Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karagwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja mbili ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Mawaziri; Mheshimiwa Daktari Mwigulu Lameck Nchemba na Mheshimiwa Profesa Mkumbo. Naomba nianze kwa kuwapongeza kwa hotuba zao nzuri ambazo zimetoa mwelekeo mzuri wa mjadala ambao tumekuwanao wiki hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa michango na ushauri mzuri kwa Serikali. Pia nawapongeza Mawaziri wenzangu kwa ufafanuzi ambao wameutoa toka kwenye hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge walijadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukrani zangu za kipekee kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa na kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuendelea kuiwezesha Wizara ya Ujenzi kutimiza wajibu wake wa kujenga barabara, madaraja, vivuko pamoja na nyumba za watumishi kupitia TBA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto ambazo mmetueleza kupitia michango yenu, yapo mafanikio makubwa ambayo tumeyapata kupitia sekta ya ujenzi. Wakati wa kipindi cha bajeti, kulikuwa na mvua kubwa ambazo zilikuwa zinaendelea za El-Nino pamoja na kimbunga Hidaya, lakini kupitia michango yenu mizuri tulikuwa wasikivu tukakubaliana kwamba, wakati wa mvua turudishe mawasiliano ya muda ili wananchi wetu kwenye majimbo yetu, kwenye wilaya zetu na mikoa, waendelee kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini mvua zitakapoisha turudishe miundombinu ya kudumu kama ilivyokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwanza niwashukuru kwa ushirikiano ambao mlitupatia kipindi kile kigumu cha mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya. Namshukuru sana Rais wetu Dkt. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, tayari ametuwezesha. Baada ya mvua kuacha, tunazo shilingi bilioni 868.56 kwenda kujenga madaraja na makalavati kwenye maeneo yote ambayo yaliharibiwa na mvua za El-Nino. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hili, tuliona tukitumia hizi shilingi bilioni 868.56 kwenda kukwangua barabara, mvua zitakaponyesha tatizo litarudi pale pale. Kwa hiyo, tumeona tutumie fedha hizi shilingi bilioni 868.56 kwenda kujenga makalavati na madaraja kwenye maeneo ambayo yameharibika ili mvua zitakaponyesha madaraja haya yaweze kutumika. Vilevile, tutakapojenga kiwango cha lami, madaraja na makalavati haya ni viwango vikubwa ambavyo hata ujenzi wa lami hatutahitaji kujenga madaraja mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana, mmefuatilia kwa jitihada kubwa kuhakikisha tunafikia hatua hii. Kipekee tumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu hizi shilingi bilioni 868.56 ni fedha za dharura ambazo tulikuwa hatujajipanga kwa kuwa hatukujua kwamba tutapata mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya, lakini kwa jitihada nzuri za Mheshimiwa Rais fedha hizi zimepatikana, zikiwemo shilingi bilioni 130 ambazo tulizitumia kipindi cha mvua za El-Nino ili kuweka mawasiliano ya muda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika madaraja na makalavati ambayo tunaenda kujenga, fedha hizi pia zingeenda kujenga miradi mipya, lakini kwa sababu ya athari kubwa ambazo zilijitokeza, nadhani mnakubaliana nami kwamba, ni bora tukajenga miundombinu hii na baadaye kwa kadiri fedha zitakapokuwa zinapatikana ndiyo tuweze kwenda kwenye miradi mipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kwenda kwenye miradi mipya, barabara zikiharibika wananchi wetu wanasubiri mawasiliano ya kudumu yarudi halafu tunakuwa hatuyarudishi. Kwa hiyo, tumeona ni vyema tukajikita kwenye kujenga madaraja na makalavati halafu kadiri fedha zitakapopatikana tukaendelea kutekeleza miradi mipya, ambayo ilikuwa kwenye bajeti, lakini fedha hii ikatumika kwenye kurudisha miundombinu ambayo iliharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mafanikio pia tunamshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Tunajivunia kwamba, katika kipindi ambacho amekuwa madarakani tumekamilisha miradi ya barabara 25 yenye jumla ya kilometa 1198.5. