Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya mimi kuchangia Wizara ya Ujenzi. Kama walivyosema wenzangu na mimi nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge humu wanaotaka kuthibitisha kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inasikia na inafanyia kazi yanayosemwa na Waheshimiwa Wabunge kwa kiasi kikubwa. Watu wanafahamu mimi tangu nimekuwa Mheshimiwa Mbunge humu 2021, 2022 na 2023 kila nikisimama nazungumzia barabara yangu ya Ifakara – Kidatu kilometa za lami karibu 67 mpaka Serikali iliposikia imetatua changamoto zile akiwepo Mheshimiwa Waziri Professor Mbarawa na baadaye kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa amerithi kijiti kile. Katika utatuzi wa changamoto tayari ameshafanya ziara katika barabara hii tumeambatana nae amezungumza vizuri sana pale Mikumi kwa maana ya Daraja la Ruaha – Mang’Ula na amefika Ifakara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ungeweza kuwaambia Wananchi wa Kilombero chochote kile wakakuelewa lakini siyo barabara ya Ifakara – Kidatu. Hivi navyozungumza na mama yangu Mheshimiwa Aleksia yupo hapa tunatokea sehemu moja. Mheshimiwa Waziri unateleza tu sasa hivi na wewe umeona kiwango cha barabara kilivyo kipana na sisi kutoka Kata ya Kidatu mpaka Ifakara tuna kata karibu 10 ambapo kuna maporomoko ya maji kutoka milima ya Udzungwa lakini vimejengwa kwa standard nzuri changamoto zipo hapa na pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa hivi ukishatoka Hifadhi ya Mikumi unataka kuja Ifakara unatembea kuna kama kilometa moja tu haijakamilika katika kilometa 67; piga makofi kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tusishukuru kwa nini? Kwa hiyo tunataka kukushukuru kwa dhati Mheshimiwa Waziri. Siyo kwamba tukishukuru hatutaomba tena, tutaomba lakini kwa jambo hili kubwa watu wanaweza wakaona lami wanateleza kwa lami, wanatembelea bajaji na pikipiki hawawezi kujua changamoto tulizopita mpaka kukamilika kwa barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. Kwa hiyo nataka kumshukuru pia Chief of TANROADS Engineer Mohamed Besta. Kwa kweli unamuona kabisa ana dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko katika nchi yetu ya barabara lakini ukitaka kumuongezea hata kipande cha kilometa moja unamuona yule mzee kama anatetemeka hivi kutokana na ufinyu wa fedha lakini ni Engineer mzuri tunampongeza. Mimi nimeona Mheshimiwa Waziri hakuna wa kukulaumu kwa kweli tulivyoona unahangaika kule Mtwara na Lindi unasafiri usiku kucha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona wataalamu wako wa TANROADS akiwepo Chief of TANROADS yupo kwenye boti. Sasa wamepanda boti hata life jacket hawajavaa, mnatafuta matatizo huko. Sisi tunataka mtuhudumie lakini kwa kweli mnatuhudumia mpaka mnapitiliza. Kwa hiyo tunashukuru sana na tunawapongeza sana na natumia fursa hii kumualika Katibu Mkuu naye afike aone barabara ile Balozi Engineer Aisha Amour afike Kilombero aitazame barabara yetu nzuri ili tuweze kutatua changamoto zinazokabiliana na ile barabara kwa karibu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri mimi nataka kusema barabara hii ni muhimu sana. Pia, mimi kwa maoni yangu ni kwamba hizi barabara za Masaki - Dar es Salaam huko hatusemi kwa njia mbaya kuna barabara za kipaumbele kama alivyosema Mheshimiwa Profesa Muhongo. Nchi hii ina barabara ya kuunganisha wilaya na wilaya hazijakamilika tupunguze hizi barabara ndogo ndogo huko. Angalia Kilombero unatoka Morogoro Mjini unafika Kilombero Ifakara huwezi kwenda Wilaya ya Malinyi huwezi kwenda Ulanga, huwezi kwenda Mlimba kama barabara hazijakamilika hizo ni wilaya nazungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika vipaumbele na kufungua nchi yetu tunavyosema kilimo ni kipaumbele sisi Mkoa wa Morogoro tunaongoza kulima mpunga lakini percent kubwa inatoka Malinyi, inatoka Kilombero kwetu, inatoka baadhi Ulanga. Unasafirishaje mazao haya kama hatuna barabara? Mwenge kwa mara ya kwanza umetembezwa kwa mguu kilometa 46 Malinyi na tumeshasaini ile barabara ya Ifakara kwenda Malinyi mpaka Kiongozi wa Mwenge anasema sijawahi kuona hiki kitu katika historia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali imetusikia barabara ya Ifakara kwenda Mlimba mkandarasi tunavyozungumza yupo site. Kwa hiyo tunasema pelekeni nguvu kule Morogoro chini katika kufungua mazao. Kwa hiyo kila barabara mnataka kujenga na Waheshimiwa Wabunge tunaomba barabara hata mimi Ifakara Mjini nina barabara ya TANROADS. Siombi sasa hivi kwa sababu kuna barabara kubwa Ifakara – Mlimba, kuna barabara ya Ifakara kwenda Malinyi ni barabara kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nataka kusisitiza hilo lakini pili nataka kusema fidia Mheshimiwa Waziri. Hii barabara yetu ya Ifakara – Kidatu kuna wananchi bado wana malalamiko na Engineer wetu Razack analijua hilo alikuwa anasema analifuatilia. Mheshimiwa Waziri niseme nimemsikia Dada yangu Mheshimiwa Ghati jana au juzi akichangia hapa anasema Engineer wa TANROADS wa mkoa wake ni bora nchi nzima; hapana siyo kweli. Engineer Razack wa Morogoro anaweza kuwa namba moja kwa nchi hii na wewe kama unataka kumpima Engineer bora aende Morogoro pale akaone. Mafuriko tuliyoyapata na changamoto tunazozipata kule ndiyo utajua kwamba huku kuna mwamba Razack.
