Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Ulinzi pamoja na JKT.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya na jitihada zake za dhati kabisa kuimarisha amani na utulivu katika Taifa letu na sote Watanzania tunajivunia kuwa katika Taifa letu na tunajivunia kuwa katika hali hiyo. Hali kadhalika nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha utulivu, mshikamano na demokrasia kwenye Taifa letu kupitia falsafa za 4R. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dunia ya hivi sasa inajielekeza kwenye kujiimarisha kwenye eneo zima la ulinzi dhidi ya vita ama dhidi ya matukio ama dhidi ya changamoto zozote zinazoletwa kutokana na matumizi hasi ya kidigitali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilishachangia mwaka jana hapa ndani ya Bunge kwamba Serikali ijielekeze katika kuwekeza zaidi katika kuwezesha jeshi kuweza kukabiliana na changamoto hizi za matumizi hasi ya kidijitali, lakini hata mwaka huu mwezi Februari niliishauri pia Serikali ione namna ambavyo italiongezea jeshi fedha ili waweze kuwa na mikakati, kujielimisha pamoja na kuwa na vifaa vya kuweza kupambana na kudhibiti electronic warfare (vita ya kidigitali). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tumeona Taifa letu pamoja na mataifa mengine tulikuwa katika hali ya kutokuwa na access, kutokuwa na mtandao kwa takribani siku tatu mpaka siku tano. Kitendo hicho kimeleta athari mbalimbali, fedha zimepotea za kiuchumi kutokana na watu kushindwa kufanya kazi zao lakini hata imeongeza athari ya kiusalama katika kipindi hicho kwa sababu moja, hata mawasiliano ya ndege yalikuwa yanashindikana kwa hiyo zipo ndege ambazo zilichelewa kutoka, bording pass ilibidi zitoke bila kuwa printed. Zipo Balozi ambazo zililazimika kuandika visa kwa karatasi na kuwapa wale wasafiri barua, lakini zipo Balozi ambazo zilifunga kabisa Balozi zao na kusitisha kutoa huduma ya visa kwa hofu ya athari ya kutokuwa na mtandao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hilo ni dhahiri kabisa yapo matendo kama hayo yanayoweza kutokea kwa bahati mbaya, lakini pia yapo matendo ya namna hiyo yanayoweza yakatokea kwa makusudi kabisa ambapo wahalifu wakaamua kutumia mwanya huo kuingilia mifumo yetu ya fedha, kuingilia mifumo yetu ya kiusalama, kuingilia mifumo yetu ya kimawasiliano na kuliweka Taifa letu katika hatari kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi kwa unyenyekevu mkubwa sana naiomba sana Serikali ichukulie jambo hili kwa dharura, ione namna ambavyo itaipa fedha Wizara hii ya Ulinzi na kulipa fedha jeshi letu ili waweze kuwa na idara madhubuti ya masuala ya cyber, wanajeshi wetu waweze kupata elimu madhubuti ya namna ya kukabiliana na matukio haya, lakini pia na jeshi letu liweze kuwa na vifaa thabiti vya kuweza kudhibiti na kupambana na electronic warfare (vita ya kidijitali). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili, nilishasema mwaka jana na narudia tena kusema, kuna msemo ambao tunasema adui yako muombee njaa. Dunia imeshatambua kwamba kuna uhusiano wa karibu sana baina ya uhakika wa chakula na ulinzi na usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo inasema moja ya dira yake ni kulisha Tanzania na kulisha dunia. Hatuwezi kufikia hapo ikiwa bado tunategemea zaidi ya 60% ya mbegu zetu za chakula kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati umefika sasa, jeshi letu liweze kuwezeshwa, liweze kuingia katika kuzalisha mbegu. Ni kupitia kuzalisha mbegu ndipo tutajihakikishia usalama wa Taifa letu, usalama wa chakula tunachokula pamoja na changamoto mbalimbali ambazo wakulima wetu wanazipitia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Taifa likitaka kukuangamiza, vita ya chakula ndiyo vita nyepesi kuliko zote na ina athari kubwa sana. Tunaweza kununua mbegu kutoka nje, tukakuta mbegu zile wakulima wanapanda, chakula hakitoki. Tunaweza kununua mbegu tukakuta mbegu hizi zikifika kiwango fulani mazao yale yanashambuliwa na wadudu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mbegu ni suala nyeti sana. Ikiwa sasa hivi dunia inahakikisha na inaweka jitihada, suala la mbegu ni la ulinzi na usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka jitihada kubwa sana kuimarisha sekta ya kilimo. Mimi niiombe sana Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ikiwa jeshi letu limewekeza kwenye ujenzi, ikiwa limewekeza mpaka kwenye petrol station ni kwa nini jeshi letu lisiwezeshwe liweze kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Taasisi za ASA, TARI, TOSCI ili jeshi letu liweze kuzalisha mbegu, ili tuwe na uhakika wa mbegu tunazitumia, mbegu ambazo tunatumia kwa ajili ya mazao ya chakula chetu ni mbegu ambazo hazina athari zozote kwa kizazi cha leo na kizazi cha kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kwa unyenyekevu mkubwa Serikali iweke jitihada za makusudi kabisa kuwezesha jeshi letu katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu na Mama yangu mpendwa Dkt. Stergomena Tax kwa kazi kubwa anayoifanya na kuendelea kuing’arisha Tanzania kwa kuwa moja ya nchi ambazo zinaongea kwa vitendo jitihada ya kuhakikisha tunaongeza ushiriki wa wanawake katika eneo hili la mahusiano ya Kimataifa katika ulinzi na usalama wa mataifa mbalimbali duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nalipongeza jeshi na viongozi wote wakiongozwa na CDF, lakini narejea tena naomba sana Serikali itafute fedha za dharura kuwezesha jeshi letu kuweza kujiandaa kudhibiti na kukabiliana na electronic warfare (vita za kidijitali), lakini pia wakati umefika jeshi liwezeshwe ili liingie katika kuzalisha mbegu ili kulinda ulinzi na usalama wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja na ahsante. (Makofi)