Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, oh, samahani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia fursa hii ili nichangie kwenye Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hoja mbili zilizo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa wasilisho lao nzuri sana ambayo imetupatia faraja kubwa kutokana na taarifa kwamba uchumi wetu umeendelea kuimarika na kuhimili vyema changamoto za dunia zilizojitokeza hivi karibuni. Hii inatupatia matumaini kwamba huko tunapokwenda katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi, tunapata matumaini makubwa. Ninapenda kumpongeza tena Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uamuzi wake wa kuunda Wizara na Tume ya Mipango. Hakika inafurahisha kuona kwamba mpango na bajeti vinasomana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na timu yake kwa kutushirikisha kama Wabunge kwenye semina maalum ya kuweza kuchangia na kutoa mchango wetu katika maandalizi ya Dira ya Mpango wa Maendeleo Mwaka 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda pia kuipongeza Kamati ya Bajeti ambayo imedadavua vizuri Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti na ambayo wamewasilisha mapendekezo yao mazuri nitakuja kurudia huko baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Waziri wa Mipango kabla sijaendelea arejee kwenye ukurasa wa 17 mwishoni na 18. Kwenye vishkwambi vyetu inasomeka ukurasa wa 17 kwenye paragraph ya mwisho na 18 mwishoni wa mapendekezo ya maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2025. Sijui kama document yake inasoma kurasa hizo, lakini kitu ambacho ninataka tu ku-bring kwenye attention ya Mheshimiwa Waziri ni kwamba, takwimu zilizotolewa kuhusu hali ya umaskini nchini ni za nyuma sana. Hapa zinatajwa ni za mwaka 2011/2012, 2017/2018 ambapo katika hiyo taarifa mnasema kwamba, hali ya umasikini inakadiriwa kupungua kwa 25.7% kwa mwaka huu 2020 na kwamba umasikini wa chakula unakadiriwa kupungua hadi 7.3% mwaka 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa ninauliza kwamba, kwa leo tunavyoangalia mpango huu wa 2025/2026 takwimu hizo zinaonekana ni za nyuma na pengine zilinyofolewa kutoka kwenye maandalizi ya mpango wa malengo kipindi cha tatu cha mpango wa miaka mitano. (2021/2022 – 2025/2026). Ninaomba waangalie tu hiyo labda kuweza kusahihisha hizo takwimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilifarijika kusikia kwenye taarifa ya habari kulikuwa na tukio ambalo Naibu Waziri wa Mipango, Mheshimiwa Stanslaus Nyongo alizindua rasmi ripoti au chapisho la takwimu kuhusu kipato cha mtu mmoja mmoja na fursa za uchumi na uwekezaji kwenye Mkoa wa Dodoma. Ninawapongeza kwa tukio hilo, lakini kama Naibu Waziri alivyosema ni vizuri na mikoa mingine iige mfano wa Dodoma kuchapisha ripoti hizo ambazo zitatoa uhalisia wa kila mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia nimfahamishe Mheshimiwa Waziri kwamba kwa Mkoa wa Kagera kuna Taasisi Isiyo ya Kiserikali, ni think tank inayojulikana kama Kagera Development Foundation (KADEFO). Imeundwa na wataalam wabobezi wa masuala ya uchumi, ustawi wa jamii na inajumuisha pia wana-diaspora. Pia, inashirikiana kwa karibu na Mamlaka za Mkoa na Wizara ya Mipango kutoa chapisho kama hilo. Inaweza kufanya hivyo na mimi ni mdau na mshiriki kwenye taasisi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Mheshimiwa Innocent Bashungwa, Waziri wa Ujenzi ni mmoja wa walezi wa taasisi hiyo. Ninapenda pia nimpongeze Mheshimiwa Hajat Fatma Mwasa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera ameanzisha initiative ya Ijuk’omuka maana yake kumbuka nyumbani. Katika tukio hilo amekuwa