Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Awali ya yote ninachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono makubwa ya kuja na Wizara ya Mipango. Ni wazi kwamba bajeti hii inayokwenda mwaka 2025/2026 itakuja na sura nyingine kabisa, sura ambayo inaonyesha kwamba kweli kuna Wizara ya Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninaanza na utoshelevu wa umeme nchini; ni kweli na hapa ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha tunamaliza ule mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Ndiyo maana sasa tunasema tuna utoshelevu wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utoshelevu wa umeme nina mambo mawili ya kushauri; kwanza tunaposema umeme unatutosheleza inatia mashaka kidogo, wakati iko mikoa kwenye nchi hii bado haijaungwa kwenye Gridi ya Taifa. Sasa, tunaposema una utoshelevu mkubwa wa umeme, mfano mzuri, nitoe mfano kwenye Mkoa wetu wa Lindi, hasa Wilaya ya Liwale, tunachangia Bwawa la Mwalimu Nyerere kwa 26%, lakini bado hatujanufaika na umeme wa Gridi ya Taifa. Kwa hiyo, ni matumaini yangu, wakati tunakwenda kujitosheleza kiumeme, basi nione mipango ya bajeti inayokuja kuhakikisha mikoa ile ambayo haijaingizwa kwenye Gridi ya Taifa inaingia kwenye Gridi ya Taifa ili tuweze kufaidi keki hii wote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine, niende kwa walipakodi; je, population yetu ya Kitanzania inalingana na idadi ya walipakodi tulionao? Hapa ninaomba niwashauri Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha kuhakikisha kwamba kila mwaka tunakuja na takwimu, ambazo zinaonyesha kwamba mwaka jana tulikuwa na walipakodi kiasi gani na mwaka huu tuna walipakodi kiasi gani vis-a-vis ongezeko la idadi ya watu hapa nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu zipo nchi zina population ndogo, lakini zina walipakodi wengi kuliko sisi ambao tuna population ya watu milioni 60, lakini tuna walipakodi wachache. Kwa hiyo, hapa ninaomba nilishauri Serikali niishauri Wizara, ihakikishe kila mwaka inazalisha walipakodi wapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itapunguza hii kimbizakimbiza ya walipakodi wachache, kwa sababu hawa walipakodi wachache tunawakamua sana ili tuweze kukidhi bajeti zetu, lakini Serikali ichukue jambo hili kwamba, kila mwaka ihakikishe inaongeza idadi ya walipakodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine, ni kweli bajeti ya kilimo imeongezeka kwa kiwango kikubwa sana. Hapa ninaendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa maono makubwa ya kuipandisha Wizara hii ya Kilimo kuwa na bajeti kubwa kiasi hiki na matokeo yameanza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba baada ya Wizara ya Kilimo kupandishiwa bajeti tayari tuna ziada ya chakula. Mfano, sisi kule Mikoa ya Lindi na Mtwara uzalishaji wa korosho umepanda sana. Hapa ushauri wangu tunaunganishaje kupanda huku kwa kilimo na miundombinu ya barabara, tunazalisha sana, wakulima wetu wanazalisha sana. Tunahitaji sasa mazao haya yafike kwenye masoko, mazao yanatakiwa yaende viwandani, mazao yanatakiwa yafike kwenye masoko lakini je, tumejiandaa vipi na ujenzi wa barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sikosei huu ni mwaka wa tatu, mimi kwa mtazamo wangu sijaona mradi mkubwa wa barabara kwenye nchi yetu ambao umekamilika ndani ya hii miaka miwili mitatu. Kwa hiyo, ninaomba kwenye bajeti hii inayokuja...

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: ... tuone kwamba bajeti yetu hii inakuja na mpango wa ujenzi wa barabara, barabara ambazo tutakwenda kuunganisha na wakulima ili mazao yao yafike kwenye masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri Mkoa wa Lindi na Mtwara...

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: ... ni wazalishaji wakubwa sana wa mazao ya korosho na mazao ya ufuta...

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kuchauka, kuna Taarifa.
TAARIFA

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumpa Taarifa mzungumzaji kwamba Barabara ya Kidatu - Ifakara imekamilika na anachokisema Mheshimiwa Mbunge ni jambo la muhimu sana kwamba kukamilika kwa mradi wa Barabara ya Ifakara - Kidatu ndiyo kunaunganisha barabara yake moja ya kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Lindi, Mkoa wa Morogoro Malinyi kwa sababu...

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kuchauka.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: ...na kwenda Njombe, kwa hiyo nataka nimsisitize ataje hizo barabara kwa sababu zinaenda kwake.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Asenga ahsante. Mheshimiwa Kuchauka, endelea. (Makofi)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninaipokea Taarifa yake. Nilichokuwa nazungumza kwamba ufungamanishaji wa kilimo cha kisasa na miundombinu ya barabara. Nikatoa mfano Mkoa wa Lindi pamoja na uzalishaji mkubwa wa korosho na ufuta, lakini ndiyo mkoa pekee ambao hauna mradi mkubwa wa barabara. Mkoa wetu wote hausomani kutoka wilaya moja kwenda wilaya nyingine, kutoka Mkoa wa Lindi kwenda mkoa mwingine bado barabara zetu hazisomani. Kwa hiyo, utaona kwamba kuongeza kwa bajeti ya Wizara ya Kilimo hatutaiona ile tija ya kuongezeka kwa bajeti kwa sababu ya shida iliyopo kwenye barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ninaomba nitoe ushauri wangu kwenye ujenzi wa vituo vya afya, shule na kadhalika. Hapa vilevile niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa namna alivyotekeleza miradi hii kwa upande wa elimu na upande wa afya. Ninaomba nione kwenye mpango huu namna ya kupata watumishi na hapa niseme tu kwamba, kwa upande wa vifaatiba navyo vinafanya vizuri lakini bado tuna tatizo kubwa la ajira. Utakuta kituo cha afya kina ikama zaidi ya watu 25 kinahudumiwa na watu watatu. Kwa hiyo na hapa ninaomba kwenye bajeti hii inayokuja tuone namna ya kuongeza idadi ya watumishi iendane sawasawa na uwekezaji uliowekezwa kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kwenye Sekta ya Bandari, ni ukweli usiopingika Bandari yetu ya Dar es Salaam uwekezaji ni mkubwa na tumeshaanza kuona manufaa ya uwekezaji ule, ninaomba sana tuone na bandari nyingine ili Bandari ya Dar es Salaam iweze kupata msaada. Kuna Bandari ya Mtwara, kuna Bandari ya Maziwa Makuu na hapa ninaomba nisikitike sana kwenye Bandari yetu ya Mkoa wa Lindi, Bandari ya Lindi ndiyo imesahaulika kabisa; lakini kwa namna ya uzalishaji mkubwa uliopo Lindi, nilitegemea nione sasa twende na Bandari ya Lindi nayo ionekane kwenye bajeti hii na siyo tu kuonekana kwenye bajeti, ionekane ikipewa kipaumbele na iweze kutekelezwa kwenye Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, ninakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)