Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja na niwaombe Wabunge wenzangu wote tuunge mkono hoja ya Wizara yetu hii muhimu kwa usalama wa nchi yetu, sote tunalala na tunaishi kwa amani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana nilisimama hapa Mheshimiwa Waziri, nikamwambia hivi Kikosi Namba 191 cha kule Kazimzumbwi, Kisarawe walifika katika Ofisi ya Serikali ya Kijiji kwa ajili ya kuomba eneo lenye mita 202 na kwa sababu tunafahamu jeshi na tunafahamu kwamba ardhi ni mali ya umma ambaye msimamizi wake mkuu ni Rais, sisi tukasema sawa kabisa walete barua ama maombi ya eneo hilo la mita 200.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuwakubalia na kuwaletea barua wakati wanakuja kupima hizo mita 202, wakaenda zaidi wakachukua zaidi ya mita 202 na hapo ndipo sintomfahamu ilipoanza kati ya Wananchi wa Kazimzumbwi pamoja na Jeshi Kikosi Namba 191 kule Kisarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikamwambia Mheshimiwa Waziri kwamba baada ya ile mivutano ikafika mahali tukakubaliana mtatulipa fidia, lakini tangu mwaka 2011 na leo tunazungumza mwaka 2024 fidia hiyo takribani miaka 13 bado hamjatulipa. Mheshimiwa Waziri nitaomba utakapokuwa unakuja kujibu hapa katika shilingi bilioni 11 ulizozisema katika hotuba yako, Kisarawe Kazimzumbwi na kule Tondoroni tupo mahali gani au tuna kiasi gani za kulipiwa fidia ya maeneo yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya sisi kuridhia kabisa mchukue hili eneo kwa sababu tunafahamu umuhimu wa jeshi, tunafahamu kazi ya jeshi, kilichofuata ni kwamba kuna ambush, mnatukataza tusiendeleze, kujenga, kulima mnatukataza na mmeweka pale mabango kwamba hili ni eneo la jeshi huruhusiwi kufanya kitu chochote. Kama hivyo ndivyo, tunaomba mtuambie fidia yetu mnatupatia na mtatupatia lini? Mheshimiwa Waziri mimi nitakuomba kama nimetangulia kusema tunaunga mkono bajeti yako na Wabunge wote wa Bunge hili tunaomba tuunge mkono kwa uzito wa Wizara hii, lakini nikuomba sana mara baada ya Bunge hili, tunakuomba uje Kisarawe, uzungumze na wananchi wa Tondoroni pamoja na wananchi wa Kazimzumbwi. Tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho kabisa Mheshimiwa Waziri mimi nitakuomba ukija kujibu uje utuambie kwa sababu watu wa kutoka Wizarani kwako walivyofika wao wakasema wanafanya utambuzi, sisi hatuelewi utambuzi ni kitu gani, sisi tunaelewa tathmini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kufidiwa maeneo yetu tunachokijua sisi tunatakiwa kufanyiwa tathmini na sio utambuzi kwa sababu hatujapigwa picha na wala wale wananchi hawajajaza fomu wale wananchi. Sasa utakapokuja kutoa majibu hapa utuelezee kwamba huo utambuzi ndiyo tathmini na tutaenda kulipwa kwa minajili ipi ili hali fomu hatujajaza na wala picha hatujapigwa, tunaenda kulipwaje lipwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, atakapokuja kujibu Mheshimiwa Waziri anaomba atuambie shilingi bilioni 11 ni kiasi gani inaenda kwa wananchi wa Kisarawe, Kata ya Kazimzumbwi, Kijiji cha Kazimzubwi pamoja na Kijiji cha Tondoroni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nipende sana kumpongeza sana tena sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia nakupongeza wewe Mheshimiwa Waziri ninyi ni wanawake na nusu. Mnafanya kazi kubwa sana wamama ninyi, Taifa letu lipo limetulia kabisa, nchi yetu ipo imetulia kabisa chini ya wanawake mahiri na madhubuti. Kwa hiyo mimi nipende kuwapongeza sana kwani ulinzi wa nchi yetu upo imara. Kwa hiyo, nitaomba sana utakapokuja hapa utupatie majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja na ahsnate sana. (Makofi)