anahamasisha uwekezaji. Kitu ninachoomba ni kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Bajeti kwamba ni vyema Serikali itenge bajeti kwa ajili ya kufanya utafiti wa mapato na matumizi kwa kila kaya ili kupata takwimu ya hali halisi ya umaskini nchini na maendeleo ya watu kwa kutumia taasisi kama hiyo niliyoisema ya KADEFO. Kwa hiyo, ninaunga hilo pendekezo la Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakumbuka pia Mzee wangu Marehemu Mwalimu Nobert Rutageruka alikuwa kila mara akinisikia ninaongea ni kwenye majukwaa au warsha alikuwa ananiambia, “Liberata ninasikia unatoa takwimu, unazipata wapi mbona hamtuulizi?” Kwa hiyo, ninadhani tukifanya hizo tafiti zitaweza kujumlisha wananchi kwa upana na wigo mpana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaomba niongelee kuhusu vipaumbele vya bajeti ambavyo ni vya mpango mzima, ambapo pamoja na mambo mengine ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji na kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu maeneo haya yakisimamiwa vizuri yanaweza kuwatoa Watanzania wengi kwenye wimbi la umaskini na kutuvusha kama Taifa kuelekea kwenye maendeleo makubwa na endelevu. Swali ni nini kifanyike? Kumekuwa na maelezo mengi kwenye hayo mapendekezo lakini tunasema we need to put money where our mouth is. Utaona kwamba mchango wa viwanda ni mdogo sana wakati tumesema ni Tanzania ya viwanda. Kwa hiyo, nimekuwa ninaiongelea sana. Ninaomba hili liangaliwe na hasa ukiangalia mikoa ambayo ina rasilimali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kama Kagera kuna Kagera Kabanga Nickel. Ikipewa kipaumbele na msukumo wa uwekezaji katika hili viwanda vya kuchenjua madini haya, kwa kweli itatuvusha sana Mkoa wa Kagera na inaweza ikawa kitovu cha uchumi wa nishati na viwanda vya madini ya nishati. Ninajua of course kuna Liganga na Mchuchuma imeongelewa sana lakini ninaomba niongelee madini ya Nickel ya Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ninaomba nigusie kidogo Diplomasia ya Uchumi ambayo ninashukuru sana kutokana na juhudi za Mheshimiwa Rais kama mwanadiplomasia namba moja ametufungulia fursa nyingi na watendaji wakuu ni Ofisi zetu za Ubalozi. Kama Kamati ilivyosema kwamba, Ofisi za Ubalozi hazipewi fedha za kutosha kuweza kufanya na kutekeleza Diplomasia ya Uchumi na hatutumii vizuri fursa ya kusafirisha Walimu na wataalamu wa Kiswahili nje ya nchi. Ninaomba nimpongeze hapa kwa dhati sana Balozi wetu wa Cuba Mheshimiwa Polepole, kwa kuandaa Tamasha kubwa la Kiswahili Mjini Havana Cuba, ambalo litafunguliwa rasmi na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye yupo kwenye ziara katika nchi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba mfuatilie tarehe 8 Novemba pia atazindua Kamusi ya Kiswahili na Kihispania siku hiyo. Kwa hiyo, huu ni mfano wa kuigwa, lakini vema Balozi zetu ziwezeshwe, ziweze kufanya haya ambayo kwa kweli ndio yanasukuma Diplomasia yetu ya Uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niseme katika mpango wa bajeti uliopita Mheshimiwa Waziri wa Fedha alisema; “kusudi tuwe na matokeo chanya, inabidi tuwe na mfumo thabiti na endelevu wa ufuatiliaji na tathmini (monitoring and evaluation) na utolewaji wa taarifa.” Pamoja na kutambua azma ya Waziri wa Fedha kuviongezea nguvu vitengo vya ufuatiliaji na tathmini ninakumbuka huko nyuma Kamati ya Bajeti ilishauri kuwepo sera malum na sheria ambazo zimebainisha kwamba msingi wa….
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Balozi Mulamula.
MHE. BALOZI LIBERATA R. MULAMULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kurudia hiyo na ninaomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)