Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kipindi hichi ambacho tumepata mvua nyingi kwa kweli wewe na timu yako tumeona mmefanya kazi kubwa tunawapongeza sana. Pia, bado kuna kazi nyingine kubwa mbele ya kuhakikisha barabara zetu zinapitika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia sera yenu wenyewe mliyojiwekea Sera ya Wizara ambayo inaeleza kwamba mtahakikisha mnaunganisha mikoa na mikoa kwa kiwango cha lami. Sisi Wilaya ya Karatu tuna barabara kuu mbili muhimu ambazo zinaunganisha Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara inayotoka Njiapanda Karatu kwenda Mang’ola mpaka Lalago mpaka Simiyu inaenda kuunganisha Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Simiyu ni barabara ya muda mrefu sana ambayo mlituahidi mtajenga kwa kiwango cha lami kilometa 129 kwa upande wetu wa Karatu kabla kuunga upande wa Simiyu. Mmeahidi na mmekuwa mkituambia usanifu unafanyika na upembuzi yakinifu lakini miaka na miaka tunakaribia sijui miaka mingapi leo toka Waheshimiwa Wabunge waliopita toka 1995 mpaka leo mnatuahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ni muhimu sana kwa uchumi. Hii barabara ndipo ambapo kuna bonde kubwa la umwagiliaji. Mnapeleka fedha nyingi kwa upande wa kilimo inajengwa miundombinu mikubwa ya umwagiliaji halafu hakuna barabara ya kufikisha hayo mazao kwenda sokoni. Kuna kilimo huku watu wanalima, tunapata wateja mpaka South Sudan, Uganda, Kenya wanakuja kuchukua vitunguu kule lakini barabara ni mbaya ni mbovu haipitiki mmetuahidi mtajenga kwa kiwango cha lami lakini hakuna. Hayo maneno yenu ya upembuzi yakinifu sijui usanifu tumechoka kuyasikia, tumechoka Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani kuona ile barabara mnaifungua kwa kiwango cha lami kwa sababu ni wenyewe kupitia sera zenu mnasema mtafungua kati ya mkoa na mkoa na ni kilometa 129 tu. Nina imani mkiamua kuweka nguvu na kutokana na mapato yanayopatikana katika hilo bonde inawezekana. Gharama mnayotumia kufanya marekebisho ya mara kwa mara kwa miaka yote hiyo mimi naamini hiyo gharama mliyotumia tungeshapata angalau kupunguza hizi kilometa 129 mngepunguza angalau sasa tungekuwa tuna kilometa kadhaa baadaye mnaongezea hatimaye tunakamilisha hizi kilometa 129. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani kusikia baadaye Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha hoja yako lakini usije ukatupiga sound hapa kwa sababu unaweza ukasema. Tumeshapigwa sound muda mrefu sana kuhusu hii barabara. Tunatamani na wananchi wanatamani kusikia ni lini kwa uhakika barabara hii mtajenga kwa kiwango cha lami hata kwa kuanza kilometa chache kwanza. Fungueni kilometa chache tu baadaye halafu muendelee, hiyo ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Karatu – Mbulu. Kwa sisi upande wetu wa Karatu – Mbulu ni kilometa 51 tu mlishakuja mkasaini pale na mkatuletea wakandarasi mkafanya kasherehe kadogo mpaka leo. Ndiyo maana nasema mnatupiga sound, mpaka leo hakuna. Najua kwa upande ule wa Manyara imeshaanza lakini upande wetu pia bado; ni lini? Au tuendelee kusikiliza habari ya upembuzi yakinifu sijui mchakato sijui na nini? Siku hizi mmetuletea na hichi kitu kinaitwa EPC+F yani kila siku mnatupiga maneno maneno fulani hivi ambayo yanatupa matumaini lakini kule field hakuna kinachotokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara pia ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu inakutanisha Mkoa wa Manyara na Mkoa Arusha. Kumbuka Karatu ni kitovu cha utalii na barabara nyingine inayotoka Mang’ola watalii wanaenda kule kuangalia Wahadzabe ndipo walipo. Wahadzabe wanapatikana kule mtu anatoka all the way from Marekani wapi wapi anaenda kumtafuta Muhadzabe lakini akifika kwenye