Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Jumapili nilikuwa na mkutano wa hadhara kwenye Kata Weruweru na wananchi wa Kata ya Weruweru wakanambia Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa alizofanya Mheshimiwa Rais, kila ukisimama hata kama ni kuuliza swali anza kwanza kumshukuru Rais. Kwa hiyo, nami natumia formula hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa miradi mingi aliyofanya ndani ya nchi yetu lakini kwa Jimbo la Hai ni miradi kedekede aliyotuletea ambayo kihistoria haijawahi kutokea, tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri najua una ‘zigo zito hili hapa’ na ni lazima liende kwa sababu ni la kwako. Kwa hiyo, ninakupongeza kwa kazi unazozifanya wewe na Naibu Waziri, Katibu Mkuu pia na Meneja wangu Ndugu Kyando wa Mkoa wa Kilimanjaro. Huyu Mama anafanya kazi nzuri sana, kama ni kumpandisha cheo mpandishe cheo na mshahara uongezeke lakini abaki palepale Kilimanjaro, anatusikiliza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri alitusaidia fedha tukajenga daraja lile la Msomali, lilikuwa linasumbua sana. Niseme kwamba naomba sana mfanye utafiti chanzo cha yale maji yanatokea wapi kwa sababu hata haya mafuriko yaliyokuja juzi yalivuka tena daraja. Kwa hiyo, maana yake kazi inapaswa kufanyika pale. Nakushukuru kwa fedha ulizotuletea, tunajenga daraja la Makoa na kazi inaendelea vizuri haijasimama na haijayumba. Ninakushukuru pia kwa ajili ya fedha ambazo umeshatuletea na mkandarasi amepatikana kwa ajili ya ujenzi wa daraja lile la Kikafu kwa maana ya barabara ya Kalari kwenda Uswaa.
Mheshimiwa Spika, ninachokiomba lile daraja la zamani lisivunjwe kwanza, yaani lisivunjwe kwa sababu hakuna diversion road isije ikawa kama vile la Makoa, lijengwe pembeni na hili liendelee kuwepo. Nakuomba maombi machache kabisa kwenye eneo langu, nakuomba ile barabara ya kwa Sadala – Kwale, kilomita 15 tu na nimeambiwa imeshawekwa feasibility study, iwekwe feasibility study na hii barabara ipatikane, kwa sababu ndiyo barabara inayokuletea chakula kule nyumbani kwako. Hii ndiyo inaleta chakula pale kwenye Soko la kwa Sadala. Ni sambamba na ile ya kwa Sadala kwenda Longoi, hii na yenyewe ni kilomita 17 tu lakini imepangiwa bajeti kwenye Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, ninakuomba pia hii barabara ya Machame kwenda Kyalia tusaidie taa, kuna taa mlifungua pale KIA, mngetupa zikawekwa kwenye hii barabara ili ifanane na barabara nyingine. Pamoja na pale Bomang’ombe, tumepata barabara zile TANROADS zote zina taa lakini barabara kuu haina taa.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nakuomba sana, tuna barabara ya Bomang’ombe – Chekimaji – TPC, TARURA wametuwekea kilomita tatu lakini hii ya barabara najua ni ya TARURA, ninyi TANROADS ni walaji wakubwa kwa sababu hii barabara ina hadhi ya Kimkoa, hii barabara lile daraja likiharibika ndilo inayotumika. Naomba angalieni namna ya kukaa na TANROADS muwaongezee nguvu ili hii barabara ijengwe kwa kiwango cha lami na ikamilike.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine hili Mheshimiwa Waziri unisikilize vizuri. Tuna madeni ya fidia tunawadai, barabara ya mashine tools kwenda Kyalia tangu mwaka 2007 wananchi walianza kuwekewa X kwa awamu mbalimbali, hawajalipwa na hawajaambiwa barabara endeleeni na matumizi. Tunaomba sentensi moja, pamoja na kesi zilizopita barabara tuendelee kutumia au mtatulipa fidia? Unapohitimisha nakuomba sana utoe sentensi kwenye barabara hii kwa sababu watu wamebaki hawaelewi kinachoendelea.
Mheshimiwa Spika, iko fidia nyingine ya daraja la Kikafu, mlifanya tathmini wananchi wanaendelea kukaa pale hawajui watalipwa lini. Nakuomba unapokuja kuhitimisha utuambie lini unalipa fidia kwani wananchi walishaacha kujenga, wameacha kuendeleza mashamba yao na wako stranded kwa sababu hawajapewa majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, tulipitisha kwenye RCC kikao cha mwisho ambacho kinakuja kwako kupandisha hadhi barabara. Zikiwa ni barabara zile za vijiji kwenda TARURA na zile nyingine zilizokuwa TARURA kwenda TANROADS, naomba utakapokuja kuhitimisha utupe majibu.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nikushauri kuwa mfuko wa barabara umeweza kukarabati barabara kwa asilimia 40.8 tu, lakini nilikuwa natazama mkakati uliouweka pale kwamba ni nini kifanyike ili kufanya mfuko huu uwe na nguvu. Mmesema mnaenda kubadilisha sheria, mimi sioni kama mkakati huu utatufikisha mahali, lakini nimejiuliza kwa nini tunatengeneza sana barabara? Matengenezo ya barabara yaliyofanyika ni kilomita 34,383.67 na zile barabara maalum, matengenezo maalum, mmefanya zaidi ya kilomita 3,600. Kwa nini tunafanya matengenezo mengi? Jibu ni rahisi, barabara zinajengwa below standard ndiyo maana kuna matengenezo mengi.
Mheshimiwa Spika, inawezekana Mheshimiwa Waziri kuna mahali unapigiwa kona hapa, kwamba hizi barabara ni miradi ya watu wanaipenda, kwa sababu pesa za matengenezo ni nyingi sana hizi. Nimesoma hotuba yako ukurasa wa 129, mngeweka mkakati ni kudhibiti, barabara zitengenezwe kwa kiwango kinachotakiwa ili zidumu muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, naona aibu sana nikikuta watu wa TANROADS wameweka vitoroli barabarani wanaziba shimo la barabara, hii ni aibu! Kwa nini tusitengeneze barabara zetu kwa ubora ili tupunguze gharama hii? Naomba kwenye hotuba yako ukaongeze neno linguine la kuhakikisha barabara zinajengwa kwa kiwango kinachostahili ili kupunguza gharama hizi za matengenezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nimeona kuna tatizo, nauliza TBA kwa nini tunawapa ruzuku ya Serikali wakati wanafanya kazi kama wakandarasi wengine? Basi kama TBA mnawapa ruzuku naomba na wakandarasi hawa watanzania ambao mnataka kuwainua, kwanza, mnawacheleweshea malipo yao, wajengeeni uwezo, wapeni ruzuku kwa kuwapa vifaa kwa bei nafuu ili wawe na uwezo wa kufanya hizi kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa wafanyabiashara wanaoitwa wakandarasi unaosema unaenda kuwainua na umewatengea pesa nyingi, wengi sasa hivi wana magonjwa, wengi wamekuwa frustrated, kwa nini? wanawadai hela nyingi, mimi nina mmoja nilikuwa naongea na KM wako hapa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge kengele ya pili imeshagongwa, ahsante sana.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)