Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Luhaga Joelson Mpina

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisesa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumpongeza Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb) kwa uwasilishaji wake mzuri wa hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na taasisi nyingine chini ya Wizara hii kwa namna wanafanya kazi. Aidha, nimeshindwa kujizuia kumpongeza kwa dhati Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor H. Seff, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Boniface Mkumbo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Gaston Pascal na Meneja wa Wilaya ya Meatu, Mhandisi Elieza Mayengo kwa namna wanavyosimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja katika Jimbo la Kisesa na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla. Hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, mambo ya kiujumla na nianze na miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja yaliyokamilika miaka ya nyuma kurejewa kwenye hotuba ya Waziri ya mwaka 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Waziri Ibara ya 18 na baadhi ya Ibara zingine imeorodhesha miradi mingi ya barabara na madaraja yaliyokamilika miaka ya nyuma na kuanza kutumika na hivyo siyo sehemu ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2023/2024 na mipango ya bajeti ya 2024/2025. Nini sababu za Waziri kurejea miradi iliyokamilika tangu mwaka 2021 kwenye hotuba ya bajeti yake?

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya Bariadi-Kisesa-Mwandoya –Ngh’oboko kilometa 102; barabara hii kwa muda mrefu imekuwa ikiripotiwa iko kwenye hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na tulitegemea leo tutaambiwa hatua ya awali imekamilika na ujenzi umeanza, lakini cha kusikitisha hotuba ya Waziri Ibara ya 131(c)(viii) ukurasa wa 73 inaeleza kuwa Serikali ipo katika taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mhandisi mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Spika, barabara hii ipo kwenye ahadi zilizotolewa na viongozi wakuu wa kitaifa na katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020. Waziri atuambie, je, ni nini kinachosababisha Serikali kuwapiga danadana wananchi wa Jimbo la Kisesa na Mkoa wa Simiyu kuhusu barabara yao hiyo ya lami?

Mheshimiwa Spika, miradi mingi imeorodheshwa ikiwa haina kasma ya Bajeti, kwa mfano Barabara ya Kolandoto-Lalago-Sanga Itinje-Ng’ohobokoMwanhuzi kilometa 122 na miradi mingi ya barabara na madaraja imeorodheshwa na Serikali, lakini haijatengewa fedha hali inayopelekea matumaini hewa kwa wananchi. Utaratibu mzuri wa mipango miradi inayoorodheshwa ni ile iliyopangiwa fedha katika mwaka husika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa viwanja vya ndege; hotuba ya Waziri Ibara ya 20 ukurasa wa 19 anaripoti viwanja vya ndege ambavyo vilishajengwa miaka mingi iliyopita na kuanza kutumika. Nini sababu ya Waziri kurejea kutaja majina ya viwanja hivyo?

Kuhusu barabara za michepuo hotuba ya Waziri imeonesha orodha ndefu ya miradi ya ujenzi wa barabara za michepuo zinazofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili baadaye zijengwe kwa lengo la kupunguza msongamano katika miji mbalimbali nchini. Nimepitia miradi hiyo mingi haina ulazima kwa sasa na Serikali isiondoke kwenye jukumu la msingi la kupeleka barabara za lami maeneo mengine ambayo hayajafikiwa, haiwezekani tukaanza kuweka vipaumbele vya barabara za michepuo na kuwaacha Watanzania wengine wakiwa na shida ya barabara za lami kwa miaka mingi. Waziri wa Ujenzi awe makini na mipango ya aina hii ambayo inaweza kuwa ni sehemu ya kufuja fedha za umma na kufanya upendeleo katika ugawaji wa raslimali za nchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu fedha zilizoombwa; fedha za maendeleo zinazoombwa ni shilingi trilioni 1.628 ikiwa ni ongezeko la 14.88% ya bajeti ya mwaka 2023/2024 ambapo pia ongezeko hilo ni fedha za kutoka nje. Miradi mingi imetajwa katika hotuba ya Waziri lakini haina kasma ya fedha na miradi mingi ni ahadi za muda mrefu, Kamati kwa kuliona hilo imeomba bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo iongezwe hadi kufikia shilingi trilioni tano ili kuwezesha ujenzi wa viwanja vya ndege, barabara na madaraja kote nchini, lakini pia kuna miradi hewa ya EPC+F.

