Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi. Nitaanza kwa kuzungumzia suala zima la utafiti. Utafiti pia ni chanzo cha mapato. Ninasema hivyo kwa sababu mara nyingi tafiti zinapofanyika tunategemea iwe mikoani ama kwenye halmashauri kule, tunategemea kwamba, wale wanaopata nafasi ya kufanya tafiti warudishe majibu (dissemination) katika mikoa au wilaya wanazofanya. Vibali vinatolewa, wanapewa vibali, lakini mara nyingi unakuta hawarudishi ripoti kwenye wilaya au mkoa ule ambao wamefanya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, eneo ninalotaka kulizungumzia hasa ni tafiti zifanyike, kubwa kwenye eneo la vifaa vya watu wenye ulemavu wa aina zote. Utafiti wa kina ufanyike na ukishafanyika tutatambua vifaa gani vinahitajika kwa aina za watu wenye ulemavu waliopo nchini. Wakishafanya hivyo ndipo tutawapatia jukumu Wizara ya Fedha au Serikali kuondoa kodi kwenye hivyo vifaa vya watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo vifaa huko mitani ni ghali mno, lakini Serikali ikiondoa kodi, hawa watu wanaweza wakapata hivyo vifaa na zile tafiti zitaonesha faida. Pia, vile vifa tutajua vya aina mbalimbali katika makundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ninataka kulizungumzia hapa ni kuangalia majengo yetu kwa hao watu wenye ulemavu pia.
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Sheria ya Mwaka 2018 ya Umoja wa Mataifa, imetoa maelekezo katika nchi zote ambazo ni Wanachama wa Umoja wa Mataifa kutoa exemption kwa vifaa vya watu wenye ulemavu vikiwemo vitendea kazi kama kompyuta zao, baiskeli zao na vifaa vingine. Ninampongeza sana mtoa hoja hii kuwa amelenga malengo ambayo ni mazuri na tunamwomba Waziri wa Fedha alisimamie hili kwa kupitia TRA itoe suala la exemption kwa vifaa vya watu wenye ulemavu. Ninashukuru. (Makofi)
MWENYEKITI: Dkt. Ntara.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninaipokea taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje kwenye majengo. Haya majengo pia yanapojengwa unakuta zile sehemu za kupandia watu wenye ulemavu wanalijenga ile kitu mnaita loop, ile slope au mnaita lamp. Sasa ile lamp inajengwa…
MWENYEKITI: Siyo lamp ni ramp.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, that’s why I was asking because I don’t know.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuta kwamba kwenye ghorofa la chini utaiona hiyo ramp imejengwa. Ghorofa ya pili, tatu na ya nne huko juu hakuna. Kwa hiyo, mara nyingi ujenzi ule wafanye ukaguzi kuona kwamba yanajengwa katika ghorofa zote. Kama zipo tatu au nne basi yajengwe kote, yasijengwe tu hapa chini kwa kuonesha halafu yanabaki kule juu hakuna kitu.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Ikupa.
TAARIFA
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza mchangiaji anayeendelea kuchangia. Kwa upande wa miundombinu, siyo tu ramp, pia hata sehemu za vyoo siyo rafiki kwa watu wenye ulemavu na hasa ukiingia kwenye hoteli unakuta choo ni kidogo sana hata mtu akiwa na wheel chair hawezi kuingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, wakati anazungumzia suala la vifaa vya watu wenye ulemavu. Vifaa vya watu wenye ulemavu viliondolewa kodi, lakini unakuta bado ni ghali. Kwa hiyo, Serikali labda iendelee kufuatilia kwa nini kodi iliondolewa, lakini bado vifaa hivi vinapatikana kwa bei kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna vifaa vingine kwa mfano kama zile quick (baiskeli za mota) zinapatikana kwa bei kubwa, lakini pia mtu akinunua…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ikupa, sasa unachangia. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Amenisaidia.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Ntara.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Ahsante sana Mheshimiwa Ikupa.
Mheshimiwa Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yote anayosema Mheshimiwa Ikupa, ninaomba Waziri wa Fedha na Mipango wayachukue hayo, ndiyo imekuwa ni changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninataka kulizungumzia ni kuhusu Kiswahili. Kiswahili ni bidhaa na sasa hivi tunatangaza Kiswahili ni bidhaa na inatumika huko SADC, East Africa na AU kote huko tunatumia. Sasa hivi kuna idadi ya watu karibu milioni 500 wanatumia Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, wakati mwingine nilishangaa hapa walikuja Wabunge wanaomba Ubunge East Africa, badala ya kukitangaza Kiswahili sasa ninarudi ninaona tuliwapa interview kwa Kiingereza. Sasa ninasema hivi tunafanya nini? Huko ukienda kwenye haya Mabunge yote unakuta mtu Kiingereza chenyewe hajui, lakini wanaongea hivyo hivyo, wanachotafuta kule ni utaalam. Sasa sisi tujiandae, hivi ni lazima tuwapatie interview ya Kiingereza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninataka niombe tafiti iendelee ndani ya kuona kwamba hicho Kiswahili tumekwenda nacho kiasi gani, ili tutoe elimu kwa wahadhiri wapate umahiri kamili wa kuweza kufundisha hicho Kiswahili hasa eneo la ukalimani. Hilo eneo linaonekana bado hatuna wataalam wa kutoa ukalimani pia maarifa ndani ya Kiswahili chenyewe ili iwe bidhaa kama ambavyo sasa hivi tunataka Kiswahili hicho kiwe bidhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana. (Makofi)