Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na quotations mbili; ya kwanza iliwahi kutolewa na Nelson Mandela, na quotation ya pili iliwahi kutolewa na Mahatma Ghandhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nelson Mandela aliwahi kusema, “Uongozi mzuri unahusisha kuwajibika kwa heshima na uaminifu.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahatma Gandhi aliwahi kusema; “Uadilifu ni kufanya yaliyo sahihi, hata kama uko peke yako.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nianze na quotations hizi mbili. Taifa letu ni Taifa changa linaloendelea kupiga hatua. Tunatambua zipo changamoto ambazo zinaweza kuibuka katika maeneo yetu, lakini msingi wa Taifa letu, Baba wa Taifa ametuhusia, ni umoja na mshikamano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa sisi viongozi wenyewe, kwa viongozi wa kuchaguliwa na viongozi wa kuteuliwa tukavutana wenyewe kwa wenyewe, lazima tutambue kwamba matamanio ya Taifa letu hayawezi kufikiwa kwa mivutano baina yetu sisi viongozi wenyewe, hatuwezi kufikia matamanio hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyakati hizi ninawaomba sana viongozi tuheshimiane, kila mmoja kwenye nafasi yake. Kwa sisi viongozi wa kuchaguliwa na viongozi wa kuteuliwa, ni vyema sana tukavumiliana na kuheshimiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi huu siyo wa kwangu, ni msingi ambao tumeachiwa na Baba wa Taifa. Ili tuweze kupiga hatua kama Taifa ni lazima tuvumiliane, ni lazima tuheshimiane kama Taifa. Nilisema nilianze hili kwa sababu Mheshimiwa Sendeka amezungumza hapa kuhusu changamoto zilizoibuka Simanjiro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua alinipigia, nami nilimpigia Mkuu wa Mkoa kujua kitu gani kinaendelea katika Mkoa huo wa Manyara, lakini niliarifiwa kwamba Mkuu wa Mkoa amepokea taarifa kutoka kwa Katibu wa CCM Mkoa pamoja na Mwenyekiti wa Chama kwamba kuna vurugu zinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii ilithibitishwa kwa picha za video pamoja na picha zilizopigwa katika eneo la tukio ambazo zilionyesha watu wamepasua, wamevunja ofisi pamoja na kupasuana na sime. Hali hii ndiyo ilisababisha Mkuu wa Mkoa kuamua kuchukua hatua hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuwasisitiza viongozi tuheshimiane. Ni vyema tukaheshimiana, kwa sababu msingi wa Taifa hili kesho tutaulizwa. Kama tutakuwa tunavutana na maendeleo yatachelewa. Huo ndiyo ukweli. Wewe utaamua kuvuta huku na mwingine atavuta huku, maendeleo yatachelewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana viongozi, hasa kipindi hiki kuelekea kwenye chaguzi mbalimbali, tuheshimiane. Nataka niwathibitishie, viongozi hawa wa mikoa na wilaya wanafanya kazi kubwa sana. Wakurugenzi wa Halmashauri wanafanya kazi kubwa sana kwa Taifa hili. Ni vyema tukiheshimiana, tutaweka mipaka ya utendaji ili kila mmoja wetu ajue wajibu wake katika kulitumikia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, misingi hii ni ya Baba wa Taifa. Ninawaomba kila mmoja wetu kujikumbusha kusoma misingi hii. Nyakati za TANU, wakati kinaanzishwa chama kimoja, nyakati za utawala wa chama kimoja, na hata wakati wa kuanzishwa Mfumo wa Vyama Vingi miaka ya 1990, mambo haya yalisisitizwa sana na Baba wa Taifa. Kwa hiyo, nawaomba sana viongozi tuheshimiane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyakati zote za utendaji wa kazi, pale tunapowahudumia Watanzania, kama sisi wawakilishi wa wananchi, lakini pia wale waliokasimiwa mamlaka na Mheshimiwa Rais, ni vyema sote kwa pamoja tukajikita katika misingi ambayo Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia amesisitiza katika nyakati zote za uongozi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuchangia. Nachukua fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Sisi tunatambua kwamba TAMISEMI ni Wizara nyeti na Wizara muhimu ambayo inaweza kusogeza mbele maendeleo ya Taifa letu. Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa 2025/2026, unalenga kujenga uchumi shindani, uchumi jumuishi na wenye viwanda kwa maendeleo ya watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu ni wa mwisho katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa miaka mitano. Mpango huu una dhamira ya kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia ukuaji wa kiuchumi unaogusa maisha ya kila mmoja wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ustawi wa wananchi umezungumzwa sana katika vitabu mbalimbali. Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezungumza kuhusu ustawi wa wananchi. Unaposoma kuanzia Ibara ya nane na kuendelea, inazungumza kuhusu ustawi wa wananchi katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hulka ya kiongozi yeyote, kiongozi wa watu, hujikita katika mambo makuu yanayohusu ustawi wa wananchi wake. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema, “The purpose of development is people.” Maendeleo ya kweli ni lazima yajikite katika misingi ya kuwaangalia Watanzania au kuwaangalia wananchi katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ni dhahiri kabisa, kazi anayofanya Rais wetu imejikita moja kwa moja katika kutafsiri ustawi wa Watanzania katika maeneo yao yote. Sisi tunaona namna gani Watanzania wanakuwa na furaha na Serikali yao. Hakuwezi kufanyika maendeleo kama Watanzania au wananchi husika hawana furaha katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanafalsafa na Mwanamapinduzi Che Guevara aliwahi kusema; “The true revolutionary is guided by great feeling of love.” Hili tunaliona kwa Rais Dkt. Samia. Mapenzi yake kwa Watanzania katika ujenzi wa shule mbalimbali, ujenzi wa vituo vya afya, na uboreshaji wa miundombinu. Eneo hili Rais Dkt. Samia amelitendea haki kwa Watanzania, na sisi ndiyo sababu tunasema kazi anayoifanya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia, ni mambo ya msingi ambayo Baba wa Taifa aliyaasisi kwa Taifa letu hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo Baba wa Taifa aliyapigia kelele, mimi na ninyi ni mashahidi. Wakati wa Mapinduzi mbalimbali yaliyotokea duniani, msingi wa Mataifa katika maeneo hayo ni wananchi. Wakati wa kupigania uhuru wa Taifa hili, msingi wa Taifa letu, wakati Baba wa Taifa na waasisi wa Taifa hili wanapigania uhuru wa Taifa letu, ilikuwa ni msingi kuhusu ustawi wa Taifa letu hili Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mapinduzi ya Serikali za Mitaa chini ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tuliweka misingi ya uwajibikaji na utumishi ulioweka kipaumbele mahitaji ya wananchi. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema, “Uhuru wa kweli ni kuwa na uwezo wa kuwahudumia watu wetu kwa njia bora kabisa.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni Dhahiri, kama kuna mwakilishi yeyote wa wananchi, yeye anafikiria kuhusu maisha yake kuliko maisha ya Watanzania, basi huyo amekosea. Lazima nichukue fursa hii kuwapongeza. Sijawahi kuona Wabunge wanachangia vyema kama kipindi hiki cha kushauri Serikali kuhusu eneo hili la Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa Wabunge ndiyo umesababisha mafanikio makuu ya Serikali ya Awamu ya Sita. Lazima tukiri, katika nyakati ambazo hazijapata kutokea kabisa, Serikali imefanya kazi kubwa ya kuimarisha mifumo ya utolewaji huduma kwa wananchi wa Tanzania. Leo hii hakuna Mbunge hata mmoja hapa anayeweza kusimama akasema kwamba kipo kijiji, kijijini kwake kule katika eneo la wananchi wake, ambako Serikali haijapeleka hata senti tano, hayupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi huu ni msingi ambao Rais