Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajadili mpango hapa Bungeni. Sisi watu wa afya kwa kweli tunaujadili kwa kujiamini kwa sababu tunaye jemedari wetu ambaye ni Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ni mtafutaji. Pia, tusisahau ndiye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye kwa uwekezaji mkubwa alioufanya kwenye kila sekta inatufanya Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi tukirudi Bunge la Januari tunakuja tukiwa tumeshinda vijiji kwa 100%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi afya kama unakumbuka Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alipohutubia Bunge kwa mara ya kwanza hapa, alipofika eneo la afya hasa kwenye eneo la mama na mtoto aliongea kwa kurudia na kusisitiza. Alipoongea hakuishia hapo aliweka shilingi trilioni 6.7 kwenye Sekta ya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapinduzi makubwa yalitokea kwenye eneo hili la afya kutokana na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kutumbukiza shilingi trilioni 6.7; aliipokea hii nchi tukiwa na CT scan mbili tu kwenye hospitali za mikoa, lakini leo tunavyozungumza kila hospitali ya mkoa kwenye nchi hii imefungwa CT scan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa makadirio na maelekezo ya Shirika la Afya Duniani inatakiwa katika kila watu milioni moja pawepo na CT scan moja, lakini alichokifanya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya Tanzania badala ya kuwa na CT scan moja katika watu milioni moja, leo Tanzania hii kila CT scan moja inahudumia watu laki nane. Maana yake Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan amevunja ile rekodi ambayo ingetegemewa na Shirika la Afya Duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hospitali zetu za kanda zote zina MRI machine; hakuna hata hospitali moja ambayo haina. Rais wetu kutokana na uwekezaji mkubwa ambao ameuwekeza kwenye teknolojia, miundombinu, madawa na mambo mengine pamoja na elimu, leo kushuka kule chini, tuliposimama hapa tulitegemewa mwaka kesho tushushe vifo kutoka 556 mpaka 225 na ilitegemewa mwaka kesho, lakini kwa sababu ya uwekezaji huu mkubwa ambao Rais wetu amefanya kwenye Sekta ya Afya tumeshusha vifo mpaka 104. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba, kwa muda mfupi ambao Rais wetu amekaa hapa amepunguza vifo vya akina mama kwa 81.2%. Tumebakisha 18% ili kuweza kumaliza vifo vya akina mama moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan siyo hivyo tu, pia wakati anapokea nchi ilikuwa ukienda Ocean Road 90% ya Watanzania wanafika Ocean Road wakiwa tayari kansa ni zile za kungojea kufa. Maana yake kansa iko kwenye terminal stage, lakini kwa sababu ya uwekezaji huu mkubwa wa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan wa shilingi trilioni 6.7, leo ukienda Ocean Road 78% ya watu wanaokuja wanakuja na kansa katika stage za mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni nini? Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye eneo la kansa kwa kuweka resources kwenye infrastructure, teknolojia na mambo mengine amepunguza vifo kwenye eneo la kansa kwa 78%. Maana yake tulikuwa na 78% ya watu waliokuwa wafe kwa kansa, lakini kwa sababu ya kazi ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan leo watu hao wako na familia zao wanaishi na wanaendelea na maisha ya kulijenga Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan akiingia madarakani kulikuwa na tiba dawa ambayo ukiwekewa inasaidia kinga zako wewe mwenyewe ziweze kwenda kuua zile seli za kansa, yaani mwili wako unatengeneza chembechembe zinazokwenda kuondoa kansa mwilini. Ilikuwa tukitaka kupata tiba hiyo ni lazima uende Ulaya au India.