Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru lakini nianze kwa kusema asiyeshukuru watu hata Mungu hawezi kumshukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatumia nafasi hii moja kumpongeza sana sana Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Maji kwa Mpango mzuri pamoja na kaka yangu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. Ninachotaka kukisema, nimesoma Mpango ambao nataka nilithibitishie Bunge na Watanzania kwamba Mpango umepangika kweli kweli, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii nayo kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri katika Mpango, pia katika suala zima la eneo letu la maji. Niseme kwamba maoni na ushauri tumepokea na tunajipanga kwa ajili ya utekelezaji zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa lolote lazima liwe na mwelekeo unaojulikana na unaotabirika. Taifa lolote lazima liwe na dira kujua limetoka wapi liko wapi na linataka kufika wapi? Taifa lolote lazima lione kesho likiwa leo, ndiyo maana Tanzania chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina dira, ina mwelekeo na sasa inachora ramani kwa ajili ya Tanzania kubwa tunayoitaka na maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema, tunapozungumzia suala la maji, huko nyuma na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, ilikuwa ikifika suala la maji katika hili Bunge lako Tukufu palikuwa hapatoshi. Bajeti ya Maji ilikuwa zikikataliwa siyo mara moja siyo mara mbili. Mwenyekiti ni shahidi, ipo miradi ambayo ilitolewa fedha nyingi sana hasa miradi ya vijiji 10, Mheshimiwa Katibu Mkuu Mstaafu kaka yangu Dkt. Kitila analifahamu miradi ambayo ilikuwa inafadhiliwa na World Bank. Ilifikia hadi wakati baadhi ya magari kwa maana ya wenzetu wa Wizara ya Maji, Wahandisi kila sehemu walikuwa wakipigiwa kero na kupewa lawama mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tarehe 22/4/2021 Dkt. Samia Suluhu Hassan alihutubia katika hili Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na alitoa maelekezo mahususi juu ya Wizara yetu ya Maji, alisema kwamba yeye ni mama na asilimia kubwa wanaoteseka juu ya adha ya maji ni akinamama. Hataki kusikia, hataki kuona wamama wa nchi hii wanateseka juu ya adha ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie ndugu zangu Wabunge, ukitaka kujua umefanikiwa ama haujafanikiwa, lazima ujifanyie tathmini wapi ulipotoka? Nataka niseme, kwa kipindi kifupi cha Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kazi kubwa imefanyika chini ya uongozi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ya Tanzania kwa mujibu wa TAMISEMI, tuna vijiji takribani 12,318. Kutokana na changamoto kubwa sana hasa eneo la vijijini mkaona haja juu ya uanzishwaji wa Wawakala wa Maji Vijijini kwa maana ya RUWASA, kwa kipindi hiki cha muda mfupi tumeshafika takribani vijiji 10,000 tumebakiza vijiji 2,000. Hii ni kazi kubwa ambayo imefanywa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, niliwahi kwenda Simanjiro kwa Mheshimiwa Olesendeka Mzee wangu, tuliwahi kuona akimama wanatembea zaidi ya kilometa 40 kwa punda hawana maji. Namshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani kwa muda wake mfupi, zaidi ya shilingi bilioni 42 zimewekezwa Simanjiro kwenye mradi wa Orkesument, Wanasimanjiro wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Kakonko hali ilikuwa ni mbaya. Moja ya changamoto kubwa sana ni suala zima la maji, kwa muda mfupi ambao Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia ndani ya miaka mitatu, leo Kakonko hana sababu ya kuukosa Ubunge. Hii ni kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda maeneo mbalimbali ya Longido, maeneo ambayo wananchi kule ni wafugaji ambao wanateseka, wanahangaika juu ya adha ya maji wao pamoja na mifugo yao, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza shilingi bilioni 16 Wanalongido leo wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini ambacho nachotaka kukisema? Wizara ya Maji huko nyuma ilikuwa Wizara ya kero na lawama, haya mageuzi ambayo yamefanywa, yamefanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenge wa Uhuru wa mwaka 2022, umeitangaza Wizara ya Maji ndiyo Wizara namba moja kwa kufanya vizuri hasa kwenye Miradi ya Maji. Mwaka huu World Bank ilianzisha programu ya P4R, zimeitwa nchi 42 tu zilishindanishwa na wakaitwa Mawaziri wa Fedha akiwemo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Waziri wa Maji zaidi ya nchi 42. Nchi ya Tanzania imetangazwa na World Bank, ndiyo nchi kinara kwa miaka miwili mfululizo juu wa uwekezaji wa miradi ya maji nchini Tanzania hasa maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge tusione haya, tusione aibu kuzungumza ndani ya Bunge, nje ya Bunge kazi kubwa iliyofanywa na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Bunge hili litaingia katika historia hasa katika suala zima la maji. Leo tumebakiza vijiji 2,000. