Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenitunuku uhai hadi leo nikapata fursa kuchangia hapa kwenye bajeti hii muhimu kwa Taifa letu. Pili, namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mara ya kwanza anakwenda kutengeneza historia ndani ya Mkoa wa Morogoro, ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, Jimbo la Mlimba.
Mheshimiwa Spika, ninampongeza Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri ni Waziri makini, msikivu, mchapakazi na mwenye kujituma kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, mimi huwa sisifii hovyo hovyo, ukiona ninasifia maana yake kuna kazi inafanyika, kwa kweli ni mtu rahimu, kama jina lake lilivyo Innocent. Vilevile Mheshimiwa Naibu Waziri wake, Katibu Mkuu pia na Mhandisi ndugu yangu Razack, Mhandisi wa TANROADS Mkoa wa Morogoro na msaidizi wake Patrick, wanafanya kazi nzuri kwa kweli.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi na shukurani, ninaomba kueleza kwa nini nina kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais. Kwa mara ya kwanza na jambo hili mtashangaa sana, Mkoa wa Morogoro ni mkoa mkongwe, siyo mkoa mpya, lakini mpaka leo ni mkoa ambao ulikuwa hauwezi, haujaunganishwa kwa kiwango cha lami na Mkoa wa Ruvuma, haujaunganishwa kwa kiwango cha lami na Mkoa wa Lindi, haujaunganishwa kwa kiwango cha lami na Mkoa wa Njombe hadi leo na Mkoa wa…, siyo Mkoa wa Songwe kwa maana mkoa mpya, Mkoa wa Morogoro ni mkoa ambao ni mkongwe, bado ulikuwa haujanganishwa na mikoa yote mitatu.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa nini ninasema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anakwenda kutengeneza historia, kwa mara ya kwanza nimeanza kujenga hoja hapa Bungeni na Mheshimiwa Spika utakuwa shahidi, nikizungumza kwa habari ya Barabara ya Morogoro – Njombe Border, nikieleza umuhimu wa barabara hii, nikasema barabara hii inakwenda kuunganisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na ni barabara muhimu sana na ni barabara ya kimkakati katika uchumi wa Taifa letu na sasa Mheshimiwa Rais amesikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hapa, kwa mujibu wa Ilani, Ilani ilisema barabara hii itajengwa kilometa 50, lakini Mheshimiwa Rais ameruhusu barabara hii ya Morogoro – Njombe Border mpaka pale Madeke yenye urefu wa kilometa 223, ameruhusu ianze kujengwa kwa kiwango cha lami kilometa 100. Kwa nini nisishukuru hapo? Yaani amepitiliza hata ahadi ya Ilani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninasema tu kwa dhati kwamba nitasikitika sana kama kuna Waheshimiwa Wabunge ambao hawataunga mkono bajeti hii na hasa wale ambao hawajabahatika kuwa na viwanja vya ndege na wale ambao hawana hata ndoto za kuwa na viwanja vya ndege, kwa sababu zaidi ya 90% ya Watanzania kama siyo 100%, wanategemea barabara. Kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote kwa kauli moja, tuunge mkono bajeti hii ili ipite kwa kishindo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama haitoshi, kilometa 100 tayari zina wakandarasi wawili, Lot 1 kutoka Ifakara – Mbingu eneo la Igima pale Miale kilometa 62.5 mkandarasi yuko site anasubiri tu apewe fedha anazodai kwenye malipo ya awali shilingi 9,000,000,000. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Fedha ananisikia hapa, ninaamini hawezi kuruhusu mdogo wake nikose kurudi tena hapa Bungeni kwa sababu ya barabara, atalipa tu hiyo advance payment mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kutoka Mbingu – Chita JKT kilometa 37 na nusu kukamilisha kilometa 100, lakini kutoka pale Kihansi kwenda Madeke, napakana na ndugu yangu Mheshimiwa Swalle pale Lupembe, tayari kuna Benki ya Maendeleo ya Afrika wanafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii, nayo nina matumaini makubwa kuwa itajengwa. Kwa hiyo, nasema tu kwa dhati kwamba nina kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine nieleze hapa kuhusu bajeti. Bajeti hii tunayokwenda kupitisha hapa ni 1.7 billion, lakini nikawa najiuliza maswali, deni peke yake, watu wanasema ni shilingi 929,000,000,000, hili deni ni madeni ya nje, deni la ndani ni shilingi 257,000,000,000, uki-plus unapata one trillion point something, lakini bajeti ni shilingi bilioni 1.7. Maana yake ni kwamba kama Mheshimiwa Waziri atatumia fedha hizi akalipe madeni, hatuna bajeti ya mwaka huu wa fedha na hivyo hakuna kinachokwenda kufanyika, hamna hela inayobaki.

Mheshimiwa Spika, sasa rai yangu na ombi langu Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo hapa ni muhimu sasa ikae na Kamati yako tukufu ya bajeti wafanye mapitio au Waziri wa Fedha atusaidie kutafuta fedha zingine nje ya bajeti hii tulipe madeni. Tukilipa madeni kwa fedha zingine nje ya bajeti ninahakika Mheshimiwa Waziri atafanya kazi nzuri sana ya kutukuka na barabara zetu zitapitika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nimeona jana la anakusurubu he is very innocent kwa sababu katika hali ya kawaida wewe angalie bajeti ya five point seven billion, anaenda kufanya nini? Deni trillion moja plus, sasa rai yangu Bunge lako Tukufu na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Kamati yako Tukufu ya Bajeti iende ikafanye mapitio au kama kuna njia yeyote ile ya kupata fedha za kulipa deni hili ambalo TANROADS wanadaiwa ili kunusuru hizi fedha zikafanye kazi inayokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine nieleze kuhusu maombi, wananchi wa Mrimba wanaomba vitu vidogo sana kama ifuatavyo; kitu cha kwanza wananchi wa Mrimba wanasema kwa kuwa tulichelewa sana mikoa mingine wanahangaika na kuunganisha wilaya, sisi Mrimba tunahangaika na kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Njombe, Serikali itupe kipaumbele hasa kwenye malipo ya Wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, maombi yao kupitia Wizara ya Fedha Mkandarasi huyu ambaye anadai bilioni tisa malipo ya awali alipwe mara moja kwani amekaa site huu mwezi wa tano hajaanza kazi anasubiri fedha hizo na hii hasara yake ni nini? Mwisho wa siku atakuja kudai riba na taarifa zinaonyesha kila mwaka madeni yanayotokana na riba ni bilioni 73. Sasa niombe Mkandarasi huyu alipwe mapema ili aanze kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi la pili kwa wananchi wa Mrimba wanasema Waziri wa Ujenzi ni muhimu Mkandarasi huyo aliyesaini Mkataba Lot two hii ya awamu ya pili kilomita 37 na nusu akabidhiwe site. Kwa sababu kwa mujibu wa sheria mara tu Mkandarasi atakaposaini mkataba yeye anahesabu yuko site. Kwa hiyo, ukimwacha mtaani miezi sita hajakabidhiwa eneo la kazi maana yake anahesabu yupo site. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kaka yangu kama ulivyo na una uungwana wako tukimaliza bajeti hii ya kwako ebu twende pale tukakabidhi site aendelee na majukumu yake.

Mheshimiwa Spika, ombi lingine la mwisho…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa, kengele imeshagonga…

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, wanaomba kuunganisha Barabara ya Morogoro na Iringa kupitia Kihansi mpaka hapa kwa ndugu yangu Chumi – Mafinga. With all I due respective Mungu akubariki sana. (Makofi)