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunavyozungumza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaleta Tanzania hiyo teknolojia. Leo Watanzania hawaendi India na walikuwa wakienda India wanatumia shilingi milioni 100 kutibiwa; leo tunatumia shilingi milioni 10 na Watanzania wanapona hapa hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa pia ukipata kansa labda iko pembeni ya ini kwenye organ iliyoko karibu na ini; ukipigwa mionzi unapiga mpaka na ini ambalo halihusiki. Ndani ya nchi hatukuwa na teknolojia ambayo ingesaidia kupiga mionzi tu eneo lile lenye tatizo na mtu akaondoka maeneo mengine hayajapata madhara. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaleta teknolojia hiyo na sasa Watanzania wanapigwa hapa nchini Tanzania. Ilikuwa wanafuata hiyo teknolojia nje kwa zaidi ya shilingi milioni 90. Leo hapa Tanzania wanatibiwa kwa shilingi milioni 10 na wanabaki hapa hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais wetu anapokea nchi hatukuwa na PET/CT scan. Kuna mashine ambayo imeunganishwa PET scan na CT scan kwa pamoja; mashine hiyo ina uwezo wa kugundua kansa ambayo itatokea miaka 10 ijayo. Maana yake ina uwezo wa kuangalia uvimbe na kwenda kwenye seli yako inaangalia kama kuna dalili za kuanza kansa unatibiwa mapema kabla ya kansa kuwa kansa kamili. Hatukuwa na teknolojia hiyo, ukitaka teknolojia hiyo ilitakiwa uende Ulaya au sehemu nyingine. Leo ndani ya Tanzania hii teknolojia hiyo ipo, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuletea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaambiwa mpaka jana watu waliotoka nje ya Tanzania kuja kutibiwa kwa maana ya Kenya, Rwanda, Zambia, Comoro na sehemu nyingine kwa mwaka huu wamefika ni 10,931. Maana yake ni nini? Uwekezaji aliouwekeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Sekta ya Afya haujatatua tu matatizo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake hawa watu 10,000 walitakiwa watoke Comoro, Zambia na Rwanda waende Ulaya na India. Leo wanakuja karibu hapa Tanzania. Maana yake uwekezaji aliouwekeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Sekta ya Afya umefika mahali ukajaa halafu ukasaidia na majirani zake. Maana yake ameleta solution ambayo imevuka mipaka ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo badala ya watu kulipa nauli kubwa kwenda India leo wamekuja, solution zao ziko Tanzania. Ninyi ni mashuhuda mliona Spika wa Bunge la Comoro alikuja hapa na juzi walimuona Waziri wa Ulinzi wa Comoro alikuja hapa na wote wanakuja kwa ajili ya kuingia mikataba watu wao watibiwe Tanzania. Maana yake kazi ya huyu Rais ni kubwa kiasi kwamba siyo tu kwamba inaleta suluhu Tanzania bali inaleta suluhu na nje ya mipaka ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie, tofauti ya Tanzania kwenye Sekta ya Afya na nchi ambazo zimetuzunguka kama Kenya ni moja tu, sisi public sector ina nguvu sana. Sisi wakikushindwa private sector unaletwa Serikalini unakuja kusaidiwa.