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mama anajua changamoto wanazopata akinamama wenzie, kwa hivi vijiji 2,000 akaniambia mimi Waziri wa Maji, sihitaji asilimia, ninachotoka vijiji vyote vya Tanzania viweze kupata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitupatia fedha za UVIKO. Tumefanya miradi katika kila Jimbo kuhusu miradi ya UVIKO, lakini akaona haja na maelekezo yake tununue mitambo ya uchimbaji wa visima. Nini maana yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mitambo hii, katika kila Mkoa uwe na mtambo wake. Nini maana yake? Ni kwamba katika kila kijiji ambacho hakina maji twende tukachimbe maji. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, Waziri wa TAMISEMI kwa ushirikiano wake mkubwa, naamini kwa ushirikiano huu tunakwenda kumaliza matatizo ya maji katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, achana na hilo, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameenda mbali zaidi, siyo maeneo yote ukichimba kisima utapata maji. Yapo maeneo aina ya Chemba hayana maji chini ya ardhi lakini yanatambua nchi yetu si maskini juu ya unyeshaji wa mvua. Kuna haja juu ya uvunaji maji ya mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametununulia mitambo seti tano kwa ajili ya uchimbaji wa mabwawa katika kila Kanda ya Tanzania. Nataka niwaambie Rais aina ya Dkt. Samia Suluhu Hassan hapatikani kila mahali, Rais aina ya Dkt. Samia Suluhu Hassan; hapatikani kila wakati. Tumempata ndugu zangu Watanzania, lazima tumtumie kwa maslahi ya Watanzania katika kuhakikisha tunapata maendeleo makubwa katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania yetu, maendeleo yetu; ili tuweze kwenda, ni sawa na gari ambayo imenasa kwenye matope, hatuwezi kumwachia Rais wetu Dkt. Samia Suluhu peke yake. Mawaziri lazima tusukume, Waheshimiwa Wabunge lazima tusukume na Watanzania lazima tusukume, tutafika mbali kwa sababu ametutengenezea mazingira makubwa katika Taifa letu tuweze kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hamu yao Waheshimiwa Wabunge, wanatambua kabisa nchi yetu ya Tanzania tuna maziwa, tuna mito, kwa nini Watanzania wapate changamoto ya maji? Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Rais wa kusema na Kutenda. Ameianza ndoto ya kuhakikisha tunatumia maji ya Ziwa ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuhakikisha watu wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, seeing is believing, yaani kuona ni kuamini; amechukua maji ya Ziwa Victoria kutoka Mwanza ameyapeleka Tabora, ameyapeleka Igunga, ameyapeleka Nzega na sasa hivi ametupa maelekezo maji yale tunayapeleka Sikonge, Kaliua, Urambo kwa Mheshimiwa Mama Sitta. Mnataka Mheshimiwa Rais afanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maji tunayotoa Ziwa Victoria katika Jiji la Mwanza, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia maelekezo Wizara ya Maji, unapokuwa karibu na uwaridi lazima unukie. Haiwezekani wananchi wa Jiji la Mwanza wateseke juu ya adha ya maji ilhali ziwa lipo pale. Ametupatia fedha zaidi ya shilingi bilioni 70, tumejenga chanzo kikubwa cha Butimba, mradi umekamilika. Kazi iliyobaki ni kwa ajili ya usambazaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwambie Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula, baada ya dhiki siyo dhiki; baada ya dhiki ni faraja na faraja ni Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumempata Mkandarasi ambaye tumeshaanza kusainiana naye na tunakwenda kufungua mradi ule kwa ajili ya kufanya utandazaji na Mkandarasi ni SINOHYDRO. Maeneo ambayo hayana maji tunakwenda kuyatandazia ili watu waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, achana na hilo, tumepewa maelekezo kwa maeneo ya Katavi, Kigoma pamoja na Rukwa tuna Ziwa Tanganyika. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais Ziwa Tanganyika lazima litumike kwa ajili ya kutatua matatizo kwa wananchi. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tabasam, tafadhali kaa.

