Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kuunga hoja bajeti hii ambayo ipo mbele yetu. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kuiletea maendeleo Tanzania na hasa jinsi anavyopigania miundombinu yetu kufanya iwe ni kati ya nchi zinazokuwa na miundombinu bora na mingi katika Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu. Nikushukuru sana Mheshimiwa Spika, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti ambao mnatuongoza vizuri sana katika Bunge letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru sana Kamati ya Miundombinu chini ya Mheshimiwa Kakoso - Mwenyekiti wetu na Mheshimiwa Anne Kilango - Makamu Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wote jinsi ambavyo wamekuwa wakitusimamia na kutupa miongozo. Nawashukuru sana Wabunge wote kwa michango yenu lakini pia kwa ushauri wenu na tunaahidi tu kwamba michango tutaichukua, ushauri tutauchukua na tutayatekeleza yote yale ambayo kwa kweli yanatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Waziri wa Ujenzi. Sina haja ya kueleza nini Mheshimiwa anafanya Wajumbe wameshaeleza, hongera sana Mheshimiwa. Sisi tunajivunia kuwa na wewe na tunaona jinsi Wizara inavyokwenda kasi. Kwa shukurani tu na mimi niishukuru familia yangu kwa kunipa ushirikiano mkubwa ili niweze kutekeleza majukumu yangu.

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu inasimamia taasisi kubwa tatu: TANROADS, TBA na TEMESA. Nitaanza na TANROADS na kwenye TANROADS naomba kwa kweli Wabunge na wananchi wa Tanzania tukubaliane kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa kujitolea kwake lakini na kujitoa kwake kukabiliana na changamoto kubwa ambalo lilikuwa ni janga kubwa ambalo kama nchi tumeweza kwa kweli kukabiliana nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alitutahadharisha kama Serikali lakini na wananchi kupitia TMA kwamba kutakuwa na changamoto. Bahati nzuri alituandaa vizuri sana watu wa Serikali lakini pia na wananchi kwamba kutakuwa na janga. Changamoto ilikuwa ni kupima uzito huo utakuaje wa changamoto ambao nadhani hakuna aliyeota ama kutabiri changamoto itakuwa vipi. Tukianzia Katesh - Hanang, Mheshimiwa Rais aliacha shughuli zake zote akaenda kule. Ukitaka kujua wema, shukurani kwa Mheshimiwa Rais, mtu yeyote aende akaulize wana-Katesh Mheshimiwa Rais wanamsemaje au wanamuonaje? Walikuwa wamekata tamaa lakini leo amerudisha maisha ya wana-Hanang na wanaona kwamba kweli Serikali ipo, hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuishia hapo, tumeona changamoto kubwa sana ambayo imekumba mikoa yetu ya Dar es Salaam, Lindi, Rukwa, Morogoro na mikoa mingine. Takriban mikoa yote 26 Tanzania Bara imepata changamoto kubwa lakini pongezi hizi wanazotoa Waheshimiwa Wabunge kwa mameneja wetu kwa kweli na mimi niwapongeze managers wetu. Kila palipotokea changamoto walikuwa haraka kurejesha miundombinu. Tunavyoongea sehemu kubwa hapakuwa na bajeti ya hiyo emergency kubwa lakini leo tumerejesha na kama mlivyomsikia Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Rais anatafuta fedha kuhakikisha kwamba miundombinu inarudi katika hali yake ya kawaida ilivyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara ya Lindi Kibiti ni kweli imechakaa na imeathirika sana. Serikali kwa kweli tunajipanga kuhakikisha kwamba barabara ile ijengwe upya lakini kabla ya kujenga upya maeneo yote yaliyoharibika yarejeshwe katika hali yake ya kawaida. Barabara nyingi za Tanzania zinaharibika haraka kutokana na ukweli kwamba kumekuwa na ukuaji mkubwa sana wa uchumi. Hatukufikiria kutakuwa na Dangote wakati tunajenga, kwa hiyo barabara kiwango kilichojengwa hakikuwa kikubwa kwa kubeba magari yale. Ukienda barabara za Kusini makaa ya mawe wanapo-design barabara mara nyingi wanaangalia magari ya aina gani yatapita lakini kutokana na ukuaji wa uchumi ndiyo maana barabara nyingi kwa kweli zimeenda kuchoka mapema tofauti na ilivyokuwa ime-design-iwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tumejifunza kwamba kila barabara inayo design-iwa iwe ina-design-iwa kwamba itabeba mizigo mikubwa. Niwahakikishie wana-Mtwara kwamba kupitia mradi wa TanTIP kuanzia Mtwara - Mingoyo hadi Masasi barabara inaenda kujengwa. Songea, TanTIP barabara ambayo imeongeleWa sana ya Makambako Songea, tunaanza Songea mpaka Lutukila pamoja na bypass, ni World Bank watafadhili. Tuna barabara nyingi ikiwepo ya Mheshimiwa Waziri wangu Jenista, Likuyufusi - Mkenda kilometa 60 pamoja na daraja la Mitomoni. Mheshimiwa Benaya Kapinga unajua wakandarasi wapo ndani. Suala la mkandarasi yupo site nadhani changamoto tutazirekebisha na barabara hii tutaikamilisha kuanzia Kitai - Litui mpaka Ndumbi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ameongea sana Mheshimiwa Kunambi lakini na Mheshimiwa Reuben. Kutokana na umuhimu wa barabara na kuunganisha mikoa, Mheshimiwa Waziri ameamua kupandisha hadhi ya barabara ya kutoka Kibena – Lupembe - Mlimba hadi Ifakara iende kwenye trunk, iwe trunk road. Sambamba na hiyo, kutoka Mikumi kwenda Dumila, kwenda Turiani, Mziha hadi Handeni ipande ili hiyo barabara iwe na uwezo wa kuunganisha mpaka bandari ya Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Reuben, Mbunge wa Handeni naomba usishike shilingi. Katika bajeti hii kama umeipitia barabara hii tunaendelea kuijenga. Tumeshajenga kilometa 45 kuanzia hapa Dumila mpaka Turiani na sasa tutaanza kujenga kilometa 30 kutoka Handeni kuja upande wa Mziha.

