Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuniona na mimi kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitoe shukrani kwa Serikali kwa nia ile ya kutujengea barabara ya kutoka Kitai – Amani Makolo – Rwanda – Litui. Kwa nini nasema kwa nia? Barabara hii tayari kilometa 35 mkandarasi yupo site na kwa maelezo ya kwenye hotuba tayari kilometa 54 za kuanza Rwanda – Litui tayari mkataba umesainiwa, lakini kwa bahati mbaya hizi kilometa 35 tulikuwa tunatarajia barabara ikamilike tarehe 18 ya Mwezi wa Kumi na Mbili, mwaka jana. Hadi leo hata siyo kilometa, hata kipande kidogo tu cha lami hakuna.
Mheshimiwa Spika, nazungumza hapa kwa masikitiko makubwa. Tulienda na Mheshimiwa Waziri, aliona utendaji katika barabara hii na alitoa maelekezo pale kadhaa lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri hadi leo hamna kinachoendelea katika ile barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara hii ipo busy kweli kweli. Barabara hii ndiyo inayopitisha makaa ya mawe kutoka Rwanda Mgodini, pia kutoka pale Amani Makolo ambapo pana dry port. Kwa hiyo, magari kwa siku ni zaidi ya 1,000 yanapita hii barabara. Ni huzuni sana wananchi wanaokaa Amani Makolo, Paradiso na Rwanda kuanzia huu Mwezi wa Tano, Sita, Saba mpaka wa Kumi na Moja kabla ya mvua kunyesha, huwezi kuzitambua nyumba zao. Huwezi kutambua nyuso zao wanavyotembea. Ni watu waliooga vumbi, nyumba zilivyooga vumbi, kwa hiyo, ni hatari kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunazungumza mara kadhaa na wananchi hawa kuwatia moyo kwamba, hii barabara inaenda kukamilika na sasa wataondokana na adha hii ya vumbi. Mwezi wa Kumi na Mbili ilikuwa ndiyo mwisho angalau wananchi hawa wafurahie, lakini mpaka leo hakuna hata doti moja ya lami kwenye hizi kilometa 35. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa sisi tumekubaliana hatutakubali kula vumbi tena mwaka huu, hatutakubali kwa sababu tumekula vumbi kwa miaka yote makaa ya mawe yanachotwa pale. Hatuwezi kuendelea kula vumbi hizo. Tutasimamisha mgodi mpaka tupate barabara ya lami pale Amani Makolo mpaka Rwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu wakati fulani wale wananchi walikuwa wanalaumu kwamba, Mbunge hasemi. Nimempeleka Waziri wakagundua tatizo siyo la Mbunge, tatizo lipo kwa mkandarasi. Waziri akatoa maelekezo pale sasa wanauliza mbona maelekeo yale ya Waziri hakuna linalotekelezwa hata moja? Kwa sababu Waziri alisema tunafukuza mkandarasi na mhandisi mshauri, bado wapo wanafanya kazi. Kwa nini waendelee kufanya kazi? Kazi yenyewe hawafanyi wame-park tu magari pale hamna kazi inayoendelea. Kwa hiyo tumekubaliana safari hii hakuna makaa ya mawe kutoka pale kama hatuoni barabara ya lami pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ninalotaka kulizungumzia ni eneo la barabara hizi ambazo zipo siyo za lami ni za changarawe. Zipo barabara kipindi hiki cha mvua zimetutatiza sana. Barabara ya kutoka Peramiho kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama kuja Litumbandyosi hadi Paradiso kuna maeneo ya Mlima Sanga pamoja na maeneo yenye mito, yalifunga barabara ile kwa muda wa miezi miwili. Wananchi walikuwa wanatembea zaidi ya kilomEta 100 kufuata huduma kwa mguu. Kwa hiyo, niombe kwamba kwenye maeneo yenye mito kama hayo nimeona baadhi ya maeneo mmeanza utaratibu wa kuweka reli. Basi niombe na barabara hii ya kutoka Paradiso – Kingole – Peramiho tuwekewe reli angalau hawa wananchi watumie barabara hii kwa mwaka mzima.
Mheshimiwa Spika, pia vivyo hivyo niongelee suala la Ahadi za Viongozi. Sisi tuna ahadi pale, Mheshimiwa Rais alifika Mwaka 2020. Barabara ya kutoka Kigonsera kwenda hadi Matiri, pia barabara ya kutoka Mbinga kwenda hadi Litembo. Nimeuliza maswali hapa nashukuru kwamba, Serikali imeahidi kwamba sasa hivi ilikuwa na nia ya kufungua njia hii lakini imeshafunguliwa ambako wanaongelea kufunguliwa ni kutoka Matiri kuelekea Mbaha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa niombe hii ahadi ni ya Rais na wananchi wale kila siku wanakumbusha. Pia kwa kutoka Mbinga kwenda Litembo mwaka jana mliahidi uthamini unafanyika. Tufanye ule uthamini ile barabara, hata tukakosa hii ambayo Mheshimiwa Rais aliahidi kutokea Ndengu kwenda Mbuji hadi Litembo itakuwa suluhisho au itakuwa majibu ya barabara hii ambayo Rais aliahidi, ni kilometa 22 tu. Niombe sana kwa sababu pale pia kuna ombi la Mhashamu Askofu John Ndimbo la kumwomba Makamu wa Rais wakati anaenda kufungua Chuo cha Afya kule kwamba ile barabara itekelezwe. Kule Litembo ndipo kuna hospitali ambako wananchi wa Jimbo la Mbinga Vijijini wanatumia kutibiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwsiho nililotaka kushauri ni namna tunavyoweka matuta barabarani. Zipo barabara unapita kwa uzuri sana kwamba, unaweza ukawa hata kwenye speed ya 50 unapanda lile tuta vizuri, unashuka, lakini zipo barabara hata ukiwa kwenye speed ya sifuri (gari linaseleleka tu hivi) ukifika kule chini lazima gari lilie boom! Mkito mkubwa. Sasa, ombi langu Mheshimiwa Waziri hivi hatuwezi kuwa na viwango vya usawa. Ukipita barabara ya kutoka Makambako kuja Iringa hapa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
MHE. BENAYA L. KAPINGA: … matuta yake ni mazuri sana. Hivi hatuwezi kuwa na matuta ya namna ile nchi nzima? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)