Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote, naomba nikushukuru wewe pamoja na wasaidizi wako, kwa maana ya Wenyeviti wetu wa Bunge kwa jinsi ambavyo mmeendesha mjadala huu vizuri sana. Nawashukuru tena Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa jinsi walivyotoa maoni yao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia maoni yao kwenye kurasa zote 79, kwa kweli maoni yao ni mazuri na tumeyachukua. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mpaka tunamalizia na Mheshimiwa Ole-Sendeka. Tulianza na Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, na tumepata wachangiaji 84.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wenzangu kwa jinsi ambavyo wamejibu hoja na kutoa maoni yao na kueleza jinsi ambavyo Serikali inafanya kazi, wamefanya kazi yangu iwe rahisi sana katika kuhitimisha mjadala huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba, ofisi yangu hii ambayo ninaisimamia haiwezi kufanikiwa bila uhodari na ushupavu wa Waheshimiwa Mawaziri, kwa namna ambavyo wameonesha hapa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa ushirikiano ambao tunao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unavyofahamu, Wizara ya Fedha na ofisi yangu kwa kweli ni mapacha. Tangu nichaguliwe kwenye nafasi hii Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amenipa ushirikiano sana, tunashirikiana kwa karibu, ni mtu muungwana sana, Mungu ambariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha duniani kote anapimwa kwa microeconomic fundamentals. Tangu awe hapo uchumi wetu ni tulivu, na hizo ndizo sifa kubwa za kumpima Waziri wa Fedha popote duniani. Kwa hiyo, mnyonge mnyongeni, lakini haki yake lazima apewe. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amefanya kazi nzuri katika kusimamia uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa kazi nzuri ambayo anaifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi Waheshimiwa Mawaziri walivyozijibu hoja hapa, walivyotoa maoni yao na walivyopokea michango ya Waheshimiwa Wabunge utakubali kwamba una Serikali imara sana. Yote haya ni kwa sababu tunaye kiongozi shupavu ambaye anatusimamia. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaenda kisekta kwa sababu Waheshimiwa Mawaziri wameshakueleza. Tumepokea michango na mapendekezo 96 kutoka kwenye Kamati yetu ya Bajeti, na yote ni ya maana. Tumepokea michango 84 kama nilivyosema ambapo maoni hayo yapo katika sekta mbalimbali. Kwenye maoni ya Waheshimiwa Wabunge unaona kabisa kwamba yanaakisi aina ya vipaumbele ambavyo Serikali inavitekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea maoni mengi zaidi kuliko yote kwenye eneo la kilimo, mifugo na uvuvi. 15% ya michango yote imekwenda huko, inafuatiwa na barabara pamoja na miundombinu 13%, tunakwenda kwenye nishati, madini, uchumi, uwekezaji, viwanda na biashara pamoja na elimu, yote hiyo inaakisi aina ya vipaumbele ambavyo tunavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza wakati ninawasilisha mapendekezo haya na jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge wameeleza, Mpango huu ambao tunaupendekeza utakuwa ni wa mwisho katika kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano, lakini pia ni Mpango wa mwisho kwenye kutekeleza Dira yetu ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025. Hivyo ni muda mwafaka wa kufanya tathmini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapokuja mwezi wa Nne wakati wa bajeti tutaeleza tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano. Kupitia kikao hiki, Waheshimiwa Mawaziri wameshaeleza mafanikio kwenye sekta mbalimbali. Niongeze matatu tu katika ya yale ambayo wameyasema. La kwanza, kwenye aspect ya maendeleo ya watu, ambao ni sehemu kubwa sana ya Mpango, ni muhimu kuzingatia tumetoka wapi na tupo wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotoka. Ni kwamba, kati ya wanafunzi 100 waliokuwa wanamaliza darasa la saba ni wanafunzi 20 pekee ndio waliokuwa wanajiunga na shule ya sekondari. Tunapozungumza leo kati ya wanafunzi 100 wanaomaliza shule za msingi hapa Tanzania, wanafunzi 70 wanakwenda sekondari. Yote hii ni kwa sababu mbalimbali, lakini moja ya sababu kubwa ni kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi iliamua kufuta ada za sekondari, kwa hiyo, ikaondoa kikwazo kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vizuri kujitolea mfano, lakini naomba nijitolee mfano. Mwaka 1989 nikiwa form two, mimi nilifukuzwa shule kwa sababu ya kukosa ada, shilingi 2,000. Kwa hiyo, jambo hili ambalo Serikali ya CCM imelifanya limekuwa ni jambo kubwa, limeokoa watoto wengi wa Kitanzania walio maskini. Mimi isingekuwa wasamaria wema walionisaidia, pengine nisingekuwa Profesa leo. Kwa hiyo jambo hili ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili la haraka sana kwenye hilo ni kwamba, tumetoka kwenye 32% ya coverage ya maji vijijini, mpaka leo mdogo wangu Mheshimiwa Aweso, anatamba na 79%. Wakati tunaanza kutekeleza dira, pato la mtu mmoja Tanzania lilikuwa Dola za Kimarekani 384 ama shilingi 384,000. Leo tunazungumzia Dola za Kimarekani 1,200, zaidi ya shilingi milioni tatu. Wachumi wote ambao wamefanya tathmini ya uchumi wa Tanzania wanasema katika miaka 20 ukuaji wa uchumi wa Tanzania katika Bara la Afrika umekuwa siyo wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba mwaka 2000 ilikuwa ukiitafuta Tanzania kwenye ligi za kiuchumi Afrika ilikuwa ni lazima uanzie chini. Tanzania ilikuwa ranked miongoni mwa nchi za Kiafrika tatu za chini kiuchumi. Leo ukitafuta nchi 10 za kiuchumi lazima Tanzania uipate. Tunazungumzia kutoka Dola za Kimarekani bilioni 13.37 mwaka 2000 hadi leo ambapo pato la Taifa ni Dola za Kimarekani bilioni 80. Kwa hiyo, ni jambo kubwa, na wakati mwingine tunajifanyia tathmini ambayo siyo halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa mchakato huu wa dira tumefanya tathmini ya ndani na nje. Tulipomleta mtu wa nje kufanya tathmini ya dira yetu ya miaka 25, alisema mkibaki hivi bila ya kuongeza jitihada zozote, uchumi wenu unaweza kukua mara mbili na nusu katika miaka 20 ijayo. Mmekuwa katika kiwango ambacho ni kizuri. Mkiweka bidii kidogo ifikapo mwaka 2050 mtakuwa upper middle-income country. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yote haya yametoka wapi? Mambo haya yanatoka wapi? Mafanikio haya ni kielelezo cha usahihi wa sera za CCM. Mafanikio haya ni kielelezo cha ushupavu wa CCM katika kuisimamia Serikali. Mafanikio haya ni ushupavu wa kiongozi mkuu anayeiongoza nchi hii, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mafanikio haya ni kielelezo cha ushupavu wa Bunge lako katika kuisimamia Serikali hii ambayo tunaiongoza. Kwa hiyo, hili ni jambo la muhimu sana kuendelea kulizingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee ufafanuzi mambo mawili tu kwa sababu hatua tuliyonayo sisi hapa ni kupokea ushauri wa Waheshimiwa Wabunge ili kuboresha mapendekezo ya Mpango tulionao ili tuwe na Mpango mzuri zaidi. Kwa hiyo, hapa hatuna sababu yoyote ya kueleza moja moja kwa kila Mheshimiwa Mbunge. Mapendekezo yao tumeyapokea na tunaamini Mpango utakaokuja mwezi wa Sita utakuwa bora zaidi kuliko ambao tumeuleta hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya kutolea ufafanuzi ni mawili. Kwanza ni miradi mikubwa ya kimkakati ambayo tunaitekeleza ambayo Waheshimiwa Wabunge wameizungumzia hapa; Liganga na Mchumchuma pamoja na LNG. