Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nzega Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango. Pili, natumia nafasi hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nawapongeza sana Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha kwa document waliyoileta mbele yetu katika Bunge hili ikiwa ni Mpango wa mwisho kabla ya kuwa na Mpango wa Miaka 25 inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia baadhi ya maeneo. kwanza, natumia nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa ushauri na maoni yao. Mengi tutaendelea kuyafanyia kazi polepole kadri ambavyo Mwenyezi Mungu anatujaalia na uwezo wa kibajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, ni Bunge hili hili ndiyo liliiomba Serikali ianze jitihada za kubadili bajeti ya Wizara ya Kilimo. Maeneo makubwa ambayo Bunge hili lilishauri ni kuwekeza kifedha kwenye maeneo ya utafiti, uzalishaji wa mbegu, ugani, tuanze kutoa huduma za umwagiliaji, tuhangaike na tatizo la upotevu wa mazao, tufungue masoko na kuwahakikishia wakulima wanapata masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapitisha bajeti ya kwanza kutoka shilingi bilioni 294 kwenda shilingi bilioni 750, ukuaji wa sekta ya kilimo ulikuwa 2.7%. Leo tunapoongea mwaka 2023/2024 ukuaji wa sekta ya kilimo umefika 4.2%. Wakati tunaanza utekelezaji wa bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Sita, uzalishaji wa chakula katika nchi yetu ulikuwa ni jumla ya tani milioni 17.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2024 mabadiliko yaliyofanyika kipindi cha miaka miwili uzalishaji wa chakula umefika tani milioni 22, asilimia 128. Lengo letu la mpango wa miaka mitano kwa mwaka 2025/2026 tufike asilimia 130 ya food security katika nchi yetu. Tutafikia lengo hili mwaka mmoja kabla ya mwaka ambao mpango ulituwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, ninataja hizi takwimu ili ziweze kukaa kwenye kumbukumbu kwa sababu Waheshimiwa Wabunge tuna matamanio, nami nayaunga mkono sana kwamba ni lazima fedha za Serikali ziwekezwe katika sekta hii. Hii ni kauli ya Waheshimiwa Wabunge wote na Watanzania na matamanio yenu na ndiyo sekta iliyoajiri watu wengi. Mwaka 2021/2022 export value ya sekta ya kilimo ilikuwa ni Dola bilioni 1.2, mwaka 2023/2024 tumefika Dola bilioni 2.3. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote tumekuwa tukijadili suala la tija, uzalishaji wa zao la mahindi mwaka 2021 wastani per hector ilikuwa ni tani 1.9. Leo tunamzungumzia mkulima mdogo, kwa takwimu za msimu wa kilimo ulioisha tumefika per hector tani 2.5, lengo letu ni kufika wastani wa tani 4.5. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie mazao ya kibiashara, wakati tunaanza bajeti ya kwanza uzalishaji wetu wa zao la kahawa ilikuwa ni wastani wa tani 65,000, mwaka huu uliokwisha tumefika tani 85,000. Bei ya mkulima imetoka wastani wa shilingi 700 mpaka 1,000 hadi kufika wastani wa shilingi 6,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nilitolee mfano ni tumbaku. Mwaka 2021 tulikuwa tunazalisha wastani wa tani zisizozidi 60,000 mwaka 2023, msimu wa kilimo uliokwisha tumezalisha tani 120,000 na Tanzania kuwa recorded ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa tumbaku Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya mkulima imeongezeka kutoka wastani wa dola 1.6 mpaka wastani wa dola 2.2. Hatua hizi tulizofikia ni za muda mfupi. Sote tunafahamu matumizi yetu ya mbolea. Mwaka 2021 tulikuwa tunatumia tani 360,000, mwaka huu msimu wa kilimo uliokwisha nchi yetu imetumia jumla ya tani 920,000 za mbolea. Sababu ni moja, Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia alivyoamua kuweka ruzuku kwenye bei ya mbolea. Sasa tumeanza kuweka ruzuku kwenye eneo la mbegu na tumeanza na zao la kwanza la mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais anatoa hotuba hapa alituambia haiwezekani tukabadili sekta hii ya kilimo bila kuwekeza katika umwagiliaji. Nami natumia nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, nawashukuru sana Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango na ninalihakikishia Bunge lako