Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupewa nafasi, naomba nianze kwanza kuongea kwa kifupi ya Jimboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais alipokuwa Musoma Vijijini nilimwomba miradi miwili mikubwa ya barabara ya kilometa 92 na kufufua kilimo kikubwa cha umwagiliaji. Nashukuru kwamba vyote nimefanikiwa, pongezi kwake na pongezi kwa TANROADS. Barabara wakati huo ilikuwa na gharama ya dola milioni 50, matangazo yametoka, wakandarasi wengi wameshabikia tuko kwenye hatua za mwisho za manunuzi. Barabara hiyo lina daraja vilevile ambalo litagharamiwa na World Bank nako manunuzi yanakamilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji nashukuru Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe na Wizara wanaenda vizuri hivi karibuni nadhani mwakani tunaanza kujenga miundombinu ya umwagiliaji. Kwa hiyo, kutokana na hayo mapendekezo haya nayaunga mkono yote kwa sababu yana mambo ya Musoma Vijijini, baada ya hiyo sasa nije kwenye mambo makubwa ya kitaifa kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mapendekezo nayaunga mkono na ninaboresha, huko vijijini kwa wakati huu hii bajeti tunayoitayarisha mwakani, maeneo matatu lazima tuyawekee mkazo sana nayo ni maji, umeme na barabara. Hivi vitatu vinahitajika kwelikweli na nadhani bajeti tutakayoitayarisha mwakani itazingatia hayo, lakini fedha itakua ni tatizo kwa sababu tuna miradi mingi huenda fedha zisitoshe. Napendekeza kwamba mbali ya vyanzo vya fedha za TRA, tuanze kufanya majadiliano ya kimkakati na benki zetu ili tuweze kupata concessional rates yaani tukope kwa riba ndogo ya asilimia mbili ili kusudi tuweze kutekeleza miradi ya maji, umeme na barabara. Vilevile tutumie stock exchanges kupata fedha huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa vipaumbele vinne ambavyo ni muhimu kweli tukiwa tunamalizia miaka mitano na tunaanza miaka mitano kuelekea 2050. Kipaumbele cha kwanza ambacho naomba tuzingatie ni uhusiano wa elimu na ajira na ajira tuzipate ndani ya nchi na nje ya nchi. Sasa ninafuatilia sana ajira nchi za nje, kuna upungufu mkubwa sana karibu nchi zote hata uchaguzi uliopita wa Marekani jana usidhani kwamba Wamarekani hawataki wageni, hapana! Wanataka wageni mabingwa wenye utaalam hawataki hawa economic refugees wataendelea kutakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Nchi kama Ulaya wameanzisha kitu kinaitwa U Blue Card, blue card ni kama ile green card ya Marekani, watahitaji watu. Nchi kama Ujerumani inahitaji wageni, wataalam wageni wa kaliba mbalimbali laki nne kila mwaka, laki nne kwa uchumi wa Wajerumani inahitaji watu, sasa maeneo ambayo yanahitajika nimeyaweka pamoja ni sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni kwenye sekta ya manufacturing; eneo la pili, IT; ya tatu, Health Care; ya nne, Engineering; ya tano, Constructions and Building Trades; yaani wanahitajika hata hawa wajenzi, waashi na kadhalika wanahitajika nchi huko; na sita ni Agriculture na Forestry. Ukichukua Nchi kama Ufaransa unahitaji zaidi maeneo zaidi ya 25, sasa Watanzania tusing’ang’anie kazi nchini hapa, lazima tuzitafute na za huko nje, lakini lazima elimu yetu, lazima elimu yetu iendane na mahitaji ya huko nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu hapa peke yake lazima tuwekeze kwenye masomo ya sayansi na watu wetu wajue lugha. Kuna lugha hii ya Kiingereza hata kama unashabikia sijui lugha gani huwezi ukakikwepa Kiingereza na huko wanakotangaza kazi Kiingereza ndiyo kinatumika, hakuna lugha nyingine, sana Kiingereza na Kifaransa. Sasa sayansi hapa Tanzania ndiyo wakati ule niliongelea kuhusu mitaala lazima tuirudie. Masomo ndugu zangu yanayohitajika ili hawa watu wapate hizo skills unahitaji mathematics, physics…

(Hapa Simu Iliita)

