Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia na kuhitimisha. Awali ya yote, kama ambavyo kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kitila alitangulia kusema, tumepokea hoja zote ambazo Waheshimiwa Wabunge wamechangia pamoja na hoja za Kamati, tumezipokea na tunakwenda kuzifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia, tunashukuru Kamati ikiongozwa na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Njeza, tunakushukuru wewe mwenyewe pamoja na Mheshimiwa Spika kwa kuendesha mjadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru wataalam wetu wa Wizara zote mbili kama alivyotangulia kusema Mheshimiwa Prof. Kitila, kaka yangu tunafanya kazi kwa pamoja vizuri sana, naye ni Mwalimu wangu, tunaendelea kushirikiana vizuri, ndiyo maana mnaona hata hoja tunazozileta zina ushirikishwaji mpana wa Wizara zetu ambazo zina mambo yanayofanana, lakini pia na Kamati ambazo zinatusimamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimekuja hoja nyingi na nyingi zilikuwa zinaboresha Mpango pamoja na Mwongozo na sisi tumepokea, tutaenda kuyafanyia kazi mambo hayo yote ya msingi ambayo yametolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo machache tu ambayo ningependa kuyasema, moja ikiwa ni Serikali, itenge bajeti kwa ajili ya kukamilisha majengo ikiwa inamaanishwa maboma ikiwemo majengo ya vituo vya afya pamoja na upande wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa sekta ameliongelea vizuri, ni kweli tumeongea vizuri na tunaendelea kujipanga ndani ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaunga mkono jitihada za wananchi katika maeneo ambayo wananchi wamejenga maboma na tunaamini tutatoa utaratibu wa namna ya kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba katika maeneo mengi tuna maboma ya vituo vya afya, maboma ya zahanati na madarasa, tumelijua hili, tunalijua hili tumelipokea na hata sasa tunaendelea kulifanyia kazi. Tunakamilisha taratibu za kifedha na punde taratibu za kifedha zitakapokamilika tutazipeleka TAMISEMI kama Waziri alivyosema ili ziweze kuwafikia Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alishaelekeza Wilaya zote zitakapopokea fedha hizi Wabunge wajulishwe ili muweze kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wake, kwa sababu ni mambo ambayo mmeyasemea sana na mmeyafuatilia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mmesema Serikali ilipe fidia kwa ajili ya wananchi wanapopisha miradi. Ni dhahiri kwamba katika Serikali ya Awamu ya Sita tumejitahidi sana kulipa fidia, kuna maeneo ambayo tayari tumeshalipa fidia yakiwemo yale ambayo yalishakaa siku nyingi sana bila fidia hizo kulipwa. Fidia hizo zimeshalipwa, pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alisema tulipe fidia hizi katika maeneo ambayo yanaenda kutumika kwa maslahi mapana ya Serikali na tunaendelea kulipa katika maeneo mengine yaliyosalia. Kwa hiyo, Wabunge wote ambako wana masuala yanayohusu fidia wajue kwamba Serikali tunaenda hatua kwa hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusingeweza kulipa siku moja kwa sababu maeneo mengine ni ya siku nyingi na yanahusisha fedha nyingi na ni lazima maeneo mengine pia yanayohitaji fedha yaendelee kutekelezwa. Ishara kwamba Serikali ipo committed kwenye masuala haya ni kwamba kuna maeneo mengi na yanahusisha mabilioni ya fedha tayari tumeshaanza kulipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka tumelipa kwa Mkoa wa Njombe, tumelipa kwa Mkoa wa Mara tumelipa na maeneo mengine mengi. Hata sasa nakumbuka jambo ambalo limekuwa likifuatiliwa sana la Dar es Salaam, Kipunguni tunakumbuka na fedha, exchequer tulishatoa na maeneo mengine mengi Waheshimiwa Wabunge ambayo wamekuwa wakifuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatufanyi makusudi wala hatuwadharau wananchi lakini ni kwamba taratibu za kuweza kutekeleza mambo yote ambayo ni ya muhimu kwa wananchi wa Tanzania ndiyo yanayotufanya tumegemege maeneo