Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii ya kupata nafasi ya kuongea Bungeni leo. Pia namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa nafasi ambayo ameruhusu Bunge liendelee kuwepo, ili tutoe michango yetu kwa kadiri Mungu anavyopenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Innocent Bashungwa kwa nia njema anayoionesha kwa sababu naona miradi mingi imeendelea kusainiwa na kutekelezwa japokuwa kuna changamoto kadhaa ambazo zinaendelea kusemwa ndani ya Bunge hili. Pia nimpongeze Mheshimiwa Mhandisi Godfrey Kasekenya kwa kumsaidia Waziri kwa kiwango kikubwa hadi hapa tulipofikia sasa. Nampongeza sana Katibu Mkuu Balozi Aisha, kwa uratibu mzuri wa kazi ambazo tunaona zinaendelea na wataalamu wote katika Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, taarifa hii inaonesha wazi kwamba tangu ameingia madarakani tulikuwa na kilometa za lami 10,830.2 na sasa tuna 12,024.7 maana yake kuna ongezeko la 1,198.5. Kwa hiyo, kama kuna ongezeko maana yake kuna kazi kubwa inafanyika na kwenye awamu hii kazi hii imeshaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii inayoonekana kwenye maeneo yetu na hata hii nia njema inayoonekana. Katika hili inaonekana wazi miradi 25 imekamilika, ikaja na kilometa hizi 1,198 lakini bado kuna miradi 74 ambayo ipo katika hatua mbalimbali tunaamini hii ina kilometa 3,774 itakapokamilika basi hazitakuwa tena 1,100 na kitu, itakuwa 5,000. Ninaamini hizi nazo ziendelee kukamilishwa ili Mheshimiwa Rais nia yake njema ya kuhakikisha kwamba lami inapatikana nchi hii iendelee kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nirudi sasa Jimboni kwangu Busanda; nimpongeze Mheshimiwa Waziri, nilikuwa nasoma bajeti ya mwaka huu kwamba kuna nia njema inaonekana kwenye bajeti. Kwenye bajeti ya mwaka huu barabara ambayo tumekuwa tunaisema kila siku ya kutoka Geita kwenda Kahama sasa inaonekana ina nia njema ya kuanza kushughulikiwa na kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kipande ambacho kinatoka Kahama kuja Bulyanhulu pale Kakola Junction tayari kina fedha ambayo inaonekana takribani shilingi bilioni 14 zinaanza kufanya kazi. Pia kuna kipande cha kutoka Bulyanhulu kuja Geita ambacho tayari kimekwishatangazwa na sasa tunaamini kwamba wanakwenda kusaini mkataba kwa ajili ya kuanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu katika eneo hilo basi haya tunayoyasikia kwamba imetangazwa na imesainiwa mwaka mzima na hamna kilichofanyika isiwe sehemu ya barabara hii ambayo tunaisema sasa. Vilevile bado nimeona kuna Barabara ya kutoka Katoro – Nyikonga – Ushirombo pia kwenye page 228 inaonesha kutengewa fedha kidogo kwenye hizo kilometa 22.5 kwa ajili ya kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niombe sana kwamba, tunapokwenda kwenye hatua hizo za upembuzi yakinifu kwenye barabara hii ya kutoka Katoro – Nyikonga – Ushirombo ina miaka mingi na upembuzi huu sasa nafikiri hata inapoenda kuanza kushughulikiwa ni lazima irudiwe tena kwa sababu itakuwa ule upembuzi yakinifu sasa hauwezi kuwa up to date.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana haya ambayo yameandikwa hapa yaweze kufanyiwa kazi na sisi Busanda sasa tuone. Sisi ni wachimbaji wa madini tunazihitaji barabara hizi zipite kwenye migodi yetu ili tuweze kufanya kazi yetu vizuri na kuongeza uchangiaji wa Pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kila aliyesiamama hapa anaonesha ipo miradi yetu ya EPC+F imekwama. Kila anayesimama anaonesha tukilipa deni la karibu bilioni 929 ukiongeza na riba inakwenda kwenye trilioni moja maana yake hii trilioni moja ambayo ni ya ndani hapa ikitolewa tutabaki na bilioni 10. Bilioni 10 hatuwezi kufanya kitu chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapata mawazo kwamba inawezekana tunatakiwa tuishauri Serikali iangalie vyanzo vyake vya upatikanaji wa fedha kwa sababu kama kila mmoja anayezungumza miradi imekwama maana yake ipo nia njema ya Wizara na ya Mheshimiwa Rais lakini mapato yetu hayatoshi kufanya miradi hii. Nimesikia ndugu yangu mmoja amesema kwamba mpaka wanataka wazuie na barabara. Sasa kama mapato hayapo wakizuia barabara maana yake mapato yatakuwa hayapatikani kabisa. Kwa hiyo, niseme wazi kwamba tunatakiwa sasa tuangalie kuna mahali fulani ambapo kwenye makusanyo yetu hapako vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nina mashaka na nidhamu ya matumizi yetu kwenye bajeti hizi, kwa sababu kila tunapopata Ripoti ya CAG tunaona kama kuna malalamiko hivi. Hebu tusimamie nidhamu ya matumizi ya bajeti na tusimamie vilevile kuongeza vyanzo vya mapato ili mapato yapatikane tuweze kutumia. Tofauti na hiyo tutaendelea kutangaza barabara kila mwaka, tutampongeza Mheshimiwa Bashungwa na Mheshimiwa Rais, ukija mwaka mwingine tunasema hazikufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ili hili tusione ni lazima twende tuhakikishe kwamba, tuna bajeti ya kutosha. Kama kuna pesa inatakiwa ipatikane kwenye kilimo ipatikane, pesa ya kwenye madini ipatikane, isimamiwe vizuri kuhakikisha kwamba tunaenda kufanya miradi hii ambayo na kwa hali halisi tunashindwa kutekeleza kwa sababu ya vyanzo vyetu vya mapato havitoshi kufanya kila mradi uliokwishasainiwa sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo naomba niunge mkono hoja nikiamini kwamba, hizi barabara nilizotaja za Busanda zitakwenda kufanyiwa kazi na watu wataanza kupata maendeleo yao, ahsanteni sana. (Makofi)