Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nami nitumie fursa hii kukushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia katika ajenda hii iliyopo Mezani. Pia naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema na Mwingi wa Ukarimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie pia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo, dira, uongozi wake imara na kwa namna ambavyo amedhamiria kabisa katika kujenga upya sekta hizi za uzalishaji ikiwa ni pamoja na Sekta ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja iliyowekwa Mezani na wabobezi wawili hawa; Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipango na Uwekezaji na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na timu nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepata maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge kadhaa. Wengi wameonesha namna ambavyo wangetamani mambo katika Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi yaende. Sisi tumechukua maoni haya, tunakwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuonesha namna ambavyo tunakwenda kuyafanyia kazi pale mbele nitaonesha na nitaeleza namna Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilivyojipanga kimkakati kwenye kuhakikisha kwamba Sekta hii ya Mifugo na Uvuvi inafanya vyema katika kuinua hali za Watanzania na katika kuweka mchango mpana zaidi kwenye pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa ilitokea hoja, na kabla sijaendelea ningetamani sana kwa ufupi nijaribu kuiweka hoja ile vizuri. Katika wachangiaji wazalendo wanaotamani kuona kwamba, tunatumia vyema rasilimali za nchi yetu kwenye kujenga Taifa letu na kuinua hali za Watanzania, walipata nafasi ya kueleza kwamba, kwa nini tunayo maziwa, bahari kubwa na mito lakini bado tunaagiza samaki wengi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie Watanzania na Bunge lako kwamba, tunathamini mchango ule na kwa hakika tunajua ya kwamba, usemaji ule umetokana na ukweli wa kwamba wanatamani kwa nia zao za kizalendo waone maziwa, mito na bahari yetu tukizalisha zaidi. Tunakubaliana na ukweli huo, lakini nitoe takwimu sahihi ya kwamba, mpaka mwaka 2018, nchi hii ilikuwa ikiagiza samaki zaidi ya tani 22,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya mabadiliko makubwa sana ya kimkakati. Lengo la mabadiliko yale ni kutaka kuonesha kwamba tunatoa fursa ya shughuli za ufugaji wa samaki katika nchi ili zishamiri na hizi nitazieleza huko mbele. Ndiyo maana tukatoa vizimba vingi na tunaendelea kutoa vizimba hivyo. Matokeo ya vile vizimba yako wazi. Ukienda pale Mwanza yanaonekana wazi. Watu wa Ilemela, vijana wamefanya kazi nzuri sana na tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, imekuwa ni sehemu ya mfano. Huko mbele kidogo nitaeleza jambo hili. Ukweli ni kwamba hivi sasa katika nchi siyo zaidi ya tani 9.5 tu za samaki zinazoingia. Tena tani hizi 9.5 za samaki zinazoingia ni samaki aina maalum, wengi katika hao sisi hatuzalishi katika Taifa letu. Kwa mfano, samaki aina ya salmon ambao hawapatikani hapa, wanatoka katika nchi nyingine duniani. Wapo wageni wanaokuja katika Taifa letu ambao wanahitaji aina hiyo ya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoka tani 22,000 mpaka tani 9.5 tu, kihisabati inaelekea kama ifuatavyo: kilo moja ya samaki imported ana gharama ya mpaka dola 4.7. Sisi peke yetu fisheries tunachukua dola 2.5, bado kuna gharama za bandari, usafirishaji na kadha wa kadha inafika dola 4.7. dola 4.7 ukiibadilisha inakwenda takribani shilingi za Kitanzania 12,700 kwa kilo moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiichukua kilo moja shilingi 12,700 unaweza ukaona kwamba, samaki huyo ukimweka sokoni hauziki. Ndiyo maana nikasema ya kwamba, tulilifanya jambo hili kimkakati kwa lengo na dhamira ya kutoa nafasi ya ufugaji wa samaki nchini uweze kushamiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, tumepata rai kwa sababu mahitaji ya samaki nchini bado ni makubwa sana. Uzalishaji wetu ni takribani tani 500,000, mahitaji ni tani zaidi ya 1,000,000. Kwa hiyo, samaki wamekuwa gharama kubwa sana na watu walio wengi hawamudu kununua kitoweo cha samaki. Wataalamu wangu wamenishauri na bado tunafanya mazungumzo na wenzetu wengine hasa wadau ya kwamba nini tufanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sisi samaki tunaofuga na tunaoshamirisha kufuga hivi sasa ni samaki aina ya Sato na Kambale, lakini vipi kama vibua vikitazamwa uwezekano wa kuja kupunguza hili gap? Tumekubaliana ya kwamba tuendelee kufanya mashauriano na wadau mbalimbali ili kusudi tuone uwezekano wa kuweza kuwasaidia Watanzania