Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nianze na utangulizi. Katika utangulizi wangu nitaanza na shukrani. Ninaomba uniruhusu nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo mawili. Jambo la kwanza; alipokuwa amefanya ziara Wilaya ya Kilombero kwa maana pia na Jimbo la Mlimba kwa sababu lipo ndani ya Wilaya ya Kilombero, tulipewa fursa Wabunge kuzungumza changamoto za wananchi. Pamoja na mambo ambayo nilizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mlimba, nilimwomba Mheshimiwa Rais atusaidie kupitia Wizara ya Kilimo, NFRA waanze kununua mpunga jimboni kwangu Mlimba. Kwa hiyo, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais mpaka sasa wananchi wanapata huduma hiyo. NFRA inanunua mpunga jimboni kwangu na wananchi wamekuwa wakinufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli wananchi wa Mlimba wamenipatia salamu niwashukuru sana Mheshimiwa Rais, Waziri wa Kilimo na Mtendaji Mkuu wa NFRA katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ninamshukuru Mheshimiwa Rais. Bunge lililopita wakati wa bajeti nilieleza kwa habari ya fedha za mradi wa shilingi bilioni 345. Mimi na wananchi wa Mlimba, kwa kuwa sisi ni wazalendo kweli kweli kwenye nchi hii tulipinga zile fedha shilingi bilioni 345 ambazo zilikuwa zipo chini ya Wizara ya Ardhi na kupinga kwangu kumeleta matokeo chanya na hapa ninampongeza Mheshimiwa Rais; amechukua hatua, amebadilisha matumizi ya fedha zile. Ninamshukuru Waziri wa Fedha kwa kubadilisha zile fedha shilingi bilioni 345 ambazo zilikuwa zinakwenda kuliwa na wajanja wachache. Ninamwomba, kwa kuwa zile fedha zimerudi Wizara ya Fedha, ni muhimu sasa zikawekezwa kwenye sekta muhimu hasa barabara. Ninamshukuru Mheshimiwa Rais, sasa ninaanza kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza mchango wangu kwa Sekta ya Kilimo na hapa ninaomba nirejee Azimio la Iringa, mwaka 1972. Baada ya Azimio la Arusha kuboresha Azimio la Arusha mwaka 1972, mwaka 1971 tulikuwa na Azimio la TANU, ambalo lenyewe lilikuwa linasema, “Uhuru wetu siyo Uhuru wa Bendera. Hata Wimbo wa Taifa siyo uhuru wa kweli, bali mali zote tuzimiliki sisi Watanzania.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio la Mwaka 1972 pale Iringa, lilikuwa ni mahususi kwa ajili ya kilimo. Lenyewe lilikuwa linasema “Siasa ni Kilimo”, sasa ninazungumzia Sekta muhimu ya Kilimo. Ni kweli Taifa letu Mungu ametujaalia rasilimali nyingi kama Taifa, lakini kupanga ni kuchagua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Serikali, kwenye mipango ya Serikali wawekeze kwenye kilimo, kwa nini kwenye kilimo, kwa sababu Watanzania walio wengi wanajishughulisha na kilimo. Tunaambiwa hapa takwimu, 75% ya Watanzania wanafanya kilimo. Kwa hiyo, tukiwekeza kwenye kilimo maana yake mapato yataongezeka, lakini pia tutauza nje ya nchi mazao yanayotokana na kilimo na tukapata fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe takwimu kidogo kwenye Sekta hii ya Kilimo, mwaka 2020/2021, Wizara ya Kilimo iliweza kusimamia mauzo ya nje Dola za Kimarekani (USD) bilioni 2.3. Zilikuwa zimetokana na mauzo ya nje kutokana na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nieleze matarajio ya Sekta ya Kilimo na hii ninaomba Mheshimiwa Waziri wa Mipango unisaidie na unisikilize vizuri eneo hili. Wenzetu wa Kilimo wamekutangulia; Kilimo wamekuja na mpango wa vision 2030. Wao wanasema, wanataka ifikapo mwaka 2030 mauzo yatokanayo na kilimo yawe Dola za Kimarekani bilioni tano. Sasa wewe unapaswa kuwawezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unawawezeshaji? Ni kuchukua mpango wao kuuleta kwako na kuuchakata na kuuboresha zaidi ili Wizara ya Kilimo ifikie malengo yake, lakini pia na financing, ukitaka kupata fedha weka hela. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, tumeona hapa mashahidi, sisi wote Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, Bajeti ya Kilimo imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka. Mwaka wa fedha 2023/2024, tunaona Bajeti ya Kilimo ilikuwa kama shilingi bilioni 900, sasa wamekuja na shilingi trilioni moja point something. Kwa kweli ninaona Mheshimiwa Rais ana utashi wa kisiasa katika kuiwezesha Sekta ya Kilimo. Kwa hiyo, tumsaidie Mheshimiwa Rais kuiwezesha Sekta ya Kilimo ili ifanye vizuri na sisi Watanzania tunufaike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nieleze hapa, nchi yetu ina ardhi, tumejaaliwa ardhi kubwa sana nchi yetu, takribani kilometa za mraba 950,000, Tanzania, lakini eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta milioni 44. Sasa, kwenye umwagiliaji sidhani kama tumefikia hata nusu. Sasa, tukiwekeza kwenye kilimo nina imani kubwa tutatoka kwenye umaskini tulionao na kwenda juu zaidi, kwa sababu kilimo na niwaambie kwa dhati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo