Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rombo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa fursa hii. Maua mengine ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanakuja kwenye elimu. Kwanza kabisa, naomba niunge mkono hoja. Vilevile, niwapongeze sana watoa hoja, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Kamati yetu ya Bunge na Wabunge wote ambao wamechangia katika hoja iliyombele yetu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajaribu kueleza kwenye elimu, lakini jambo ambalo limezungumzwa kwa namna moja ama nyingine ambalo linahusisha elimu, ujuzi na ajira, limezungumzwa kupitia Bodi ya Mikopo, mfumo wa elimu na kadhalika. Nitajaribu kulielezea kwa yale ambayo yanafanyika sasa hivi kwa ajili ya kutatua changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ingawaje elimu ni kitu muhimu. Unaweza ukahitaji elimu hata kama huhitaji ajira wala kujiajiri. Ukweli ni kwamba wengi wanaosoma, matarajio yao wakimaliza ni kupata ajira. Vijana tulionao ni wengi zaidi, watoto ni wengi zaidi. Huko tunakoenda, kweli tunavyoambiwa demographic dynamic yetu kama hatukujipanga vizuri badala ya idadi ya watu tulionao kuwa ni baraka itakuwa ni changamoto moja kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kabla sijaeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais na utekelezaji wake katika suala hili, tujue kwamba hapa duniani sasa hivi elimu na ujuzi ni kivutio, siyo cha uzalishaji mali tu katika nchi lakini cha kuvutia uwekezaji. Misamaha ya kodi sawa, miundombinu sawa, huduma za kiuchumi sawa, lakini wataalamu wanasema uwekezaji katika masuala ya teknolojia ya hali ya juu na uwekezaji unaoajiri vijana wengi unahitaji nchi ambayo vijana wake wamesoma vizuri, wana ujuzi mkubwa na hivyo wanaajirika kirahisi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni kweli changamoto zilizoelezwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa kwamba elimu yetu ikidhi matakwa hayo ya kuandaa vijana wetu kwenye ujuzi ni jambo muhimu sana kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, tunakumbuka Mheshimiwa Rais wetu alivyokuja kuhutubia Bunge hapa tarehe 22 Aprili, 2021, takribani mwezi mmoja na kitu tu tangu aapishwe kuwa Rais wetu. Katika ahadi alizozitoa kwa Watanzania aliahidi kwamba Serikali yake itapitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2024 pamoja na mitaala kwa ajili ya kuboresha elimu na kuandaa wanafunzi wahitimu wenye ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajirika. Baada ya ahadi hii ya Mheshimiwa Rais wetu, kazi imefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nieleze kidogo mageuzi haya ya elimu ambayo kwa kweli ni maagizo ya Mheshimiwa Rais wetu na maono yake. Kwenye mfumo wetu na sera na jinsi ambavyo utatupeleka kutatua changamoto hii ya kutoa elimu ambayo wahitimu wanapata shida kujiajiri na kuajirika na hii ni pamoja na mitaala ambayo tumeibadilisha. Tuanze na mfumo wa elimu tulionao sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu unaitwa (1) 7 + 4 + 2 + 3 + maana yake ni kwamba Elimu ya Awali mwaka mmoja, Elimu ya Msingi miaka saba, miaka minne sekondari ya chini, miaka miwili sekondari ya juu, halafu mitatu kuendelea na elimu inayofuata. Ni mfumo wetu huu ambao kuna baadhi ya changamoto nitajaribu kuzieleza ambazo tunajaribu kuzitatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza kabisa kwenye mfumo huu ni kwamba elimu ya lazima Tanzania tunayoifanya sasa hivi ni miaka saba. Kila mtoto ni lazima kwa amri akae shuleni mpaka amalize Darasa la Saba. Akiondoka shuleni, tunahangaika na mzazi na mtoto na umri wa kuanza shule ni miaka sita. Kwa hiyo, mtoto akianza na miaka sita akimaliza Darasa la Saba ana miaka 13.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoto huyo akiacha shule tutajaribu kumtafuta, kama anataka kwenda sekondari tutapambana na mzazi aende, lakini hakuna sheria inayomlazimisha kusoma, inayomlazimisha mzazi kuendelea kumpeleka shuleni. Kwa hiyo, anamaliza elimu ya lazima akiwa na miaka 13 halafu tunasema elimu hii imwandae kuajiriwa na kuajirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria yetu hairuhusu kuajiri mtoto wa miaka 13. Kwa hiyo, elimu yetu ya lazima na umri wa kuanza shule kwa kweli haumwandai mtoto kuajiriwa labda aende sekondari, lakini sheria haimlazimishi kwenda sekondari, huu ndiyo mfumo tulionao sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo mpya baada ya Sera ya Elimu na Mitaala sasa hivi elimu yetu itakuwa na mfumo ufuatao: huu utaanza kutekelezwa rasmi mwaka 2027/2028, Elimu ya Awali mwaka mmoja, kwa sababu tunajitahidi kusambaza iweze kuwa ya lazima. Sasa hivi ni muhimu lakini hatuwezi kuilazimisha. Elimu ya Msingi itakuwa miaka sita, Elimu ya Sekondari ya chini miaka minne, Elimu ya Sekondari ya Juu miaka miwili au mitatu nitaeleza, na baada ya hapo kwenda kusoma tena miaka mitatu na zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Elimu ya Msingi miaka sita, lakini elimu ya lazima sasa itakuwa siyo miaka saba tena, itakuwa ni miaka 10. Maana yake ni kwamba mtoto atakapoanza Darasa la Kwanza itakuwa ni lazima asome amalize Elimu ya Msingi miaka sita na ni amri aendelee kukaa shuleni kuanzia Form One mpaka Form Four. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtoto haendi shule, tunabadilisha sheria, tunahangaika na mzazi tutamtafuta mtoto arudi shuleni asome. Huyu mtoto akianza na miaka sita shule ambayo ndiyo umri wa kuanza Darasa la Kwanza, akimaliza Form Four atakuwa na miaka 16. Angalau tumemsogeza karibu zaidi na umri ambao anaweza akajiajiri, kuajiriwa na norms za kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar wenzetu elimu ya lazima ni miaka 10, Kenya sasa hivi nadhani ni miaka tisa. Kwa wastani duniani nchi zote zinakimbilia elimu ya lazima miaka tisa, 10 au 12. Sisi miaka saba kwa kweli tumechelewa sana kusonga mbele huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litaanza kwa wale watoto ambao wako darasa la tatu sasa hivi, ambao wameanza na mtaala mpya. Wakienda darasa la nne, la tano, la sita wamemaliza shule ya msingi. Kwa hiyo, mwaka 2027 wale itakuwa ni lazima waende form One na kuendelea. Ndiyo maana uwekezaji kwenye shule, miundombinu hasa kupitia wenzetu wa TAMISEMI ni mkubwa na utaongezeka kuwa na shule ya sekondari katika kila eneo ambalo mtoto anaweza akatembea na kufika shuleni kusoma ili wote wamalize shule wakiwa na hiyo miaka 16. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kabla sijafafanua zaidi nieleze kidogo katika mitaala na hayo ndiyo maono ya Mheshimiwa Rais wetu, maana alisema tufanye elimu tuhakikishe mtoto anaajiriwa. Aliyasema haya kabla hata hajahutubia Bunge hapa, alizungumza tarehe 6 Aprili, 2024 katika Elimu ya Msingi, na hili limezungumzwa humu ndani, Kiingereza kitaanza darasa la kwanza, kitafundishwa kimawasiliano zaidi halafu baadaye ndiyo kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kuanza kukazia kanuni, unamweleza verb, adverb, noun, past tense, present participle tense, mtoto anakaa haelewi lakini ukienda sasa hivi kwenda kujifunza Kimasai ukajifunza mawasiliano utaanza kuongea Kimasai. Matokeo yake, mtoto anamaliza darasa la saba haongei Kiingereza. Tunaanza darasa la kwanza na tunabadilisha namna ya kufundisha kimawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika lugha sasa hivi kuna options unaweza ukaongeza lugha ya kigeni. Ukiacha Kiswahili, Kiingereza unaweza kuongeza Kifaransa kama unataka na walimu wapo na tutajitahidi wawepo. Unaweza ukasoma Kiarabu kama kuna mwalimu utaenda kusoma pale. Unaweza ukasoma Kichina, tumeongeza options kwa ajili ya ukalimani, nalo lilisemwa hapa ili watoto wakimaliza waweze kwenda duniani mahali popote kutafuta ajira, lakini Kiingereza bado kitafundishwa vizuri zaidi na kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kumaliza Elimu ya Msingi, sekondari inagawanyika mikondo miwili, mkondo wa elimu jumla na mkondo wa elimu ya amali. Amali ni masuala ya kazi. Mafunzo ya kazi ndiyo yale tunayoita sasa hivi ufundi na ufundi stadi. Ufundi ni kama Technical Secondary School tunayoizungumzia, ni mambo ya uhandisi. Ufundi stadi ni mafunzo mengine ya kazi kama mapishi, sports academy, music academy, fisheries, kushona nguo na kadhalika. Kwa hiyo, mafunzo ya amali ni seti kubwa, humo ndani kuna ufundi na kuna ufundi stadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyoongea tayari tumeanza ujenzi wa shule 100 za ziada za ufundi Tanzania. Siyo amali, ni amali ufundi na tumezipeleka kwa wale Waheshimiwa Wabunge ambao katika wilaya zao, VETA inajengwa kwa Mheshimiwa Mbunge mwenzake, yeye hana chochote. Yeye tunampelekea Technical Secondary School, siyo secondary school ya amali tu lakini ni amali ya ufundi. Huyu akimaliza form four, mafunzo ya amali ana cheti cha form four na ana cheti cha NACTIVET, watu