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunayo miradi 87 yenye jumla ya kilometa 3,140.7 ambayo ipo hatua mbalimbali za utekelezaji. Katika mjadala, Wabunge mmezungumzia changamoto za ukandarasi kusuasua katika utekelezaji, ninawahakikishia kwamba jitihada kubwa zinaendelea chini ya Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, kuhakikisha kadri fedha zinavyopatikana tunaendelea kulipa wakandarasi ili miradi hii 87 yenye jumla ya kilometa 3,140.7 iweze kuendelea. Kwa hiyo, ningependa kuwatoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge Serikali hii ni sikivu, tunatambua changamoto zilizoko huko site na tutafanya kadri ya uwezo wetu ili kuhakikisha wakandarasi hawa wanaendelea kulipwa ili kazi iweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mkakati wa kupunguza foleni kwenye majiji. Nikianzia na hapa Dodoma, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi yetu panapokua kwa kasi kwa sababu Watanzania wanakuja kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kuwajulisha kwamba kazi nzuri ambayo Rais wetu alituanzishia ya kujenga barabara za mzunguko wa pete - ring road kilometa 112.3 kwa network ya kutoka Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa yenye kilometa 52.3 tuko 85% ya utekelezaji, kwa maana imebakia 15% na kufika Januari, mwakani Mkandarasi atakuwa amekamilisha ujenzi wa hizi kilometa 52.3 kwa 100%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kipande kingine cha barabara hii ya pete ambacho kinatoka Ihumwa – Matumbulu – Nala chenye urefu wa kilometa 52.3. Sasa hivi utekelezaji upo 80% na tunatarajia kufika mwezi Machi, mwakani hiki kipande pia kitakuwa kimekamilika. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutuwezesha, wakandarasi wanapata fedha kwa wakati na kazi zinaendelea vizuri, sambamba na ujenzi wa airport ya Kimataifa ya Msalato na yenyewe kazi inaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika kujenga Makao Makuu yetu ya nchi hapa Dodoma, zimekuwepo na foleni hapa mjini, lakini katika Mpango huu ambao tumeujadili, tunapanga kujenga barabara ya njia nne mpaka sita kuanzia hapa Kimbinyiko, hapa nje ya Bunge kwenda hadi njia panda ya kwenda Ikulu – Chamwino kilometa 32. Sehemu nyingine zitakuwa ni njia nne, sehemu nyingine ni njia sita kulingana na usanifu ambao tumeufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapanga kujenga barabara ya njia nne kuanzia round about ya kuelekea Singida pale Machinga Complex kwenda mpaka eneo la Msalato ambapo barabara ring inakutana na hii barabara ya kutoka mjini kwenda Arusha. Vilevile kutoka Singida round about hapa mjini kuelekea Iringa Road tunapanga kujenga barabara ya njia nne mpaka kwenye barabara ya pete ambayo inatoka kule Ihumwa – Matumbulu kuelekea Nala. Mipango ni mizuri, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kwamba mipango hii iwe ni moja ya vipaumbele katika kusaidia kujenga Makao Makuu ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna Barabara ya Inner ring road ambayo tunategemea kuijenga kuanzia pale Machinga Complex - Iringa Road itapita maeneo ya kule juu ya jengo la Takwimu kuunganisha na kule upande wa Makulu ili kupunguza foleni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie baadhi ya barabara ambazo kwa kipindi cha mwezi uliopita tumepata advance payment ya shilingi bilioni 53.9. Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuwezesha. Pia namshukuru kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kuendelea kutupa ushirikiano mkubwa, kwa sababu barabara hizi ni barabara ambazo mmezisubiri muda mrefu, ni sehemu ya barabara ambazo zinahitaji shilingi bilioni 166 ili ziweze kupata advance payment kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea shilingi bilioni 53.9, tayari mkandarasi ameshapewa fedha kuanza ujenzi wa barabara ya Ubena - Zomozi – Ngerengere kwa Mheshimiwa Babu Tale na Mheshimiwa Innocent Kalogeris na barabara ya Ifakara – Bungu yenye kilometa 62.5 kwa Mheshimiwa Asenga pamoja na Mheshimiwa Kunambi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Barabara ya Ndungu – Mkomazi kule Same – Kilimanjaro kwa Mheshimiwa Mama yangu, Mheshimiwa Anne Kilango; Barabara ya Kibanda – Mwasonga – Kimbiji kule Kigamboni tayari mkandarasi ameshapata advance payment