Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Simanjiro
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru wewe kwa kunipatia nafasi ya kuchangia mchana wa leo taarifa zote mbili. Pia, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa zawadi ya uhai hadi siku ya leo. Pia, kwa namna ya kipekee niwapongeze sana Waheshimiwa Mawaziri wote wawili Profesa Kitila Mkumbo na Daktari Mwigulu Lameck, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na wasaidizi wao kwa taarifa nzuri ambayo imewasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia, kutoa pole zangu za dhati na za wananchi wa Simanjiro kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Tatu wa nchi yetu, Afande Jenerali David Musuguri. Pia, kwa namna ya kipekee nieleze bayana kwamba, Taifa letu limempoteza kiongozi maarufu, mashuhuri, aliyejitoa, kwa ajili ya uhai wa Taifa lake na kusaidia kuliunda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, lakini pia, aliyetoa mchango mkubwa katika vita vya kumwondoa fascist Iddi Amin Dadaa katika ardhi ya Tanzania. Kwa hiyo, kwa minajili hiyo nitumie nafasi hii kuendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema na ampe pumziko lililo jema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba, baada ya ripoti na taarifa iliyotolewa na Waziri, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, amebainisha bayana juu ya sifa za aina ya miradi itakayopewa kipaumbele katika Mpango wetu wa Maendeleo wa 2025/2026. Pia, niseme dhahiri kabisa naungana naye kwamba, sifa za miradi hiyo ambayo ameitaja bayana kuwa, ni miradi ambayo itachochea ukuaji endelevu wa uchumi, miradi itakayozalisha ajira kwa ajili ya wananchi wetu, miradi itakayochochea kupunguza umaskini wa watu, miradi itakayoongeza uwezo wetu wa kiushindani na mwisho miradi itakayoimarisha utawala bora na utawala wa Sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumzia suala hili la utawala bora na utawala wa Sheria, ziko sifa ambazo hazibishaniwi miongoni mwa sifa nyingi alizonazo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi aliyeonesha uungwana wa hali ya juu na aliyeonesha kuwa ni kiongozi wa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ushahidi wake pamoja na mengi ni maamuzi aliyoyaonesha hivi karibuni, ambayo amesikia kilio cha wafugaji wa nchi hii na kuweza kuwaagiza Mawaziri wake wote wawili, Mheshimiwa Lukuvi na Mheshimiwa Profesa Paramagamba Kabudi, kwenda kumaliza suala la tatizo lililokuwepo Ngorongoro. Vilevile, kumtuma Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, alipokuja katika ziara ya Mikoa ya Kaskazini kutoa tamko juu ya usalama wa ardhi ya wafugaji kwamba, haitabadilishwa matumizi kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, kwa niaba ya wafugaji wa nchi hii na kwa niaba ya wafugaji na wananchi wa Simanjiro, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uungwana wake na vitendo vyake vya haki. Liko jambo moja ambalo ningetaka tena kushajihisha maneno haya niliyoyasema kwa kueleza uzoefu uliojidhihirisha katika siku za hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote ni mashahidi kwamba, Mwaka 2023 Mheshimiwa Rais aliunda Tume ya Rais, Haki Jinai, katika kuendeleza misingi ya utawala bora katika nchi yetu na taarifa hiyo ya Tume ya Haki Jinai ilikuja kupokelewa na yeye mwenyewe. Pia, baadaye akaiunda tena na kuiboresha tume hiyo kwa kuwapa magwiji wawili, Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Mheshimiwa Mkuchika, kuungana na timu hiyo, ili kuja na mapendekezo ya utekelezaji wa Taarifa ya Tume ya Haki Jinai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri katika kufanya hivyo, Mheshimiwa Rais, alisema yeye mwenyewe kwa kauli yake kwamba, amesukumwa na mambo mawili makubwa katika suala zima la kusimamia misingi ya utawala bora, kwamba, amesukumwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2025 na pia, amesukumwa na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, ninaongeza la tatu na hili liko bayana kwamba, sababu nyingine ya tatu ni kwa sababu, unaweza kuwa na ilani nzuri ya uchaguzi, unaweza kuwa na katiba nzuri ya nchi, lakini kama hakuna utashi wa kisiasa, hakuna litakaloweza kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba, sababu