Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika Wizara yetu ya Ulinzi na JKT.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini napenda kumpongeza Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na Katibu Mkuu, lakini kipekee niwapongeze Mkuu wa Majeshi Jenerali wetu Jacob Mkunda, lakini nimpongeze Mnadhimu Mkuu, Jenerali Salumu Othman kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Kwa kweli nchi yetu ipo katika mikono salama, tumekaa kwa amani kwa sababu ya watu hawa pamoja na Wakuu wa Kamandi wote, Maofisa na Maaskari, tunatambua mchango wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba nianze kwa kulipongeza jeshi letu kwa kazi kubwa wanayofanya, tumekwenda tumeona miradi ya Chuo cha NDC wamejenga majengo mazuri sana kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza mambo yote ya kiuongozi lakini pamoja na usalama. Ni kazi nzuri na ningependa hata halmashauri zetu zingeenda zikaone jinsi ambavyo jesho letu linatumia vizuri fedha na linafanya kazi kwa weledi na umakini mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo ningependa jeshi letu liweze kufanya tafiti mbalimbali, wanafanya tafiti lakini wapewe fedha kwa ajili ya kuendelea kufanya tafiti nyingine mbalimbali za masuala ya magonjwa mbalimbali. Nchi nyingine magonjwa haya mbalimbali wanapewa jeshi/kitengo cha jeshi kufanya tafiti na kuja na outcome yake. (Makofi)
Kwa hiyo, ningependa kushauri jeshi letu liweze kupewa hiyo nafasi na kuona namna ambavyo wanaweza wakafanya kazi hii nzuri kwa weledi mkubwa ili kutoa matunda yanayotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia jeshi letu huko mbele nafikiria waweze kupewa kitengo cha utafiti wa vyakula vinavyoingia nchini lakini pia na mbegu na mazao ambayo tutazalisha nchini. Ninasema hivi kwa sababu tunaona athari ya vitu mbalimbali ambavyo vinakuja. Kwa hiyo, jeshi letu likipewa fedha kwa ajili na kufanyia kazi tafiti hizi wananchi tutakuwa salama kiafya na kila kitu na jeshi letu litafanya kazi kubwa. Tunaona JKT wamekuwa wakifanya kazi ya kilimo vizuri na kwa weledi mkubwa. Tunaomba wapewe fedha ili wafanye kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya Misri, jeshi linafanya kazi kubwa ya kilimo na linachangia zaidi ya 50% ya bajeti ya Serikali yao. Kwa hiyo, na sisi tukiiga mfano huo jeshi letu linaweza likafanya kazi kubwa sana ya kuzalisha na kulisha wananchi, pia kuchangia katika bajeti yetu kama watawezeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninawapongeza kwa kazi wanayofanya, lakini waongezewe bajeti ili waweze kufanya kazi kubwa zaidi na tunaweza tukauza hadi mazao nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni uwepo wa madeni. Majeshi yetu yamekuwa yanadai, taasisi mbalimbali za umma, halmashauri zetu hawalipi na wamekuwa wanafanya kwa kidogo wanachokipata wanafanya kwa weledi mkubwa sana. Ningependa Wizara msaidiane na taasisi zetu na mashirika yetu. Kwa mfano Kampuni Tanzu ya Mzinga inadai zaidi shilingi bilioni 1.9 kwa halmashauri zetu. Kuna halmashauri karibu nne ambazo zinadaiwa ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze lakini na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba wawapelekee hawa wanajeshi wafanye kazi kubwa. Tunaongea hapa wametengeneza mabomu kwa ajili ya wanyama tembo lakini wanafanya kwa weledi mkubwa wangeweza kusaidia kama na fedha hizo zinaweza zikapatikana kwa wakati wakafanyia kazi. Kwa hiyo, hawa wanajeshi wanafanya kazi kubwa, Shirika la Nyumbu linafanya kazi kubwa ya kutengeneza vifaa vingi vya kiteknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba Serikali muwapelekee fedha ili waweze kuandaa vifaa, magari na vitu vyote ambavyo ni mazao ya kazi za jeshi ili waweze kufanya kwa weredi mkubwa kwa sababu kwa kweli ukienda pale unaona jinsi ambavyo wanajituma kwa moyo na wanafanya kazi. Ukiangalia thamani ya kitu wanachokitoa na fedha iliyotumika, unakuta kabisa ni tofauti ya ambavyo tunaona nje. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iyawezeshe haya majeshi yetu yaweze kufanya kazi yake kama inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna vifaa vinaagizwa kutoka nje; Jeshi linaagiza vifaa kutoka nje vinafika hapa, lakini vinatozwa kodi na vifaa hivi ni mazao ya Jeshi. Sasa kama ni mazao ya Jeshi, yanakaa pale bandarini, tunaomba wawatolee kodi au wawawekee kwenye bonded warehouse yakae pale. Kikubwa ni watoe hizi kodi kwa sababu hivi ni vifaa vyetu na mazao yetu ya kijeshi. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali iweze kuangalia na kuwasaidia, Jeshi letu liweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)