(Hapa kengele ya kwanza ililia)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda majirani zetu private sector ndiyo ina nguvu kuliko public sector. Huyo ndiye Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye tunataka kusema tunaondoka kwenye Bunge hili zawadi ambayo tunatakiwa kumpa tukienda, turudi na 100% ya vijiji Chama Cha Mapinduzi tumeshinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan huyu, ninyi Wabunge ni mashahidi haijawahi tokea kwa wakati mmoja zikagawanywa ambulance 727. Tumeshindwa kumaliza ambulance. Mpaka jana Mheshimiwa Mzee Lukuvi hapa ndiyo alichukua ambulance yake, bado hatujamaliza, zinaendelea kugawanywa. Huyo ndiye Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tulikwenda nae Marekani wakati Rais wa Marekani akikutana na Marais wa Afrika na Marekani walitaka wajenge kituo kimoja cha kansa cha umahiri kwa Afrika kwa ajili ya nchi zote za Afrika. Walikuwepo Marais wengine lakini jinsi ambavyo Rais wetu anajua kucheza tuliibuka kidedea na kituo hicho kinajengwa Tanzania na kinajengwa hapa Dodoma; tayari ujenzi umeanza na mkitaka kutembelea nendeni Benjamin Mkapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mashine ambayo inaitwa proton therapy yenye thamani ya shilingi bilioni 178 na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshakubaliwa na inakuja ndani ya Tanzania kutibu Watanzania na kwa Afrika tutakuwa ni nchi ya kwanza kuwa nayo. Maana yake Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anapozungumzia Royal Tour ya utalii wa kuangalia wanyama, anaupiga mwingi tena kwenye tour ya utalii wa tiba ndani ya Tanzania. Anaenda kuigeuza Tanzania iwe ni hub ya Afrika kwa maana ya eneo la tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaweza kutokea uvimbe chini kwenye uvungu/sakafu ya ubongo; ilikuwa ukipata uvimbe kama huo inabidi upelekwe India au Ulaya, lakini alipoingia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta mashine na leo tukitaka kutoa uvimbe chini ya uvungu wa ubongo wako tunaingia tu kwenye pua tunakutoa unanyanyuka kwenda kukuta familia yako unaanza kuongoza Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa mtu akipata stroke inabidi tukufungue kichwa kizima ili tukuhudumie na tufungue fuvu lote, lakini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia amenunua mashine, sasa tunaenda kwenye mshipa mkubwa mguuni halafu tunatembea tunaenda kichwani kwako tunakutibu tunakwambia, rudi na ukaseme Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe umeona Tanzania tumekuwa tuna watu wengi wenye vibiongo. Unazaliwa mgongo umepinda unakuwa namna hiyo hiyo na unaishi maisha yako namna hiyo. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amenunua microscope maalum yenye thamani ya shilingi bilioni 21 imeunganishwa kwenye mashine nyingine. Ukizaa mtoto mwenye kibiongo unakuja Muhimbili kwa hisani ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tunakunyoosha unakuwa kama binadamu mwingine yeyote. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaenda kumalizia kwa kusema, ninyi wote mnajua na wengine mko hapa, ugonjwa wa sickle cell (seli mundu), ilikuwa ukipata seli mundu inakuwa ni ugonjwa ambao utaishi maisha yako yote. Ni ugonjwa ambao huwezi kufanya kazi. Wengi hawapitishi umri wa miaka 48, lakini Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, siyo tu amenunua vifaa, lakini ametoa fungu kwa ajili ya kuwatibu watoto bure. Ndani ya Tanzania hii haijawahi tokea ukimzaa mtoto mwenye seli mundu anatibiwa ndani ya Tanzania na anapona na anaishi kama binadamu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu kwenye tiba hii tumekuwa tukitumia uroto, maana yake tunatumia stem cell, tunaingia tunaondoa zako tunachukua za ndugu yako halafu tunaingiza zile ambazo hazina, halafu unaendelea, amesema twende kwenye gene therapy. Maana yake hata kama unaumwa, sasa tunakuja na teknolojia ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameanza kututayarishia ambayo sasa tunaenda kule kwenye gene zako...
MWENYEKITI: Mheshimiwa, malizia.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: ... ile sehemu ambayo inasababisha itokee hiyo sickle cell inaenda inaondolewa halafu unanyanyuka unaendelea na shughuli zako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia, tunaye dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, ni jembe limeshika kasi. Nataka kuwaambia tutaenda kuwashangaza kwenye eneo la afya kwa sababu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yupo na niwahakikishie Wabunge wenzangu, haya ni makubwa. Hakuna sababu ya kumaliza Bunge kesho halafu tukaenda majimboni wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaondoka nikiwa ninajiamini. Waliochukua fomu kutokea vile vyama vingine wanagombea kwenye jimbo langu naenda kuwapokea wote wanarudi CCM halafu tunarudi na 100% ya ushindi na naomba sote tukafanye hilo. Tunyooshe mambo tumalize mambo mengine. (Makofi)