Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Bashungwa na Naibu wake Mheshimiwa Kasekenya pamoja na Katibu Mkuu Injinia Aisha kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika hii Wizara na kwa namna ya pekee jinsi ambavyo waliweza kutatua changamoto za uharibifu wa miundombinu wakati wa kipindi cha El Nino, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza awamu zote za Serikali za Chama Cha Mapinduzi kwanzia awamu ya kwanza mpaka awamu ya sita. Naipongeza kwa sababu mnamo Juni, 2022 Nchi yetu ya Tanzania ilitangazwa kuwa ni nchi ambayo ni ya kwanza kabisa katika Afrika kwa kuwa na mtandao mrefu zaidi wa barabara (Road Network) katika nchi zote za Afrika, ambapo ilikuwa na kilometa 86,472 kwa ujumla wake na kati ya hizo kilometa 12,786 ni trunk road na 21,105 ni barabara za Mikoa, zilizobakia ni barabara za Wilaya, Miji pamoja na feeder roads. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali yetu kwa awamu zote kwa sababu kazi hii imefanywa kwa awamu na imefanyika vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia kwamba nchi yetu pamoja na kwamba ni kubwa lakini huwezi kulinganisha na nchi zile 10 ambazo ni kubwa zaidi katika Bara letu la Afrika. Kwa hiyo, ina maana kwamba Serikali yetu imeji-commit kuhakikisha kwamba miundombinu ya barabara inawasaidia wananchi katika ngazi zote kuanzia vijijini hadi mikoani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kupongeza ukamilishaji wa uwanja wa ndege katika Mkoa wa Mtwara na kilichobaki sasa hivi tunaambiwa ni control tower pamoja na jengo la abiria, likishakamilika tutakuwa na uwezo wa kupokea ndege aina ya Dream Liner pale Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza sana kazi ambayo inafanywa na Engineer wa TANROADS, Engineer Dotto. Kwa kweli anafanya kazi nzuri sana huyu engineer wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia kwamba, barabara ya Mnivata – Newala – Masasi sasa imeshapata wakandarasi wawili na wako site, ina maana kwamba sasa huu mtandao wetu wa barabara pamoja na barabara zingine katika nchi yetu utazidi kuongezeka na kuwa zaidi ya hizi kilometa 86,000 na pengine mpaka hata 90,000 au zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee niombe sana Serikali, hapa ndiyo mahali pekee ambapo tunaweza tukawasaidia wananchi wetu katika kuhakikisha kwamba tunatekeleza ile Sheria ya manunuzi ya kutenga zile asilimia 30 kwa ajili ya makundi maalum. Siamini kabisa kwamba makundi maalum, wanawake, vijana na watu wenye ulemevu watashindwa kufanya supply hata ya cement. Kwa sababu naona kwenye barabara huwa tuna-supply, tunatumia cement. Kwa hiyo, niombe sana tuangalie kanuni zile ambazo nafikiri zinaruhusu yule contractor mkuu kuwa na sub-contractors ambao wanaweza wakafanya kazi ndogo ndogo. Tuangalie na kazi zingine ambazo zinaweza zikawasaidia wananchi wetu ili kusudi waweze kuinua kipato chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli bilioni zaidi ya 230, kusema zote zinaenda kwa mkandarasi mkuu kwa kweli siyo sawa. Naomba sana na wananchi waweze kunufaika kwa kutumia ile sheria yetu ya manunuzi ili kusudi tuweze kuhakikisha kwamba tunawasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa uwezekano upo kwa sababu kuna mikopo yetu ya kina mama, vijana na watu wenye ulemevu, tunaweza tukaitumia hii mikopo tukawasidia hawa vijana, kina mama na watu wenye ulemavu angalau hata bilioni tano basi ziweze kwenda kwa hao wananchi wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza tena kwamba tuna barabara ya kutoka Mangaka kwenda Msimbati ambayo inafanyiwa sasa maandalizi kuanza utekelezaji wa ujenzi, lakini kwa namna ya pekee napongeza jitihada za TANROADS kupitia Engineer Doto, ambapo sasa wanakwenda kutoa kipaumbele kuwapa wakandarasi wanawake. Hii ni hatua nzuri sana. Nimesikia hata wachangiaji wengine wanasema kwamba, wakandarasi wanawake wanapewqa kipaumbele, naomba Serikali yetu iendelee na jitihada hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, napongeza maandalizi ya barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi, tuna taarifa hizo kwamba maandalizi ya ujenzi yameanza, nawatakia kila la kheri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee naomba nilete ombi langu, barabara ya Kibiti – Lindi ni tatizo kubwa, ikiwa na maana kwamba mashimo yanapokarabatiwa na tumekuwa tukiuliza sana hapa ndani, ukarabati unafanyika lakini ndani ya siku chache yanabomoka tena yanatengenezwa mashimo makubwa zaidi na hii ni kutokana na magari ambayo yana uzito kupita ule uwezo wenyewe wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wakati wa kuhitimisha hoja yake Mheshimiwa Waziri atupatie majibu kwamba wana mkakati gani wa kuhakikisha kwamba barabara hizi zinapofanyiwa matengenezo hazibomoki ndani ya muda mfupi. Vilevile, watuambie mkakati mahsusi ambao utasaidia kukabiliana na matatizo au athari za mabadiliko ya tabia ya nchi pindi mvua za El Nino zinapotokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia mara kadhaa Mheshimiwa Waziri akisisitiza kwamba maeneo yale ambayo yanakuwa na usumbufu yasirejee tena hasa katika hii barabara yetu ya kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma hapa karibu na maeneo ya Jirani na Gairo hapa au Kibaigwa. Amekuwa akitoa msisitizo kwamba maeneo hayo yafanyiwe ukarabati wa kudumu au hatua za kudumu zichukuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo eneo hilo pekee, Mheshimiwa Waziri mwenyewe ameona ile Barabara ya kwenda kule kwetu Kusini imeleta matatizo makubwa lakini hata barabara zingine katika nchi yetu zitakuwa zina matatizo makubwa, kwa hiyo ninaomba wafanye mapitio kuona maeneo gani yana uwezekano wa kuathirika na mabadiliko ya tabianchi ili kusudi maeneo yote yaweze kufanyika utatuzi wa kudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nashukuru tena kwa kunipa nafasi na niseme naunga mkono hoja kwa asilimia 100, ahsante sana. (Makofi)