Waheshimiwa Wabunge, nawaomba tuungane na Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini tuikatae bajeti hii na tuirudishe Serikalini ikafumuliwe na kuandaliwa upya.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mikataba ya ujenzi wa barabara kwa utaratibu wa EPC+F; tarehe 16 Juni, 2023 Serikali ilisaini mikataba saba ya ujenzi wa miradi saba ya barabara zenye jumla ya kilometa 2,035 kwa gharama ya shilingi trilioni 3.75 kwa kiwango cha lami kwa kutumia utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC + F) na kama pia ilivyoelezwa katika hotuba ya Waziri miradi hiyo ni kama ifuatavyo; Mafinga-Mtwango-Mgolololo (kilometa 81); Igawa-Songwe-Tunduma (kilometa 218); Uyole-Songwe (kilometa 48.9); Masasi-Nachingwea-Liwale (kilometa 175); Arusha-Kibaya-Kongwa JCT (kilometa 453.42); Ifakara-Lupiro-Malinyi-Kilosa,Kwampepo-Londo-Lumecha/Songea (kilometa 435); Karatu – Mbulu - Haydom-SibitiRiver-Lalago-Maswa(Simiyu) (kilometa 339); na Handeni-Kibirashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboroti - Mrijochini-Chambalo- Chemba - Kwa Mtoro - Singida (kilometa 374.24).

Mheshimiwa Spika, tangu kusainiwa kwa mikataba hii leo ni takribani mwaka mzima umepita ujenzi haujaanza, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa Mnyaa na Waziri wa Ujenzi wa sasa Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa walikuwa wakieleza kuwa wakandarasi bado wanafanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na baadaye maelezo yakabadilika kuwa Serikali inatafuta fedha za kuwalipa wakandarasi malipo ya awali 10% ya thamani ya mradi kiasi cha shilingi bilioni 375.51 ndiyo kazi iweze kuanza.

Mheshimiwa Spika, awali siku ya kusaini mkataba huu ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge tulishiriki tukio hilo nilipinga wasilisho la Waziri la kuitambulisha miradi hiyo kwa kuwa hapakuwa na maelezo ya kina. Miradi hiyo inatekelezwa kwa utaratibu upi kwani masharti na vigezo vya mikataba hiyo havikuwekwa wazi, ilikuwa ni siri kati ya Waziri na wakandarasi.

Mheshimiwa Spika, siku ya kusaini mikataba na ndani ya Bunge nilihoji nini faida ya kutumia EPC+F badala ya utaratibu wa kawaida wa Serikali kuajiri na kulipa wakandarasi, wakandarasi wa EPC+F watalipwa kwa utaratibu gani baada ya miradi kukamilika au kwa kipindi gani? Na kwa kuwa huu ni mkopo kwa nini tunapanua dirisha la ukopaji fedha nje ya utaratibu uliowekwa? Ulinzi wa ajira za vijana nchini utalindwaje katika miradi ya aina hii? Na kwa kuwa miradi hii wakandarasi watatumia fedha zao, nafasi ya CAG na Bunge itakuwaje katika utekelezaji wa miradi hiyo? Kwa kiufupi maswali haya hayakupata majawabu hadi leo.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ya mwaka 2022/2023 imethibitika kuwa mikataba hii ilisainiwa bila kuwa na ufadhili wa uhakika wa miradi hiyo na wakandarasi wameshindwa kuwasilisha dhamana ya benki ya utendaji kazi yenye thamani ya shilingi bilioni 375.51 kama matakwa ya mkataba na ndiyo sababu ya miradi hii kushindwa kuanza hadi sasa.

Mheshimiwa Spika, hawa wakandarasi walipatikanaje hadi wakasaini mikataba wakiwa hawana sifa na uwezo wa kifedha? Mkataba wa EPC+F uliwezaje kusainiwa bila kujiridhisha na masuala ya msingi ikiwemo ufadhili wa fedha za mradi? Hapa kuna kila dalili ya harufu ya rushwa na Taifa letu kuingizwa kwenye nikataba ya kinyonyaji.

Mheshimiwa Spika, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amekuwa akitumia nguvu kubwa kulipotosha Bunge na umma wa Watanzania kwa makusudi kuhusu faida za miradi ya EPC+F na akituita baadhi ya Wabunge tuliohoji mikataba hii kuwa ni wapotoshaji na tuna nia mbaya. Pia Waziri Mbarawa alikiri kwamba hata alipowashirikisha TANROADS walipinga utaratibu wa EPC+F, lakini yeye akatumia madaraka yake kulazimisha utaratibu huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetumia gharama kubwa kuandaa miradi hewa na kupeleka ahadi hewa kwa wananchi wa maeneo yaliyotajwa na mbaya zaidi wananchi wa mikoa inayopitiwa na miradi saba ya barabara wameondolewa kwenye mipango na bajeti ya mwaka 2023/2024 na 2024/2025 kwa kuwa barabara zao zitajengwa kupitia utaratibu wa EPC+F.

