Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi, lakini pia naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu. Ninaipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake wote akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi na wasaidizi wake wote, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, naomba kwenda moja kwa moja.
Mheshimiwa Spika, brabara ni uchumi. Mazao yote, bidhaa zote na mambo yote mengi ambayo yanakuza uchumi wa nchi hii yanategemea sana uwepo wa barabara, barabara ambazo ni nzuri na zilizoimarika. Ametoka kuongea hapa Mheshimiwa Hokororo, kwa kiasi kikubwa ameni-pre-empty.

Mheshimiwa Spika, ukianza na Barabara ya Kibiti – Lindi, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake, walijitoa sana, kwa sababu mawasiliano yalikatika ya kwenda Lindi na Mtwara. Tumemuona Mheshimiwa Bashungwa alikuwa anashinda kule, anakula kule, anatembea na wananchi wa kule. Hayo wakati yanatokea, najua ni madhara ambayo yametokea kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi kwa sababu ya uwepo wa kimbunga kile, hatuna jinsi, lakini yalipandisha kwa kiasi kikubwa sana maisha ya wananchi wetu wa Mikoa ya Lindi na Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutoka Dar es Salaam kwenda Newala bei ya kawaida ya basi ni shilingi 35,000, lakini watu walikuwa wanalazimika kuzunguka Newala – Songea – Dar es Salaam kwa nauli ya shilingi 120,000 kwenda tu. Kwa hiyo, utaona namna ambavyo mzigo ulikuwa mkubwa kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwa jitihada za Serikali, kwa dharura ambayo wameifanya sasa hivi barabara ile inapitika, lakini tuendelee kuomba Mungu kwa sababu kilichofanyika pale ni matengenezo ya dharura. Ikitokea leo kikaja kimbunga chenye jina lingine ile barabara inaondoka tena na mawasiliano yanakatika.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimeangalia kwenye bajeti, taarifa ya Mheshimiwa Waziri inasema kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa sehemu za kuanzia Kongowe – Malendego – Nakungurukuru – Mbwenkuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba hii iwe ni hatua ya dharura, kwa hiyo, lazima kuwe na short term plan na long term plan. Short term plan iwe ni hii ya kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati, lakini ile barabara haikarabatiki, ile barabara inatakiwa kujengwa upya kwa sababu sehemu zote zimeoza. Waliotangulia kusema wamesema, ina viraka kila sehemu. Kwa hiyo, ilikuwa ni kufanya tu ukarabati, lakini sasa tuijenge iwe imara. Tutakapokwenda kujenga tuwatafute wakandarasi ambao wana uwezo ili waijenge barabara ile kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kipande ambacho kimeharibika mno ni kutoka Somanga – Nangurukuru – Lindi, ndiko ambako madaraja yalitoka. Ile barabara ilijengwa kwa wakati mmoja kutoka huku Kongowe – Lindi. Kwa hiyo, ukiangalia kuna sehemu ambazo ziliimarika na sehemu nyingine ambazo hazikuimarika. Ninaomba tutafute wakandarasi wenye uwezo, watakaoijenga barabara kwa uimara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naenda sasa Barabara ya Mtama – Mkwiti – Newala, kilometa 74. Kwa mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 ilitengewa bajeti ya shilingi 145,000,000 kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Nimesikitika kidogo kuona kwamba barabara hii mpaka leo kwenye taarifa ya leo ya Mheshimiwa Waziri inasema kuwa wapo kwenye hatua ya taratibu za manunuzi na kumpata mhandisi mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tumebakiza siku tu kadhaa ili mwezi uishe, lakini ndiyo kwanza taratibu zinafanyika, yaani nimechoka kidogo. Ninaiomba Serikali, wananchi wa Newala wanategemea barabara hii ambayo ndiyo wanapita kwenda Mtama na Dar es Salaam kila siku kwa ajili ya kuchukua bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha maisha yao. Tulishawapa matumaini kuwa barabara inakwenda kufanyiwa upembuzi yakinifu ili iende kwa stage nyingine ya ujenzi kwa ajili ya lami, lakini leo ndipo taratibu zinaanza kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni taratibu inawezekana hata bajeti hii ikaisha ilhali taratibu hazijakamilika. Ninaiomba Serikali, ninaiomba sana, wananchi wa Kusini wamekaa muda mrefu na barabara mbovu. Leo tumeshaweka kwenye vitabu, basi tunaomba fedha zipatikane ili wananchi wale wanasuke na shida za kila siku za ubovu wa barabara ambazo wanakabiliana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kutoka Mtama kwenda Newala sasa hivi wanaopeleka mabasi kule hawapeleki mabasi mazuri. Ukiwa unafika Newala ukitokea Mtama leo hii ni lazima ukaoge ili kuondoa vumbi ndipo uendelee na mambo mengine. Tumekwishatoka huko, sasa hivi tuko karne ya 21. Ninaomba Serikali itufanyie hima ili tuondokane na hii kadhia ya kwenda kuoga halafu ndipo uendelee na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitoka maeneo mengine sasa hivi, mtu anaondoka, anafika anaendelea na shughuli zake, Newala hicho kitu hakipo. Kwa hiyo, ninaiomba sana Serikali, tumechelewa na tunakubali kwamba tumechelewa, lakini sasa muda umefika, tukomboeni na sisi ili tunapofika mjini, wasitushangae, maana unatoka pale, unafika mjini umekuwa mweupe wa vumbi kama unaenda kucheza ngoma, hapana. Naona huo muda umeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nasisitiza Barabara ya Mnivata – Newala – Masasi…

(Hapa kengele ililia muashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Spika, kengele imekwisha…

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi, ahsante sana nna naunga mkono hoja. (Makofi)