Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa ufanisi mkubwa sana ambao unalenga kuchochea uchumi shindani na shirikishi. Kwa rai hiyo hiyo, naomba nitumie fursa hii kumpongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, wote kwa kazi nzuri wanazozifanya za kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Nishati tunaongozwa na kiongozi mchapakazi, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati. Tunaendelea kumpongeza kwa kuhakikisha Sekta ya Nishati inaendelea kuchangia katika uchumi wa Taifa letu na kutupatia utulivu ambao tunao hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze watoa hoja, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kazi nzuri wanazozifanya katika Wizara zao za Fedha na Mipango. Mtakubaliana na mimi kwamba, wanafanya kazi nzuri sana katika kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sekta wezeshi, lengo la mpango ni kuhakikisha Sekta ya Nishati inachangia katika ukuaji wa biashara, viwanda pamoja na ukuaji wa uchumi na shughuli nyingine za jamii. Kwa kipindi chote cha utekelezaji wa mpango, Sekta ya Nishati imejikita kuhakikisha tunaboresha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme. Tunaboresha misingi ya kiuchumi katika Sekta ya Mafuta na Gesi, vilevile tunaendelea kuboresha mazingira wezeshi ya kuhusisha sekta binafsi katika sekta hii muhimu ya nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewasikia Waheshimiwa Wabunge juu ya michango yao kwenye vyanzo vya uzalishaji wa umeme. Nimewasikia wakitoa mawazo kwamba, inabidi tuboreshe vyanzo zaidi, ili kuboresha upatikanaji wa umeme katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaanza utekelezaji wa mpango huu 2021, tulikuwa tuna megawatt 1,571 ambazo zilikuwa zinachangia katika gridi yetu ya Taifa. Leo ambapo tunakwenda kumaliza Bwawa la Mwalimu Nyerere tunakwenda kuwa na uwezo wa takribani megawatt 3,914. Ni kazi kubwa sana imefanyika kuweza kufikia megawatt hizi ambazo tunazo leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewaelewa Waheshimiwa Wabunge katika azma yao ya kuhakikisha tunaendelea kuwa na vyanzo vingine vya uzalishaji. Pia, Serikali tayari tuna mipango hiyo ambayo inatekelezeka na tunayo mipango ya mbeleni. Pamoja na Mradi mkubwa wa Julius Nyerere ambao Waheshimiwa Wabunge wametoa pongezi juu ya utekelezaji wake, kwa sasa hivi tuna mitambo minne inayozalisha megawatt 940.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi mingine ya uzalishaji ambayo pia, inaendelea. Tunao Mradi wa Malagarasi kule Kigoma, ambao ukikamilika utakwenda kuzalisha takribani megawatt 49.5. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, alitupatia fedha dola za Kimarekani milioni 144, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu na mkandarasi yuko site.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mradi wa Malagarasi, tunao Mradi wa Kakono kule Kagera ambao ukikamilika utakwenda kuzalisha takribani megawatt 87.8. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais alitupatia fedha takribani Dola za Kimarekani milioni 161.47, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hii mitatu tunao mradi wa uzalishaji wa umeme kwa jua Kishapu ambao unaenda kuzalisha megawatt 150, na tumeanza awamu ya kwanza ya megawatt 50 na tunaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais alitupatia fedha takribani Euro milioni 130.7 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Waheshimiwa Wabunge nataka kuwahakikishia kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayo azma na nia ya kuhakikisha tunaendelea kuwa na miradi ya uzalishaji na ninyi wote mmeona miradi ambayo yote wakandarasi wako site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hiyo tunayo azma ya kuendeleza miradi mingine hapo mbele, tunao mradi wa Ruhuji ambao kama utatekelezwa utaenda kuzalisha takribani megawatt 358, Rumakali megawatt 222, pia tunao mradi wa Somanga - Fungu ambao utaenda kuzalisha takribani megawatt 300, vilevile tuna mraadi wa Mtwara gas fire ambao utaenda kuzalisha takribani megawatt 330. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hiyo nimewasikia Waheshimiwa Wabunge wakionesha umuhimu wa Serikali kuanza uzalishaji wa umeme kupitia rasilimali yetu ya jotoardhi, nami nakubaliana na ninyi Waheshimiwa Wabunge. Rasilimali hii ya jotoardhi ipo katika ukanda wa nchi ambazo zinapitiwa na Bonde la Ufa, katika nchi hizi zote kama rasilimali hizi zitatumika katika kuzalisha umeme zitaweza kuzalisha umeme wa takribani megawatt 40,000. Tanzania pekee yake tunakadiria uwezo wa kuzalisha takribani megawatt 5000, kwa hiyo, ninakubaliana na ninyi ipo azma ya Serikali kuanza kuzalisha umeme kwa jotoardhi. Kinachotupa nia na faraja na moyo ni kwamba katika miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita tumepiga hatua kuelekea uzalishaji wa umeme kwa kutumia jotoardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, tumewawezesha kwa uwezo - training mbalimbali wataalam wetu ili waweze kubobea katika jambo hili ambalo ni jipya kwetu. Pili, tulifanya tafiti za awali za kubaini maeneo ambayo yana rasilimali yetu hii, tulibaini maeneo matano ikiwemo Lutoi, Natron, Mbozi, Songwe pamoja na Kyegombaka. Kwa hiyo, baada ya kubaini maeneo yale ilitakiwa sasa twende ku-confirm resource kuhakikisha tuna rasilimali kiasi gani kwenye kila eneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa Rais ametupatia fedha na tumeshamweka mshauri mwelekezi (KenGen) ambaye sasa yuko site kwa ajili ya kufanya zoezi la confirmation of resource. Pamoja na hiyo tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais ametupatia fedha bilioni 15.7 kwa ajili ya kununua mtambo wa uchorongaji kwa ajili ya zoezi hilo. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwa kipindi hiki cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuelekea uzalishaji wa umeme kwa jotoardhi hakika tumepiga hatua, tumewasikia Waheshimiwa Wabunge tutaendelea kusimamia kazi hii kwa weledi mkubwa sana chini ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ili kuonyesha kwamba tunaenda kule ambako ni matamanio ya ninyi Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kuendeleza zaidi vyanzo vya nishati jadidifu ili kupunguza utegemezi wa kiuchumi, lakini kuongeza usalama wa nishati, vilevile kuleta uendelevu wa kinishati ambao unachangia kiasi kikubwa sana katika kulinda mazingira na kwa kweli tupo kwenye njia salama sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi ya uzalishaji, nimewasikia Waheshimiwa Wabunge wakichangia kuhusiana na umuhimu wa Serikali kuwekeza zaidi katika miradi ya usafirishaji pamoja na usambazaji. Serikali inawekeza katika miradi mbalimbali ya power transmission, miradi ya msongo mkubwa wa umeme ambao utaweza kusaidia kuimarisha umeme katika maeneo mbalimbali, vilevile na miradi ya msongo mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miradi mingi na miradi ambayo ni ya ndani ya nchi na miradi ambayo itasababisha pia sisi kwenda katika mkondo wa umeme wa nchi jirani vilevile. Baadhi ya Wabunge wamechangia hapa, tunao mradi ambao utatu-connect kwenye south African power pool na nchi zaidi ya nchi nane, huo ni mradi ambao umeanza na mkandarasi yuko site na utajenga pia vituo vya kupooza umeme kuanzia Iringa, Mufindi, Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga. Kwa kweli ni mradi mkubwa sana ambao utaimarisha umeme hapa nchini, lakini utatufanya tu-connect na nchi nane za Ukanda wa Jangwa la Sahara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalojivunia ni mafanikio makubwa ambayo tumeweza ku-connect na East African Power Pool, kupitia mradi wetu wa njia ya kusafirisha umeme lakini tumejenga kituo pale Remuguru, Arusha ambacho kina-connect na kituo upande wa pili wa Kenya na sasa hivi tuna uwezo wa kutoa umeme na kuingiza umeme kutoka katika nchi 14 za ukanda wa Afrika Mashariki. Kwa kweli, pamoja na changamoto ambazo tunazo tumepiga hatua kubwa sana katika zoezi la usafirishaji wa umeme ndani ya nchi na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la usambazaji wa umeme nimewasikia Waheshimiwa Wabunge juu ya matamanio yenu kuhakikisha tunaendelea kuboresha miradi kwenye vitongoji. Katika Bunge hili mwaka 2021, Wabunge waliishauri Serikali kuweka mradi wa kupeleka umeme kwenye vijiji vyote, mwezi Machi, 2021 tulianza mradi huu. Mheshimiwa Rais alitoa fedha shilingi trilioni 1.573 kuhakikisha tunapeleka umeme vijiji vyote na hadi leo tumebakisha