Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa nafasi hii. Awali ya yote na mimi namshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii ya kuweza kuchangia hoja ya Wizara ya Ujenzi.
Mheshimiwa Spika, pili namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoendelea kufanya hususani katika Wilaya na Jimbo la Kilolo. Mheshimiwa Waziri atakumbuka kuwa alikuja mwaka jana, akasaini mkataba wa ujenzi wa barabara kilometa 33 kutoka Ipogolo - Iringa Mjini – Kilolo. Furaha yetu Wana-Kilolo ni kwamba barabara ile sasa inajengwa tena inajengwa kwa kasi kubwa sana. Hii ni historia kwa Wana-Kilolo, na ndiyo maana Wana-Kilolo wanaona juhudi za Mheshimiwa Rais na pia wanaona juhudi za Wizara, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watumushi wote, pia juhudi za watumishi wa TANROADS Mkoa wa Iringa, tunashukuru sana barabara inajengwa na inaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alipokuwa amekuja Kilolo, nilimwomba na ninajua kwamba barabara kilometa 33 inaishia Kilolo, lakini barabara ile ni ya kutoka Ipogolo – Iringa Mjini – Idete. Nikamwomba kwamba kwenye hii barabara yapo maeneo korofi ambayo jumla yake ni kilometa sita. Kilometa sita ni zile ambazo kila msimu wa mvua unapoanza hayo maeneo ni lazima tupate disaster, yaani hayawezi kupitika.
Mheshimiwa Spika, mimi najua kwamba bajeti yetu hatuwezi kila mtu kuomba barabara ndefu. Unapokula lazima ujue na wenzako wapo. Mimi namwomba kilometa sita za maeneo korofi either iwekwe zege au iwekwe lami kwenye yale maeneo kwa sababu ndiyo maeneo yanayosababisha kukatika kwa mawasiliano kipindi cha mvua. Halafu hayo maeneo mengine yakishindiliwa vizuri na kokoto ndipo tunapoweza sasa kuendelea kujenga taratibu. Kwa sababu barabara yote kutoka Kilolo – Idete imekwishafanyiwa usanifu na kwa hiyo, inaweza ikajengwa wakati wowote. Kama fedha hakuna basi iwe kwa maeneo korofi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mlima Msonza, nilimwomba wakati ule, nikamwambia ni kilometa mbili, tumepewa meta 200. Sasa meta 200 kwa kilometa mbili kwa kweli bado lile eneo linabaki kuwa korofi. Hata kwenye banda pale niliwaambia wale watu wa TANROADS Mkoa, nikawaambia, tungeweza kupata kilometa mbili, tukaumaliza ule Mlima Msonza tunakuwa tumetatua tatizo, halafu tukapata kilometa nne kwenye Mlima unaoitwa Mizani. Mlima ule unaitwa mizani kwa sababu lazima washushe mzigo ndipo waanze kupanda kwa sababu ule mlima hauwezi ukapanda na mzigo mkubwa kutokana na ubovu wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukapata hizo kilometa nne tukaweka pale Mlima Mizani tunakuwa tumepunguza tatizo kwenye ile barabara na kwa hiyo, kipindi cha mvua, sitawasumbua sana. Hilo ndilo jambo bado halijafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo hii barabara inaishia pale Idete, ikitoka pale Idete inakwenda kilometa 18 inafika Mlimba. Hii ina daraja moja tu la Mto Mngeta na TARURA tumeshaichonga ile barabara. Kwa hiyo, kwanza haiwezi kubaki kule na tayari RCC tulikwishasema kwamba barabara ikiishia Idete na inaunganisha Mlimba, maana yake hiyo ni barabara inaunganisha mikoa. Kwa hiyo, kile kipande cha kilometa 18 inabidi kihamie TANROADS ili TANROADS waendelee na ile barabara kwa sababu imekwishachanwa na TARURA na ikishachanwa daraja la pale Mlimba linatakiwa lijengwe.
