Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkoani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge letu Tukufu nami kuweza kuchangia hoja hizi mbili zilizoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia fursa hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Prof. Kitila pamoja na timu yote ya wataalamu kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kutayarisha hoja zetu hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutuongoza vizuri, kutusimamia vizuri na kutoa kipaumbele cha kipekee kwa miradi ya mikakati kwa sekta ya uchukuzi, kwani tunafahamu sekta ya uchukuzi ni sekta wezeshi kwa sekta nyingine zote hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia natumia fursa hii kuwashukuru sana sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao, na michango yote tumeichukua na tunaenda kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hoja iliyoko mbele yetu hapa ya Mpango, imezungumzwa vizuri kuhusu mipango mbalimbali inayohusu miundombinu ya usafiri na usafirishaji. Mpango ambao umeeleza kwa kina kabisa ilikuwa ni Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwamba Mradi wa SGR unatengenezwa au unajengwa kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza inahusu ujenzi wa kutoka Dar es Salaam – Mwanza yenye urefu wa kilometa 1,200. Kipande hiki cha kutoka Mwanza – Dar es Salaam au Dar es Salaam – Mwanza kinagharimu takribani shilingi trilioni 16.97.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu umegawanyika katika vipande vitano, kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Salaam – Morogoro chenye urefu wa kilometa 300 na ujenzi umefikia 99% na kwa sasa mradi umeanza kufanya kazi na sote tunafaidi matunda ya usafiri wa SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha pili ni kutoka Morogoro – Dodoma chenye urefu wa kilometa 422 na mradi umefikia 98.6% na sasa mradi unatoa huduma na sote tumeanza kufaidi matunda hayo kutoka Dar es Salaam – Dodoma tunakwenda kwa kutumia treni za SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha tatu ni kutoka Dodoma – Tabora chenye urefu wa kilometa 368, mkandarasi yuko site na mradi umefikia 14.39%. Kipande cha nne ni kutoka Tabora – Isaka chenye urefu wa kilometa 165 na kazi imefikia 5.63%, Mkandarasi yuko site. Kipande cha mwisho ni kipande cha kutoka Isaka – Mwanza ambacho kina urefu wa kilometa 341 na mkandarasi amefikia 66% na sasa yuko site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwamba mradi huu umegawanyika kwenye awamu mbili, awamu ya kwanza ni kutoka Dar es Salaam – Mwanza na awamu ya pili ni kutoka Tabora – Kigoma. Kipande hiki kimegawanyika katika sehemu mbili; sehemu ya kwanza ni kutoka Tabora – Kigoma chenye urefu wa kilometa 506, ujenzi umefikia 4.9% na Mkandarasi yuko site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni kutoka Uvinza – Msongati – Gitega – Burundi ambayo ina urefu wa kilometa 367, hatua tuliyofikia ni hatua ya manunuzi na tunaamini itakapofika mwisho wa mwezi wa Desemba, mkandarasi atakuwa amepatikana kwa ajili ya kipande hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ni mara ya kwanza Mheshimiwa Rais anaitoa reli nje ya mipaka ya nchi yetu, reli ya SGR, tunakushukuru sana Mheshimiwa Rais. Jumla ya kilometa 1,560 za ujenzi wa SGR zimeanzishwa na kutekelezwa ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo hii inafanya iwe sawa na 68.4% ya ujenzi wa Mradi wote wa SGR. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna budi kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi hiyo kubwa. Gharama ya mradi huu wote ni shilingi trilioni 23.3 ambazo tunaendelea kutekeleza. Kwa kipande cha kwanza kutoka Dar es Salaam – Mwanza na maeneo mengine, tayari shilingi trilioni 10.53 zimetumika, tumewalipa Wakandarasi kutokana na certificates mbalimbali ambazo wamewasilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu, Serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha kipande cha kutoka Dar es Salaam – Dodoma chenye urefu wa kilometa 722 ambazo imejumlisha njia kuu pamoja na njia za kupishana. Hivi sasa tunavyozungumza sote tumeona Reli ya SGR inasafiri kutoka Dar es Salaam – Dodoma kwa masaa sita. Leo tunavyozungumza, tunazo route nne kwa siku, tunaamini mwakani tutakuwa tunaenda zaidi ya route sita kwa siku. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kila baada ya masaa mawili, kutakuwa na treni kati ya Dar es Salaam – Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vitendea kazi, jambo moja ni kujenga njia ya treni; jambo la pili na muhimu ni kuwa na vitendea kazi. Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya manunuzi ya vitendea kazi mbalimbali kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumenunua mabehewa ya mizigo 1,430 ambayo awamu ya kwanza itawasili mwezi Desemba mwaka huu, pamoja na mwakani. Baada ya kuwasili mabehewa hayo, tutafanya majaribio na baada ya hapo tutaanza kazi ya kusafirisha mizigo kati ya Dar es Salaam na Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali ya Awamu ya Sita imenunua seti za treni za kisasa ambazo tunaziita mchongoko. Treni sita zimefika hapa nchini na zimeanza kufanya kazi. Mwezi huu hivi ninavyozungumza tutapokea treni mbili na baadaye treni mbili za mwisho zitapokelewa mwezi Desemba mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tumenunua mabehewa 89 pamoja na vichwa vya treni 17 ambavyo vimeanza kutoa huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma. Gharama ya vitendea kazi vyote hivi ni takribani shilingi trilioni 1.147.