tofauti tofauti na tutangulize maeneo tofauti tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aliwahi kusema Mwanafalsafa mmoja kwamba, kwenye nchi zetu hizi maskini zinazoendelea, lugha aliyotumia wakati ule, kila kitu ni kipaumbele. Hata sisi hapa leo hii tukisema tuchukue tu maeneo matano ndiyo tuseme kipaumbele, mtaona jinsi ambavyo shughuli itakavyokuwa ngumu, kwa sababu kila kitu kinatakiwa kuendelezwa kwa maana hiyo ndiyo inayoleta changamoto kwenye kugawa fedha iliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, pongezi ziende kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu ameongeza bajeti kwenye kila sekta, na siyo kuongeza bajeti tu na fedha kwenye maeneo hayo zimeongezeka. Ninyi ni mashahidi sasa hivi siyo jambo la ajabu kusikia kwenye kijiji zimekwenda shilingi bilioni saba, kwenye kijiji zimekwenda shilingi bilioni 15, kijiji zimekwenda shilingi bilioni 30. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuhamisha kutoka kwenye kasungura na ametupeleka kwenye tembo. Ni vile tupo wengi ndicho ambacho kinafanya bado tuendelee kuwa na uhitaji mkubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipunguze matumizi ya kawaida, hiki ni kipaumbele na Mheshimiwa Rais kila wakati anatuelekeza kwamba kipaumbele cha kwanza ni miradi ya maendeleo. Ukiona kuna sehemu matumizi ya fedha zimekwenda kwenye matumizi ya kawaida zimekwenda kwenye utekelezaji wa miradi, ni kwa sababu miradi pia haiwezi kujiendesha yenyewe lazima miradi itekelezwe na inatekelezwa na wanadamu. Kwa hiyo, kunakuwepo na sehemu ya uendeshaji na sehemu hiyo inakwenda kwenye matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vingi ambavyo vinahusika na utekelezaji wa miradi, lakini katika dirisha la masuala ya uhasibu yanaingilia kwenye fedha za matumnzi ya kawaida. Kipaumbele kikubwa ambacho tunakizingatia ni miradi ya maendeleo na ishara kubwa ambayo inakwambia kwamba tupo makini kwenye masuala ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na fedha za miradi ya maendeleo ni hii miradi ya kimkakati ambayo imeweza kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote ambayo haipo makini, haiweki focus kwenye fedha kupelekwa kwenye miradi ya maendeleo. Nawahakikishia, haiwezi ikatekeleza miradi mikubwa kama hii ambayo Tanzania imetekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ambayo inatekelezwa Tanzania hakuna nchi za SADC wala EAC wala hapa Afrika inatekeleza miradi mingi kwa mara moja kama inayotekelezwa hapa Tanzania, hakuna. Ninyi nendeni mkafuatilie na hata wenzetu wanaotufuatilia wanashanga kwamba tumewezaje kutekeleza miradi mikubwa ya aina hiyo katika nchi ya Tanzania na katika kipindi ambacho dunia nzima inapita kwenye msukosuko wa kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea, reli ni moja ya mradi wa kielelezo ambao umetekelezwa Tanzania na itakapokamilika itakuwa miongoni mwa reli tano ndefu zaidi duniani. Nchi tano zenye reli ndefu na Tanzania itaingia; kwa Afrika itakuwa ya kwanza. Hili siyo jambo dogo, Watanzania wanatakiwa watembee kifua mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, tunalo Daraja la Kigongo - Busisi ni moja ya mradi wa kielelezo na wenyewe upo hatua za mwisho. Bwawa la Mwalimu Nyerere ni mradi mwingine wa kielelezo ambao bajeti yake ya mara moja wakati upo kwenye peak ya utekelezaji ni fedha nyingi. Hiyo inaonesha ni nchi ambayo ina kiongozi ambaye yupo committed kwenye kupeleka fedha kwenye masuala yanayowahusu wananchi wake kama ambavyo amefanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa certificate moja ilikuwa inatokea tunalipa takribani shilingi bilioni 400, shilingi bilioni 300, shilingi bilioni 400 mpaka shilingi bilioni 450, dola milioni 130, dola milioni 140 kwa certificate moja ya mwezi mmoja. Hii inawezekana tu kwenye nchi ambayo kiongozi wake kipaumbele chake kikubwa ni maisha ya wananchi anaowaongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania imetoa