Mheshimiwa Spika, ninajua na Mheshimiwa Kunambi, Mbunge wa Mlimba anajua, ili yeye aweze kuunganisha pale kwa maana kwamba hiyo itakuwa ni alternative ya watu wanaotoka Iringa kwenda Morogoro kupitia Ifakara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo tunaomba liangaliwe kwa mtindo huo kwa sababu linaweza kusaidia sana kwenye ile kazi.
Mheshimiwa Spika, lingine tunashukuru sana kwa kazi inayoendelea pale Mlima Kitonga. Mheshimiwa Waziri hilo ni mojawapo ya vitu vinavyoashiria usikivu wenu na jinsi ambavyo mnaelewa kwa sababu kwa ujenzi wa Mlima Kitonga na upanuzi wa ile barabara maana yake ni kwamba uchumi wa nchi yetu utafunguka kwa sababu foleni za pale zilikuwa zinaathiri kwa kiwango kikubwa sana. Namna ambavyo barabara ile ilivyo ilikuwa wakifika pale chini ni lazima wasubiriane au kusababisha ajali mbalimbali kwenye eneo lile.
Mheshimiwa Spika, maombi yetu ni kwamba barabara ile iendelee kujengwa kwa kasi kubwa na fedha itolewe ili kwamba kusisimame, maana ni barabara ambayo kama itasimama hata kidogo tu, tayari wamekwishatindua na pale kunaweza kukasababisha kero zaidi. Kwa hiyo, tunaomba katika utoaji wa fedha, Mlima Kitonga pazingatiwe kwa sababu pakisimama kidogo panaweza pakaathiri nchi yetu kwa kiwango kikubwa sana ambacho kinaweza kusababisha changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni kwamba ninashukukuru kwamba barabara ya kutoka Ilula inayopita Mkalanga kwenda Kilolo, ambayo ndiyo barabara kubwa ya ndani ya Kilolo ya TANROADS, ile barabara kwa kweli matunzo yake ni mazuri kwa kiwango cha changarawe na ina maeneo machache ambayo ni korofi. Kama ilivyo kwenye barabara nyingine, mimi hofu yangu ni kwamba inapofika kipindi cha mvua na yale maeneo korofi tunayafahamu, lakini hatuchukui hatua ya kuyapiga kiwango cha zege kama ilivyo pale Mlima Kitonga au kwa lami kama tunaweza.
Mheshimiwa Spika, mara nyingi ndio usafirishaji wa mazao unakuwa mgumu. Barabara hii Mheshimiwa Waziri Mkuu bahati nzuri yeye mwenyewe yupo tangu wakati huo, alipita pale Ilula na aliahidi kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, basi sasa kwa kuwa aliahidi Mheshimiwa Waziri Mkuu ianze kidogo kidogo, hata kilometa tano/tano, hata tatu/tatu. Sisi tutawaonesha maeneo ambayo yanatakiwa kujengwa ili kuzuia kusitisha shughuli za maendeleo kwenye lile eneo kwa sababu ni ahadi ya viongozi na ninyi mnafahamu ahadi za viongozi zinatakiwa zitekelezwe.
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo maeneo ambayo kwa ninavyoona, kama watayafanyia kazi basi yanaweza yakasababisha mabadiliko ya kiuchumi kwenye yale maeneo.
Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba ile ahadi ya kilometa mbili, ambapo tumepata meta 200, kwa kweli meta 200 ni chache, Mheshimiwa Waziri aongeze tu, basi iwe kilometa moja kwa sababu sasa meta 200 ni padogo, ni viwanja viwili tu vya mpira, padogo tu. Kwa hiyo, nakuomba sana uwaagize wale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi najua akiwaagiza yeye mkoani pale, watajua wenyewe hiyo hela wanatafuta wapi, wakaweke angalau kilometa moja pale Mlima Kitonga ili angalau na mimi nikirudi, niwaambie Mheshimiwa Rais mnaona ametupenda, tumeongezewa hii kilometa moja, kwa sababu wananisikia naongea, basi wajue kuongea kwangu humu ndani huwa kunaleta maana kwa sababu sasa …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana…
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: …kama nitashindwa hata kupata kilometa moja, nitakuwa na sababu gani nisimame kuongea? Kwa hiyo, mimi naamini mimi kwamba hiyo angalau itanifanya niondoke nikiwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)