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye dira ijayo moja ya kibebeo cha kuchochea uchumi wetu ni hii miradi. Mradi wa LNG tunaouzungumzia utaingiza Dola za Kimarekani katika uchumi wetu shilingi bilioni 40, nusu ya GDP ya leo. Hakuna Serikali yoyote duniani ambayo ingeweza kufanya mchezo na mradi kama huu. Ni mradi muhimu ambao ni lazima Serikali iukumbatie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri pale kwamba mradi huu tunao na Mheshimiwa Rais anao, hatuwezi kuuachia, na bado tunazungumza na wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mikubwa kama hii ambayo ikiingia katika uchumi itatikisa, inahitaji umakini, haihitaji ku-rash, lazima tupatie, kwa sababu tukikosea tunakuwa tumekosea kwa muda mrefu sana. Imechukua muda mrefu kwa sababu ni mradi mkubwa na hivyo ni lazima tuhakikishe kwamba utakapoanzwa kutekelezwa nchi yetu ni lazima ifaidike kwa sababu ni rasilimali za Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo kwa mradi wa Liganga na Mchuchuma, tayari tunaye mwekezaji, Maganga Matitu pale Liganga. Kwa hiyo, tumeshaanza wakati tukisubiri mradi mkubwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba miradi hii mikubwa yote ikiwepo hii miwili, Serikali inayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho la kulifafanua hapa ni suala la hali ya umaskini nchini. Waheshimiwa Wabunge wengi, na pia kwa umakini mkubwa Mheshimiwa Mulamula amehoji takwimu za hali ya umaskini nchini, akionesha kwamba ni za siku nyingi mno kwa sababu ni za mwaka 2017/2018; kwanza tunapopima takwimu za hali ya umaskini Tanzania tunaangalia mambo manne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna umaskini wa kipato, umasikini wa mahitaji muhimu, umasikini wa huduma duni za jamii pamoja na umaskini hata wa kukosa kauli. Ndiyo maana kuna aspect ya governance, na tunapima kila baada ya miaka mitano. Tangu tuanze, tumeshapima hali ya umaskini mara tano kuanzia mwaka 1991. Kwa hiyo takwimu za mwisho ambazo tunazo ni za mwaka 2017/2018, miaka mitano iliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tupo kwenye mchakato wa kuzifanya nyingine, na tunatarajia tupate takwimu mpya ya mwaka 2025. Kwa hiyo, tutakapokuja Bunge lijalo, kwa maana ya Bunge la Bajeti, tutatoa taarifa ya hali ya umasikini iki-reflect data mpya ambazo NBS wanakwenda kuzifanyia kazi. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, takwimu hizo ndivyo zilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, tunakwenda wapi kutoka hapa? Kama nilivyosema kwamba uchumi wetu umekua vizuri sana, wastani wa 6.7% katika kipindi cha miaka 20, ukiondoa miaka ya COVID kote huku nyuma ulikwenda vizuri sana. Lengo letu lilikuwa tufike asilimia nane katika kipindi hiki cha kuelekea mwaka 2025. Wote mnafahamu kuwa tuliyumba kutokana na hali ya COVID pamoja na ukweli kwamba nchi yetu haikuyumba sana ukilinganisha na nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo tumekuwanayo ni ujumuishi, na ndiyo maana unaona Mpango uliopo tunazungumzia neno ujumuishi. Ni lazima uchumi wetu ukue katika hali jumuishi ili tuongeze kasi ya kupunguza umaskini. Kwa sasa ukiangalia takwimu za mwenendo wa ajira za NBS kwa Tanzania Bara za mwaka 2024, uanzie mwaka 2020 mpaka mwaka 2024 unaona kwamba 61% ya ajira zetu zipo kwenye kilimo, 11.4% hivi zipo kwenye biashara za jumla na biashara rejareja, 6.3% utazikuta kwenye huduma za malazi na chakula na huduma nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka Kwenda, moja, bado kilimo kitaendelea kuwa sehemu muhimu ya uchumi wetu. Kwa hiyo, ni lazima tuendelee kuwekeza katika suala la kilimo. Tunashukuru kwamba Mheshimiwa Rais katika kipindi chake hiki tumeongeza sana bajeti ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo hatulizungumzi, ambalo Mheshimiwa Rais na Waziri wa Kilimo wamelifanya, nalo ni kufanya kilimo kianze kupendeka kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mapinduzi mengi kwenye kilimo lakini kwangu mimi mapinduzi makubwa sana ni kukifanya kilimo kianze kupendwa. Sasa Mkulima wa Tanzania anaweza