mfano na maeneo tunakozunguka kule wanaitolea mfano, viongozi wa sekta wamesema lakini kila tunapokaa Mawaziri wa Fedha, Tanzania inajitokeza ya mfano kwenye miradi ya maji. Hivyo vinakuwa vinahusisha Mawaziri wote wa Afrika, inajitokeza nchi ya mfano kwenye mageuzi ya elimu na hii inajitokeza kwenye nchi zote za Afrika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia inajitokeza nchi ya mfano kwenye masuala ya umeme, zinakuwepo nchi zote za Afrika; inajitokeza nchi ya mfano kwenye afya, kwenye mageuzi ya kilimo, kwenye mageuzi ya mifugo na uvuvi na sekta nyingine. Hapa tumetaja chache kwa sababu ya maslahi ya muda, lakini tuna sekta nyingine nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote ni mambo yanayohusisha fedha na hiki ndicho ambacho kimekuwa kikimfanya Mheshimiwa Rais mara zote akose usingizi, azunguke huku na kule mara zote awe macho kuhakikisha kwamba miradi hii yote inasonga mbele kama alivyosema wakati anaapishwa na alichokisema sasa hivi Watanzania wanakiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshuhudia siku moja nilipata bahati ya kuongozana na Mheshimiwa Rais kwenye moja ya ziara katika kipindi ambacho kilikuwa na ibada, yupo kwenye mfungo ikatokea tunatakiwa tuwe na kikao wakati wa kufuturu, alikwenda kufuturu kwa maji ili tu Watanzania wapate maji, wapate Barabara na vituo vya afya. Huko ni kujitolea kwa kiwango cha juu ambacho Tanzania inaonesha kupitia kiongozi wake Mkuu na Serikali yake anayoongoza na uimara wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liliongelewa jambo lingine linahusisha Lugha ya Kiswahili. Kwa kumalizia, upande wa taasisi za kifedha tayari tumeshapata ruhusa ya Kiswahili kuanza kutumika kwenye vikao vya Benki ya Dunia. Sasa hivi tunakamilisha kuhusu utaratibu ufanyike, kuhusu kupata wakalimani watakaokuwa wanafanya kazi ya ukalimani kutoka Kiswahili kwenda kwenye lugha nyingine ambazo zinatakiwa zitumike katika mikutano hiyo. Hii ni moja ya jambo lingine kubwa kwenye diplomasia ambayo imetokana na umahiri wa Mheshimiwa Rais wetu ambao ameufanya katika kuifungua nchi yetu kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liliongelewa jambo la mifumo, tumelipokea na kama nilivyosema, kazi inaendelea kufanyika, tunaendelea kukamilisha mifumo yote ya upande customs pamoja na mifumo ya kodi za ndani. Yote hii itatuhakikishia kuongezeka kwa mapato ya Serikali na itatuongezea utaratibu mzuri wa masuala ya makusanyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mengine yaliyoongelewa kuhusu masuala ya utawala wa kodi pamoja na mifumo ya kikodi Mheshimiwa Rais, alishaunda Tume ambayo inaendelea kufanya kazi kama nilivyosema wakati natoa hoja. Tume hiyo itakapomaliza kazi, itakuwa imetusaidia kuhusu utaratibu wa masuala mazima ya kiutawala ya kodi, viwango vya kodi na namna ya kuongeza wigo wa kodi ili kodi iweze kulipwa na watu walio wengi na hivyo kupunguza mzigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ambayo ni ya kiutawala tumeshapata mwongozo ambao tunaendelea kufuatilia kuhusu matumizi ya risiti za kielektroniki. Kwenye jambo hili tunaendelea kutengeneza na utaratibu wa kuongeza hamasa pamoja na elimu. Siku siyo nyingi tutakuja na utaratibu ambao utaongeza hamasa kwa Watanzania wao wenyewe kudai risiti wanapofanya manunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja na utaratibu tutautangaza utakapokuwa umekamilika, lakini upo hatua za manunuzi ambao utaleta bahati nasibu za kuweza kuongeza kasi ya Watanzania wao kwa wao kudai risiti wanapokuwa wamefanya manunuzi na kila wanapouza waweze kutoa risiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilikuwa limeongelewa lilihusisha masuala ya TEHAMA. Mheshimiwa Rais alishatoa siku ya mwisho kwa ajili ya mifumo kusomana. Jambo hili linahusisha na Wizara nyingine, kazi inaendelea, kazi inaendelea ngazi ya watalaamu na ni jambo la muhimu ambalo tumelipa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine waliongelea kuhusu kushusha VAT, ni moja ya mambo ambayo yataongelewa punde tutakapokwenda kupokea taarifa ya Timu yetu ya Wataalam. Itahusisha watu wengi, naamini hata upande wa Bunge, kama siyo Bunge lote kwa uwakilishi wa Kamati, naamini maoni yenu nanyi yatakwenda kwenye Kamati ili mweze kutoa maoni hayo na kuweza kuboresha utaratibu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liliongolewa lingine kuhusu bajeti ya mafungu iende sambamba na uidhinishwaji wa miongozo ya bajeti. Tumeyapokea sambamba na maoni mengine kama ambavyo yalitolewa, tumeyapokea na sisi tutaendelea kuyafanyia kazi.
Mheshimia Mwenyekiti, mambo mengine yaliyokuwa yametolewa yalihusiana na kutenga fedha kupitia ruzuku ya maendeleo kwa ajili urejeshwaji wa mwaka wa fedha, tumelipokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine yalihusisha utaratibu wa matumizi ya nishati safi na incentives ambazo zinahusisha matumizi ya gesi, tumeyapokea na tumeshaanza tangu mwaka wa fedha huu wakati tunapitisha Sheria ya Fedha ya mwaka huu. Hiyo na yenyewe tumeipokea na tutaendelea kuiboresha ili kuweza kuvutia zaidi na zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa ambalo liliongelewa ilikuwa kuhusu madeni ya wazabuni. Hili ni eneo la muhimu sana na Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo sana. Kinachotokea siyo kwamba Serikali hailipi wazabuni, kinachotokea, tunapata kazi ya kugawanya kuhusu kulipa madeni ambayo yalishalimbikizwa muda mrefu na haya mapya. Kwa hiyo, tunaendelea kulipa ambayo yalishalimbikizwa na tunalipa ya sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao mna wazabuni marafiki, waulizeni watawaambia. Kuna wengine walikuwa na madeni ya mwaka 2014, mwaka 2015 na mwaka 2016 sasa hivi wamepokea fedha zao. Kuna wengine ambao wanaendelea na kazi, wanaendelea kupokea fedha zao, kwa sababu katika nchi pia hatuwezi tukakaa mwezi mmoja, wa pili na wa tatu tunalipa madeni tu, nchi lazima iendelee na kazi za uzalishaji za sasa lazima ziendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti inayohusiana na kulipa madeni imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, bajeti iliyopo kwenye mafungu ya kisekta na bajeti ambayo ipo kwenye Wizara ya Fedha, bajeti ya kulipa wakandarasi imeongezeka. Tulianza na shilingi bilioni 200, mwaka uliofuata tukaenda shilingi bilioni 400, mwaka uliofuta tukaenda shilingi bilioni 600 na mwaka huu uliopita bajeti yake iliongezeka kwa zaidi ya 100%. Hii yote ni kwa sababu tu wigo ulikuwa mpana sana, tunaendelea kuhakiki na tunaendelea kuyalipa madeni ya wazabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais mara zote ameelekeza kwamba tuelekeze fedha kulipa wazabuni, watoa huduma na wakandarasi ili kuweza kuongeza fedha kwenye mzunguko wa fedha hapa ndani ya nchi. Hili linafanyika ndiyo maana katika maeneo mengi mnaweza kuona jinsi ambavyo viashiria vingine vimepokea kama kupungua kwa mikopo chechefu ni ishara kwamba wale wanaofanya kazi ndani ya nchi wanapata malipo, nao wanaweza kurejesha mikopo kwa wale ambao walikuwa wamepata mitaji kwa kupitia mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya uhimilivu wa kiuchumi, kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kitila, ameshasema, tutaendelea kuyafanyia kazi kama tulivyokuwa tumeahidi wakati tunasoma Bajeti ya Serikali.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, windup.
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi, nawashukuru sana Wabunge, niwahakikishie kwamba tumepokea hoja zote na tukitoka hapa tutazifanyia kazi hoja hizi na Wizara ya Fedha tufanyia kazi pia utoaji wa fedha kwenye maeneo ambayo mmeyaongelea ambayo mmesema yapate fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, wakati natoa hoja niliomba tuiombee Simba, nikasahau Yanga. Naona huko nako hali inakuwa mbaya, naomba tuiombee Yanga na yenyewe maana hali imekuwa siyo hali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Kicheko/Makofi)