Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote ninapenda kuanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye anaendelea kutuwezesha kutimiza majukumu yetu ya kibinadamu. Ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa Mama msikivu, Mama ambaye anashaurika na kutufanyia mambo mengi sana na mpango thabiti wa maendeleo ya nchi yetu tunaweza kuona namna wasaidizi wake tunavyoendelea kumsaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nasi tuko pamoja na wenzetu kuhakikisha Mpango wa Maendeleo ya Taifa tunausimamia kwa thabiti, kwa sababu bila mawasiliano thabiti mambo yote haya tunayoyapanga huenda yasiende vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuongelea uhuru wa Vyombo vya Habari kwa sababu haya yote tunayoyafanya, tumekuwa tukijifunza kutoka kwa wenzetu walioendelea zaidi yetu, lakini na sisi pale tunapofanya kwa lengo la kuwafikishia wananchi wetu lazima Vyombo vya Habari vihusike. Vyombo vya Habari vimeendelea kuimarika nchini Tanzania na kwa namna ambavyo Dkt. Samia ameendelea kuongoza nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyombo vya Habari vimeweza kupata Bodi ya Ithibati ambayo lengo lake kubwa ni kuhakikisha taarifa zote zinazowafikia wananchi ziwe zenye maudhui rafiki na siyo za kubomoa maadili ya Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha Vyombo vya Habari tunaendelea kulinda uhuru wake tumepiga hatua kubwa sana, tumeweza kuvuka hatua 46 tokea mwaka 2023, Chombo chetu cha Habari kilikuwa cha 143 lakini mwaka 2024 tumeshika nafasi ya 97 kwa maana hiyo tumeweza kuvuka kwa asilimia kwa hatua 46 zaidi, maana yake tumepita nchi nyingi sana katika kuona kwamba tunatetea na kuishi Uhuru wa Vyombo vya Habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchumi wa kidigitali sisi kama Wizara ya Habari, Mawasiliano, Teknolojia ya Habari tumeweza kuhakikisha tunajenga miundombinu ya kutosha ili tunavyoingia sasa kwenye uchumi wa kidigitali tuweze kufanya kazi vizuri. Tuna mradi wa minara 758, Waheshimiwa Wabunge wote watakuwa mashahidi katika kila Jimbo tumeweza kufikisha minara mitatu na zaidi kwa lengo la kuona kwamba tunaboresha usikivu maeneo yote na tunaendelea kuiboresha huduma hii ya minara kadri ambavyo tunawezeshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika minara hii iko idadi ya minara ambayo inajengwa kwa ajili ya kuboresha kutoka teknolojia ya 2G na inakwenda kwenye teknolojia ya 3G hadi 4G, maana yake nini? 2G ni zile simu ndogo maarufu kama viswaswadu zamani tumekuwa tukivitumia kwa ajili tu ya kuongea voice, lakini tumeboresha minara mingi sasa iweze kutumia teknolojia ya 3G na 4G kwa maana ya kuruhusu data na hii ndiyo inayoendelea kutusogeza katika dunia ya ulimwengu wa kidigitali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nitoe taarifa katika hii minara 758 tayari minara zaidi ya 302 imewashwa. Tuko zaidi ya 40% minara imewashwa na tumeweza kuongeza usikivu maeneo mbalimbali. Kwa maeneo yale ambayo bado hatujayafikia ni ile minara zaidi ya 400 Waheshimiwa Wabunge niwaombe tuendelee kuwasiliana na ndiyo maana juzi tumeweza kugawa hicho kitabu ambacho kinatoa taarifa ya utekelezaji wa minara hii na kila Mbunge hapa inaonesha Jimboni kwake wapi mnara unajengwa. Kwa hiyo, kama kuna makosa ya kibinadamu yaliyofanywa na wataalam wetu tunawakaribisha ninyi mko hapa kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania huko nje, basi tuweze kuwasiliana tuweze kurekebishana kuona tunaujenga mnara eneo halisi lenye changamoto kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya hiyo minara 758 tuna minara mingine ambayo ipo kwenye mradi inajulikana kama rural connectivity, hii kazi yake ni kusogeza huduma kule pembezoni mwa miji kabisa nayo ni minara 636. Kati ya minara hii minara 621 ni maalum kwa ajili ya usikivu wa simu na minara 15 ni kwa ajili ya redio. Haya yote tumeyafanya kwa kuzingatia jiografia ya Tanzania maeneo ya mipakani tumeyazingatia kule mipakani kwa mfano kwa Mkoa wa Mbeya ukifika Kyela ama ukifika Tunduma kwa Mkoa wa Songwe unaona kuna mwingiliano wa mawasiliano, lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema huu ni wakati sasa Watanzania wanatakiwa kupata mawasiliano thabiti kutoka ndani ya nchi na siyo mwingiliano wa mawasiliano kutoka nchi jirani kwa sababu ya minara iliyopo kwenye mipaka yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote tunayafanya