wetu amedhamiria kwenda kuufikisha katika maisha ya Watanzania wa kawaida kabisa, na msingi huu nimetangulia kusema kwamba uliasisiwa na Baba wa Taifa, ukaendelezwa na marais wote waliotangulia baada ya Baba wa Taifa; Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Awamu ya Tano na sasa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia anafanya mambo ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza alitamani kuyafanya katika nyakati zake. Nimeona hapa nizungumzie mambo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la elimu, Baba wa Taifa alizungumza sana katika hotuba zake kuhusu elimu. Kwenye eneo hili Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita amejikita katika kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata elimu. Mitazamo ya Rais Dkt. Samia ninaifananisha na mitazamo iliyowahi kutolewa na Mheshimiwa Rais wa kwanza mweusi kule Afrika ya Kusini ambaye aliwahi kusema, “it is not beyond our power to create a world in which all children have access to a good education.” Msingi huu anaufanya Rais Dkt. Samia, na tunaona kwamba katika kila jimbo la nchi hii Rais Dkt. Samia amefika na ameweka fedha katika maeneo ya miradi ya elimu msingi na elimu sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia ameweka mpango imara wa kuimarisha na ujenzi wa shule katika maeneo mbalimbali nchini. Rais Dkt. Samia amejenga shule 380 za msingi katika maeneo mbalimbali nchini, amejenga shule za sekondari 830, lakini pia kati ya shule hizo kuna shule 26 maalum zenye vipaji kwa ajili ya watoto wa kike ili kuweza kuwajenga na kuwanyanyua. Rais Samia amejenga madarasa 4,411, amejenga madarasa ya awali 556.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi, kila Mtanzania ni shahidi. Katika Taifa letu tangu tupate uhuru vituo vyetu vya afya na hospitali zetu za wilaya hazikuwahi kuwa na majengo ya dharura, wala hazikuwahi kuwa na majengo ya wagonjwa mahututi. Aliyelifanikisha hili siyo mwingine ni Rais Dkt. Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii zipo halmashauri ambako kuna mitambo ya kuzalisha hewa tiba. Hewa tiba hizi tuliziona tu kwenye hospitali za rufaa na hospitali za mikoa, lakini hili limefanywa na kutekelezwa na Rais Dkt. Samia. Katika kipindi kifupi Serikali ya Rais Samia imejenga hospitali za wilaya na halmashauri zaidi ya 129, imekarabati hospitali kongwe 50, imejenga vituo vya afya 367; na kwa maelekezo yake Rais Dkt. Samia kila Mbunge inatakiwa atengewe fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo kimoja kipya cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani, leo wakati nazungumza na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, amenithibitishia kwamba leo wanaendelea na vikao, lakini atatoa taarifa ndani ya Bunge lako Tukufu ni lini fedha hizi zitaingia TAMISEMI ili tuweze kuzipeleka katika halmashauri zote nchini ili kila Mheshimiwa Mbunge aweze kupatiwa kituo kipya cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya miundombinu kazi kubwa imefanyika. Msingi wa uboreshwaji wa miji na majiji ni fikra za Rais wetu, Dkt. Samia. Naomba nikuthibitishie, kwamba Mheshimiwa Rais ametukabidhi zaidi ya shilingi tilioni 2.9 ambazo zinakwenda kuboresha miji na majiji, ujenzi wa masoko, ujenzi wa barabara mbalimbali na ujenzi wa stendi. Kwa Dr es Salaam ameelekeza zijengwe barabara kilometa 250 ili kila kona ya Dar es Salaam iwe na barabara kiwango cha lami. Eneo hili litagusa maeneo kote nchini katika mikoa yote 26, kwenye majiji na kwenye miji. Miradi hii ambayo ameibuni mwenyewe Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, itawahudumia Watanzania katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi, lakini naomba niunge mkono hoja na ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia. (Makofi)