Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia na mimi hii Bajeti ya Wizara ya Ujenzi. Kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa afya njema, kuendelea kuwasemea wananchi wangu wa Jimbo la Rorya Mkoa wa Mara lakini pili niseme neno moja kwamba leo nasimama hapa kuchangia juu ya Barabara ya Mika – Utege – Shirati – Kirongwe ni kwa mara ya nne. Lakini tumekwisha uliza maswali, mimi binafsi toka nimeingia Bungeni nimeuliza maswali ya nyongeza kama mara nane kwa namna tofauti tofauti lakini nje ya hapo nimeuliza maswali ya msingi kuhusiana na barabara hii kama mara nne, barabara ya Mika – Utegi – Shirati – Kirongwe.
Mheshimiwa Spika, barabara hii imekuwa ikitajwa kwenye Ilani toka mwaka 1995 kwenda mwaka 2000 ikatajwa 2000 kwenda 2010 Mheshimiwa Rais wakati huo akiwa Jakaya Mrisho Kikwete, lakini pia ikatajwa baada ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa maana ya 2015 kwenda 2020.

Mheshimiwa Spika, kipekee kwa niaba ya Wananchi wa Rorya nimesimama hapa kutoa shukurani zangu za dhati kabisa kutoka moyoni kwa kazi kubwa nzuri aliyotufanyia Mheshimiwa Rais. Tazama barabara hii imetajwa kwa zaidi ya miaka 20 na kuendelea lakini mimi Mbunge nimesimama ukiacha siku ya leo ni zaidi ya mara kumi tano naizungumzia barabara hii. Rais huyu huyu Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kuwiwa na kuona umuhimu wa barabara hii, akaridhia barabara hii ya Mika – Shirati – Kirongwe kilometa 56 na leo kilometa 27 zinakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami na akaridhia kuiweka kwenye bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimesimama hapa kutoa shukurani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais kwa kuona utashi huo wa kisiasa na kuona namna ya kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Rorya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sembuse tofauti na Mheshimiwa Rais, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri pongezi unazoziona kwa Waheshimiwa Wabunge hapa ni kwa sababu unajua namna ya kuishi na wao, unajua namna ya kuzungumza nao, unajua lugha ya kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge hata kama hauna fedha. Lakini bado umekuwa miongoni mwetu kuzungumza na kututia moyo kiukweli ndiyo maana unaona pongezi nyingi tunakupa pamoja na kwamba tunajua hauna fedha siyo makosa yako. Lakini kwa namna unavyojishusha na kuzungumza na Wabunge, kwa namna unavyoshughulika na changamoto Mwenyezi Mungu aendelee kukutia moyo sisi tunakuombea sana uendelee kufanya kazi nzuri na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa kukuweka kwenye Wizara hii. Sisi, kama Wabunge vijana tunajivunia sana kuona kijana mwenzetu ukifanya kazi kubwa nzuri na tutakuwa nyuma yako wakati wote, wakati wote utakapohitaji tutakusemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nichukue nafasi hii kumpongeza sana Naibu Waziri kwa namna ambavyo alikuwa akisimama hapo mbele anajibu maswali ya Wabunge. Barabara zote unazoona zinazungumzwa humu Naibu Waziri amekuwa akizungumza kwa kutitia moyo, hata pale anapoona kwamba barabara hii imeulizwa hakuna fedha lakini amekuwa akitufariji, faraja zile za Mheshimiwa Naibu Waziri lazima tuendelee kumshukuru sana na yeye tumtie moyo kwa namna ambavyo ameendelea kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu wa tatu nimshukuru sana Katibu Mkuu wa Wizara hii Balozi Aisha Amour kwa namna ambavyo na sisi Wabunge tunavyokimbia kwenda Wizarani anatupokea, anatufariji na kutupa matumaini ambayo kimsingi tunaamini haya yote si makosa yao, kama Wabunge wenzangu walivyosema tatizo ni fedha. Kwa hiyo, hawa wenzetu wanatufariji kwa namna ambavyo nje ya uwezo wao kwa sababu hakuna namna ambavyo wanaweza wakafanya zaidi ya hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini mwisho nichukue nafasi hii ya kipekee kabisa kumpongeza sana Meneja wetu wa Mkoa wa TANROADS, Meneja wetu Mkoa wa Mara, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, ndugu yangu Vedastus Maribe. Huyu ni mtu ambaye kila muda ukimpigia simu sisi Wabunge wa Majimbo ya Mkoa wa Mara kila muda ukimpigia simu anapatikana, kila ukimpa changamoto anapatikana.

Mheshimiwa Spika, leo tunavyozungumza hakuna barabara ambayo inahitaji maintenance kwa Wilaya ya Rorya ambayo haipitiki. Barabara inaweza isipitike upande wa TARURA lakini TANROADS Meneja huyu amekuwa akifanya kazi zake kwa ufanisi sana, tumpe maua yake na nikuombe Mheshimiwa Waziri usije ukatuhamishia Meneja huyu sisi tunamuhitaji sana kwa sababu kiukweli anatufaa sana sisi Wabunge.