na nitoe mfano, kwa mfano zao la mchele; mchele duniani, idadi ya watu takribani shilingi bilioni 3.5 wanakula mchele. Nchi za Asia wanakula mchele, Nchi ya India wanakula mchele na Afrika. Ninawaambia mchele ndiyo chakula pendwa duniani ukiacha ngano. Sasa, tukiwekeza kwenye mazao ya chakula tunaweza kuuza nje ya nchi na tukapata urari ulio chanya kwa Taifa letu. Kwa hiyo, ninaeleza haya ili tuisaidie Sekta ya Kilimo kwenye mipango yake ifanye vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Waziri wa Kilimo na ninamwambia kwa dhati; kama kuna jambo ambalo Mheshimiwa Waziri unakwenda kuweka alama kwa Taifa letu, ni Mradi wako wa Umwagiliaji wa Bonde la Mto Kilombero. Ninaomba uusimamie vizuri, yaache yote, tumechelewa sana watu wa Mkoa wa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema kwa dhati, Mkoa wa Morogoro ndiyo mkoa ambao tuseme una miti ya kutosha. Hatufanani na wengine huko, sitaki kutaja. Kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, acha yote tazama Morogoro. Huu wakati wa Mama Samia, huu wakati wa Mkoa wa Morogoro kupanda kwenye Sekta ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninasema haya; tumeambiwa hapa takribani hekta 44,000 zinasanifiwa kwenye Bonde la Mto Kilombero na katika hekta hizo, karibu hekta 30,000 zinatoka Mlimba. Kwa hiyo, ninasema tu kwa dhati wananchi wa Mlimba wanasema Mheshimiwa Waziri wekeza hela pale. Umesema unafanya upembuzi yakinifu; ukianza mapema na sisi tutafurahi. Kwa sababu nikwambie kwa dhati, sisi Mlimba tunazalisha mchele tani laki sita, nchi nzima mnazalisha mchele tani laki tano, hivi hamwoni? Kwa jembe la mkono na kilimo cha mvua, sasa wakituwezesha mambo si yanakuwa vizuri zaidi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niendelee na eneo lingine, ninaenda kwenye Sekta ya Ardhi; Sekta ya Ardhi! Kama kuna jambo ambalo lazima tufanye mapinduzi kama nchi, nina mapinduzi ya fikra. Tusitazame ardhi kama migogoro, shida tuliyonayo tunaitazama ardhi kama migogoro. Kwa hiyo, hata watu wanaohusika na sekta ya ardhi ni migogoro, kazi ya ardhi siyo migogoro, hasa wizara, Wizara ya Kisekta ilikuja na sheria muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mpaka sasa ninavyozungumza, kama Taifa hatuna National Land Use Masterplan. Sasa, kazi ya Wizara ya Ardhi ni kuja na Nation Land Use Masterplan, ambayo kimsingi niwaambie, population growth rate ya nchi ni asilimia tatu. Tukiendelea na matumizi mabaya tuliyonayo sasa ya ardhi, miaka 10 ijayo, miaka 20 ijayo, watu watapigana mapanga kugombania ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Wizara ya Ardhi na Wizara ya Fedha wawasaidie kuwa-finance. Waje na mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi wa Kitaifa, ambao wenyewe utaelekeza kwenye halmashauri waje na mipango miwili; Masterplan ya Land Use na Masterplan ya Infrastructure. Ninasema tu haya, yanawezekana, haitakiwi rocket science hapa; ni utayari na commitment tu, wala siyo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, najielekeza kwenye Sekta ya Miundombinu, ninamshukuru Waziri wa Ujenzi, katika mipango yetu lazima tuwe na mipango ya kati, mipango ya muda mrefu na mipango ya muda mfupi. TANROADS ilianzishwa mahususi kwa kuhudumia barabara za Kitaifa na barabara za mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, nilidhani mpango wa Wizara ya Ujenzi, kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa nisikilize kidogo. Haya madini ninayotoa hapa ni muhimu sana, Wizara ya Ujenzi, ninaomba kidogo mkamilishe kwanza ujenzi wa trunk roads, kwa sababu watu wanashughulika na barabara za wilaya wakati nchi yetu bado mikoa haijaungana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, vipaumbele vingeanza kuunganisha mikoa, ukilinganisha mkoa na mkoa au kanda na kanda, kwa mfano, Barabara ya Morogoro – Mlimba – Njombe Border ni barabara muhimu kwa uchumi wetu. Ni barabara inayounganisha Mikoa ya Pwani na Nyanda za Juu Kusini. Haiingii akilini Watanzania mpaka leo trunk road haijajengwa, trunk, Barabara ya Kitaifa. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nimpe taarifa mzungumzaji, anachozungumza ni sahihi kabisa, bado Mkoa wa Lindi na Mtwara haujaunganishwa kwa barabara ya lami.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea, ninaomba niseme haya, nihitimishe kwa sababu kengele imegonga. Ahsante, ninataka kusema nini?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Kwa kifupi.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiijenga Barabara inayotoka Pwani – Morogoro – Mlimba – Njombe, barabara hii itainua uchumi wa Taifa letu, kwa sababu ni barabara ya Kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho mkasome Zaburi ya 90:10.
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, Mungu atubariki sote.