Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ninaomba nikushukuru sana, kwa kunipa nafasi na mimi niweke mchango wangu kwenye hii Wizara ya Ujenzi. Kwanza, kabisa ninamshukuru Mheshimiwa Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Naibu wake. Ahsanteni sana kwa kazi mnayoifanya kumsaidia Mheshimiwa Rais, wetu Mama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwatimizia wananchi ndoto yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waziri nikushukuru sana kwa kweli kipindi hiki ambacho kumekuwa na mvua si za kawaida hasa kwenye maeneo mengi sana Dar es Salaam na Jimbo la Kawe, kwa ujumla tulikubwa na mafuriko, madaraja yakakatika, mito ikapanuka na barabara zikaharibika, kwa namna ambavyo wewe na Wizara yako mlikuwa wepesi sana. Mahali pale ambapo lile Daraja la Kunduchi, lilikatika pamoja na Daraja la JKT na Daraja la Mbopo. Mlipokuja mkanihakikishia kwamba, mtajenga ndani ya saa 72 na kweli mlifanya hivyo mlijenga ndani ya saa 72, hongereni sana kwa ajili ya kazi hiyo. Nakushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TANROADS, ndugu yangu Engineer Mohamed Besta, pamoja na Katibu Mkuu Balozi Engineer Aisha, kwa namna ambavyo na wao walifika kwenye matukio hayo wakashirikiana pamoja na wananchi na jambo likaenda vizuri ndani ya saa 72, madaraja yote na barabara zote zilikuwa zimejengwa, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa moyo wako huo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ninakushukuru, kwa sababu ya barabara inayotoka Bunju B kwenda Mabwepande, kwenda mpaka geti la Mabwepande mpaka Mpiji Magohe. Wakati huo wa mvua nyingi zilipokuwa zimenyesha Mheshimiwa Waziri wewe ulikuja pamoja na Watendaji kazi wako kwenye mvua tukapita wote kwenye matope ulionesha mfano mzuri sana wa uongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, nikwambie jambo moja; tuna Mawaziri wengi sana wazuri katika Baraza letu, lakini wewe ni mmoja wa Mawaziri wazuri tulio nao. Kwenye Kitabu cha 1 Petro 5:5 inasema hivi; “Kwa maana Mungu huwapinga wenye kiburi na huwapa neema wanyenyekevu”. Kitabu cha Yakobo Sura ya 4:6 kinasema; “Mungu huwapinga wajikuzao bali huwapa neema wanyenyekevu.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Bashungwa wewe ni kati ya Mawaziri tulio nao wanyenyekevu sana, Mungu akuinue na aendelee kukupa neema iliyozidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, ningependa kutoa ushauri kadha wa kadha, kwanza, nilikuwa ninaomba mfahamu kwamba, suala la barabara is the matter of national concern na hasa kwenye Miji mikubwa kama Mji wa Dar es Salaam, barabara zote zimeharibika.
Mheshimiwa Spika, mimi kama Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, nimefanikiwa kutembea shina kwa shina Jimbo la Kawe, tuna mashina 1,000. Nimekwenda shina kwa shina barabara zote mbovu kila sehemu ziwe za TARURA na za TANROADS barabara zote mbovu.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninaomba ushauri mmoja kwamba, ni vizuri badala ya kutegemea utaratibu wa kawaida, mtengeneze special supplement, ambayo inaweza kufanya barabara za Dar es Salaam, zikapitika kwa urahisi zaidi. Kwa nini mfanye special supplement kama unavyojua Mheshimiwa Waziri, road fund (hela ya barabara) huwa tunapata hela ya barabara kwenye kila lita ya mafuta inapouzwa na Dar es Salaam, ndio mahala ambapo magari mengi sana yanaendeshwa.
Mheshimiwa Spika, barabara za Dar es Salaam, zikiwa nzuri magari mengi yataendeshwa na utapata hela nyingi ya road fund itakayokusaidia. Kwa hiyo, nilikuwa ninakuomba sana unapowaza kuhusu barabara ukitumia utaratibu wa kawaida wakutengeneza barabara za Dar es Salaam haitawezekani, lazima kuwe na special supplement itakayosaidia barabara zitengenezwe na magari mengi yaendeshwe na hela nyingi ya road fund iingie, kwa sababu kuna magari mengi Dar es Salaam. Ni philosophy ya kawaida Mheshimiwa Waziri, ng’ombe anayekupa maziwa unampa majani ya kutosha. Kwa Dar es Salaam magari yanaendeshwa sana, kwa hiyo, hiyo lita moja ya road fund inapatikana kwa wingi zaidi, tupe majani ya kutosha ili tukupe mafuta ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninakuomba Mheshimiwa Waziri ni barabara nyingi, ile barabara ya kutoka pale Tegeta kwenda Basihaya mpaka Nyaishozi imejengwa bila mitaro ni barabara ya TANROADS hiyo. Barabara hiyo inaleta mafuriko kwa watu, ninaomba sana wakati mnajaribu kuangalia barabara muiangalie barabara hiyo kwa makini sana.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine kuna hiyo barabara inayotoka Tegeta kwenda mpaka Kiwanda cha Wazo, hiyo barabara imekuwa nyembamba. Kwa hiyo, magari yanapangana kuanzia asubuhi mpaka jioni na watu wanapoteza maisha yao kwa ajili ya hiyo Barabara, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri iangalie vizuri.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya yote ninaomba sana suala la barabara katika Jiji la Dar es Salaam, liwekewe mkakati maalumu, kwa sababu barabara zote zimeharibika. Mungu akubariki sana. Mungu huwapinga wajikuzao huwapa neema wanyenyekevu. Mungu akupe neema hiyo Mheshimiwa Waziri na uendelee vilevile. Ahsante sana, kwa unyenyekevu wako, ninakushukuru sana. (Makofi)