Mheshimiwa Spika, baada ya mchango huu nilitaka niseme jambo moja na hili Waziri wa Fedha atusikilize vizuri sana. Siasa ya Mkoa wa Mara ni barabara pamoja na maji, ukituuliza vipaumbele sisi Wabunge tutakwambia moja ni barabara mbili ni maji lakini Sekta ya Maji tuiche kwa sababu leo tunazungumzia barabara. Barabara ndiyo inabeba siasa yetu ya Mkoa wa Mara, kipaumbele kikubwa cha siasa Mkoa wa Mara ni barabara.

Mheshimiwa Spika, lakini utaona hapa kwenye bajeti yetu hii, barabara karibia wilaya zote sita zimesimama. Ukimsikiliza Mbunge wa Tarime Vijijini anakwambia barabara aliyopewa fedha ya kwenda Mogabiri kwenda Nyamongo ambayo ni kilomita 25 Mkandarasi yuko site imesimama kwa nini? Hakuna fedha, Mkandarasi hajalipwa. Ukiuliza barabara inayotokea Nyamongo kwenda Mugumu kwa maana ya Serengeti imesimama kwa nini? Mkandarasi anadai zaidi ya bilioni ngapi? Hajalipwa imesimama na haifanyiwi kazi, ukiuliza Musoma Vijijini hivyo hivyo, ukiuliza Bunda umesikia Mbunge wa Ukerewe hapa amezungumza barabara inayomuunganisha Bunda na Ukerewe imesimama kwa nini? Wakandarasi hawana fedha.

Mheshimiwa Spika, mimi niseme haya yote hatupaswi kumrudishia Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, tumuombe Waziri wa Fedha alione hili barabara zote zinazotuunganisha ndani ya Mkoa, barabara ya TANROADS ndiyo barabara zenyewe za msingi za TANROADS hakuna barabara zingine. Kitendo cha barabara hizi kusimama kwa muda mrefu bila Wakandarasi kuonekana site maana yake unatusimamishia Mkoa, tunashindwa jambo la kusema, kwa nini? Wakandarasi hawajalipwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha mlione hili mtakapokuwa mmekaa. Tumuongezee fedha Waziri wa Ujenzi ili alipe Wakandarasi hawa warudi site wakatengeneze barabara hii. Dhamira na madhumuni ya Mheshimiwa Rais ni mazuri sana kwa hiyo, nyinyi mkae tuone namna ambavyo tunaweza tukafanya kutatua changamoto ya hizi barabara.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine nichukue nafasi kumshukuru sana, sana sana Waziri pamoja na Mheshimiwa Rais. Barabara ya Kuruya ya kwenda Kinesi upembuzi yakinifu nimekuwa nikizungumza hapa ndani lini utafanyika? Nimeona mtenge fedha upembuzi yakinifu unakwenda kufanyika na naamini mwakani itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa kuliko yote nimeambiwa mmetupa zaidi ya milioni 600 kwa ajili ya kujengwa box karavati kwenye Mto Tobwe ambayo inatuunganisha kwa maana kwamba kutoka Masonga kwenda Sirari. Pale ule Mto mvua ilikuwa ikinyesha Mheshimiwa Waziri, hakuna mwananchi alikuwa anavuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine, leo Meneja ananiambia mmetupa milioni 600 kutoka kwenye fedha za dharula na ujenzi umeanza, nikushukuru sana kwa kazi kubwa nzuri unayofanya.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho ni ujenzi wa maegesho. Nimuombe sana mtu wa TEMESA, Mheshimiwa Waziri nimeona mmejenga maegesho pale upande wa pili wa kivuko huko Musoma Mjini. Lakini mtambue wale wannchi wanatoka Rorya – Kinesi wanavuka kuja Musoma Mjini ni sawa ujenge egesho Kigamboni halafu uache kujenga upande wa pili huku wa Mjini, unajenga sehemu ya wananchi kumpuzikia kivuli upande wa Kigamboni halafu upande wa Mjini hujengi haina maana. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri uone hili kwa kuwa tumejenga upande wa Musoma – Kinesi kule pia uwajengee egesho kwa ajili ya kivuli pamoja na wakati wa mvua. Kwa sababu haiwezekani ukaenda upande mmoja mtu anafika anaumia kwamba kuna mvua ananyeshewa, akienda upande wa pili anapata uwafadhali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe hili watu wa TEMESA na ninaomba Mheshimiwa Waziri ulichukue hili uone namna ya kuwasaidia wananchi wetu wa Rorya.

Mheshimiwa Spika, kwa leo sikuwa na mengi sana, niliona ni muhimu tum-support sana Mheshimiwa Waziri na tumuombee Mheshimiwa Waziri wa Fedha amuongeze fedha ili haya yote tunayoyasema yaweze kufanyika, tunashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)