Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niwapongeze Mawaziri, Mheshimiwa Profesa. Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa kuwasilisha vyema hotuba zao za Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2025/2026. Katika mpango huo, Serikali imeainisha nia na mikakati ya kuboresha sekta mbalimbali za uchumi nchini ikilenga kuimarisha Sekta za Uzalishaji; Uchimbaji Madini, Nishati, Elimu, Biashara, Viwanda na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita kwenye kuishauri Serikali itekeleze kwa ufasaha mikakati yote iliyopangwa katika Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Nishati, Elimu, Viwanda na Biashara ili kuboresha uchumi wa Watanzania na Taifa kwa ujumla. Sekta za Uzalishaji za Kilimo, Mifugo na Uvuvi Nchini Tanzania zinahusisha zaidi ya nusu ya nguvu kazi ya Watanzania. Hivyo basi, ni vyema Mpango wa Maendeleo ulenge kwenye kutekeleza yale yote yaliyoainishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali Mpango uzingatie yafuatayo:-

(i) Kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao kwa kutumia mbinu bora za kilimo ufugaji na uvuvi.

(ii) Kuendelea kuboresha mifumo ya umwagiliaji na kuchimba mabwawa ya kunywesha mifugo na ya kufuga samaki.

(iii) Kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kwa kuanzisha viwanda vidogovidogo na kutengeneza vifungashio bora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

(iv) Kuzalisha mazao mengi ambayo yatakidhi uhitaji wa viwanda vya ndani na mengine kuingia katika soko la kimataifa.

(v) Kutafuta soko la uhakika kwa mazao yote ya kilimo na mifugo yanayozalishwa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yakitekelezwa kwa nidhamu, bila wasiwasi tutaboresha mapato ya wakulima, wafugaji, wavuvi na yale ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze sana Serikali kwa juhudi na uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati. Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ni wa kielelezo na umetatua changamoto ya upungufu wa umeme hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kwamba, kwenye mpango huu wa maendeleo, Serikali iwekeze kikamilifu kwenye maendeleo ya nishati mbadala yanayohusisha matumizi ya gesi asilia. Ni vyema mpango utekeleze miradi inayojikita kwenye matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme na matumizi ya nyumbani kwa kupikia na kuendesha mitambo kama magari, kwani nchi yetu ina akiba ya gesi ya futi za ujazo trilioni 57.54.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa usalama wa nchi yetu na kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, ni vyema kujiandaa na kutekeleza uwekezaji katika miradi ya nishati mbadala na endelevu itakayotumia nishati ya jua na joto ardhi kuzalisha umeme. Nchi yetu ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 2,000 za umeme wa jua na joto ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wetu, naishauri Serikali ijikite kuisaidia Sekta ya Elimu kwenye kutekeleza mitaala mipya ambayo inajikita kwenye kutoa elimu yenye ujuzi ambao utawawezesha vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari waweze kujitegemea na kuwa na manufaa kwa Taifa baada ya kuhitimu. Kwa upande wa sekondari, ni muhimu Taifa lifanye mageuzi ya haraka kwenye utekelezaji, ili tusiwe na matabaka ya wasomi. Hivyo basi, Mpango wa Maendeleo ujikite kwenye uwekezaji katika miundombinu ya shule kwa kujenga madarasa, maabara na kutoa vitabu. Vilevile Serikali itoe ajira kwa walimu ili kukabiliana na upungufu mkubwa uliopo katika shule za msingi na sekondari zilizomo vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Biashara na Viwanda ni vyema mpango ukalenga kwenye kuisaidia nchi iwe na viwanda vingi ambavyo vitatusaidia kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya Watanzania na ziada kuuzwa nje. Kwa mfano, ni vyema kuweka mazingira rafiki ya kikodi kwenye viwanda vya ndani ili waweze kuzalisha kwa tija na baadaye kuuza kwa wingi na kutusaidia kuboresha pato la Taifa. Kwenye ziara za Kibunge tulizofanya kwa kuvitembelea viwanda mbalimbali hapa nchini, kumekuwepo na kilio kinachofanana cha kodi ambazo siyo rafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.