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inakiri kwamba hakuna kinachoendelea katika miradi ya EPC+F, hotuba ya Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Innocent Bashungwa katika Ibara ya 40 ukurasa wa 36 anakiri kuwa miradi hiyo haina chanzo cha fedha na bado haijaanza na kwamba Serikali inaendelea na mazungumzo na wafadhili ili kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo. Miradi tuliyoambiwa ina ufadhili wa moja kwa moja yaani mkandarasi anayejenga atatumia fedha zake na baadaye kuidai Serikali, leo tunaambiwa anatafutwa mfadhili wa kugharamia miradi hiyo. Hii inaleta sintofahamu na mkanganyiko mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa utapeli huu wa kuajiri wakandarasi wasio na uwezo wa kutekeleza miradi ya EPC+F, kupeleka ahadi hewa kwa wananchi na kutumia fedha za umma nje ya utaratibu uliowekwa, Waziri Mbarawa aliendelea kulihadaa Bunge kuwa uchelewaji wa kuanza miradi umesababishwa na wakandarasi kufanya detailed design na kwamba wanasubiri malipo ya awali ya 10% kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Spika, ni Tanzania pekee Waziri aliyeyafanya haya Profesa Mbarawa anaweza kuwa kwenye ofisi za umma mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, nashauri mikataba yote ya EPC+F ivunjwe na miradi hiyo ifutwe kwenye vitabu vya Serikali. Pia bajeti ya Wizara ya Ujenzi ya mwaka 2024/2025 irudishwe na ifumuliwe upya ili kuwezesha majimbo, wilaya na mikoa iliyokuwa imeingizwa kwenye miradi hewa ya EPC+F ipangiwe upya fedha katika ugawanaji wa keki ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, Waziri Profesa Mbarawa ameichonganisha Serikali na Mheshimiwa Rais mbele ya wananchi, amekichonganisha Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ahadi hewa ya ujenzi wa barabara kilometa 2,035, na kwa kuwa kuna dalili na harufu ya rushwa, vyombo vya uchunguzi TAKUKURU, DCI na DPP wachukue hatua kwa Profesa Mbarawa na wote waliohusika kwenye kashfa hii, kwa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi na kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008.

Mheshimiwa Spika, kuhusu miradi ya barabara na madaraja ya PPP; maelezo yaliyotolewa katika hotuba ya Waziri katika Ibara ya 215 ya hotuba kuhusu utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara (express way) kwa utaratibu wa PPP ni maelezo hayo hayo yaliyotolewa mwaka jana na Profesa Makame Mbarawa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi ambapo iliahidi kuwa mikataba ingekuwa imesainiwa kufikia Juni, 2023 na kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukihoji sana suala hili hapa Bungeni lakini hatupati majibu kutoka Serikalini, binafsi nimehoji kwa kusema na kwa michango ya maandishi ya mara kwa mara bila majibu, Serikali inawezaje kuanzisha mchakato unaohusu kutwaa au kutumia ardhi ya umma bila kibali cha Bunge, hifadhi ya barabara tuliyonayo ni mali ya umma kwa matumizi ya umma, Wizara ya Ujenzi haina mamlaka ya kukabidhi maeneo ya hifadhi za barabara kwa mwekezaji wa sekta binafsi bila kibali cha Bunge.
Mheshimiwa Spika, kuna mkanganyiko mkubwa wa mipango ya Serikali na pengine huoni kama kuna nia njema kwani huwezi kuja na mradi wa ujenzi wa barabara ya kulipia kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro-Dodoma (express way) yenye urefu wa kilometa 531.8 kwa utaratibu wa PPP huku kuna mradi mkubwa wa SGR ambao uko hatua za mwisho kukamilika na utaanza kutoa huduma Julai, 2024. Mradi huu unatarajiwa kupunguza msongamano wa magari barabarani kwa zaidi ya 60%. Hii ni mipango mibovu na matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Mheshimiwa Spika, uzoefu unaonesha kuwa nchi zilizojenga barabara za kulipia huacha kwa makusudi kukarabati njia mbadala ili wananchi walazimike kupita katika barabara za kulipia, lakini pia makampuni ya ubia yamekuwa yakiweka bei kubwa za tozo na kusababisha gharama za usafiri na usafirishaji kuwa juu na hivyo kuchochea mfumuko wa bei za bidhaa na ugumu wa maisha.