akajibainisha kwamba mimi ni mkulima bila wasiwasi. Lazima tumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwenye eneo hili. Kipekee lazima tumshukuru sana mdogo wangu Mheshimiwa Hussein Bashe, kwa jinsi ambavyo amekisimamia kilimo kwa passion ya hali ya juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, structure yetu ni hiyo ya kwenda mbele, tunataka tutoke kwenye kilimo twende kwenye uchumi wa uzalishaji viwandani. Uchumi wowote ambao unakua unafika mahali watu wanapungua kutoka kwenye kilimo wanapungua kwenda wapi? Lazima wapungue siyo kwenda kwenye huduma tu, au kwenye biashara ndogo ndogo, tunataka wapungue watoke hapo kwenda kwenye uzalishaji viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona mikakati ambayo tunayo na dira inayokuja itatuelekeza kuwekeza nguvu nyingi sana kwenye manufacturing kwa kuanzia na agro-processing. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitoka kwenye agro-processing twende kwenye rasilimali zetu za asili. Tunataka kwa mfano, madini yetu yasitoke mashimoni moja kwa moja kwenda bandarini (from the pit to the port), no. Iwe from the pit to industries then to the port. Kutoka kwenye shimo kwenda viwandani kisha bandarini. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais, ameelekeza na ameshamwelekeza Waziri wa Madini na ndivyo mipango yetu inavyosomeka na ndivyo dira itakavyosomeka kwamba, tunataka tufike mahali madini yetu yasisafirishwe nje ya nchi bila ya kuongezewa thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna nchi yoyote duniani ambayo imeendelea kwa kusafirisha malighafi nje ya nchi. Nchi zinaendelea kwa kusafirisha mali ambazo zimeongezwa thamani na huo ndiyo mwelekeo wa kisera wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, then, ukitoka kwenye viwanda ndipo uende kwenye huduma, uende kwenye teknolojia na nyingine. So, huo ndiyo muundo wa uchumi wetu ambao tunakwenda nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe moja kwamba, mafanikio yote ya kisera na kiutendaji ni matunda ya Chama imara, Tunacho Chama imara, Chama Cha Mapinduzi na hili jambo Waheshimiwa Wabunge tuliseme waziwazi bila kificho. Utulivu mnaouona, amani mnayoiona, governance mnayoiona ni matunda ya uimara wa chama cha siasa kinaitwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio mnayoyaona ni matunda ya ushupavu wa Kiongozi Mkuu wa Nchi. Kiongozi wetu wa nchi alipokea nchi siyo katika mazingira ya kawaida, unaweza ukamhukumu kwa yote, lakini jambo moja ambalo huwezi kumnyang’anya ni ukweli kwamba kiongozi huyu ameipokea nchi katika mapito magumu, lakini amehakikisha kwamba nchi yetu imebaki kuwa salama na imebaki kuwa tulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo nchi nyingi hizi changa kama ya kwetu ambazo zinaondokewa na Mkuu wa Nchi katikati ya safari bila kutarajia, zikabaki salama. Tunamshukuru Mungu kwa kutupa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amefanya nchi yetu imebaki kuwa tulivu. Hata ukayasahau yote, lakini kumbuka tuna Taifa ambalo bado ni salama lina umoja na amani kwa sababu tuna Kiongozi Mkuu aliye shupavu, hilo ni jambo la msingi. Mafanikio haya ni matunda ya Serikali imara. Wote mmeshuhudia kwa jinsi ambavyo Waheshimiwa Mawaziri wamejieleza hapa, utatilia shaka vipi uimara wa Serikali hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho muhimu sana, mafanikio haya ni matunda ya Bunge imara ambalo linaweza kutunga sheria sawa sawa; Bunge ambalo lina uwezo wa kuhoji Serikali mambo ya maana na Serikali ikayajibu. Kwa hiyo, kwa ujumla wake tuwahakikishie Watanzania kwamba nchi yetu ipo salama, ipo mikono salama, ipo vizuri kisera, ipo vizuri kiutekelezaji na tunajipanga vizuri zaidi kwenda mbele. Tuendelee kumuunga mkono Mheshimiwa Rais, endeleeni kuiunga mkono Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)