Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaungana na Wabunge wenzangu kuchangia Mpango wetu huu wa mwaka 2025/2026. Kwanza ninampongeza Mheshimiwa Rais, Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango na timu zao nzima kwa Mpango mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanzia kwangu Kahama, Kahama wamenipatia barabara kweli kabisa za Benki ya Dunia na barabara hizi mkandarasi ameshazitifua na mvua zinaendelea kunyesha, nimwombe tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ajitahidi kumlipa mkandarasi huyu maana yake hana pesa na ni za Benki ya Dunia. Kama itaendelea hivyo ina maana tunaweza kupata maafa kwa ajili ya mafuriko kwenye maeneo ya watu ambako ametibua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo Kamati ya Elimu ya Juu, juzi hapa Bodi ya Mikopo walileta hoja kwamba hawapati marejesho kutoka kwa watu waliokopa au waliokopa elimu na wanajiandaa kuanza kufanya operation ya zoezi la kuwakamata wadaiwa wote wanaodaiwa. Sasa hoja yangu, Bodi ya Elimu ilimpa mtu wa chuo hizo pesa, mtu wa chuo akampa elimu mwanafunzi, elimu ambayo haiajiriki. Sasa anayetakiwa kushtakiwa kabisa ni nani, ni mwanafunzi au ni chuo? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu haya maneno dunia inabadilika hatuwezi kuendelea na lugha ile ile ya kusema elimu ni ufunguo wa maisha, Hapana. Elimu ni bidhaa, hawa watu walichopewa ni bidhaa wameshindwa kuuza, kwa hiyo mwenye kosa ni Bodi ya Mikopo. Ndiyo maana hoja yangu kwenye Kamati yetu na Mheshimiwa Waziri alikuwepo, kwa nini tusiweke masharti kwamba chuo chochote ambacho kinataka kuingia kwenye eneo la kupewa mikopo ki-qualify kwamba mwaka jana walimaliza wanafunzi 300 na katika hao 70% wamepata ajira ndiyo kihusike na kupata mkopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana kabisa na Mheshimiwa Profesa Muhongo, alivyosema hapa kwamba kweli watu wanahitajika kule, lakini kama Bodi ya Mkopo inazitupa tu hela kwa mtu halafu anaenda kumfundisha GPA isiyoajirika ni sahihi si itafilisika kweli. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri wa Mipango, liweke suala hilo kwenye mipango yako ili hawa watu wa chuo ndio wakatafute mitaala ambayo itafanya watu waajiriwe na zile pesa zirudi kuliko utaratibu wa sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi sisi Shinyanga na Kahama tulipata ugeni wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, miongoni mwa suala ambalo tuli-raise pale ni suala la afya. Ninajua siongelei habari ya hela lakini hospitali wananchi wamejenga wao wenyewe, kumwona daktari kwenye hospitali ya hela unatakiwa utoe shilingi 5,000, sasa mwananchi wa kawaida Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha, hii hospitali ni ya Serikali, daktari analipwa na Serikali sababu ya mwananchi kwenda kumwona kwa hela ni nini? Labda Mheshimiwa, ulifikirie kwa makini sana, kwa sababu wananchi hawa wana hali ngumu sana wote mnafahamu hali ya pesa ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukaleta pia issue kwamba Serikali kwa nini haitaki kutoa bei elekezi ya dawa na matibabu? Leo hapa tunakabana na Mheshimiwa Bashe kwenye kesi ya sukari, lakini wote humu madaktari wamo, si mnatuambia wenyewe sukari ni sumu. Sasa kwenye sumu bei inapunguzwa ili watu wakanywe sumu si ndiyo, lakini tunakataa kupanga bei ya dawa, inawezekana kweli? Maana yake wote tunalazimisha kwamba sukari lazima iwe na bei ya Serikali, lakini nyinyi wenyewe hapo hapo mnasema sukari ni sumu, sasa sumu ndiyo inapunguzwa bei na inapangiwa bei kweli? Tunakataaje kumpangia mwananchi bei elekezi ya matibabu na dawa, tunang’anganiaje sumu ipewe bei elekezi? Haiwezekani! Tunajaribu sana kuliona hili suala kwa undani zaidi badala ya kuchachamaa na vitu visivyo na maana, bora tuchachamae sehemu ambayo ina uhai wa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nitaongelea suala la Kabanga Nickel, mimi kwangu Kahama ndipo unapojengwa ule mtambo mkubwa, lakini bado tunavutana. Tumekwenda kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha mara mbili, mara tatu. Mtu anayetaka ku-inject hela kwenye ule mgodi ana dola milioni 400, lakini Serikali kwa sheria iliyopo inataka 30%, lakini Serikali hiyohiyo ina hisa ya 18% kwenye ule mgodi na hali ya yale madini ni mbaya sana, kwa sababu Wachina wanatengeneza nickel ya bandia. Sasa tumwombe Mheshimiwa Waziri, kama kuna sheria ilete sheria hiyo ibadilishwe ili huyu aweze kuingiza pesa ili mgodi ule uanze. Kwa sababu kule kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, una megawatt 600 hazina mnunuzi wa umeme, huyu Kabanga Nickel ni mnunuzi mzuri wa umeme, sasa upande mmoja unamkatalia huyu kuweka, upande mmoja unasema huna pa kuuza umeme na huyo ndiyo mnunuzi mzuri wa umeme. Kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, jaribu kulifikiria sana suala hilo ili kusudi liweze kutusaidia, lakini la muhimu sana lile suala la dawa tusaidie sanasana kutupangia bei elekezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo ninashukuru sana. (Makofi)