Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi kunipatia fursa ya kuchangia bajeti hii ya ndugu yangu Bashungwa, Mheshimiwa Bashungwa. Nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya kuliongoza Taifa letu, uongozi mzima wa Serikali yetu Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na viongozi wote wakuu wa Taifa hili. Pia niwapongeze Wizara kwa kweli wanafanya kazi kubwa chini ya uongozi wa Waziri ndugu yetu Mheshimiwa Bashungwa, Naibu wake Watendaji Wakuu wote wa Wizara kwa kweli mnastahili pongezi na pongezi za kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajikita kwenye Jimbo la Muleba, pamoja na kazi kubwa inayofanyika kitaifa tunaiona na tunaipongeza Serikali, madaraja makubwa yanajengwa na miradi mikubwa mikubwa inaendelea kujengwa chini ya usimamizi wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nawapongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake wamefika Muleba, wamekagua kazi zinazoendelea ambazo zinasimamiwa na kupewa pesa na Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Muleba tuna barabara yetu ya Muhutwe – Kamachumu – Buganguzi – Inshamba kwenda Muleba. Mheshimiwa Waziri unaifahamu sana wote wawili mnaitembelea hiyo barabara kazi inaendelea, kimebaki kipande cha kilometa 9.7. Mheshimiwa Waziri nimeangalia kwenye bajeti sijaona popote ambako mmeweka kuikamilisha, najua kuna kazi inaendelea ya kilomita moja tunawashukuru wanasema asiyeshukuru kwa dogo hata kubwa hatapata, nakushukuru kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ningeomba sasa Mheshimiwa Waziri hii barabara imekuwa ikijengwa kwa kilomita tatu, mbili na wewe mwenyewe ulipokuja kuitembelea ulisema ni kipindi kirefu imejengwa na kilometa 54, nakuomba sasa iwe ni mwisho kabla hatujamaliza kipindi hiki bajeti hii Mheshimiwa Waziri angalia tunaweza tukaja angalau tuweze kumaliza hii barabara.

Mheshimiwa Spika, lakini tuna madaraja makubwa mawili tumejenga hii barabara Muhutwe – Kamachumu – Nshamba hadi Muleba lakini tumeacha madaraja mawili, tuna daraja la Kamishango na daraja Kyabakoba. Ningeomba Serikali kupitia bajeti hii mmekuwa mkifanya upembuzi yakinifu na usanifu, sasa nimepata taarifa kwamba mmeishamaliza, niombe haya madaraja ambayo yamebaki kati kati najua yana gharama kubwa tukayajenga. Lakini naombi moja, wakati tunajenga hii barabara hatukuwa na njia ya kuendelea na shughuli za kibiashara katika hiyo Barabara, naomba wakati wa tunajenga tutafute njia rahisi ambayo itawarahisishia wananchi wa maeneo hayo waweze kuendelea na shughuli zao wakati ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Spika, ningependekeza kwamba haya madaraja tujenge kama tulivyojenga daraja la Ruvu, lile liliopo tuliache tujenge daraja jingine pembeni ili shughuli za kibinadamu na shughuli za kibiashara ziendelee. Mheshimiwa Waziri unafahamu Wilaya ya Muleba lile daraja linakwenda Nshamba na ukiacha Nshamba ndiyo sehemu ya uchumi na wafanyabiashara wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna barabara nyingine ambazo zinatusaidia unavyojua Mkoa wa Kagera ni Mkoa wa uzalishaji kahawa na hizi barabara zinatusaidia kuhakikisha kuwa zinatoa kahawa kwenye mashamba na kulileta kwenye masoko na kuleta wilayani. Tuna barabara ya Rutenge – Izimbya hadi Kishojo nadhani Mheshimiwa Waziri unaifahamu kwa sababu na hii barabara ndiyo inakuja kuinga hata Karagwe na hii barabara tunakuomba Mheshimiwa Waziri iangalieni tukaijenge itarahisisha mawasiliano lakini pia itakuza uchumi wa hilo eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna barabara nyingine Mheshimiwa Waziri anaifahamu ya Kasindaga – Kyebitembe – Karambi – Kimeya hadi Lunazi ni barabara kongwe ya TANROADS. Lakini tumeisahau Mheshimiwa Waziri, angalau tuitengee tuanze kuijenga kwa kilomita moja, kilomita mbili ili baada ya muda na yenyewe iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna barabara nyingine ya Rutenge kwenda Mushabago ni barabara ya TANROADS hii lakini mara nyingi tu huwaga tunaisahau, tuwe tunaitengea fungu la kuitengeneza ili shughuli za kiuchumi na za kibinadamu ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, la mwisho Mkoa wa Kagera bado uko kwenye giza Mheshimiwa Waziri. Tukitoka kwenda Mikoa mingine nje ya Kagera tunaona taa nyingi lakini Kagera bado tuko kwenye giza. Nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yako Miji yote ambayo kwenye Mkoa wetu hasa kwenye Jimbo langu la Muleba Kusini, Muleba pale kwa kweli mlituwekea taa kidogo, Lakini nikiangalia kwenye commitment yenu mna kilometa 1.1 naomba sasa kwenye bajeti hii Muleba ikawekwe taa lakini na Miji yote ambayo inaibukia hii barabara yote kutoka Kasindaga mpaka Bukoba kuna center nyingi sana kubwa lakini tusisahau na Kamachumu pale. Tunaomba Mheshimiwa Waziri tuweke taa za barabarani tutoke kwenye giza sasa Muleba na Kagera iwake imeremete ili ivutie Watalii na ivutie wakazi wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na nipende kuomba kwamba tuongeze bajeti ya Wizara, bajeti tuliyonayo ni ndogo, ninaunga hoja mkono. (Makofi)