Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo na mimi kuchangia Bajeti ya Wizara hii ya Ujenzi, Wizara muhimu kabisa. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii ya Ujenzi kwa kazi nzuri. Wizara hii nimeona imepitia katika changamoto na kipimo kikubwa cha ku-test uwezo wao, uvumilivu na kujitoa kwao kutokana na mvua za El Nino pamoja na Kimbunga cha Hidaya, lakini binafsi niseme naona wamefaulu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu amewajalia wamefaulu kwa sababu tumewaona katika maeneo mbalimbali katika kuangalia namna gani ya kurejesha miundombinu katika hali yake ya kawaida. Kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Bashungwa kwa kufika katika Daraja la Mpiji Chini katika kuangalia namna gani ya kuweza kuendeleza ujenzi wa daraja hili. Nataka nimwombe Mheshimiwa Bashungwa nimeona kwenye hotuba yake kwamba ameeleza daraja hili ambalo linaunganisha Bagamoyo na Kinondoni. Daraja hili lilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati anafungua Kituo cha Mafunzo Maalumu cha Kijeshi kule eneo la Mapinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa daraja hili kwa kweli mkandarasi tangu amepewa mkataba mwaka jana, Januari 2023 kazi haiendelei vizuri tunakushukuru kwa maelekezo yako, lakini nikuombe Mheshimiwa Bashungwa daraja hili ambalo pia linaingiliana na barabara ya Mingoi – Kiembeni, ulifika na uliona wananchi wanavyolalamika barabara inaenda mpaka kwenye Kituo hiki Maalum cha Mafunzo ya Jeshi na ambayo inaunganisha Vitongoji vya Kiembeni, Mingoi, Udindivu, Kiharaka na maeneo hayo katika Kata ya Mapinga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimwombe Mheshimiwa barabara hii ni mbaya sana. Nikuombe kilometa tano zinazobaki zihamie TANROADS ili Wananchi wa Msongola, Tungutungu, Minazi Minane wote ambao wanaunganishwa na daraja hili waweze kutengenezewa barabara hii na pengine hata kama isifike kiwango cha lami basi kiwango cha moramu. Nilitembelea kuona namna gani wanawake wanapata shida, Mbunge wa Jimbo naye ameisemea hii barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niipongeze sana Wizara hii kwa mara ya kwanza kwa kupitia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mipango ya kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa na wakandarasi wanawake. Kwa mara ya kwanza tumeona dhamira ya dhati ya kuwainua wakandarasi wanawake kwa kuwatengea barabara ya lami kilometa 20 Mkoa wa Songwe na kazi hiyo imetangazwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Engineer Aisha - Katibu Mkuu wa Wizara hii na tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumpangia Katibu Mkuu mwanamke. Tunaona namna gani anavyopambana kuhakikisha maslahi ya wakandarasi wanawake na wahandisi wanawake katika Wizara hii yanazingatiwa. Kwa hiyo nimwombe sana, pamoja na azma nzuri ya kuwazesha lakini tuangalie namna gani taasisi za fedha zinaweza zikawapa mitaji wakandarasi hawa wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee itazame pale watakapopewa kazi yale malipo ya certificate zao yazingatiwe. Kwa sababu kama nia ni kuwajengea uwezo basi mnyororo wa kuwajengea uwezo huo uzingatie namna ya kuwawezesha ili zile kazi watakazopewa wafanye vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda niishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara unaondelea wa Tanga – Pangani na Mkange – Makurunge. Hapa naomba niwasilishe kilio cha madai ya fidia kwa kipande cha Mkange – Saadani – Makurunge. Mheshimiwa Mbunge amefuatilia, Naibu Waziri wetu Mheshimiwa Ridhiwani lakini mimi pia naomba, shilingi milioni 840 siyo kiwango kikubwa. Naomba mmalizie kuwalipa fidia ili ujenzi huo uendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo naomba niishukuru sana Serikali kwa ujenzi unaoendelea wa Barabara ya Nyamwage – Utete, kazi inaendelea, pia Daraja la Mbambe. Kipekee kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge mwenyewe (Mheshimiwa Waziri Mchengerwa) amekuwa akifuatilia ndani ya Serikali lakini naomba Serikali iongeze kasi. Nishukuru sana kwa ubunifu na utayari wa Mheshimiwia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza kuanza kwa upembuzi yakinifu wa Barabara ya Chalinze – Utete ambayo itakuwa ni shortcut. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kasi katika kuona barabara hii inaanza upembuzi yakinifu. Pia niishukuru sana Serikali yetu kwa kuamua kuanza upanuzi wa Barabara ya Mbagala – Vikindu kwa sababu ina foleni nyingi sana. Ina maana itarahisisha mawasiliano na uharaka kwa Wilaya za Mkuranga, Kibiti, Rufiji na hatimaye Mikoa ya Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba haitoshi naomba niielezee Barabara ya Makofia – Mlandizi – Maneromango – Vikumburu. Barabara hii imekuwa ikitajwa karibu kila Ilani, kuanzia Ilani ya 2010, 2015 na hii 2020. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, umesema sentensi moja tu kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami. Nikuombe sana, kuna malalamiko ya fidia katika kipande hicho cha Makofia – Mlandizi – Maneromango – Vikumburu, barabara hii ya muda mrefu. Niiombe Serikali iitazame, kwa sababu Serikali imejenga bandari kavu na inatarajia kujenga eneo la viwanda Bagamoyo, hii barabara inaweza ikasaidia. Kwa hiyo niombe uharaka wa fidia lakini pia kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho pamoja na changamoto zinazoendelea za madai katika Wizara hii lakini nina matumaini baada ya kukamilika kwa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Wizara hii na Serikali inaweza ikatenga fedha kwa ajili ya malipo ya wakandarasi. Niombe kasi ya malipo ya wakandarasi ili kuchachua uchumi wa ndani ya nchi yetu. Dhamira ni njema lakini tuangalie wakandarasi wanataka kufilisika. Kwa hiyo niombe kama Serikali namna gani mtakavyojielekeza hasa wakandarasi wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kabisa niendelee kumpongeza na kumshukuru Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Pwani kwa namna ambavyo amejipanga kuwezesha makundi ya wanawake. Utekelezaji wa 30% ya Sheria ya Manunuzi kwa ajili ya makundi maalumu, nakuomba Mheshimiwa Waziri mlisimamie hili. Nimefurahi kuona namna gani mnahusiana na Wizara ya Fedha katika mapitio ya Sheria ya Manunuzi tuliyoitenga hapa ili safari hii 30% ya manunuzi kwenye makundi maalumu hususan kwa wanawake iweze kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa wanawake wenzangu wakandarasi, wale wanaofanya masuala ya labour based katika mikoa mbalimbali Serikali yetu ya Awamu ya Sita imejipanga na sisi tuendelee kujipanga tusiiangushe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya napenda kuunga mkono na nakuomba Mheshimiwa Waziri urudi tena Mapinga kwa ajili ya Daraja la Mpiji Chini na barabara zake ili kazi iendelee, ahsante sana. (Makofi)