vijana wengi kupata ajira, hivyo itakuwa ni mapinduzi makubwa katika sekta ya ujenzi. Nimshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa kuwa makini kwa kuteua Waziri wa namna hii. Kwa eneo hili la sekta ya ujenzi hapa pamepatikana mtu mahususi, hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mpango huu wa kuwajengea uwezo wazawa utasaidia kuimarisha uchumi wa vijana wetu na pia utasaidia kupunguza fedha za kigeni ambazo wanalipwa wakandarasi wa nje. Kwa hiyo, Watanzania tutakuwa tumejengewa uwezo mkubwa kwa uchumi wa ndani na tena tutakuwa tumeondoa umaskini katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, wakandarasi wamekuwa wakitumia riba na kudai riba kubwa. Riba hizi zimekuwa zikipunguza mapato katika sekta hii ya ujenzi.
Mheshimiwa Spika, sasa ombi langu, niiombe Serikali ipunguze au wakati inapopanga mpango wa kujenga barabara au mpango katika sekta ya ujenzi iwe na uwezo kwanza wa fedha na iwe na uhakika wa fedha kuliko kutangaza tender na hatimaye tupate riba kubwa, wakandarasi waweze kupata hiyo riba na sisi Watanzania tunazidi kuathirika katika sekta hii ya ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hali hii imekuwa ni ngumu sana, tumetembelea miradi mingi na tumekuta mapungufu hayo ya riba katika maeneo kadhaa. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iangalie maeneo hayo kwa umakini sana.
Mheshimiwa Spika, niongelee kuhusu TEMESA, tunaiomba Serikali iweze kuijengea uwezo TEMESA na pia iweze kuitafutia ubia na hasa katika miradi ya vivuko. Kumekuwa na ile Kampuni ya Songoro Marine inafanya vizuri sana, kwa hiyo, TEMESA kama itajengewa uwezo na kuingia ubia na kampuni ile ya Songoro Marine itasaidia kujenga vivuko vingi na vilevile itakuwa na manufaa katika nchi zinazotuzunguka kwa kujenga vivuko vingi, si Tanzania tu bali na nchi zinazotuzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee Mkoa wa Dar es Salaam; Mkoa wa Dar es Salaam sisi hatuna ruzuku na wala hatuna mashamba. Sisi tunahitaji barabara na mifereji, mito imeharibika, barabara zimeharibika, madaraja yameharibika, lakini bajeti mliyotutengea ni ndogo. Ukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam na ukubwa wake na uchumi unaotokana na wafanyabiashara na wananchi wa Dar es Salaam ni mkubwa. Kwa hiyo, tunaomba hata bajeti wanazozipanga waiangalie Dar es Salaam kwa jicho la pembeni. Tunashida sana Mkoa wa Dar es Salaam. Siasa zetu za Dar es Salaam ni barabara, tumekuwa tukipiga kelele barabara, barabara, barabara. Sisi hatuhitaji kingine, ni barabara, barabara, barabara, ndizo siasa za Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii tena kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa mradi wa mabasi ya mwendokasi, mradi ule ujenzi wake unakwenda kwa kasi sana. Tunaomba na zile awamu nyingine zifanyiwe kwa haraka ili kunusuru wakazi wa Dar es Salaam ambao wanakaa masaa mengi njiani, wanatumia zaidi ya saa nne kufika kwenye shughuli zao. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iwaangalie kwa jicho la huruma wananchi wetu wa Mkoa wa Dar es Salaam na ile bajeti ya vivuko au bajeti ya mito, maana kuna mito mingi Mkoa wa Dar es Salaam, tunaomba bajeti yake iwe kubwa, hali ni mbaya.
Mheshimiwa Spika, tumeona wamepanga kwamba watajenga daraja la pale Jangwani, lakini ikitokea siku mvua imenyesha mkoa mzima una-collapse, kunakuwa hakuna kazi. Kuna siku tumekaa kwa saa 12 magari hayatembei na watu hawafiki nyumbani mwao, vilevile watu hawafiki kazini. Hiyo inatokana na kile kiwango kidogo wanachotupatia kwenye bajeti ya ujenzi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba nikushuru na naunga mkono hoja. (Makofi)