Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi kwa dakika hizi nane. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais, maombi ya Musoma Vijijini yamekubaliwa kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba barabara tumepewa. Tumeomba mambo ya umwagiliaji tumepewa, naomba kuwathibitishia kila mtu amemsifia Waziri Bashungwa na Naibu wake labda mimi ndiyo nitawathibitishia zaidi. Hawa nimefanya nao kazi kabla ya wao kuwa wanasiasa, wakavuka viwango vyangu vya utendaji. Narudia, wakavuka viwango vyangu, kwa hiyo msiwe na wasiwasi nao hawa wawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara yangu ya Musoma – Makojo – Busekela, Waheshimiwa Wabunge nadhani wakati tunaomba barabara vilevile tuwe tunaweka na vigezo. Mimi barabara yangu ina vigezo vyote vya maana vya kiuchumi. Kilimo, tunalima pamba inatumia barabara hiyo hiyo, samaki wanaopelekwa viwandani wanatumia barabara hiyo, maziwa yanayopelekwa viwandani yanatumia barabara hiyo, kule Musoma Vijijini tunachimba dhahabu na shaba inatumika barabara hiyo hiyo, Makao Makuu ya Halmashauri yanatumia barabara hiyo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina barabara moja ambayo inaunganisha vijiji 67, kwa hiyo Mheshimiwa Bashungwa na kijana mwingine japokuwa nimewasifia msisahau barabara yangu lakini mmenipa ahadi mko kwenye kumtafuta mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, kilichonifanya mimi nisimame hasa ni mambo ya fedha. Wote tunakiri fedha hazitoshi, naomba unipatie muda niwaeleze mahali pa kutoa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hesabu ni kwamba fedha za miradi ni trilioni 1.69. Tumekumbushwa hapa madeni na riba ukipiga inafika karibu trilioni moja. Kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hii Wizara wanazo bilioni 700 za kutekeleza Barabara, zilizobaki ni bilioni 700, tuende kwa mahesabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi shilingi imeshuka kidogo, barabara iliyokuwa inajengwa kilometa moja kwa shilingi bilioni moja sasa hivi nadhani inakaribia shilingi bilioni 1.5. Kwa hiyo kwa shilingi bilioni 700 ukigawa kwa vyovyote vile huyu Mheshimiwa Waziri anakazi ya kilometa 500 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shilingi bilioni 500 kwa mikoa 26 lazima tumuombee fedha. Ambao tumekaa Bungeni kwa muda suala la kumuombea fedha siyo geni wala siyo la ugomvi, ni sisi Waheshimiwa Wabunge tupendekeze kwamba kile kipindi cha majadiliano Mheshimiwa Waziri wa Fedha akikaa na Jirani yangu hapa Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti lazima waongezewe fedha hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ilikuwa imependekeza wapewe shilingi trilioni tano. Mimi kwa udadisi wangu nikauliza Engineer wa barabara maombi yetu wanapaswa kuwa na shilingi trilioni 15. Hata hizi tano Kamati ilisema kwa kuwa hatuna fedha wapewe tano. Sasa Waheshimiwa Wabunge mimi nawashawishi tumuombee, tuombee hii Wizara ipewe angalau shilingi trilioni 3.5 ili akitoa shilingi trilioni moja kulipa madeni abaki na na shilingi trilioni 2.5 ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mahali pa kutoa fedha. Kwanza nampenda Mheshimiwa Mbunge wa Lindi aliongea jamani mwaka ujao na miaka inayokuja tusije tena kulumbana humu lazima Tume ya Mipango ifanye kazi yake. Yani kwenye mambo ya uchukuzi na usafirishaji tuwaulize kipi kipaumbele? Kuna surface transportation yani ardhi inamaanisha reli na barabara halafu kuna air (ndege), kuna maji (meli); kipi namba moja tuwekeze hela nyingi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Tume ya Mipango itusaidie sana kwenye hilo la vipaumbele. Kitu cha pili namalizia, utunzaji wa barabara tulizozijenga. Mtaalamu ameniambia asset (thamani) ya barabara zote tulizojenga zina thamani ya shilingi trilioni 40 na utunzaji wake unataka trilioni mbili. Kwa mwaka unaona yeye hata bajeti ya shilingi trilioni mbili za kutunza barabara hana. Kwa hiyo lazima tumuombee fedha. Sehemu nyingine ya kupata fedha ni kwenda nje. Hiyo wala hii tusione kwamba ni aibu na Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri aendelee kutafuta fedha nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zitapatikana World Bank, IMF na Africa Development Bank. Wenyewe riba yao ni kati ya 0% mpaka 2%; twende huko. Pengine pa kupata fedha ni hii ya EPC+F (Engineering, Procurement, Construction and Finance) lakini hatuwezi kuongea na hawa wa EPC+F bila sisi Watanzania kujua thamani ya hiyo barabara. Kama ukimuachia kila kitu tutapigwa. Isitoshe hii ni 100% private kwa nini tena wanataka Serikali iwasaidie kutafuta fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ya kupata fedha ni Sheria yetu ya P3 (Public, Private, Partnership). Zinajengwa barabara kama ya Kigamboni zinakuwa na road toll. Ukienda miji yote Duniani watu wanapita kulipia hizo barabara. Kwa hiyo hayo ndiyo yalikuwa mawazo yangu kwamba tuombe wapewe fedha wakati wa majadiliano yetu na utakuwepo tuwaombee shilingi trilioni 3.5, ahsanteni sana. (Makofi)