Mheshimiwa Spika, kama nchi tumejipangaje kabla ya kuiendea miradi ya namna hii? Ikumbukwe kuwa barabara hii inatoka kwenye lango kuu la uchumi wa nchi yetu yaani Bandari ya Dar es Salaam kwenda kwenye mikoa na mataifa mbalimbali ya nchi jirani. Mchakato unaoendelea wa kumpata mkandarasi ni kinyume cha Sheria ya Ardhi na Sheria ya Rasilimali inayotaka hatua zote kuwa wazi na Bunge kujulishwa.

Mheshimiwa Spika, leo Waziri atuambie ukweli juu ya faida ya mradi huu, nchi yetu imejenga na imeunganisha mikoa yote kwa barabara za kiwango cha lami, tumejenga mtandao mkubwa wa SGR, leo hatuna fedha za kujenga njia nne kutoka Kibaha-Chalinze-Morogoro hadi Dodoma? Au kuna jambo lililojificha nyuma ya pazia kwenye miradi hii ya PPP.

Mheshimiwa Spika, tulishaanza safari ya upanuzi wa barabara ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ambapo ujenzi wa barabara wa njia nane umeshakamilika kutoka Kimara hadi Kibaha na hivyo tunaweza kuendelea kutenga bajeti kwa awamu hadi Chalinze na baadaye Morogoro na Dodoma ikizingatiwa kuwa miradi mingi ya kimkakati iliyokuwa inachukua fedha nyingi inakamilika ya Bwawa la Nyerere, Daraja la JPM (Kigongo Busisi) na SGR. Tume ya Mipango iko wapi hadi mipango mibovu kama hii kuendelea kwenye nchi.

Mheshimiwa Spika, miradi mingine inayoainishwa kutekelezwa kwa njia ya PPP haina tija na inaweza kusababisha hasara kubwa mfano Daraja la Pili la Kigamboni (Magogoni -Kivukoni). Daraja hili linapendekezwa kujengwa wakati tunalo Daraja la Nyerere (Kigamboni) lilojengwa na Mfuko wa NSSF hivyo kujengwa daraja lingine la kulipia litaua biashara ya daraja lililopo na kushindwa kurejesha mtaji wa uwekezaji wa shirika hilo, lakini pia eneo linalopendekezwa kujengwa daraja la pili kuingilia meli katika Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ifute michakato inayoendelea wa kutafuta mkandarasi wa kujenga mradi wa barabara ya kulipia kutoka Kibaha hadi Dodoma kwa utaratibu wa PPP na badala yake ifanye tathmini upya kubaini maeneo na miradi yenye faida kiuchumi kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP.

Mheshimiwa Spika, hitimisho; Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Innocent Bashungwa anashauriwa kuwa makini katika uandaaji wa bajeti na kuepuka kurudia miradi iliyokwishatekelezwa miaka ya nyuma, kutokuorodhesha miradi ambayo haina kasma ya fedha na kujiepusha kuanzisha miradi isiyo na tija kwa Taifa.

Mheshimiwa Spika, ni jambo la kushangaza kuona mipango mibovu kiasi hiki wakati tuna Tume ya Mipango, Wizara inayotekeleza miradi mikubwa ya madaraja, barabara za lami na changarawe, viwanja vya ndege na vivuko kutengewa fedha ndogo kiasi cha shilingi trilioni 1.6 tu huku miradi mingi ya kimkakati iliyokuwa inachukua fedha nyingi imekamilika na mingine iko hatua za mwisho kukamilika.

Mheshimiwa Spika, aidha, ifahamike kuwa mipango mibovu inaliangamiza Taifa letu kwa kiasi kikubwa, hivyo kupitia Tume ya Mipango ni lazima kufuatilia upya na kuongeza fedha katika Wizara hii na miradi yote isiyo na tija ifutwe katika vitabu vya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mambo mengine ni mepesi hayahitaji hesabu ngumu, ni rahisi mno, it does not need hot calculations to do it like calculus, statistics, combination and permutation, it is a low hanging fruit. Ni lazima mipango yetu iwe ya wazi na uwajibikaji katika kuliletea Taifa letu maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.