Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayotufanyia Watanzania kupitia Serikali yake ya Awamu ya Sita. Nampongeza kwa maamuzi yake ya kuunda hii Wizara ya Mipango na Uwekezaji, hii inaonesha upendo na maono makubwa ya Mheshmiwa Rais kwa Taifa lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara hii chini ya Waziri wake, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na watendaji wote wa Wizara hiyo kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii. Nitazungumzia kuhusu mapitio ya utekelezaji wa mpango na hapa ninazungumzia utekelezaji wa vipaumbele vya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, yaani 2023/2024 na pia, robo ya 2024/2025 na hapa nitazungumzia utekelezaji wa programu na miradi ya kimkakati ya kisekta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijikite kwenye suala la utawala bora na utawala wa sheria. Kwenye mipango ya nyuma imeendelea kuimarisha mifumo ya utawala bora na utawala wa sheria kwani sio ubishi, mifumo hii inatakiwa kuendelea kuimarishwa. Nimejaribu kupitia mpango huu wa 2025/2026 sijaona kabisa sekta hii ya utawala bora ikijadiliwa, imenishtua. Hakuna ubishi kabisa kwamba rasilimali watu ndiyo rasilimali inayotegemewa na rasilimali zote kwa kuwa, rasilimali hizo haziwezi kujiendesha bila ya usimamizi bora wa rasilimali watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mpango uweze kufanikiwa lazima kuwepo na rasilimali watu, hivyo basi mpango huu wa Mwaka wa Fedha 2025/2026, lazima useme bayana kwamba, awamu hii imepanga kufanya nini katika kuimarisha mfumo wa utawala bora, mwisho wa siku rasilimali watu iweze kusimamia vyema miradi na programu za kimkakati na kisekta na, ili iweze kusababisha Serikali iweze kufikia dhamira ya maisha bora kwa wote, kama iliyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025. Ninaendelea kuipongeza Serikali, pamoja na kuimarisha mifumo ya utawala bora pia, imeshughulikia kwa kiwango kikubwa suala la maslahi ya watumishi, hususani wa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwakilishi wa wafanyakazi nimeweza kuzifikia halmashauri 184 za Tanzania Bara na kuzungumza na watumishi wa halmashauri hizo. Wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uboreshaji wa maslahi mbalimbali ya kiutumishi, lakini wana changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba nizungumzie changamoto kubwa ya makazi kwa watumishi. Makazi bora kwa watumishi imeendelea kuwa tatizo kubwa hasa kwa halmashauri zilizopo pembezoni ambazo pia, zimehamisha makazi ya awali kwenda kwenye makazi mapya ya sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile makazi kwa mtumishi yeyote ni usalama na ni heshima, ninashauri badala ya kujenga nyumba kubwa na chache za Wakuu wa Idara, Taasisi na Halmashauri, zijengwe nyumba hata za vyumba viwili za kutosha, ili ikiwezekana watumishi wengi wapate makazi na ikiwezekana watumishi watakaoishi kwenye nyumba hizo wachangie kiasi kidogo cha pesa, kwa ajili ya ukarabati mdogo mdogo utakaojitokeza. Ninashauri mpango uje na mkakati wa muda mfupi, wa kati na mrefu wa kutatua tatizo hili kubwa na sugu la kukosekana kwa makazi ya watumishi. Ninashauri Serikali ishirikiane na wadau mbalimbali pamoja na taasisi na mashirika mbalimbali, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.