ya tatu ni Mheshimiwa Rais mwenyewe amesukumwa na utashi wake wa kisiasa wa kuwatendea haki Watanzania na ndio maana akaamua kuunda Tume hiyo ya Hakijinai. Vilevile akaamua kuunda Kamati ya Utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Hakijinai, wakati huo huo akafanya semina kwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Bunge lako Tukufu pia, lilikuwa ni miongoni mwa watu waliopata semina ya taarifa hiyo ya Haki Jinai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa ibara ya 5(1) ya Katiba yetu, inasema, “Shughuli zote za utendaji wa shughuli za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitatekelezwa na watumishi wa Serikali kwa niaba ya Rais”, hakuna mashaka kwamba, mtumishi yeyote wa umma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anapofanya shughuli za utendaji, anafanya kazi hizo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais. Hata hivyo, kitendo kilichotokea hivi karibuni katika Mkoa wangu wa Manyara ni kitendo ambacho kinaonesha kwamba, baadhi ya viongozi wetu hawawezi kutii na kuheshimu maelezo ambayo wanapewa na uongozi wa juu wa nchi yetu. Sikutarajia baada ya kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi tu wananchi wapatao saba, ambao ni viongozi katika Wilaya ya Simanjiro waliwekwa ndani kwa siku saba bila dhamana. Watu hawa ni viongozi wanne kutoka Kata ya Kitwai, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Kata hiyo, pamoja na viongozi wengine wa mila na madiwani wawili wastaafu. Vilevile, viongozi wa Kata ya Langai wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Langai Mheshimiwa Jackson Sipitieck, pamoja na viongozi wawili wa mila na kiongozi mmoja wa chama, waliwekwa ndani mahabusu kwa siku saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifanya mawasiliano na Waziri wa Mambo ya Ndani, namshukuru sana Mheshimiwa Engineer Masauni na nikafanya mawasiliano na Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Mchengerwa na wote walipokea simu, hadi usiku wa manane. Hata hivyo, mwishoni waliniambia kwamba, wanafungwa mikono kulielekeza Jeshi la polisi kutoa dhamana kwa wananchi hawa kwa sababu, wamewekwa ndani kwa amri ya Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Mkuu wa Mkoa, kwa masikitiko makubwa nazungumzia vitendo vilivyofanywa na nafasi kama niliyowahi kuwa nayo. Saa za Mkuu wa Mkoa mwisho ni 48 na kwa tukio lililotokea lenye sura ya jinai mbele yake na baada ya kutoa amri hiyo ya kumweka mtu ndani, anawajibika kwenda kwenye kituo cha polisi au mahakamani kuandika maelezo ya sababu zilizosababisha kumweka huyo raia ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha ni kwamba, wananchi hawa wamekaa mahabusu siku saba. Wakiwa ndani siku ya tano, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa Mkoa na Katibu wa Mkoa walikwenda kuwajulia hali na walipoomba wakutane nao, walimpigia simu Mkuu wa Mkoa na kuweka sauti na kumwambia, “Mkuu tumekuweka kwenye sauti, watu hawa tumewakuta, ni viongozi saba, viongozi wa jamii, viongozi wa chama na waheshimiwa madiwani.” Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa bila aibu, mbele ya wale ambao wametuhumiwa na wamekaa ndani siku tano, akatamka yeye mwenyewe kwa kinywa chake, “nimewaweka ndani, najua hawana makosa, lakini wataendelea kuozea hapo mpaka Mbunge wao atakapokuja kupiga magoti kwangu.” Kitendo hiki nisingepiga simu kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, wala nisingepiga simu kwa Waziri wa TAMISEMI, kama ningekuwa na mahusiano mazuri na Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi mmoja uliopita, baadhi ya Wabunge wa Mkoa wa Manyara tulikwenda kwenye mkutano mmoja pale Manyara, aliwasalimia Wabunge na akakataa mkono wangu na kukataa salamu zangu. Baada ya hapo nikasema si neno, siwezi kuendelea kulazimisha salamu. Hata hivyo, katika hili ambalo linahusu raia wangu, wananchi walioniweka madarakani na Rais Samia madarakani, nitaendelea kuwasilisha kilio hiki kwa wale ambao wanamwakilisha Mheshimiwa Rais, ambao ni Mawaziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alichokitamka na ambacho kilionekana kwenye mitandao ya simu na wale wananchi wakisikitika baada ya kutolewa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni kwamba, kitendo hicho hakiingii kwenye akili ya kiongozi yeyote. Hata hivyo, anasema mpaka nimpigie magoti. Nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba, nitapiga magoti Kanisani kwa Mungu wangu aliye hai, nitapiga magoti kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa Nchi yangu, akiniamuru fanya hiki. Hata hivyo, nataka nimpe taarifa, sitakaa nipige magoti kwa Queen Sendiga wala kwa Mkuu yeyote wa Mkoa katika Jamhuri ya Muungano kwa sababu, siyo nafasi yangu kujitweza kwa kiwango hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, tunapozungumzia misingi ya utawala bora, utawala wa Sheria, hakuna aliyepo juu ya Sheria. Hata kama Mkuu wa Mkoa ana maslahi yake na kumwandaa mgombea wa Simanjiro ambaye wala hana madhara kwangu, mimi siyo mtoto wa kufikia kwa chama hiki. Mimi siyo mtoto wa kufikia kwenye uraia wa nchi yangu, wala siyo mtoto wa kambo kwa mamlaka ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba, ifike mahali wanaopewa dhamana na Rais, wajiweke kwa namna ambayo wananchi wakiwaona, waone wamemwona Rais. Nilikuwa Mkuu wa Mkoa, miongoni mwa ma-DC wangu ni pamoja na Komredi Kassinge, huyu hapa, hatujawahi kumweka mtu ndani kwa masaa yoyote yale kwa miaka yangu minne, sijawahi kumweka mtu ndani.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Olesendeka, pole sana kwa kadhia uliyoipata. Nikuombe sasa uchangie maoni na ushauri.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, safi kabisa nakushukuru. Maoni yangu katika eneo la utawala bora ndio hayo. Naomba sasa niende katika eneo lingine ambalo ni sehemu ya Mpango wa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mashaka kwamba, Wilaya yangu ya Simanjiro inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinapaswa kupata msaada wa Serikali katika kipindi hiki na hasa baada ya mvua kubwa za mwaka 2023. Hivi leo nimepokea taarifa kwamba, Bwawa la Sukura limekauka, bwawa ambalo lilichimbwa tangu wakati wa Marehemu Sokoine na karibu kata mbili zinazotegemea bwawa hilo sasa mifugo itatawanyika. Ninamwomba Waziri Mwigulu na Waziri mwenye dhamana katika masuala ya mabwawa ya mifugo watenge fedha, kwa ajili ya dharura hiyo iliyojitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo pia korongo lililowaathiri sana wananchi wa Kata ya Shambarai, Mirerani, Endeamutu na Kata ya Naisinyai, ambalo jana watu wa Bonde pamoja na Mkuu wa Wilaya, Kopro Lulandala walikwenda kule, kwa ajili ya changamoto ambayo wananchi wanayo katika lile eneo. Ni rai yangu kwa wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tusaidieni kupata fedha, kwa ajili ya kunusuru kadhia hiyo ambayo imewakabili wananchi katika mvua zilizopita. Hii ni pamoja na barabara za Kata za Msitu wa Tembo na Kata ya Ngorika ambazo hivisasa hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho, ni muhimu sana tunapozungumzia habari ya maendeleo na ustawi wa wananchi, ipo miundombinu ambayo inatakiwa iangaliwe, na hasa katika Sekta ya Ufugaji. Tunapozungumzia ufugaji wa kisasa, ufugaji wenye tija, ng’ombe wenye nyama ya kutosha, ng’ombe wenye maziwa mengi ni lazima kuboresha miundombinu. Huwezi ukadai kuwa na fresian, jersey na Ayrshire katika mazingira ya nyanda kame, bila kuwa na mabwawa ya kumwagilia majani na kuotesha majani yatakayotumika na ile mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi pia, kutarajia kuwa na boran, simmental, Brahman, ng’ombe wa maziwa na nyama halafu ukategemea waweze kustawi katika ukanda ambao nyumbu, swala, pundamilia, nyati na tembo wanatoka katika hifadhi na kuleta aina ya kupe ambao wanaambukiza magonjwa ya anaplasmosis, East Coast fever, MC na malignant catarrhal fever and foot-and-mouth disease. Wakati umefika sasa mipango yetu ijielekeze kwenye uwekezaji wa kusaidia wafugaji kuwa na mbegu bora. Pia, ranchi zetu za NARCO zifanye kazi waliyopangiwa, ya kuwa na mifugo bora ambayo wananchi wataweza kuiga kutoka kwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda Kongwa leo, wale ng’ombe wote wa Wagogo ni wafupi. Ni wafupi kwa sababu, Kongwa haijatimiza wajibu wake wa kuwasaidia majirani kuwa na mifugo bora yenye nyama nyingi na maziwa mengi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza katika Bunge lako Tukufu, ahsante.