vijiji 78 tu. Kwa hiyo, azma ambayo tulikubaliana hapa katika mpango huu wa kupeleka umeme kwenye vijiji 4,071 Waheshimiwa Wabunge imetekelezeka na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutenga fedha kwa ajili ya jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tunaanza zoezi la vitongoji na kwa kweli Serikali haijapoa, tumeanza na mradi wa vitongoji 3,070 na saa hivi tunaweka mradi wa vitongoji 4,000, ni azma yetu kati ya miaka mitano mpaka saba tuweze kukamilisha vitongoji 32,000 ambavyo vimebakia. Kwa hiyo, ndugu zangu maendeleo ni hatua ni lazima yafanyike kwa awamu ili tuweze kufika huko, lakini tulikotoka siko ambako tuko sasa hivi, tumepiga hatua kubwa na Serikali imejizatiti kuendelea kupeleka umeme kwenye vitongoji ili wananchi wetu waweze kuboresha shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamechangia katika Sekta ya Mafuta na Gesi, kwa kweli nimewasikia juu ya matamanio yao ya kuona mradi wetu wa LNG unaendelea na ndiyo matamanio ya Serikali. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge waendelee kusubiri nia ya Serikali ni kuona mradi huu unatekelezeka. Huu ni mradi ambao utazalisha takribani futi za ujazo trilioni 45. Kwa hiyo, tuendelee kusubiriana, tunaendelea kufanya kazi nzuri nataka niwahakikishie tuko sehemu sahihi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamechangia juu ya miradi ya mafuta na gesi katika mkondo wa juu, mkondo wa kati na mkondo wa chini, lakini nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge hapa wamesema pamoja na ugunduzi wa gesi takribani TCF 57 tunazalisha katika vitalu viwili tu vya Songosongo pamoja na Mnazi Bay. Nataka niwaambie, baada ya miaka 16 leo Serikali imetoa development license katika kitalu cha Ruvuma Ntorya na kitalu hiki kina jumla ya futi za ujazo trilioni 1.4. Kwa hiyo, baada ya miaka 16 Serikali ya Awamu ya Sita imepiga hatua kwa kutoa development license kwa ajili ya kitalu cha Ntorya, kwa hiyo kwa kweli tumepiga hatua, lakini baada ya miaka takribani 12 tunaenda kwenye duru la tano la kunadi vitalu ifikapo mwezi Machi mwakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia yetu ni kuhakikisha vitalu ambavyo tunavyo takribani 24, ambavyo 21 vipo katika Bahari Kuu na tatu vipo Lake Tanganyika, tunafanya matumizi mazuri ya rasilimali ambazo tunazo. Kwa hiyo, ninataka niwaondoe hofu Serikali ya Awamu ya Sita iko katika mchakato sahihi sana kuhakikisha tunatumia rasilimali zetu za mafuta na gesi kwa mstakabali wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio mengine Wabunge wengine wamesema hapa ni pamoja na Mradi wa EACOP, vilevile tunaendeleza utafiti katika kitalu chetu cha Eyasi, Wembere kwa hiyo kwa kweli mambo yanaendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamechangia juu ya umuhimu wa kutumia gesi asilia kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea. Nataka niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwamba mkakati huu tunao. Tunao mpango kabambe wa matumizi ya gesi ambao ni wa 2017 hadi 2046 na mpango huu umejikita katika kuwezesha viwanda hivi vya Petro-chemicals kwa ajili ya kutumia gesi asilia katika uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vina matumizi makubwa kwa hiyo suluhisho lake ni hii gesi ambayo tunategemea kuwa na mradi wa LNG na TPDC wamejipanga kutoa eneo pale kwa ajili ya kongani la viwanda ikiwemo viwanda hivi vya kuzalisha mbolea.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Malizia.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naamini Wizara ya Viwanda pamoja na Wizara ya Kilimo tutashirikiana kwa karibu kuhakikisha katika Mradi huu wa LNG, TPDC wanatenga eneo kwa ajili ya kongani la viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mafanikio haya ambayo tunayaona katika Sekta ya Nishati ni jitihada za Mheshimiwa Rais. Miradi hii inatekelezeka kwa sababu Mheshimiwa Rais anatafuta fedha za kutekeleza miradi hii, lakini inatekelezeka vizuri sana kwa sababu Mheshimiwa Waziri, Dkt. Dotto Mashaka Biteko anahakikisha miradi yote inatekelezeka kwa ufanisi na weledi mkubwa sana, tunaendelea kumwombea Mheshimiwa Rais afya njema ili tuweze kunufaika na matunda yake kama Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)