Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipatia nafasi. Kwanza kabisa nawashukuru sana Mawaziri wote wawili waliowasilisha taarifa yao, Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango. Kipekee kabisa nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ameendeleza kuikuza Sekta ya Madini. (Makofi)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, kwa mamlaka ya kiti ninaongeza muda mpaka tumalize shughuli zetu ambayo haitazidi saa 2.30 kutokana na umuhimu wa ajenda yetu na Road Map ya Taifa letu. Kwa hiyo, tuvumilie. Tunapata mambo muhimu ya kurudi nayo majimboni. (Makofi)

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi nianze kwa kuelezea jinsi ambavyo Mpango huu umeakisi maendeleo ya Sekta ya Madini. Katika historia ya Wizara ya Madini miaka yake yote, Wizara hii haijawahi kupokea fedha nyingi za bajeti kama ambavyo imepokea kipindi cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Wizara ya Madini imeongezeka kutoka shilingi bilioni 89 mpaka kwenda shilingi bilioni 231 na kiasi kikubwa cha fedha kimeelekezwa kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina. Pamoja na utafiti wa kina, pia kiasi kikubwa cha fedha kimeelekezwa GST ambayo imekuwa ni ushauri wa Waheshimiwa Wabunge kwa sababu GST ndiyo moyo wa Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utafiti wa kina, pia kiasi kikubwa cha fedha kimeelekezwa GST ambayo imekuwa ni ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu GST ndiyo moyo wa Wizara ya Madini. Kwa hiyo, tunategemea kupitia GST baada ya kufanya utafiti wa kina tutawaongoza vizuri Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti iliyoongezeka, zaidi ya shilingi bilioni 115 imeelekezwa kwenda GST ambayo itafanya kazi zifuatazo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ya kwanza itakwenda kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa, ambayo itajengwa hapa Dodoma, Geita, na Chunya ili kuwaongoza vizuri wachimbaji ambao wamekuwa na changamoto kubwa ya kupeleka sampuli zao, wengine kwenda mpaka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika historia ya Taifa hili, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anakwenda kujenga maabara kubwa na ya kisasa hapa Dodoma ambayo itawahudumia wachimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika kulitekeleza hilo, Wizara ya Madini imejiwekea mkakati wa kuhakikisha kwamba tunapima nchi yetu kwa kufanya utafiti wa kina na kuwaongoza vizuri wachimbaji. Mpaka sasa hivi tumekwisha kufanya utafiti wa kina kwa 16% ya nchi yetu ya Tanzania. Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumewezeshwa fedha ambazo tutakwenda kununua helkopta kwa ajili ya kusaidia upimaji wa madini kwa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tunao mradi ambao utakwenda kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina. Tunao mradi ambao tutautekeleza katika mwaka huu wa fedha 2024/2025, ambao utakwenda kuligusa eneo la kilometa za mraba 165,934 za nchi yetu ya Tanzania, sawa sawa na 18% ya nchi nzima. Tutapima kupitia utaratibu huo. Tunaamini kabisa tukiyafanya haya, tutakuwa tumewaongoza vizuri wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa Sekta ya Madini katika pato la Taifa umeendelea kuongezeka. Mwaka 2022 Sekta hii ya Madini ilichangia kwa 7.2% kwenye pato la Taifa. Leo tunavyozungumza, Sekta hii ya Madini inachangia kwa 9.0% na tumewekewa malengo na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, kwamba ifikapo mwaka 2025 tuwe tunatoa mchango kwenye pato la Taifa kwa zaidi ya 10%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari njema ni kwamba, tumeanza hatua moja baada ya nyingine kufikia malengo hayo. Hatua ya kwanza ni kwenye hatua ya ukusanyaji wa maduhuli. Baada ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini, na tukaanzisha masoko na vituo vya ununuzi, sasa hivi nchi yetu tumeanza kuona manufaa ya Sekta ya Madini kutoa mchango wake kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015/2016, Sekta ya Madini iliingiza katika Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi bilioni 161 kwa mwaka mzima. Baada ya kufanya marekebisho ya sheria chini ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tukaweka na vituo vya ununuzi na masoko ya kuuzia madini, katika siku 121 tu za mwaka huu wa fedha, Sekta ya Madini imeingiza katika Mfuko Mkuu shilingi bilioni 354. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunakusanya shilingi trilioni moja kuingiza katika Mfuko Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, katika masoko yetu ya madini na vituo vya ununuzi 102, jumla ya fedha ambayo imekuwa transacted ni zaidi ya shilingi 1,700,000,000,000 kwa mwaka. Hii ni kuonyesha kwamba sekta hii inaendelea kukua siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeshuhudia mchango mkubwa wa Sekta ya Madini katika upatikanaji wa fedha za kigeni. Katika mwaka wa fedha uliopita 2023/2024, Sekta ya Madini imechangia katika upatikanaji wa fedha za kigeni kwa zaidi ya 56%, na tumefanya mauzo ya bidhaa nje ya nchi ya zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 3.1, ambayo imesaidia sana katika kuchochea uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo katika Mpango huu, pia tunazungumza mchango wao mkubwa katika kuimarisha Sekta ya Madini. Sasa hivi kazi ambazo tunazifanya ni kuhakikisha kwamba, kwanza tunawatengea maeneo wachimbaji wadogo, na hii inatokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu leseni, Mheshimiwa Rais alielekeza leseni zote ambazo hazifanyiwi kazi na maeneo yote ambayo yamehodhiwa na watu, tuweze kuyafuta na kuyatenga kwa ajili ya machimbaji wadogo. Tumefuta leseni zaidi ya 2,648, ambapo sasa hivi tumeyatenga maeneo hayo kwa ajili ya wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, pia kupitia STAMICO tumenunua mitambo ya kuchoronga ambayo ni Drilling Rigs, ambazo zitafika tarehe 15 mwezi huu wa 11, 2024, na lengo lake ni kuwasaidia wachimbaji wadogo kuondokana na gharama kubwa ambayo wanaitumia sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchimbaji mdogo sasa hivi akienda kuchoronga kwenye shimo la mita 100, akienda kumtafuta mtu mwenye mashine anayefanya kibiashara, atatumia zaidi ya shilingi milioni 25 kwa shimo la mita 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya Mheshimiwa Rais kupitia STAMICO, sasa hivi mchimbaji mdogo ana uwezo wa kuchoronga mita 100 kwa shilingi 10,700,000 na fedha inayobaki ni ruzuku ambayo Mheshimiwa Rais ameitoa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili tuweze kuwasaidia na wenyewe pia waweze kufikia malengo. Sambamba na hilo pia hiyo inaendana na huduma za ughani ambazo tunazitoa kwa wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la Madini Mkakati. Wote tunafahamu kwamba sasa hivi dunia inauhitaji mkubwa wa Madini Mkakati. Mahitaji ya Madini Mkakati ifikapo mwaka 2050, inatazamiwa kuwa ni zaidi ya mara 150 ya mahitaji ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumebarikiwa kuwa na Madini Mkakati, na katika eneo hili, katika Madini ya Kinywe (Graphite) ambayo hivi sasa yana uhitaji mkubwa sana duniani, kwa zaidi ya tani 6,500,000 kwa mwaka. Nchi inayoongoza kwa uzalishaji ni nchi ya China. China wanazalisha 64% ya mahitaji yote ya Graphite duniani, lakini kwa Afrika, anayeongoza kwa uzalishaji wa Madini Kinywe ni nchi ya Madagascar, anazalisha 13% ya mahitaji yote ya Madini Kinywe duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wa pili ni Msumbiji, anazalisha 10% ya mahitaji yote ya Madini Kinywe duniani, na wa tatu ni Tanzania, ambaye anazalisha 0.64%. Hii 0.64% hapa, huyu ni mzalishaji mzawa ambaye yupo kwa Msisi pale Handeni Tanga, anaitwa God Mwanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi zaidi 10 ya Madini Kinywe ambayo haijaanza kufanya kazi. Ikianza kufanya kazi Tanzania itakuwa ni kinara wa uzalishaji wa Madini Kinywe hapa Afrika, ikiwapiku Msumbiji pamoja na Madagascar, kwa reserve ambazo tunazo ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la manunuzi ya dhahabu yanayofanywa na Benki Kuu ya Tanzania, imekuwa ni hoja ya Waheshimiwa Wabunge. Mheshimiwa Rais alitupa maelekezo ya kwamba, haiwezekani nchi yetu ya Tanzania imejaaliwa madini ya kutosha lakini hatuna akiba ya kutosha ya madini ya dhahabu, na hivyo kusababisha kuwepo na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi, na hasa kukosekana kwa Dola za Marekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulifanya marekebisho ya sheria; kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Madini kilirekebishwa na kutaka kila anayesafirisha madini nje ya nchi kutenga 20% ya madini yote kwa ajili ya kumuuzia BoT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali palikuwepo na sintofahamu, tumeiweka sawa. Habari njema, kwa hivi sasa Afrika, anayeongoza kuwa na akiba ya dhahabu ni nchi ya Algeria ambaye ana akiba ya tani 173 ya dhahabu, lakini wa mwisho wa 10 ni Msumbiji, ambaye ana tani 3.6 za dhahabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuanza kununua dhahabu katika nchi yetu ya Tanzania, kuanzia Oktoba tarehe mosi mpaka leo, nchi yetu imeshanunua, kwa maana ya BoT, dhahabu tani moja ndani ya mwezi mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni mafanikio makubwa sana na tunategemea kwamba ndani ya muda mchache ujao tutaingia katika 10 bora kuwa na hifadhi ya dhahabu kupitia BoT. Haya yatakwenda kusaidia kuimarisha uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo ninataka nilisemee, ni kupitia STAMICO. Sasa hivi tunajipanga katika makaa ya mawe pale Kiwira, tuweze kuja na mradi wa uzalishaji wa umeme na tumepata kampuni...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, malizia.

WAZIRI WA MADINI: ...ambayo itazalisha zaidi ya megawatts 2,000, ambayo itasaidia sana katika kuingiza kwenye gridi yetu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)