Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya ujenzi. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Bashungwa namna ambavyo anafanya kazi kubwa na nzuri sana, anaitendea haki Wizara yake. Mheshimiwa Waziri Bashungwa endelea na moyo wako huo unaokutuma kufanya kazi za Watanzania. Sina mashaka na wewe unafanya kazi nzuri sana Mwenyezi Mungu aendelee kukusimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kaka yangu Kasekenya, unafanya kzi nzuri sana. Yaani wewe umekuwa unaifahamu Tanzania karibu yote. Maana hata maswali unayojibu hapa unajibu kwa uhakika kabisa na kujiamini. Pongezi nyingi sana kwako kaka yangu Kasekenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze Wizara yote kwa ujumla wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri wanayoifanya hawa viongozi wa Wizara hii ya Ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mkuu wa Mkoa wangu wa Mbeya kaka yangu Juma Zuberi Homera, yeye pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama anafanya kazi nzuri ndiyo maana Mkoa wetu kwa sasa uko shwari kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoani Mbeya tuna Meneja wa TANROADS Engineer Matari Masige, huyu engineer anafanya kazi nzuri sana pale Mkoani kwetu Mbeya. Yeye pamoja na watumishi wote wa TANROADS wa Mkoa wa Mbeya, mara tu wakisikia kwamba kingo ya barabara au kwenye Daraja imebanduka, imechomoka au gari imegonga, anaposikia yeye na timu yake wanakwenda haraka sana kurudishia kingo zile kwa ajili ya usalama wa Watanzania wanaopita na magari. Nakupongeza sana Mheshimiwa Masige, kazi yako na timu yako ni nzuri sana. endelea kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naamini Mtendaji Mkuu wa Taifa wa TANROADS anasimamia vizuri sana hawa Ma-engineer wa mikoa maana nimeona Wabunge wengi sana wanaposimama hapa wanawapongeza mameneja wao wa Mikoa wa TANROADS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, barabara ya kwetu Mkoani Mbeya tunaishukuru sana Serikali kwa kumleta Mkandarasi na kuanza kazi pale. Wananchi wa Mkoa wa Mbeya tuna imani na matumaini makubwa sana kwamba, barabara ile itakwenda kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa kweli mara baada ya kusainiwa barabara ile ambayo Mkandarasi alisaini 14 Februari, 2023 mkataba ule unaonesha barabara ile ikamilike 14 Aprili, 2025. Barabara ile nimeona hapa mmeeleza kwamba asilimia 14 imekamilika. Hofu na mashaka ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya ni kwamba, ile barabara hatuna uhakika kama itakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa yule mkandarasi fedha ambazo aliomba za awamu ya kwanza kiasi cha shilingi bilioni 13.6 alikabidhiwa kwa wakati. Awamu ya pili aliomba bilioni 6.8 hajapewa, awamu ya tatu aliomba bilioni 4.3 alipewa bilioni nne pekee, milioni 300 hajapewa, awamu ya nne ameomba fedha bilioni 2.8 hajapewa kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mashaka sana, sasa mkandarasi anahitaji fedha, hapewi kwa wakati ile barabara inakwenda kwa kusuasua na ile barabara ni ya muhimu sana. Watanzania kwa maana ya wananchi wanaoishi Mkoa wa Mbeya ni ya muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara Wilaya zote iwe Rungwe, Kyera, Mbalali, Mbeya Vijijini wote wanaitegemea barabara ile. Lakini mpaka sasa ile barabara inakwenda kwa kusuasua. Kama ni asilimia 14, sasa ni miezi 16 imepita na barabara ile haileti matumaini kwamba hiyo miezi kumi iliyobaki itakamilika? Kwa sababu kama ni asilimia 14 bado asilimia 86 ili barabara ile ikamilike. Je, ile barabara itakamilika lini?
Mheshimiwa Spika, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri, unapokuja hapa naomba sana, kwa sababu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kwamba barabara ile inatakiwa ikamilike na barabara ile kwa kuanzia kutoka Uyole mpaka Ifisi ilitakiwa itumike kwa kilometa 23. Lakini Mheshimiwa Rais kwa mapenzi yake mema akasema kwa kuanzia muanzie na kilometa 29, kama ni kilometa 29, mpaka sasa hivi hapaeleweki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachoelewa na Watanzania, atakachosema Mheshimiwa Rais hayo ni maagizo inatakiwa utekelezaji. Sasa ni kwa nini hampeleki fedha kwa wakati? Mpaka sasa hivi mkandarasi yule anadai shilingi bilioni 9.9 ambapo mngekuwa mmempa, barabara ingekuwa inakwenda kwa kasi, sasa inakwenda taratibu inasuasua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara ni ya muhimu sana, ukizingatia kule Mkoani Mbeya kiuchumi ukienda kwa maana ya Nyanda za Juu Kusini ile barabara pale Mkoa wa Mbeya ni kitovu cha wafanyabiashara kwa Nyanda za Juu Kusini lakini haitiliwi maanani hofu ya Wananchi wa Mkoa wa Mbeya. Wananchi wa Mkoa wa Mbeya wanataka kujua ile Barabara kwenye hii miezi kumi itakamilika? Katika fedha kwa sababu fedha za ujenzi ule ni shilingi bilioni 138 mpaka sasa hivi ni shilingi bilioni 17 tu zilizotolewa. Je, hiyo barabara itakamilika? Tuna mashaka makubwa sana sijajua mnafikiria kitu gani na tunalia kila siku juu ya ile barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile barabara ya kutoka Uyole kwenda Ifisi ni barabara muhimu sana iko tu moja hatuna service road pembeni ni pamoja hapohapo makontena yanapita hapo, petrol tank hapohapo, magari ya mizigo hapohapo, mabasi makubwa hapo, daladala hapo baiskeli, bajaji, bodaboda. Sasa kama kuna mgo njwa anatoka kwenye wilaya nyingine zile za Rungwe, Kyela, Mbarali au Mbeya Vijijini anapitapitaje sasa kwa sababu pamebanana ili wamuwahishe mgonjwa rufaa ukizingatia hospitali ya rufaa iko mbali kabisa kule, wanamfikishaje kwa haraka? Kusema apae haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana Serikali na Wizara ya Ujenzi naomba itazameni kwa makini sana ile barabara. Ile barabara yenyewe iko Mbeya Jiji, Jiji lenyewe ndio la Dkt. Tulia Ackson ambaye ndiye Spika wetu hapa. Dkt. Tulia Ackson kwa mapenzi mema Mheshimiwa Rais akampa ruhusa ya kwenda kugombea kuwa Rais wa Mabunge ya Dunia kule, amekuwa Rais wa Mabunge ya Dunia kwenye njia za watu kule akifika kule duniani tumeona anapita na ving’ora kwa usalama kabisa wanamtembeza yeye kwenye barabara yake anapita wapi? Wakimtembelea atapita wapi? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba sana sana Serikali tuna kilio kikubwa sana Mbeya …
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: ...ni kweli kabisa mawasiliano Mbeya ni shida maendeleo yamekwama unapokwenda mjini lazima utumie masaa mawili unavyorudi tena masaa mawili masaa manne yanapotea huko barabarani…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Suma.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: ...wakati tunajua kabisa wakati ni mali time is money. Tunaomba sana Mbeya jamani barabara ile tuna kilio kikubwa sana Mkoa wa Mbeya tunaomba mtupe heshima. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma tafadhali.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)