Mheshimiwa Spika, yote hiyo ni kuiunganisha Tanga, Handeni, Kilosa hadi Ifakara. Kwa hiyo mpango upo na tumeshaanza kujenga na mwaka huu tumeweka kwenye mpango huo wa kuijenga.

Mheshimiwa Spika, nikija Ifakara, Lupilo hadi Malinyi barabara imeathirika sana kwa Mheshimiwa Mgungusi. Hii barabara ipo kwenye EPC mimi nimeitembelea. Tulichokubaliana hata kama tutaanza kwa EPC ama kwa namna yoyote lakini maeneo yote yale ambayo ni makorofi hata kama yaanze kujengwa madaraja pamoja na maeneo korofi ili wananchi hawa hata wakati barabara inajengwa lakini yaweze kuwa yanapitika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nigusie barabara ya jiji la Mbeya, dada yangu Mheshimiwa Suma Fyandomo ameiongelea lakini na mimi pia ni mnufaika kwa sababu ili nifike Ileje lazima nipite Mbeya. Tunajua changamoto kubwa ukiwa unasafiri kwenda huko ndiyo unajiuliza nitapitaje?

Mheshimiwa Spika, kweli kumekuwa na kuchelewa lakini kuna sababu mbili kubwa. Barabara iliyokuwa inajengwa ndiyo kulikuwa na miundombinu ya maji, miundombinu ya umeme na miundombinu ya simu ambayo imechukua muda sana kuiondoa kwa sababu ilikuwa lazima uiondoe kwanza, uiunganishe ndiyo uitoe na ndiyo barabara zijengwe lakini kukaja pia na mvua ikanyesha sana. Nina hakika kwa jinsi ulivyochangia Mheshimiwa Suma Fyandomo tumesikia na kwa sababu mkandarasi yupo site sasa hivi ni kumsukuma aweze kwenda kwa kasi inayostahili ili hizo kilometa 29 ziweze kukamilisha na nikumbushe tu ndiyo barabara ambayo inapeleka magari yote yanayotoka Dar es Salaam kwenda Tunduma. Kwa hiyo ni moja tu katika Jiji la Mbeya. Kwa hiyo Wizara inatambua na ndiyo maana ilikuja na huo mpango wa kuijenga hiyo barabara.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uwezeshaji wanawake na vijana tumekuja na mpango mpya, tuliona wanawake wengi wanaachwa nyuma. Tunavyoongea hizo kilometa 20 tulishatangaza na kuna kandarasi tano zitakazo kuwepo hapo ambazo tayari tupo kwenye manunuzi kuwajengea uwezo. Tutakachokifanya kama Wizara pamoja na TANROADS ni kuwasaidia kwenye management namna ya kuendesha miradi mikubwa kama hiyo. Pia, tulichofanya Wizara yetu pamoja na Wizara ya Fedha kwamba sasa tutoke wazawa kuwa na miradi inayoishia thamani ya shilingi bilioni 10 twende shilingi bilioni 50 ikiwa ni kuwajengea uwezo lakini pia kuhakikisha kwamba fedha nyingi na miradi mingi inajengwa na wazawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee kidogo kuhusu TBA; kuna watu wamegusia TBA. TBA ni wakala wa nyumba. TBA kazi iliyokuwa inafanya ni kujenga majengo ya viongozi wa Serikali na watumishi. Haikuwa inafanya biashara. Mheshimiwa Rais alipoingia akasema hapana toka nje ya box na hasa baada ya kuona Magomeni Quarters. Tumebadilisha muundo na sasa hivi TBA watafanya kazi na private sector. Kwa hiyo yale mawazo mliyokuwa nayo watafanya biashara na watapangisha. Kwa hiyo tunahakika watakuwa na uwezo mkubwa wa kujenga majengo mengi hususan katika Mji wa Dodoma, kwa sababu ilikuwa siyo rahisi kufanya hivyo kutokana na sheria yake ya muundo.