lengo ni kuhakikisha mpango huu wa Taifa ambao Waheshimiwa Wabunge wameujadili hapa na kutoa maoni yao ya kina na kuona Serikali tunaweza kuwajibika vizuri kuleta maendeleo kwa wananchi, mawasiliano haya ndiyo yatakayowezesha haya yote tunayoyafanya kwa sababu pia katika maagizo ya Mheshimiwa Rais tunakumbuka ametusisitiza wasaidizi wake wakati ananiapisha mimi, wakati anamwapisha Mheshimiwa Jerry Silaa lakini katika mikutano mbalimbali tuhakikishe mifumo inasomana, nasi tumeshafanya kazi sasa ni zaidi ya 99% na kufika Disemba tutazindua rasmi kuonesha kwamba mifumo ya makampuni mengi sasa yanaweza kusomana na kila kitu kinakwenda kidigitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhakikisha tunaimarisha namba jamii kwa maana ya kila Mtanzania sasa badala ya kumiliki ile namba ya NIDA ambayo inam-favor mtu kuanzia miaka 18 na kuendelea, sasa namba ya kijamii ni namba hiyo hiyo na NIDA, lakini sasa inaboreshwa kwa kuongezewa taarifa itaanzia mtoto anayezaliwa leo. Kwa hiyo, wananchi wote Watanzania wataweza kutambulika, kuanzia yule mwenye siku moja mpaka yule ambaye atakwenda siku yake ya kufariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende sasa kwenye suala la Artificial Intelligence (AI). Tuna kila sababu ya kujipongeza sana kuwa na kiongozi imara kama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweza kusimamia suala hili na kwa uongozi mahiri wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, kaka yangu Dkt. Nkundwe ameweza kufanya kazi nzuri sana. Ninakumbuka nilisafiri naye kwenda nchini Estonia tulikwenda kujifunza kule kuhusiana na akili umbwe na akaahidi kuja kuandaa kongamano kubwa ambalo litaibua vipaji na kuvitambua vipaji vingi vilivyopo nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa kwamba mwezi Oktoba, tarehe 13 mpaka 17 tulikuwa na kongamano kubwa sana pale Mwalimu Nyerere Convection Center na iliweza kuonyesha namna vijana wa kitanzania wako vizuri kwenye suala la artificial intelligence kwa maana ya akili umbwe. Tulianza kuwahusisha jamii ya wanawake ambao wanafanya biashara kidigitali na waliweza kuja pale na kuelezea manufaa makubwa sana wanayoyapata kupitia kufanya biashara kidigitali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuko hatua kubwa katika matumizi ya akili umbwe. Siku ya pili tuliweza kuwashirikisha vijana mbalimbali wa kike na wa kiume. Wao pia waliweza kuja kuonesha kazi mbalimbali wanazozifanya. Ni furaha iliyoje? Watoto kwenye level ya shule ya sekondari waliweza kuja na vifaa walivyovitengeneza na kuonesha namna ambavyo akili umbwe inaweza kufanya kazi. Hata nchi mbalimbali zilizokuja kushiriki kongamano lile hazikutarajia kama Tanzania tuna vijana wadogo level ya sekondari wanaweza kufanya mambo makubwa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ni ubunifu ambao unaendelea kusimamiwa na Dkt. Mkundwe na kuhakikisha kwamba Tanzania nasi hatubaki nyuma. Tunaendelea kuiweka sawa mifumo ya akili umbwe ili iendelee kuleta chachu katika maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia niseme kwamba katika kuona tunaendelea kuboresha mawasiliano nchini, tumeweza sasa kuwa na satellite kubwa ambayo kama nchi itakwenda kutuongezea heshima na kutusogeza zaidi katika dunia ya kidijiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanafanyika kwa kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameweza kuruhusu fedha nyingi zinaweza kutumika na miradi mingi inaendelea kufanyika. Haya yote yanawezekana, lakini kubwa na kwa sababu pia tuna Waziri anayesimamia vizuri, kaka yangu Mheshimiwa Jerry Silaa, anasimamia vizuri kila kitu kinakwenda kama ambavyo kimepangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongea haya yote sasa naomba kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge. Ninaendelea kuomba ushirikiano baina yenu na sisi Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Tunawategemea kwa sababu ninyi ndiyo taswira ya Taifa letu. Wanapoweza kuleta mrejesho wa mawasiliano katika maeneo yenu tunaendelea kuona wapi tuongeze nguvu na wapi tupeleke teknolojia ya juu zaidi, kwa sababu kwenye maeneo ambayo bado tunatumia 2G, lakini wananchi wake bado hawana simu hizi za kufuta na wao pia tunaamini siku moja wataweza kusogea na kutumia teknolojia ya 3G na 4G. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nakushukuru sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)