Mheshimiwa Mwenyekiti, anakuwa na uhaba wa pesa na changamoto lakini kwa kweli anajitahidi kwa kazi kubwa sana; tunataka tumpongeze sana. Kwa hiyo nataka kusema hilo la fidia Mheshimiwa Waziri timu ile iende Ifakara – Kidatu tumalizane na watu wale wenye nyumba za kijani wapewe fidia zao. Kuna fidia ya Ifakara kwenda Malinyi ile barabara, kile kipande cha Ifakara kutoka Ifakara Kikwawila kwenda mpaka Daraja la Magufuli inapita Kata ya Mbasa, Kata ya Katindiuka wananchi miaka minne hawajaendeleza majengo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fidia hiyo wanasema kila mwaka wana-review wana-review. Sasa hivi nikienda Mbasa kule hawataki kuniona kama Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ya fidia yao jambo ambalo watu wanadanganywa. Barabara hii mkandarasi yupo site sasa hivi wananchi wanalalamikia njia panda kwa sababu tuta ni kubwa. Barabara za kuingia kwenda kwenye kata zao zile hazipitiki. Kwa hiyo lazima mumsimamie mkandarasi vizuri tuhakikishe barabara hizi zinapitika zote kwa kiwango kizuri. Kwa mfano Signal nimepata taarifa jana kuna mtu ameanguka maevunjika kutoka kwenye barabara ya lami kuingia kwenye barabara ya kata kubwa wameweka tuta kubwa. Sasa msipokomalia watu wale hawasikii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusaidieni wekeni tuta vizuri ambalo linaweza kwanza likatunza barabara yenyewe. Hii barabara lazima tuilinde kwa ma-culvert, vituo kuna maeneo hayana vituo wananchi wanaenda kushukia mbali na taa za barabarani. Mheshimiwa Waziri umeniahidi taa Mang’Ula nakukumbusha, taa ya Daraja la Ruaha nakukumbusha na taa ya Ifakara mjini kuendelea kuziweka katika barabara ya TANROADS kutoka Ifakara kwenda Daraja la Magufuli kwenda Lumemo na kwenda Kibaoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaziweka taa baadhi lakini umeniahidi ulivyofika pale ukanisaidia kuweka hizo taa nyingine. Kwa sababu ya muda nataka kusisitiza Mheshimiwa Waziri sisi tutakuombea fedha na naamini jambo lako litapita vizuri zaidi. Tunasisitiza sana fikirieni vyanzo vingine vya mapato na sisi kama Kamati ya Miundombinu na Mheshimiwa Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Selemani Kakoso tumeshauri, document yetu ipo pale. Sasa hivi kuna hii mnaita carbon 14 tunapata mapato. Kwa nini tusichangie kwenye barabara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ile CIF ya bandari ambayo inatozwa kwenye reli kwa nini isitozwe pia kwenye barabara? Hata ile shilingi 100 ya mafuta tunayotoza, tupendekeze ni shilingi 100 halafu ikusanywe yote iende kwenye mfuko wa barabara. Kwa hiyo sisi tunataka barabara, tunataka vitu vya barabara na tunataka pesa; lazima tufikirie nje ya box tunapataje fedha zaidi zinazotusaidia kukuza mfuko wako ili uweze kujenga barabara zinavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusisistiza kwenye madeni. Tumezunguka Mheshimiwa Waziri umesema mwenyewe na umeona watu wanadai. Tuliona Mchina analia kule Beijing – Mtwara construction na kuna ma-sub constructer wanalia. Lipeni kwa awamu, hamuwezi kulipa yote tangazeni tunalipa mwezi huu hawa, wengine wasubiri watu wataendelea kusubiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kushauri kuhusu kutumika kwa Jeshi letu la Wananchi. Mimi ni miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge tulioenda kule JKT, kuna vijana kule Engineers wapo. Sasa kama tulivyofanya Suma JKT je, kwenye construction hii hatuwezi kuwa na kampuni ya Jeshi au utaratibu utakaoonekana unafanyika katika kupunguza gharama wakapewa baadhi ya barabara zinapotokea dharura ikafanyika kama baadhi ya nchi inavyofanya? Mheshimiwa Waziri mimi nakuunga mkono hoja mimi sina nongwa na wewe. Nina imani tutakupitishia bajeti yetu hapa. Waheshimiwa Wabunge wote mliosema mtashika shilingi nawaombeni sana, chonde chonde mimi nina lami kilometa 67 tusishike shilingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)