Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Innocent Sebba Bilakwate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyerwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mungu kunijalia afya na nguvu za kuendelea kuwatumikia wananchi wangu wa Kyerwa na kuwepo katika Bunge hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi. Ninampongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa jinsi alivyomwaga pesa nyingi kwa wananchi na kwa msimamo wake wa kutowasikiliza wasiotutakia mema; walipiga kelele za kuzuia DP World, ujasiri na uimara wake umeanza kuleta neema kupitia uwekezaji kwa Bandari ya Dar es Salaam. Mungu aendelee kumlinda na kumpa maono zaidi mama yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu na wasaidizi wake kwa kazi kubwa na nzuri ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha. Ndiyo maana tunaona kila kona ya nchi yetu miradi inaendelea kwa kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Mipango, Profesa Kitila Mkumbo, kwa mpango mzuri wa kuisogeza Tanzania mbele. Ushauri wangu ni, pamoja na miradi mingi iliyopelekwa kwa wananchi bado haijakamilika. Ninaishauri Serikali, pamoja na mipango mizuri Serikali iweke nguvu kubwa kwenye miradi ambayo haijakamilika ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo barabara nyingi, miradi mingi ya maji haijakamilika, miradi hii ikikamilika italeta unafuu wa maisha kwa wananchi kwa kupunguza gharama za maisha, lakini pia, kwa kuchukua muda mrefu inaiingiza Serikali kwenye gharama za kupigwa faini za kuwacheleweshea wakandarasi malipo. Miradi hii ikikamilika kwa wakati itawapatia huduma wananchi na unafuu wa maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi. Naipongeza Serikali kwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa kuboresha kilimo, mifugo na uvuvi, ninaamini tukiamua kuongeza nguvu kwenye sekta hizi tunaweza kuongeza fedha nyingi za kigeni maana mazao haya yanayotokana na kilimo, mifugo na uvuvi yanahitajika sana nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunayo mazao ya kimkakati na zao la kahawa likiwa mojawapo ya mazao hayo, ambapo tayari tumeshapata soko la uhakika katika nchi ya China. Hili ni soko kubwa na la uhakika, tukilitumia vizuri tutainua Pato la Taifa na la mwananchi mmoja mmoja, lakini kilimo hiki, ili kiwe na tija ni lazima Serikali iongeze utafiti kwenye mazao haya ya kimkakati, tupate mbegu bora na kupata uzalishaji mkubwa. Mfano, pamoja na zao la kahawa kuanza kupata bei nzuri na soko la uhakika, zao hili limeanza kushambuliwa na ugonjwa wa mnyauko na wadudu wanaokula majani ya kahawa mpaka inakauka na hapa Serikali ituambie imejipangaje kukabiliana na ugonjwa huu unaoshambulia kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ya kuinua uchumi. Ninaishauri Wizara ya Mipango kuweka nguvu kwenye matumizi ya gesi majumbani na kwenye magari. Wataalam wengi wanasema matumizi ya gesi ni nafuu kuliko umeme na mafuta. Mungu ametujalia neema hii, sasa ni wakati wa kuitumia, ili kuongeza pato la Taifa na itapunguza gharama za maisha kwa wananchi na uharibifu wa mazingira ambao unaendelea kuwa mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchuchuma na Liganga. Miradi hii imekuwa ikiongelewa. Naishauri Serikali ifike sehemu ya kufanya maamuzi magumu, kama uamuzi uliofanyika kwenye Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere na Mradi wa SGR, ili tuweze kufikia hitimisho la miradi hii ambayo imekuwa Wimbo wa Taifa. Ninashindwa kuelewa shida iko wapi na nini kinakwamisha. Waziri atueleze kama kuna kizuizi katika ulimwengu wa roho tuiteni watumishi wa Mungu ili tumkemee yeye azuiaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ulinzi wa miradi yetu. Naishauri Serikali, haya mafanikio tunayoyapata kwa miradi yetu ya kimkakati, kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR na Bomba la Gesi hapa tunatangaza vita ya kiuchumi. Lazima kwenye mipango yetu tuweke mkakati wa kuilinda dhidi ya hujuma yoyote inayoweza kutokea kwa maadui wa ndani na maadui wa nje maana hii ni vita ya kiuchumi. Maendeleo ni vita, wako maadui zetu wasingependa waone tunafanikiwa kwa hiyo, katika hili Serikali ni lazima ijipange kukabiliana kuhakikisha miradi yetu iko salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja zote na ninaomba kuwasilisha. Ahsante.