ameanza ku-mobilize, na barabara ya Nachingwea – Ruangwa yenye urefu wa kilometa 57.6 mkandarasi ameshapata advance kwa ajili ya kuanza kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kyerwa – Omurushaka kilometa 50 kwa Mheshimiwa Innocent Bilakwate; pia barabara ya Singida – Sabasaba – Sepuka – Ndago kule Singida – Kizaga, barabara katika Mji wa Mbeya kwa Mheshimiwa Spika pale na penyewe kuna changamoto kubwa ya foleni, napo mkandarasi tumempa fedha ili aendelee na kazi ya barabara ya Igawa – Songwe – Tunduma eneo la Uyole – Ifisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa Dar es Salaam, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wiki mbili zilizopita tumesaini na tumemkabidhi mkandarasi kuanza ujenzi wa Daraja la Jangwani. Daraja ambalo mvua zikinyesha Dar es Salaam sehemu ilikuwa inafunga lakini tunaenda kusahau, kwa sababu tunaenda kujenga daraja lenye urefu wa mita 390 na barabara za maungio mita 700 sawa na shilingi bilioni 97.1. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam tunao Mpango huu ambao tumejadili wa kujenga, kupanua barabara kutokea Mbagala Rangi Tatu kuelekea Vikindu. Mheshimiwa Ulega pamoja na Mheshimiwa Chaurembo na Wabunge hata wa Mikoa ya kule Lindi na Mtwara, pale eneo lina changamoto kubwa ya foleni. Hivi ninavyozungumza, kwenye shilingi bilioni 868.56 ipo package ya kwenda kujenga pale Daraja la Mzinga ili kuondoa bottleneck ya foleni ambayo iko eneo la Mbagala Rangi Tatu kuelekea Vikindu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango ya baadaye, mpango wetu ni kujenga barabara lanes za kutosha kama ilivyo barabara ya kutoka Kimara kuja Kibaha, basi kuanzia Mbagala Rangi Tatu mpaka eneo la Mwanambaya kule ili kuweza kufungua Jiji la Dar es Salaam kuelekea Mikoa ya Lindi pamoja na Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Miradi ya BRT wakandarasi wako site, kazi inaenda vizuri na barabara ya kuelekea Bagamoyo eneo la Basihaya Mheshimiwa Askofu Gwajima najua amefuatilia sana, tumefanya addendum ya kumwongezea mkandarasi kusanifu lile eneo la Basihaya tusahau mambo ya mvua ikinyesha mawasiliano ya barabara kukatika. Itajengwa vizuri pale ili maji yaendelee na safari yake ya kwenda baharini huku wananchi wakiendelea na mawasiliano ya usafiri na usafirashaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupunguza adha ya foleni kwa Mkoa wa Dar es Salaam, vilevile barabara ya Mwai Kibaki tunao mpango wa kuijenga njia nne kuanzia Morocco kwenda Mikocheni kule Kawe kuunganisha Lugalo, na kwenda nayo mpaka kule njia ya kuelekea White sands na kupandisha mpaka Afrikana, tunaamini mipango hii itasaidia sana kuifungua Dar es Salaam sambamba na kupanua barabara kuanzia Ubungo kwenda Kimara ili iungane na ile barabara ya njia nane kutoka Kimara kuelekea Kibaha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mikakati yetu ya kupunguza foleni, ipo barabara ya Victoria – Mpiji - Magohe – Bunju kwa Mheshimiwa Askofu Gwajima, pamoja na Ndugu yangu Mbunge wa Jimbo la Kibamba tunaendelea na mipango hiyo pamoja na barabara ya Kimara Bonyokwa na yenyewe iko mikakati yetu ya kupunguza foleni ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa vivuko, najua Waheshimiwa Wabunge ambao wanatoka maeneo ambayo wananchi wetu wanahitaji vivuko wamekuwa wakifuatilia kwa muda mrefu. Habari njema, namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha wiki iliyopita tumepata shilingi bilioni 8.87 kwenda kukamilisha vivuko ambavyo viko kwenye ukarabati na vivuko ambavyo vinajengwa vipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, ziara ambazo amekuwa akizifanya kwenye maeneo haya, alitoa maelekezo kwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametufanyia wepesi tumepata fedha hii tunaenda kukamilisha vivuko vipya; Kisolya – Lugezi ambacho… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia…
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwilo – Bukondo – Mafia – Nyamisati – Nyakaliro – Kome – Buyagu – Mbalika na vilevile tunaenda kukamilisha ukarabati wa vivuko MV. Nyerere – MV. Kome II – MV. Kilombero II – Mv. SabaSaba – MV. Old Ruvulu na MV. Ukala One. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)