Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi ili niweze kuchangia katika Mapendekezo ya Mpango pamoja na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali 2025/2026.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niwapongeze sana Mawaziri wawili waliohusika kabisa kwenye matayarisho haya ya awali ya mapendekezo haya yaliyopo mbele yetu. Hali yetu ya uchumi, kama nchi, ina mwelekeo mzuri na kwa kweli, ukilinganisha na majirani zetu Tanzania tuna kila sababu ya kusema tuna uongozi bora na imara wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rahisi sana kutotambua au kuona mambo yanakwenda kawaida, lakini ukitaka ujipime kama unafanya vizuri, jilinganishe na wenzako katika eneo ambalo unafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa eneo letu sisi tunaangalia Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za SADC. Kwa ujumla wake Tanzania kiuwekezaji ni nchi ambayo inafanya vizuri zaidi kuliko nchi karibu zote za East Africa ukiacha Rwanda ambayo ina sababu zake maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuangalia mpango na mapendekezo ya mpango huu kuna mambo mengi ambayo yanajitokeza. Mpango huu dhima yake kubwa ni uchumi shirikishi na shindanishi na mimi ndipo mahali ambapo napenda hasa niweze kuongelea angalau kwa kifupi kwa muda ambao nimepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna sekta ambayo tunatakiwa tuiangalie kwa makini sana katika kuangalia dhima hii ambayo tunaingalia iko mbele yetu ni Sekta ya Kilimo. Sekta hii mchango wake kwenye pato la Taifa ni 26.5% wote tunafahamu ni sekta ambayo inakua na imekua mpaka kufikia kama asilimia nne, lakini bado ina potential ya kukua. Muhimu zaidi ni kwamba sekta hii asilimia kubwa ya Watanzania iko huko 45.9% ya wananchi wa Tanzania kwa sensa iliyopita wote ni wakulima, humu ndani sisi Wabunge ni wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muhimu zaidi mchango wake kwenye uchumi kwa maana ya export ni kubwa. Kwa hiyo, ushauri wangu mkubwa na hasa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo ni kwamba kwa kweli tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba miradi yote ya kilimo ambayo inaenda kubadilisha au kushirikisha wananchi walio wengi ni lazima katika mpango unaokuja tuhakikishe kwamba inapewa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya umwagiliaji ninapenda kusema kwamba ina gharama kubwa, lakini tukubaliane kwamba kilimo kina changamoto nyingi sana. Moja ya changamoto kubwa ambayo tunayo kwa nini hatuwezi kuwa na tija ni umwagiliaji. Kwa hiyo, tuombe sana tumeanza kuona dalili kwamba pembeni mambo ni mengi, lakini fedha hazitoshi. Kwa hiyo, tuangalie mambo ambayo ni msingi kwa kilimo ni mengi, umwagiliaji ni mojawapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Miradi ya BBT. Hii ni miradi ambayo inawaleta vijana kupata ajira, miradi ambayo inawaondoa vijana na tushukuru Serikali kwamba ilibadilisha mfumo mwanzoni tulikuwa na wasiwasi, sasa hivi wanachukuliwa vijana ambao tayari wako kwenye kilimo kwenye maeneo ya halmashauri zetu. Halmashauri zilizotenga maeneo tayari zimeingizwa kwenye miradi hiyo, kwa hiyo niombe Serikali isisite kuendelea kutoa fedha katika Miradi ya BBT kwa sababu ni miradi ambayo itatubadilishia maisha yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ni muhimu tukaliangalia ni eneo la uzalishaji wa viwanda. Tukiangalia Nchi kama Korea miaka 60 iliyopita Korea Kusini haikuwa tofauti na Tanzania, mchango wake kwenye pato la Taifa haukutofautiana na Tanzania na Tanganyika wakati ule na baadaye Tanzania, lakini ukweli ni kwamba South Korea imetuacha mbali sana. Ukifuata wanazuoni wa Korea na Watafiti wanasema ni mambo kama matatu tu, lakini kubwa kuliko yote ambayo ilifanya transformation hiyo ni kuingia kwenye viwanda na uzalishaji wa mazao ya kilimo kwenda kwenye viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo agro-processing kwetu sisi ni jambo ambalo ni lazima tulitilie maanani sana na ninaomba tunapoangalia agro-processing tuangalie viwanda vingi kwa ukubwa wake. Ukiangalia viwanda kama vya TBL au viwanda bia kwa ujumla wake, tutasema ni bia vinatupa mapato lakini vina impact kubwa sana kwa wakulima wetu kule katika maeneo yetu. Kwa hiyo, tujitahidi kuhakikisha kwamba tunaondoa changamoto ambazo viwanda vikubwa vyenye impact kwenye wazalishaji wakulima vinaondolewa changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba tumeanza kuona polepole kwamba Serikali inatakiwa itoe msukumo mkubwa sana kwenye kuboresha mazingira ya uwekezaji na niseme wazi naishukuru Serikali, tuseme na tuwe wakweli kwamba kwa kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tumeona kwa kiasi kikubwa, hatua kubwa za uboreshaji wa mazingira ya biashara, sisi tuitie moyo Serikali na tuwaombe kwenye mpango huu bado tuendelee kutatua mambo ambayo yanaweza yakaturudisha nyuma na kwa kweli yapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme machache ukiangalia moja ya vihatarishi ninavyoviona mimi ni jambo tunaloliita uniformity ya mifumo ya kodi katika nchi zetu za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ukiangalia kwa kiasi kikubwa tuna mikataba ambayo tumekwishaingia kwamba baadhi ya maeneo ya customs duty tutaendelea kuyaboresha na tutakuwa na harmonization. Napenda kutoa ushauri tuwe makini sana na commitment tunazozifanya kule, kwa sababu tuelewe kwamba sisi tuna advantage au tuna competitive advantage kwenye baadhi ya vitu. Kwa hiyo, tunapokwenda kuweka commitment kule tuangalie zisituondolee competitive advantage zetu na tuhakikishe kwamba maeneo ambayo tuna faida au tunaweza tukasukuma uchumi zaidi tuwe makini zaidi na wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu nipende kulisema mojawapo, kuna mpango kwa mfano kwenye maeneo ya sigara ambako nako tuna uzalishaji mkubwa na mchango mkubwa katika uchumi wetu kwa upande wa mapato. Sasa ukienda kule kinachoongelewa sasa kupitia kwa multi-lateral organization kuna mpango wa ku-harmonize excise duty kwamba Tanzania tuna-charge kidogo sana ukitulinganisha na wenzetu juu ya Mlima wa Kilimanjaro, kwamba wao wako juu sana kwenye excise duty, kwa hiyo na sisi na nchi nyingine zote tupande tuwafikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wako katika mazingira tofauti, sisi tutapata hasara kwenye makusanyo yetu kama tukienda tukalingana au tukataka kulingana na wao na mfano tumeuona tumeongeza excise duty hapa karibuni. Sasa hivi makusanyo ya Makampuni ya Bia yamekwishateremka kwa almost 20%, kwa sababu wanywaji wa bia wamepungua lakini siyo hilo tu, lina madhara mengine makubwa kwa uchumi wa nchi yetu. Watu wengi ambao hawawezi ku-afford kunywa bia wanakwenda kuanza kunywa vinywaji vingine ambavyo vinawaletea madhara makubwa katika afya zao, jambo hili linaendelea kutuumiza kwenye kukuza uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda unakimbia, hivyo niongelee kwa haraka sana kuhusu miradi mingine mikubwa. Dira ya Taifa ya Mwaka 2025 ilisema wazi na wote tunajua ili tuweze kutoa umaskini ni lazima tuhakikishe kwamba uchumi wetu unakua kwa kiwango cha asilimia nane mpaka asilimia tisa, siyo jambo jipya lipo ndani ya dira ambayo tumeifanya miaka 25 iliyopita. Ili tuweze na wengine wanauliza kwamba hii haiwezekani, inawezekana kukuza uchumi wetu kuufikisha hapo kwenye asilimia 10. Tukitekeleza miradi mikubwa miwili miwili tu tayari tuko kwenye asilimia tisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Uchakataji wa Gesi (LNG) kule Lindi ni mradi wa kimkakati ni mradi ambao tusione haya. Sasa nafahamu wenzetu ndani ya Serikali wanaendelea na majadiliano, sisi tuwatie moyo na kuwasukuma wajitihadi ili tuweze kukamilisha. Nitoe angalizo na nimelitoa angalizo hilo kabla, kwamba wenzetu wanaowekeza lazima tuangalie tuna Serikali tuna wawekezaji, tuna wanahisa na tuna Watanzania kwa ujumla wetu, lakini tukumbuke kwamba uwekezaji mkubwa wa dola bilioni 40 utategemeana sana vilevile na soko la LNG gesi katika soko la duniani. Wenzetu kama hatufanyi maamuzi ambayo yanaendana na wakati tutafika mahali kutakuwa na over supply ya LNG. Miradi ya LNG haipo Tanzania peke yake, kwa hiyo tuombe sana Serikali ilisukume. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa kumalizia kuhusu Liganga na Mchuchuma. Mradi huu umeongelewa na kila mtu, sisi tunaiomba Serikali kila mtu sasa anafahamu mradi huu hauongelewi tu na Wabunge wa Njombe, mradi huu unaongelewa na Wabunge wa Tanzania, mradi huu unatakiwa tufike mahali tufanye maamuzi. Tunatambua ugumu na complexity ya kukamilisha majadiliano, mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara nafahamu tu mwelekeo ni mzuri, lakini hatuna muda. Hatuna muda kwenye huu Mradi wa Liganga na Mchuchuma, ni mradi wa muda mrefu, ni mradi ambao utabadilisha kabisa uchumi wa nchi yetu. Utafanya growth ya economy yetu, uki-combine hii miwili peke yake, ukaongezea na kukamilisha kwa reli, ukaongezea na reli ya TAZARA tayari tuko kwenye 12% ya growth na tunaanza kupunguza umaskini, shida yetu kubwa ni umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema Wizara ya Kilimo wanahitaji kuongezewa fedha za utafiti, kule Njombe avocado inaanza kupata shida kwa sababu ya magonjwa na utafiti unahitaji uwe mkubwa katika zao la avocado. Nakushukuru sana. (Makofi)