kwenye kupata samaki kwa bei nafuu, bila ya kuathiri shughuli zetu tunazozisimamia za ufugaji wa samaki aina ya Sato na Kambale ambao hawa tumewapa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya vizuri sana katika export ya samaki na tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ukweli kwenye export ya samaki na nyama, Taifa letu linafanya vizuri sana. Hivi sasa ni fursa kubwa Waheshimiwa Wabunge na tumekuwa tukipokea wageni wengi sana wanaotaka kuwekeza kwenye eneo hili. Ukweli ni kwamba kila mmoja anajionea nyama hii leo ni fursa kubwa huko ulimwenguni ya kutoka hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia tulikuwa na tani 1,700. Leo tuna tani 14,000 nyama ya Tanzania inauzwa ulimwenguni kote. Ni mafanikio makubwa. Tunamkaribisha kila mmoja mwenye nia njema ya kutaka kuwekeza katika eneo hili, milango ipo wazi. Watu wanapenda mbuzi na nyama ya kutoka Tanzania. Karibuni tuwekeze ili kusudi tuweze kujenga Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wa kuhakikisha kwamba tunachukua hii fursa na tunaitumia vyema, tulielekezwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwawezesha vijana wa Kitanzania. Miradi ya BBT mifugo na uvuvi imefanya vizuri sana. Wale vijana waliokuwa wanafanya unenepeshaji wa mifugo ni kwamba mpaka hivi sasa wamefanikiwa kuuza ng’ombe wote na wamepata faida zaidi ya shilingi 130,000,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo vijana 158 ambao tumewakopesha sasa shilingi 1,100,000,000 kupitia Benki yetu ya Kilimo. Tunakwenda kuwapa vitalu katika eneo la Kitengule kule Kagera na Kagoma. Kila mmoja ekari 10, anakwenda kufanya kazi ya unenepeshaji. Kila kikundi cha vijana kinakuwa na vijana watano na jumla ya vikundi 25. Bado tumeichukua sera hii tumeipelekea mikoani pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia tunakwenda katika Mkoa wa Tabora, Pwani, Arusha, Morogoro na Mtwara kwa sababu kule Mtwara ipo fursa ya wenzetu wa Comoro wanahitaji sana nyama ya kutoka Tanzania na kutoka Mtwara kwenda Comoro ni karibu zaidi. Kwa hiyo, tunaichukua fursa hii na kuipeleka jumla ya fedha shilingi bilioni 4.2 tumeziweka huko ili kusudi vijana waweze kufanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sera ya Uchumi wa Bluu. Wabunge wengi wameichangia sera ya Uchumi wa Bluu, kwa kweli tunafanya vizuri. Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko imeshafika 70% hivi sasa na tunakwenda tena kutengeneza Bandari nyingine pale Bagamoyo. Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko itakuwa na eneo la uchakataji wa samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia yetu hapa ni kuweza kuchukua fursa ile ya Bahari Kuu. Meli zinazovua kule Bahari Kuu ziweze kuja katika bandari yetu, zishushe samaki, tupate faida ya kutoa huduma mbalimbali na eneo lile litakuwa pia na Kiwanda cha Uchakataji wa samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda vyema katika eneo hili la Uchumi wa Buluu. Kwa kumalizia tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia chanjo kwa wote. Imechangiwa sana mambo ya chanjo hapa shilingi bilioni 28. Kwa muda mrefu chanjo iliachwa, ilikuwa inatekelezwa na Sekta Binafsi, Serikali haikuwa imeweka mkono wake. Hivi sasa tunakwenda kuchanja na kila mfugo utachanjwa katika Taifa letu. Fedha ya Serikali shilingi bilioni 28 imewekwa kuhakikisha kwamba, tunaondoa makanjanja. Wafugaji wa Taifa hili wamepigwa sana dawa ambazo siyo za kweli na hazina uhakika. Sasa, tunakwenda kurekebisha jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia shilingi bilioni 450 ya modernization tunakwenda kujenga upya sekta yetu ya maziwa. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameridhia shilingi bilioni 450 zitakazokwenda katika maeneo ya uzalishaji mkubwa wa maziwa nchini ambao tutakwenda kubadilisha sana eneo hili la maziwa ili Watanzania waweze kutumia fursa ya uchumi wa maziwa tujitosheleze wenyewe na ikiwezekana na sisi tuweze kusafirisha nje ya mipaka ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, siyo tu maziwa katika matoleo yetu na ninaamini kabisa kwa namna ambavyo dira hii imetengenezwa, tunakwenda pia kuchechemua na kuzalisha upya breed mpya na kuendeleza eneo la chanjo na miundombinu ya mifugo katika bajeti ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa World Bank ambao utakuwa na zaidi ya shilingi bilioni 500. Hizi zitakwenda katika maeneo ambayo yanakwenda kufanya shughuli ya ng’ombe na mbuzi wa nyama tu. Lengo na dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa ni Taifa Kiongozi kwenye eneo la mifugo, uvuvi na samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)