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kujua umuhimu wa sekta binafsi, Serikali ilifanya mabadiliko kupitia Bunge lako tukufu, kubadilisha Sheria ya Reli Na. 10 ya Mwaka 2017, ili kuruhusu private sector kwa kutumia utaratibu wa open access. Kuanzia mwakani tutaruhusu private sector wenye vichwa vyao na mabehewa yao kuja kuwekeza kwenye mitandao yetu ya SGR pamoja na meter gauge. Hii tutaitumia reli yetu kikamilifu, pia, itakuwa na ufanisi mzuri na Shirika litapata mapato zaidi kuliko tunavyofanya kazi hivi kwa kutumia vitendea kazi vya TRC peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio yaliyopatikana baada ya kuanza safari za reli kati ya Dar es Salaam na Dodoma. Kabla ya safari ya Dar es Salaam na Dodoma kuanza Watanzania walikuwa wanatumia kati ya saa saba mpaka tisa kusafiri kati ya miji hii miwili. Leo hii tunapoongea Watanzania wanatumia kati ya saa nne mpaka tatu kwa kutumia SGR. Wale wanaopanda express train wanatumia saa tatu na wale wanaopanda treni ya kawaida wanatumia saa nne. Kutoka saa tisa mpaka saa tatu hili ni jambo kubwa, hatuna budi kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usafirishaji wa abiria, hadi kufikia mwezi Oktoba, 2024 shirika limeweza kusafirisha abiria 842,853 kwa kutumia SGR. Hii ni sawa na wastani wa abiria 700,000 kwa kila siku wanaosafiri kwa kutumia njia ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makusanyo makubwa yamepatikana. Tangu kuanza kutumika kwa SGR tarehe 14 Juni, 2024 hadi Oktoba, 2024, takribani shilingi bilioni 22.38 zimekusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira, tumeona mafanikio makubwa mpaka sasa. Wafanyakazi wapatao 940 wameajiriwa na reli yetu ya kisasa kwenye huduma za SGR. Tunategemea itakapofika mwisho wa mradi huu, hasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma, wafanyakazi 2,460 wataweza kufanya kazi kwenye reli yetu ya SGR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepata mafanikio makubwa kwenye utunzaji wa mazingira. Uendeshaji wa SGR unatumia nishati ya umeme na kwa hiyo, umesaidia sana kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na pia tumefanikiwa kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida treni hizi zinatumia mafuta ya diesel, lakini SGR yenyewe inatumia umeme na umeme wenyewe ni kutoka kwenye maji ambayo yanapatikana hapa nchini. Kwa hiyo, tume-save fedha nyingi sana za kununua mafuta ya diesel kwa ajili ya kuendesha reli hii ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kuhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam. Mwaka 2023, mwezi Desemba, katika Bunge lako tukufu tulipitisha mkataba hapa kwa ajili ya uanzishwaji na uendelezaji wa Bandari ya Dar es Salaam kati ya gati namba tano mpaka namba saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuripoti mafanikio yaliyopatikana kutokana na uwekezaji wa DP World katika gati namba tano mpaka namba saba. Mara baada ya DP kuanza kazi Bandari ya Dar es Saalam amewekeza dola za kimarekani milioni 250, sawa na shilingi bilioni 675 katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, DP World imenunua mitambo ya kisasa yenye thamani ya shilingi bilioni 214.45. Mitambo hii kama hatukuwekeza au kama hatukumleta DP World tusingeweza kuinunua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo DP World amewekeza ni ukarabati wa mitambo iliyokuwa inatumiwa na TPA. DP World katika kipindi alichokuwepo cha miezi mitano ameweza kufanya usanifu na usimikaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA na sasa kazi inafanyika Bandari ya Dar es Salaam katika maeneo hayo niliyoyataja, yaani gati namba tano mpaka namba saba, ufanisi wa utendaji umekuwa mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uwekezaji wa DP World tumeweza kushuhudia mafanikio yafuatayo kwenye Bandari ya Dar es Salaam katika gati namba tano mpaka namba saba. Wastani wa muda wa meli kukaa sasa umepungua. Kabla ya uwekezaji wa DP World meli zilikuwa zinakaa nangani kwa siku 46, lakini leo hii tunapozungumza, meli za makasha hazikai nangani tena. Ikiingia meli ya makasha inakwenda moja kwa moja gatini. Kwa meli za mizigo ya kichele, zamani zilikuwa zinakaa siku 46, leo hii meli hizo zinakaa siku 12 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa meli za mizigo mchanganyiko, zamani zilikuwa zinakaa nangani siku 46, lakini leo hii meli zinakaa nangani kwa siku 10 tu. Pia, tumeona kuna ongezeko kubwa la idadi ya makasha baada ya uwekezaji wa DP World. Kampuni ya DP World imeongeza ukuaji wa idadi ya makasha wastani wa 38.17% ikilinganishwa na wakati wa TPA ambayo yenyewe ilikuwa, wastani wa ongezeko la makasha ni 9.8%. Hii imesababisha wastani wa idadi ya makasha kwa mwezi kufikia 17,626 ikilinganishwa na makasha 12,727 wakati TPA inafanya kazi kwenye gati namba tano mpaka namba saba ya Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna ongezeko la shehena mchanganyiko. Kampuni ya DP World imeongeza kiasi cha shehena kinachohudumiwa hadi kufikia wastani wa tani 168,336 kwa mwezi ikilinganishwa na tani 141,889 wakati magati hayo matatu yalipokuwa yanahudumiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia ongezeko la shehena, kutokana na uwepo wa DP World, mapato ya wharfage yameongezeka kwa wastani wa 9.9% kwa kipindi cha miezi mitano ikilinganishwa na wakati wa …

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbarawa, hebu rudia tena. Wharfage anakusanya nani?

WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, wharfage inakusanywa na TPA, wao ndio wenye mamlaka kisheria. Bunge lako Tukufu lilipitisha hapa kuiruhusu TPA kukusanya wharfage kwa ajili ya uendelezaji wa Bandari za Tanzania. Kupitia ongezeko la shehena kutokana na uwepo wa Kampuni ya DP World, mapato ya wharfage yameongezeka kwa wastani wa 9.9% kwa kipindi cha miezi mitano ikilinganishwa na 6.5% kwa kipindi kama hicho, wakati magati hayo matatu yalipokuwa yanafanya kazi chini ya Mamlaka ya Bandari Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Serikali kubadilisha shughuli ya uendeshaji wa gati namba tano mpaka namba saba kuwa chini ya Kampuni ya DP World, matumizi ya uendeshaji wa gati namba tano mpaka saba yamepungua kwa 2.7% kwa kipindi cha miezi mitano ikilinganishwa na wakati magati hayo yanasimamiwa na Mamlaka ya Bandari, matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa 15.1%. Wakati wa DP World matumizi yamepungua, lakini wakati wa TPA matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa 15.1%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miezi sita, kutoka mwezi wa Februari hadi Septemba, Serikali imepata jumla ya shilingi bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yatokanayo na shughuli za ufanyaji kazi wa DP World katika gati namba tano mpaka namba saba. Hii imetokana na makusanyo ya pango (land rent), tozo ya mrahaba, pamoja na tozo ya wharfage ambayo yenyewe inakusanywa na TPA.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia.
WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufanisi huo uliosababishwa na kuja kwa Kampuni ya DP World, sasa Mamlaka ya Bandari inatekeleza miradi yenye thamani ya shilingi trilioni 1.22. Miradi hiyo ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, mradi wa ujenzi wa kituo cha kupokea mafuta ambao ujenzi unaendelea na unatekelezwa kwa shilingi bilioni 578, mkandarasi yuko site. Ujenzi wa bandari ya kisiwa, mgao unaendelea na mkandarasi yuko site na unatekelezwa kwa shilingi bilioni 434.5. Ujenzi wa Gati la Malindi Wharf hivi karibuni tutapata mkandarasi, kwa ajili ya ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 500 ambalo litagharimu shilingi bilioni 540.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay unaendelea, mkandarasi yuko site na mradi huu utagharimu shilingi bilioni 80. Ujenzi wa Bandari ya Kemondo na Bukoba Mjini, mkandarasi yuko site na unagharimu shilingi bilioni 40. Mwisho ni Mradi wa Mwanza South ambao unaendelea, mkandarasi yuko site na mradi huu unagharimu shilingi bilioni 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yote hii isingeweza kutekelezwa kama hatukuweza kumleta DP World kwenye Bandarai ya Dar es Salaam. Matokeo yake leo miradi hii mingi ya kimkakati inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kasi ambayo tumejipangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niongelee kuhusu suala la TAZARA. Reli ya TAZARA ni muhimu sana, ni reli inayounganisha Tanzania na Zambia. Serikali ya Tanzania, Zambia na China tulisaini mkataba mwezi Septemba, kwa ajili ya kumpata mwekezaji ambapo Kampuni ya CCC iliteuliwa kufanya kazi hiyo. Hivi ninavyozungumza leo, timu yetu ya wataalam kutoka Tanzania na Zambia wako Dar es Salaam, kwa ajili ya kuzungumza kuhusu concession agreement. Tunaamini wiki inayokuja timu ya wataalam Watanzania na Zambia…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, watakaa pamoja na timu kutoka China.
MWENYEKITI: Mnayo nafasi tena kuja kutoa majibu kwenye hili. Ahsante sana.

WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)