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani kuna mtu anani-disturb na simu hapa, hebu mkate huyo, Dokta kata simu, kuna mtu alitaka kusikiliza wakati naongea siyo vizuri. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masomo yanayohitajika ni mathematics, physics, chemistry, biology, hayo hayo ni lazima tuyawekee mkazo kwenye O-level, halafu na lugha tuwekee mkazo English na French. Sasa tunachohitajika bajeti hii tunayoitengeneza ya mwakani, ninapendekeza tujenge maabara nyingi na tujenge na maktaba nyingi. Haiwezekani tupate skilled workers ikiwa kama sekondari zetu hazina maktaba, hazina maabara za sayansi. Mimi Musoma Vijijini nimeanza kujenga, lakini naomba Serikali iwekee mkazo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuonyesha jinsi ambavyo hatujafanya vizuri kwenye sayansi..,

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, looh! Tayari muda?

MJUMBE FULANI: Bado, endelea…

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, form four mwaka jana walikuwa wanafunzi zaidi ya laki tano waliochukua physics ni 25%, chemistry 31%, agriculture ambapo tumewekeza sana 1.6 percent. Kwa hiyo, mipango yetu ya uchumi haiendani na mipango ya elimu ndiyo hii inaonyesha hapa. Walioenda form six mwaka jana, waliomaliza form six bila kujali ushindi wao walikuwa karibu 97,000. Physics 23%, chemistry 36%, math’s 14%, biology 29%, agriculture tulipowekeza one percent kwa hiyo unaona mipango yetu haiendani na maeneo. Kwa hiyo tuweke bajeti kubwa kwenye masomo ya sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili nitaenda sasa kwa haraka ili twende 10% growth ni uchumi wa gesi asilia na helium, hili nimeshawahi kuliongelea na mfano hapa natoa ni Algeria inayoongoza kwa Afrika. Algeria wana GDP per capital ya five thousand two hundred and sixty dollars kutokana na mambo ya gesi, wana export gesi kwenye pipe kwenda Europe halafu wana export LNG.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni uchumi wa kilimo. Nimechukua nchi kama Vietnam iliyokuwa vitani toka mwaka 1955 mpaka 1975, miaka 20 ya vita, leo Vietnam mwaka huu inazalisha mpunga tani milioni 27, Tanzania ambayo hatujaingia vita ya miaka 20 tunazalisha tani milioni 2.5, GDP ya Vietnam iliyokuwa vitani ni four thousand three hundred forty-six US Dollars per person per annum. Sisi ni one thousand two hundred eleven dollars per person per annum, kwa hiyo tuwekeze kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne ni uchumi wa madini. Hili nimeshaliongelea sana, critical minerals na strategic minerals. Marekani wanahitaji aina hamsini, European Union aina thelathini na nne, lakini kufanikiwa hapa ni lazima geological survey tuiwezeshe na tuwekeze hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano ambayo itatufikisha kwenye uchumi wa 10% ni uchumi wa utalii. Hapa nimeangalia watalii kutoka nchi za nje waliokuja Barani Afrika, watalii wa nje siyo wa ndani. Egypt ilikuwa na watalii milioni 13.1, South Africa milioni 10.2 ya tatu ilikuwa Morocco ya nne ilikuwa Tunisia ya tano ilikuwa Kenya 5.6 million, nasi Tanzania tulikuwa wa sita, lakini ukichukua utalii maana ya utalii, ukachukua nchi inayoongoza kama Ufaransa ambayo yenyewe mwaka jana ilikuwa na watalii zaidi ya bilioni 100 na fedha ilizoziingiza zilikuwa karibu 70 billion US Dollars na mtu alitumia karibu Dola 700 kwa siku kwenda kufanya utalii Nchini Ufaransa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninadhani nia yetu hapa ni kujitayarisha kutoka kwenye ukuaji wa uchumi wa asilimia tano au asilimia sita twende 10%. Kwenda huko 10% ni lazima tuwekeze kwenye hayo maeneo manne kwamba, elimu iendane na ajira, halafu ya pili tuwekeze kwenye uchumi wa gesi na helium. Halafu tuwekeze kwenye kilimo (agricultural businesses), tuwekeze kwenye madini, tuwekeze kwenye utalii. Tukifanya hivyo ile tunayopanga kwamba ikifika mwaka 2050 tufikishe dola ziadi ya 4,500 itawezekana, ahsante. (Makofi)