Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa na afya njema na kuweza kuchangia siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napenda nimpongeze Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu katika hotuba yake ya kwanza alisema kuwa atahakikisha kwamba miradi yote inayoendelea/iliyoachwa na marehemu itatekelezeka. Kweli miradi iliyoachwa katika Mkoa wa Dar es Salaam imetekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Daraja la VETA lilikuwa halieleweki wala hatujui kwamba lingekwenda vipi, leo hii daraja lile liko katika asilimia kubwa ya kuisha. Daraja la Uhasibu, ujenzi wa barabara kutoka Bendera Tatu mpaka Gerezani, kile kipande kwa kweli kimekwisha, huwezi kudhani kwamba uko Tanzania, utafikiri uko kwenye nchi nyingine yoyote, kumbe tuko Tanzania tena katika Wilaya ya Temeke. Pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sasa napenda niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu mdogo wangu Aisha anafanya kazi nzuri na mtoto wangu Mheshimiwa Bashungwa pamoja na Naibu wake. Hawa kweli ni viongozi wakarimu, wanaosikiliza shida za wananchi wao na Inshallah Mwenyezi Mungu atawalipa mema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwapongeza sasa nije kwenye mchango wangu ambao utajikita katika hotuba ya bajeti ya Waziri ukurasa wa 10, 15 na 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na ukurasa wa 10 - ujenzi wa barabara; upanuzi wa Barabara ya Kimara – Kibaha na Daraja la Kibamba, Daraja la Kiluvya na Daraja la Mpiji, ujenzi wa Barabara ya Makongo – Goba, upanuzi wa Barabara ya Morocco, upanuzi wa Barabara ya Tungi – Kibada, upanuzi wa Daraja la Gerezani na barabara za maingiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niipongeze Serikali, miradi hii imetekelezeka kwa asilimia kubwa japokuwa kuna changamoto. Upanuzi wa Barabara ya Morocco, barabara ile mvua inaponyesha ghafla inakuwa bahari, hakupitiki, hakuendeki na msongamano unakuwa mkubwa. Pale wanatakiwa wakafanye tafiti ili kujua ni tatizo gani linalosababisha yale maji yajae kwa kiasi kile. Waangalie kwa upande mwingine namna ya wanavyoweza kufanya katika kulirekebisha hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio, lakini ziko changamoto. Niwapongeze sana kwa ile El Nino pamoja na kimbunga. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri wamefanya kazi kubwa sana. Hakukuwa na mawasiliano kati ya Mkoa wa Lindi na Mkoa wa Dar es Salaam, yalikuwa yamekata kabisa. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri na alionja taste ya wali ule wa Pwani ya Kilwa, aliona jinsi mama zake tunavyoandaa vyakula kule. Ninamshukuru sana kwa hilo, alijitoa kwa hali na mali. Kwa kweli Serikali ilifanya kazi kubwa, kulikuwa hakuna jinsi, hali ile ilikuwa ni mbaya. Yale mambo ni ya Mungu si ya binadamu, kulikuwa hakuna njia, ni lazima tufanye vile, lakini wananchi walifarijika kwa jinsi alivyolichukulia kwa upekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitaanza na changamoto, tuna changamoto kubwa kwa Barabara ya Kilwa ambapo ukifika maeneo ya Mbagala kuna msongamano wa kutisha, yaani ile barabara imezongwa, yaani kuanzia kipande cha Mbagala Rangi Tatu hakuna pa kupita. Kila siku tunaambiwa kuwa kuna upanuzi wa barabara ile au itajengwa kwa njia nne, lakini kuanzia Mbagala Rangi Tatu, Kokoto mpaka Kongowe muda umekuwa mrefu sana. Wananchi wamefanyiwa tathmini kwa muda mrefu hawajalipwa na hata huo ujenzi wenyewe bado, lakini ukiingia kwenye vitabu huu ni mwaka wa tatu sasa kutajwa Daraja la Mzinga na Barabara ya Kilwa. Mheshimiwa Waziri akifika hapa wakati anahitimisha naomba aje aniambie ni lini barabara ile itaanza kujengwa, ninataka commitment ya Serikali sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nieleze kuhusu Barabara ya Kibada – Mwasonga – Tundwi Songani. Hii barabara ni ya kiuchumi, Kigamboni tumeipa ni eneo la kiuchumi ambalo lina viwanda, lakini barabara hii imeguswa tu kidogo, imejengwa sijui kilometa moja tu na hakuna mwendelezo. Mvua hizi barabara ile ilikuwa haipitiki. Wenye viwanda kule Kimbiji wanaomba sana muwasaidie ili ile barabara ipitike, lakini na wananchi nao wanapata shida ya usafiri, wanapanda bodaboda na magari kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa pamoja na juhudi zao za kuandaa kutusaidia kwa muda, lakini tunaomba sasa barabara ile ya Kibada – Kisarawe II – Mwasonga – Pemba Mnazi, lakini na Tundwi Songani. Wananchi wa Tundwi Songani wanahisi wao kama wako kisiwani, wanahisi wao kama hawana watu wa kuwasemea. Sasa mimi leo naongea hapa kama mkazi wa Dar es Salaam na Mbunge wa Dar es Salaam, nataka anipe commitment leo hii, aniambie Barabara ya Kibada – Kisarawe II – Mwasonga – Tundwi Songani ni lini itaanza kujengwa na kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie barabara ya kutoka Kongowe mpaka Mji Mwema, barabara ile ni ya muda mrefu, imechakaa sana na imekuwa finyu. Niombe Serikali waangalie jinsi ya kuiongeza barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwneyekiti, pia barabara ya kutoka Mji Mwema – Somangira – Kimbiji – Pemba Mnazi, barabara ile isipokwisha vile viwanja vilivyokatwa kule Pemba Mnazi wananchi wa kule watazidi kukaa mji ule hautaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Waheshimiwa Wabunge ambao wana viwanja kule Pemba Mnazi wapo, lakini wanashindwa kufika. Wakiangalia wanaona kama wanapelekwa porini, lakini kumbe si porini, upori unakuja kwa sababu ya kukosa barabara yenye uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali iwaangalie wale wananchi, wananchi wale wako kisiwani sasa kwa sababu Barabara ya Kibada kwenda Kisarawe Two, kwenda Mwasonga mpaka Pemba Mnazi haipitiki na barabara ya Mji Mwema kupita Somangira kwenda Kimbiji haipitiki. Sasa watu hao wataishi vipi? Niiombe Serikali waziangalie barabara hizi kwa jicho la kipekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hizo yapo mafanikio, wote tumeona kuna mafanikio ya zile barabara za mwendokasi. Barabara ya mwendokasi kutoka Mbagala mpaka Gerezani imekamilika, lakini barabara ile imewekwa mawe na vigogo ili watu wasipite. Ikumbukwe kwamba kuna wagonjwa wanaoenda na ambulance, sasa tufike sehemu ukifika Rangi Tatu huku hakuendeki, huku hakuendeki, basi angalau yale magogo waliyoyaweka na yale mawe wapishe angalau ambulance ipite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaotoka Jimbo la Mkuranga wanatumia barabara ile kwenda Muhimbili, wanaotoka Mikoa ya Kusini wanatumia barabara ile kwenda Muhimbili kupeleka wagonjwa. Hivyo, barabara ile inapokuwa na changamoto kubwa inakuwa shida, hata wagonjwa wanaweza wakafa njiani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hizo, pia niombe barabara ya kutoka…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, hitimisha.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja na ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote. Waendelee hivyo na Mwenyezi Mungu atawabariki, ahsante sana. (Makofi)