Mheshimiwa Spika, TEMESA kwa wakazi wa Dar es salaam. Julai TEMESA watakubaliana ama wataingia makubaliano na Azam kuendesha kwa PPP ama kwa JV ili kuhakikisha kwamba sasa watu wengine private wanaweza wakaendesha vivuko pale kupunguza changamoto iliyopo. Pia, itakuwa ni kusaidia kuboresha uendeshaji wa kile kivuko ambacho tumeona kwamba kwa utaratibu uliopo hauwezi kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwakumbushe tu kabla sijamaliza kwamba wakati tunapata uhuru mwaka 1961, Tanzania tulikuwa na barabara za lami kilometa 1,360 lakini katika kipindi hiki cha Awamu ya Sita Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amejenga na kukamilisha kilometa 1,198.5. Unaweza ukaona kazi lakini kilometa tulizonazo ni kilometa 12,000 za lami. Kwa hiyo unaweza ukaona kazi kubwa ambayo ameifanya katika kipindi hiki kifupi na bado tuna miradi mingi mikubwa ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Spika, tuna miradi ya kimkakati ya hapa Dodoma na Mheshimiwa Waziri alieleza vizuri sana nini kinaendelea kuhusu ring road, inner na medium. Pia, tuna-decongest mji wa Dar es salaam. Tunatakaku- decongest mji wa Mwanza kuhakikisha kwamba watu wanakwenda kwa uharaka sana na tuna miradi ya kielezi ambayo tumeeleza vizuri sana Kigongo Busisi ambayo tuna uhakika Disemba itakamilika. Kwa hiyo kazi zote hizo zinaendelea kufanyika na tuna hakika tutafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la fidia, niongelee kidogo kuhusu fidia. Tuna mambo mawili; fidia kutokana na sheria yetu ambayo imetupeleka kwenye meta 60. Meta 7.5 ndiyo limekuwa tatizo kubwa sana na Serikali kupitia Wizara tunafanya uchambuzi kuona; je, ni kweli maeneo yote tunahitaji hizo meta 60? Kama siyo, sheria yetu lakini inatuelekeza tufanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna mipango ya ku-divert kwenye miji na kuangalia maeneo specific ambayo tutayaona kama kweli tunahitaji halafu tutapeleka Serikalini watayapitia kwa maana ya viongozi wa Kiserikali tuone halafu Serikali itakuja na tamko tufanye nini kuhusu fidia kwa watu wanaopisha barabara kulingana na sheria yetu ilivyo. Kwa sababu tumeona ni kweli watu wamesimamishiwa majengo yao kwa muda mrefu na imekuwa ni changamoto lakini kwa 22.5 kwa maana ya 45 lazima tuwafidie, tuwalipe ndiyo waweze kuondoka.

Mheshimiwa Spika, miradi ya TanTIP. Tunayo miradi sita ya TanTIP ambayo inatekelezwa na World Bank ambayo ni barabara za Iringa Msembe, Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Kiwanja cha Lake Manyara na Kiwanja cha Tanga. Miradi hii yote ipo kwenye hatua za manunuzi na tupo kwenye evaluation, kwa hiyo muda wowote miradi hiyo itaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, mwisho niendelee kuwasihi Waheshimiwa Wabunge, ili tuweze kufanya shughuli zozote tunahitaji barabara. Kwa hiyo tunaomba kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Fedha mtupitishie bajeti ili tuendelee na kazi yetu kuhakikisha kwamba Tanzania inatembea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona dhamira ya Mheshimiwa Rais ipo, anaiunganisha nchi na anaifungua nchi. Kwa hiyo niwashawishi tunaomba bajeti yetu ipitishwe tukatekeleze na kupitisha bajeti ya ujenzi maana yake umesaidia pia kwamba sekta zote, wakina mama waende wakatibiwe, watoto waende shuleni lakini pia mazao yatoke shambani yafike kwenye masoko...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)