Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Bupe Nelson Mwakang'ata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hoja iliyopo mbele yetu, hoja ya Wizara ya Ujenzi. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri wa Ujenzi, kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa na Naibu wake, kaka yangu Mheshimiwa Godfrey Kasekenya kwa kazi nzuri waliyoionesha katika kipindi kigumu cha maafa ambacho kimepita. Kwa kweli hakika upele umempata mkunaji. Mheshimiwa Rais hakukosea kuwaunganisha majembe haya. Mimi nawaombea Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki ili muendelee kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwapongeza Wizara ya ujenzi wote akiwemo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa Dada yangu Mgeni Mwanga. Ni mama shupavu ambaye katika kipindi cha shida kwa kweli ameonesha uwezo wake na umama. Amefanya kazi nuri katika Mkoa wetu wa Rukwa, kwa kweli alihakikisha barabara zinapitika, barabara zilikuwa zimeachana hasa katika Bonde la Rukwa. Lakini mama huyu amepambana akishirikiana na Mawaziri hawa akiwemo Bashungwa na Kasekenya, wamekuwa wakipishana, akitoka Waziri Bashungwa anakuja Naibu Waziri Kasekenya. Kwa kweli mmeafanya kazi nzuri hongereni sana, mmetukimbilia wakati wa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwapa pole wananchi wangu wanawake wa Mkoa wa Rukwa, wale wote waliopata maafa poleni sana Mwenyezi Mungu aendelee kuwalinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye suala la uwanja wa ndege, katika Mkoa wetu wa Rukwa tumepata bilioni 76 za uwanja wa ndege. Tumezipokea na uwanja unaendelea kujengwa na sasa imefikia 40%, tunaomba uwanja huu uishe haraka ili hizo 60% zilizobaki basi zifanye haraka ili wananchi wa Mkoa wa Rukwa waweze kufurahia matunda ya Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikua na Mradi wa barabara kupitia TACTIC, sasa kutokana na upanuzi wa uwanja wa ndege kuna kilometa 1.3. Sasa tunaomba mamlaka itupatie mbadala wa barabara ambayo wananchi watakwenda kuitumia ambayo itabadili ile kilometa 1.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuishukuru sana sana Serikali Sikivu ya Chama cha Mapinduzi, kipindi kilichopita nilisimama hapa kuomba kutolewa matuta ya barabara iliyotoka Songwe mpaka Sumbawanga. Nashukuru sana Serikali imesikia kilio cha wana Rukwa imeweza kuyatoa matuta yote, sasa hivi Mkoa wa Rukwa ni Mji mzuri, naomba sasa Serikali iweze kuweka mataa barabarani kutoka Songwe mpaka Sumbawanga ni giza, barabara ni nzuri lakini giza limetawala. Kwa hiyo Wizara iweze kuweka taa za mataa kama ilivyo barabara ya kutoka Katavi Mpaka Tabora, barabara inapendeza ina mataa na ni nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba, barabara ile inatunzwa vizuri na watendaji wa TANROADS akiwemo Engineer Selemani Bishanga ambaye ni Engineer wa Mkoa wa Songwe wakishirikiana na Engineer Mgeni Mwanga wanazitunza vizuri sana hizi barabara. Mimi naomba tuwapongeze, na Mheshimiwa Waziri ukipata wakati mwingine unawapongeza na unawatia moyo hawa watendaji, wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niingie kwenye suala la barabara za Mkoa wa Rukwa, barabara ya kutoka Mfinga – Muze – Ilemba – Kilyamatundu mpaka Mlowo, barabara hii kwanza kabisa niipongeze sana Serikali wakati wa maafa imetuletea bilioni sita za dharura. Hongera sana Serikali mnatukimbilia sana wakati wa shida, Mungu awabariki, fedha hizi zimeweza kusaidia barabara hii inajengwa lakini niombe, barabara hii ni ya kiuchumi, mazao mengi ya kimkakati yanatoka Bonde la Rukwa. Tunaomba sana barabara hii iweze kukamilika haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee suala la nyumba za TBA, hapa Dodoma kuna nyumba za TBA zimejengwa na nyingine zinaendelea kujengwa. Lakini nyumba za TBA zinakuwa zimechakaa sana, tunaomba Wizara iweze kuzikatabati na kujenga nyingine kwa ajili ya kuingiza kipato kwenye suala zima la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee suala la barabara za Dodoma. Hii Dodoma ni jiji ambalo linakwenda kuwa kubwa sana. tunaomba sasa muweze kuongeza Barabara, ukitoka hapo nje tu unakuta foleni kubwa na ndefu. Ninaomba Wizara iangalie suala la kuongeza barabara katika Jiji la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya ninaunga mkono hoja na Wabunge wenzangu hii trilioni 1.5 tuweze kuipitisha kwa kishindo. Ahsante sana.