Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kaliua
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi nimesimama katika Bunge hili Tukufu nikianza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Vilevile nimpongeze sana Waziri wetu kwa kazi nzuri aliyoifanya ya ujenzi mkubwa sana wa barabara katika nchi yetu. Mimi nisiwe mchoyo wa fadhila, naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Mtendaji Mkuu pamoja na Meneja wangu wa Mkoa wa Tabora. Viongozi hawa kwa kweli sisi watu wa Tabora wanaendelea kutuheshimisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza kwa kuwapongeza viongozi kwa sababu katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Mheshimiwa Dkt. Samia, pale Kaliua tulikuwa na kipande cha kutoka Kaziramba kwenda Chago, kilometa 36. Kipande kile, kwenda Kigoma, chote kimekamilika kwa kiwango cha lami na wametumia karibu shilingi bilioni 38 na ndiyo maana nasimama kifua mbele kuanza kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia shilingi 11,700,000,000 kwa ajili ya kujenga kilometa saba za lami kutoka katika Kijiji cha Ugansa kwenda kwenye mji mkubwa wa Usinge na ndiyo maana kwa mara nyingine ninasimama kwenye sekta ya barabara kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatu, Mji wa Kaliua pale katikati hatukuwa hata kipande cha lami, lakini kupitia TANROADS tayari wamekwishamaliza takribani kilometa tatu na sasa tunavyoongea mkandarasi yupo site na anaendelea kutokea Ushokola kwenda Relini. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Kaliua kusema tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, tunamshukuru sana Mtendaji Mkuu, tunamshukuru sana engineer wetu wa mkoa na tunamshukuru zaidi Mama Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi mema na wananchi wa Kaliua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, meneja wangu wa mkoa, wengi walikuwa wanaongea hapa, mimi nilifikiri wale ambao wamemaliza kufanya kazi kubwa kama hizi ndio wanaostahili hata promotion, ndio wanastahili hata makofi mengi sana. Mheshimiwa Waziri hajaja pale, lakini Naibu wake amekuja, kazi iliyofanyika kule sio kazi ya kawaida. Kwa hiyo, mimi nisimame na niendelee kusifu kazi nzuri inayoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo la mwisho kwa niaba ya wananchi wa Kaliua, hivi karibuni tulipata tangazo, sisi pale Kaliua barabara imepita nje ya Kaliua, lakini kabla ya ujenzi walitaka kupitisha katikati ya mji kwa ajili ya kubomoa zile nyumba za wananchi pale. Wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Dkt. Kikwete, wananchi wa Kaliua tuliomba kwamba barabara ipite mbali kule ili kuepusha athari hizi. Sasa TANROADS walikwishakamilisha kujenga na wanaendelea kujenga. Hivi karibuni tulipata tangazo kwamba zile nyumba ambazo ziko karibu na barabara zivunjwe ndani ya siku 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa hekima zake Mheshimiwa Waziri, mimi nilimpigia Mtendaji Mkuu wa TANROADS na nikampigia wa kwangu wa mkoa, kwa kweli wamefanya uamuzi sahihi wa kuona kwamba jambo lile kwa sasa halina afya wala hata kwa mwakani halina afya, kwa sababu tuliomba na tukakubaliwa. Niwaombe wananchi wa Kaliua pamoja na kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imekubali, niombe sasa tusiendelee kujenga nyumba mpya kwenye hifadhi ili kulinda vizuri barabara zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaombi kubwa sana moja, nilikwishazisoma Ilani tatu za Uchaguzi za Chama Cha Mapinduzi, zinaongelea barabara ya kutokea Mpanda, zinaongelea barabara ya Kaliua, zinaongelea barabara ya Ulyankulu, zinaongelea barabara ya Katavi na zinaongelea Kahama.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa wapi?
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa, Mheshimiwa Ngassa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ngassa, tafadhali.
TAARIFA
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naomba kumpa Taarifa Mheshimiwa mchangiaji kuhusu huyu Meneja wa Mkoa wa Tabora, Engineer Mlimaji, ni miongoni mwa mameneja ambao wanakwenda extra miles, tofauti hata na fedha anazopewa na Wizara. Ni meneja anayefanya vizuri. Kwenye Mkoa wetu kila Wilaya tumewekewa taa za barabarani na kwa Igunga tumepata kilometa nane, anafanya vizuri sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Ngassa. Mheshimiwa Aloyce Kwezi unaipokea Taarifa?
MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea Taarifa hiyo kutoka kwa Mbunge makini, Mheshimiwa Ngassa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie jambo moja kubwa, niombe pale Ukumbi Siganga na Zugi Mlole mkandarasi aliye site wambane vizuri ili aweze kukamilisha, kwa sababu kata mbili hazipitiki mpaka sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine ni taa za barabarani kutoka Kaliua kwenda Kasungu, Kamsekwa na Igagala. Jimbo hili ndilo jimbo kubwa katika Mkoa wa Tabora lenye idadi kubwa ya watu, kwa hiyo, niombe waliangalie kwa macho mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenye ile barabara wanayojenga kutoka Ushokola kuja Relini kipo kipande cha barabara yao kuna miji mingi sana ya watu, niombe kilometa moja ya lami kuelekea Zugi Mlole. Wakitupatia kilometa moja ya lami na hili ninajua ni dogo kwa Mheshimiwa Waziri, najua ni mchapakazi, halafu anafanana na mimi, kwa hiyo, ni jambo ambalo ni jepesi. Nimwombe sana kwa hekima zote, ninaomba atuongezee kilometa moja na itapendeza kama utatoa maelekezo hata jioni ya leo unamaliza, mimi hata sina shida na ninawashawishi Wabunge wenzangu sisi tumwombee ili apate hizo trilioni tatu ili nyongeza iende ikajenge Mpanda - Katavi, Mpanda – Kaliua kwenda Kahama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya naomba niunge mkono hoja, lakini niaba ya wananchi wa Kaliua nimalizie kwa kusema kwamba tunashukuru kwa kutokutubomolea nyumba zetu, ahsanteni sana. (Makofi)