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ametupatia maelekezo juu ya kutumia maji ya Ziwa Tanganyika, yaende yakasaidie Katavi, Kigoma na Rukwa. Kama nilivyosema, seeing is believing. Mheshimiwa Kilumbe yupo, leo ukienda Kigoma tumeshayatumia maji ya Ziwa Tanganyika. Wana-Kigoma Ujiji wamepata mradi mkubwa zaidi ya shilingi bilioni 40 tumeweza kutekeleza na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uthubutu wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unapaswa kuungwa mkono. Yalikuwa maandiko na maazimio ya Bunge kila mwaka juu ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda Tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kila mwaka Bunge linaazimia juu ya ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa muda mfupi ametoa maelekezo na uthubutu wake wakasema bwawa tutajenga kwa fedha zetu za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa ametoa advance payment na ninavyozungumza Mkandarasi yupo site. Mradi utaweza kuhifadhi maji zaidi ya lita bilioni 190. Wana-Dar es Salaam na Pwani suala la changamoto ya maji linakwenda kuwa bye-bye kabisa juu ya kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana Waziri wa Fedha. Pamoja na mafanikio haya, wanasema ukimwona kobe juu ya mti, amepandishwa, hapandi mwenyewe. Wizara ya Fedha imefanya kazi kubwa na nzuri ya ku-support Wizara ya Maji kutokana na maelekezo na ushauri mkubwa wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kwamba tunatatua matatizo ya maji katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Wizara ya Maji kwa maelekezo na mienendo, lazima tukubali kubadilika. Tutumie teknolojia kwa mageuzi ndani ya Sekta yetu ya Maji. Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilalamika hasa juu ya suala zima la bili za maji. Ni haki ya mwananchi kutumia maji, lakini mwananchi naye asisahau ana wajibu wa kulipia maji. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, maelekezo yake aliyoyatoa kwamba ni marufuku kwa Mwananchi wa Tanznaia kumbambikizia bili za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi uelekeo wa Wizara ya Maji tunakwenda kutumia prepaid meter kama TANESCO, kwamba tunakwenda kumfungia mwananchi LUKU ya maji. Mwananchi anataka maji ya shilingi 10,000 analipia shilingi 10,000, wala hakutakuwa na nongwa. Hayo ndiyo maelekezo, mageuzi na matokeo ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tunajua mazingira ya sasa tunakuwa na mabadiliko ya tabianchi. Ukiangalia Sera ya Wizara ya Maji ni tangu mwaka 2002. Kuna haja juu ya uanzishaji wa sera mpya. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametupatia maelekezo, sasa tunakwenda kuanzisha sera mpya ya maji ambayo itaendana na mazingira ya sasa na ya kuweza kuwashirikisha vizuri wadau mbalimbali wa maendeleo na ambayo tutakwenda kufanya mageuzi makubwa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)