Tukufu na Watanzania kwamba katika Vision 2025 - 2050 inayokuja, moja ya sekta iliyopewa kipaumbele ni sekta ya kilimo. Tume-develop masterplan ya 2030 – 2050, yeyote atakayekuja katika nchi hii mpaka mwaka 2050, kuna clear vision, clear plan na resource allocation mpaka mwaka mwaka 2050 katika sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni dhamira ya Serikali iliyoko madarakani. Utumiaji wa mbolea kwa wakulima wetu per hector tulikuwa the lowest kwa SADC. Tulikuwa na wastani wa kilo 15, Mheshimiwa Profesa Ndakidemi anafahamu, msimu wa kilimo uliopita wastani wa matumizi ya mbolea kwa wakulima yamefika per hector kilo 24. Malengo yetu tunatakiwa kufika kilo 50, ndiyo tuliyojiwekea 2025/2026 na ninaamini tutafikia huko ambako tunataka kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ilikuwa ina tatizo la extension services kwa kipindi cha miaka miwili, leo kila halmashauri imepelekewa mashine ya kupimia afya ya udongo na imekuwa huduma ya bure. Suala la soil health katika nchi yetu, siku zote lilikuwa ni donor funded. Kwa mara ya kwanza miaka hii miwili, mikoa 26 ya Tanzania Bara, mikoa 18 zoezi la upimaji wa afya ya udongo limekamilika, tumebaki na mikoa saba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatupeleka kwenye hatua gani? Tumejiwekea lengo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu 2025/2026 kupiga marufuku matumizi ya mbolea za generic. Haya maneno DAP, Urea, kuanzia 2025/2026 tunaenda kutumia mbolea kutokana na mahitaji ya afya ya udongo ya eneo husika na ekolojia inayohusika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la umwagiliaji, na nimesikia Mawazo ya Waheshimiwa Wabunge, nami nawaelewa matamanio yao, tunataka matokeo leo kwenye eneo la umwagiliaji. Nataka ku-convince wenzangu, toka tunapata Uhuru mpaka mwaka 2021/2022, tulikuwa na mtandao wa umwagiliaji ambao ulikuwa ni jumla ya hekta 600,000 na kidogo karibu laki saba. Leo ndani ya miaka miwili tunatekeleza miradi 700 yenye jumla ya hekta 520,000, lakini miradi hii ni ya namna gani? Siyo miradi ya mifereji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tusirudie makosa ambayo tumewahi kufanya huko nyuma ya kujenga miundombinu ya umwagiliaji ya mifereji ambayo mkulima anamwagilia masika badala ya kuzalisha mara mbili au mara tatu. Taifa hili lilikuwa halina feasibility study na detailed design ya mabonde yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kutoa mfano mdogo, mwishoni mwa miaka ya 1960, Kadinali Rugambwa, Askofu Kibira na Sheikh Suleiman wa Kagera walifanya feasibility study na detailed design ya Bonde la Mto Ngono. Document tuliyoenda kuitumia sisi Wizara ya Kilimo ilifanywa na wazee hawa ambapo tumeichukua document iIe kuifanyia review na imekamilika na sasa tunatangaza Mradi wa Ngono. Hatuwezi kuujenga Mradi wa Ngono kwa mwaka mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Mradi wa Rufiji. Rufiji Chini baada ya Mwalimu Nyerere, tunatekeleza miradi ya mabwawa mawili yenye jumla ya gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 220. Hatuwezi kujenga kwa mwaka mmoja, haiwezekani. Tunajenga Bwawa la Msagali ambalo ndilo litakuwa bwawa kubwa la kilimo nchi hii lenye cubic metre 92,000,000 na tunatumia zaidi ya shilingi bilioni 22, hatuwezi kulijenga kwa mwaka mmoja. Miradi yote hii tumemaliza upembuzi yakinifu wa Bonde la Lukuledi, tumeanza kutangaza miradi. Tutajenga bonde lile kwa miaka mitatu mpaka mitano kukamilisha maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunamaliza feasibility study ya Bugwema; Mradi huu wa Bugwema aliuanza Baba wa Taifa. Namshukuru sana Mheshimiwa Prof. Muhongo na Mheshimiwa Eng. Chamuriho, baada ya kwenda kutembelea kule kukuta mabomba, nikauliza tatizo ni nini? Kwa nini Mwalimu alikwama kwenye huu mradi wa kutumia maji ya Ziwa Victoria? Tuipongeze sana Serikali, nami nampongeza sana ndugu yangu Mheshimiwa Aweso. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuyatumia maji ya Ziwa Victoria, inahitaji roho ngumu. Leo tunaenda kutekeleza Mradi wa Bugwema ambao aliuanza Baba wa Taifa ukaishia njiani. Miradi hii inahitaji fedha. Leo tunaanza kutekeleza mradi wa mabwawa matano, kila siku tunalalamika mafuriko ya maji hapo karibu na Chalinze Nyama ambapo ili tuyaondoe mafuriko yale, tunahitaji kujenga mabwawa matano mpaka Kilosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata fedha kutoka World Bank dola 52,000,000 ambazo tunaenda kuziingiza kwa ajili ya kujenga hayo mabwawa matano. Miradi hii haiwezi kwisha kwa muda mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako Tukufu hili lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Export Levy. Mheshimiwa Rais alianza kutoa ruzuku, na ninavyoongea hivi sasa, msimu huu, zao la korosho litaenda kuvunja rekodi na historia ya nchi hii. Tunatarajia kuzalisha jumla ya tani 500,000, mpaka leo minadani ndani ya mwezi mmoja mauzo yamefika shilingi bilioni 924. Haya mabadiliko hayawezi kutokea siku moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumebadili mfumo wa kuuza kahawa na kakao. Kakao ya mkulima ilikuwa inanunuliwa shilingi 3,000/=. Mabadiliko yaliyofanyika ndani ya miaka miwili, leo kakao inanunuliwa zaidi ya shilingi 25,000/= mpaka shilingi 30,000/= kwa kuwaondoa watu wa kati na tunatumia Mfumo wa TMX na uzalishaji umefika zaidi ya tani 14,000 ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, uwekezaji kwenye eneo la kilimo siyo jambo la muda mfupi. Siyo sawasawa na ujenzi wa darasa, haifanani kabisa, ni long term investment na ni lazima kama Taifa tuwe na uvumilivu wa kuwekeza kwa muda mrefu kwenye sekta ya kilimo ili tuanze kupata matokeo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, nataka kutumia Bunge hili Tukufu na mbele ya Watanzania, mimi sio mzoefu sana Serikalini, wala sio mzoefu sana ndani ya Bunge. Nina term mbili, lakini kuwa na kiongozi ambaye anasikiliza na anatoa fursa ya kufanya maamuzi magumu, decision ambayo ameizindua mwezi wa Nane ya kuanzisha Mechanization Centre katika nchi hii kwa ajili ya wakulima wadogo, Taifa letu siku zote tumekuwa tukihubiri kwamba wakulima wamiliki trekta. Mkulima wa Tanzania ni nani? Anamiliki wastani wa hekta moja ambayo ni ekari 2.5, huyu hawezi kumiliki trekta la shilingi milioni 70, au shilingi milioni 80, ni kumtia umaskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua gani? Mheshimiwa kaenda India, karudi hapa, kazindua mradi wa trekta 10,000, power tiller 10,000 na kuanzisha Mechanization Centre katika maeneo ya uzalishaji ambayo wakulima wadogo watakuwa wanakodi trekta kwa bei ya ruzuku isiyozidi shilingi 40,000 kwa ekari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yanayofanyika na hivi ninavyoongea kwenye eneo la ukanda la pamba tumeshasambaza jumla ya trekta 400 na hivi sasa tunafanya utaratibu wa kupeleka Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Rukwa trekta zaidi ya 100. Tunaanza kupeleka combine harvester na power tiller kwenye mabonde ya Mbarali. Haya yanahitaji kuchukua muda na sisi sote tuweze kufanya hii kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia, leo hii Serikali inampatia mkulima ruzuku ya mbegu, Serikali inampatia mkulima ruzuku ya mbolea, Serikali imepeleka magari, pikipiki na mashine za kupimia afya katika ngazi ya halmashauri, lakini mkulima soko liko wapi? Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katoa idhini ya NFRA kuwa mnunuzi mkubwa wa mazao ya mpunga na mahindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto, haiwezekani tukakosa changamoto. Changamoto ya kwanza ambayo tumekutana nayo mwaka huu ni maghala, uwezo wa uhifadhi wa NFRA. Ni jukumu letu kama Serikali na tumeongea na Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunaweka kwenye bajeti ya mwaka kesho kuongeza uwezo wetu wa uhifadhi. Kwa msimu wa mwaka 2023 na mwaka 2024, NFRA kanunua jumla ya tani 820,000 za mahindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zilizokuwa allocated inabidi tufanye reallocation ndani ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo mwezi Desemba ili tupate fedha za ziada tuweze kuisaidia NFRA iweze kuendelea kununua mahindi ya wakulima kwa sababu bila ya kuwahakikishia soko la mazao yao, wakulima hawa watakuwa hawana mahali pa kupeleka. NFRA ikiondoka sokoni, bei ya mahindi itarudi shilingi 200, au shilingi 300. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutumia Bunge lako Tukufu kuwaambia wakulima, NFRA haitofunga mlango, tutahangaika na namna ya kupata fedha lakini mazao ya wakulima yataendelea kununuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la integration, Waheshimiwa Wabunge wameongea sana kuhusu ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Wizara ya Mifugo. Kila bwawa linalojengwa na Wizara ya Kilimo, lina matoleo na water trough kwa ajili ya mifugo. Sasa hivi tunafanya pamoja na Wizara ya Maji kwa ajili ya kuingiza components ya irrigation kwenye kuyatoa maji Ziwa Victoria kuyafikisha Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutayatumia maji yale na ile network itakayobeba maji kutoka ziwani kwa sababu kilimo hakihitaji maji yaliyosafishwa, sisi tunahitaji raw water kama ilivyo. Tumeshaanza kufanya survey katika Mkoa wa Simiyu ili ku-link katika mradi ulioko Mkoa wa Simiyu uweze kuhudumia maji ya kunywa, lakini vilevile uweze kuhudumia umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii imejadili Luiche miaka nenda rudi, Mheshimiwa Makamu wa Rais akiwa Waziri wa Fedha, kwa mara ya kwanza tumekaa tunasubiri hela ya Kuwait, Mheshimiwa Dkt. Samia akasema hamna sababu ya kusubiri hela ya Kuwait, tangazeni mradi. Mkandarasi anajenga Luiche, mradi ambao toka Serikali ya Awamu ya Kwanza ulikwama, mradi wa Mkomazi, sasa hivi kuna Mkandarasi anajenga Mradi wa Mkomazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Mkomazi hauwezi kwisha kwa mwaka mmoja au miwili, miradi hii itachukua zaidi ya miaka miwili, au miaka mitatu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bashe, malizia.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka tu kukisema, lengo letu kama Serikali ni kuhakikisha investment ya irrigation inafika shilingi trilioni moja kwa mwaka. Huu ndiyo mpango wa Serikali na kwenye masterplan inaonesha one trillion for ten years ili tuweze kufika angalau 50% ya ardhi inayotumiwa na wakulima kwa ajili ya kutumika kwa ajili ya umwagiliaji. Haya yote yanahitaji patience. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namaliza kwa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, matamanio ya kila Mheshimiwa Mbunge kama Wizara na Serikali tunayafahamu. Tutajitahidi kadiri ya uwezo wetu kuhakikisha tunafikia matarajio ya Watanzania. Sekta hii ilipokuwa, siyo ilipo leo. Juzi Mheshimiwa Rais akiwa Marekani, Tanzania imekuwa recognized na kasomeni kwenye Journal ya African Development Bank kwamba ni modal ya transformation ya agriculture katika Southern Saharan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia mkutano huo, tumepata dola 130,000,000 kwa ajili ya mradi wa vijana na akina mama. Namshukuru sana na ninampongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera na ninawaomba Wakuu wa Mikoa wengine waige mfano wa Mheshimiwa Fatma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye issue ya value addition. Ninawahakikishia, Serikali imeweka fedha kwenye Mradi wa Maranje shilingi bilioni 10, tumeshapeleka shilingi bilioni saba, tumeshaanza kujenga viwanda vya ubanguaji wa korosho. Sasa hivi Serikali inapiga marufuku export ya pyrethrum raw kwenda nje, viwanda tunavyo, vina uwezo wa ku-process tani 12,000, kuanzia mwaka kesho hakuna pyrethrum itakayokwenda nje ya nchi hii ambayo haijaongezwa thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni hatua tunachukua, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wa Morogoro, tuendelee kuisukuma Serikali nami ninakubaliana nao kabisa katika matamanio yao. Feasibility study ya Kilombero Basin inaendelea, itakamilika mwaka huu na mwaka huu itatangazwa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na tutaanza ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia tu kwa kumshukuru sana ndugu yangu Mheshimiwa Profesa Kitila. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, amekuwa msikivu yeye na Wizara yake. Changamoto za resources zipo, lakini tunaenda kukaa, tunaongea na tunagawana kasungura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)