wanakiita cha VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kama umejifunza wiring unamaliza form four tayari unaweza kwenda kazini, unaweza ukafanya wiring kwenye nyumba. Umejifunza ufundi magari, tayari unaweza kuingia kufanya shughuli za ufundi magari na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu akimaliza mkondo wa amali, labda niuelezee zaidi, akienda form five akasoma miaka mitatu atatoka na Diploma na cheti cha form six. Kama ilivyokuwa Dar Tech leo tunakamilisha taratibu za kujenga polytechnics. Moja Mwanza, nyingine Kigoma, nyingine Mtwara, nyingine Zanzibar, hapa Dodoma tumemaliza kujenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kama ilivyokuwa Dar Tech. ya kutoa tu Diploma lakini waliomaliza form four mafunzo ya amali hasa yale ya ufundi wataenda kule kupata Diploma kwa sababu ukweli ni kwamba nchi yetu bado inahitaji sana technicians. Tumeona wakati wa kujenga bomba hili kutoka Uganda kwenda huku, viwanda vingi vinapokuja wanasema hapa kwenu tunahitaji technicians lakini tunapata shida sana kuwapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, nchi imejiandaa kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu kwenda humo. Huyu atakapomaliza anaweza akaenda kufanya shughuli nyingine zozote mahali popote. Kwa hiyo, hizi polytechnics mpya ambazo zipo kwenye blueprints tutakamilisha, fedha zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, fedha zimeshatengwa kujenga hizo polytechnics nne. Waheshimiwa Wabunge siku moja nitawaalika mje mkaione Shule ya Ufundi Dodoma. Tumeikamilisha tumekabidhi DIT lakini ita-specialize kwenye Diploma tu. Watakaomaliza sekondari za ufundi kwenda kupata Diploma na cheti chao cha Form Six. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hivyo, kama mnavyofahamu sasa hivi kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu mikoa mingine yote ambayo ilikuwa haina kampasi ya chuo kikuu tunajenga matawi ya chuo kikuu. Hata hivyo, kule tutaenda kupeleka degree ambazo ni za amali siyo academic. Zina mwelekeo wa kuandaa mtu haraka kwa kuajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Njombe – UDOM inakwenda, Singida – Tanzania Institute of Accounts, Manyara - Arusha Institute of Accounts, Ruvuma hiyo hiyo. Mwanza Chuo cha ARI, Kigoma tuna MUHAS, udaktari pamoja na kwamba ni academic lakini kwa kweli ni amali. Unajifunza huku unatumia cadaver kupasua na kujifunza kila kitu, ukimaliza una ujuzi wa kwenda kuanza kazi tofauti na academic degree. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwelekeo wote huko tunakoenda huko, Kigoma, Kagera, University of Dar es Salaam; Tanga Mzumbe wanakwenda; Katavi, SUA; Lindi, UDSM; Rukwa tunaenda MUST pale Mbeya, yunaenda, Tabora, Shinyanga, Simiyu. Upande wa Zanzibar, University of Dar es Salaam imeenda ile Institute of Marine Science kwa ajili ya kuipanua kwa sababu hiyo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekti, kwa upande wa Mtwara vile vyuo viwili vya Ualimu, Mtwara Kawaida na Mtwara Ufundi, navyo vinaunganishwa vinakabidhiwa MUST Mbeya kwa ajili ya kuwa kampasi ya chuo kikuu, lakini na yenyewe itakuwa inatoa degree za elimu amali na amali ufundi kwa ajili ya kuandaa vijana wetu kwenye ajira. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ni matunda ya maono ya Mheshimiwa Rais wetu kwa sababu tusipoanza sasa hivi population dynamics ya nchi yetu na Sub-Suharan Africa huko mbele kwa kweli hali ni ngumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojiandaa hivi kwa mfumo wetu wa elimu, dunia itakuwa ni uwanja wa ajira kwa vijana wetu. Hata wakati wawekezaji wanakuja hapa, vijana wetu wanaweza wakatoka kwenda kupata ajira mahali popote duniani, maua yake Mheshimiwa Rais wetu kwa kuliona hili mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimalizie, baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais aliyotoa hapa Bungeni, Umoja wa Mataifa wakatangaza Mkutano Mkuu wa Viongozi wa Nchi wa Elimu Duniani. Walivyokuja kutuambia, tukasema mnataka kudandia treni imeshaanza mwendo, tutakwenda na ninyi lakini tutatangulia. Afrika mwaka huu ni mwaka wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona mazungumzo haya haya ambayo kwa kweli sisi tayari tumeshajiandaa, wote wanasema tujiandae kuongeza ujuzi katika elimu jambo ambalo Mheshimiwa Rais wetu alishatoa maelekezo, utekelezaji umeanza, tunamshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)