hiyo barabara ni balaa. Kwa hiyo mzingatie na hilo, mzingatie pale ni kitovu cha utalii tunataka hizi barabara zifunguliwe kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine. Hii barabara ya Makuyuni mpaka lango la Ngorongoro nataka nikwambie Mheshimiwa Waziri kwanza ukiacha kipande cha Makuyuni - Mto wa Mbu ambacho sasa hivi kinasumbua lakini kipande kingine chote kilichobaki ni miongoni mwa barabara the best ndani ya nchi hii. Ina miaka 20 ukipita pale haina hata tobo haina ukiacha hii ambayo inasumbua kati ya Makuyuni na Mto wa Mbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa imepewa muda wa matazamio miaka 15 imeshaisha sasa hivi ina miaka 20 ni barabara nzuri na barabara bora sana. Nataka nikuulize huyu mkandarasi aliyejenga hapa na hawa wakandarasi wanaojenga barabara za siku hizi hivi kwa utaalamu ni ule ule au kuna utaalamu uliobadilika ukaongezeka? Kwamba huu utaalamu wa siku hizi barabara haina hata miezi imeshaanza kuwa na matobo. Barabara ikishakuwa na mwaka inakuwa siyo barabara tena ni kichaka gharama yote iliyowekwa pale haipo. Nataka kuuliza Mheshimiwa Waziri, hivi kwa nini ule ujuzi uliyokuwa umetumika kwenye mfano wa hii barabara moja kwa nini usitumike kwenye barabara za leo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweka fedha nyingi, tunatumia fedha nyingi za Watanzania walipa kodi lakini barabara ni chakavu ni mbovu inatengenezwa kiujanja ujanja mno. Halafu mbaya zaidi barabara zikiwa wakati wa mvua sasa ndiyo eti mnaanza wakandarasi ndiyo wanaanza. Yaani kukiwa na mvua nyingi ndiyo tunaona ma-grader, ndiyo mnaanza kukwangua wakandarasi ndiyo wanaanza kufanya. Kwa nini msisubiri wakati ambao ni mzuri zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani ule wakati mbovu nyie ndiyo mnaanza kutengeneza. Kwa nini ule wakati mbovu barabara zisitazamwe kuangaliwa maji yanapitaje yanafanya nini halafu ikishakamilika mtengeneze wakati ambao siyo wa mvua ili itengenezeke katika ubora ule unaotakiwa then baadaye mkague wakati wa mvua? Je, kile ambacho kimetengenezwa ndicho ambacho kitakidhi mazingira yote wakati wa mvua na wakati wa kiangazi? Ni muhimu sana mkaangalie haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara ya Makuyuni – Ngorongoro kuna baadhi ya maeneo mmeweka drift kuna baadhi ya maeneo hakuna drift. Wataalamu wanasema wameifanya hivyo kwa sababu sisi tunapakana na hifadhi kwa maana kuna wanyama wanaotoka Ngorongoro wanaenda Manyara; ni sawa sawa lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo hiyo corridor haipo. Tunaomba mtuwekee drift.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya maeneo ndani ya mji kabisa hakuna hizo drift kwa sababu mvua zikiwa nyingi tope linatoka nje linapita kati kati ya barabara. Barabara ile ni ya watalii, magari yanakwama muda mrefu utalii nao unadorora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna baadhi ya maeneo hakuna ile mifereji mikubwa waliyoijenga. Sasa yale maeneo ambayo si corridor za wanyama tunaomba watujengee mitaro, mitaro iwepo ili maji yaweze kupita kwa sababu hii barabara iko chini sana, maji mengi yanasimama barabarani hali ambayo inaleta usumbufu kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, kuna wananchi wetu wa Manyara Kibaoni walipisha upanuzi wa uwanja wa ndege. Baadhi wamewalipa fidia na wengine hawajawalipa fidia. Wale waliowalipa fidia waliwaahidi watawalipa riba, lakini hawajawalipa riba mpaka leo na ukisoma miongozo yao inaelekeza kabisa kuwa kuna riba. Wananchi wale wanataka kujua, je, ni lini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. CECILIA D. PARESSO:…watalipwa fidia zao na riba zao ili waweze kuzipata wamesubiri kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)