Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu wa mwisho wa mwaka 2025/2026. Ni Mpango wa mwisho baada ya kutoka katika ile Dira ya Maendeleo ya miaka 25, kwa maana 2020/2025, lakini pia nipongeze kwa maandalizi mazuri na namna ambavyo tumeweza kuona Mapendekezo mapya ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya miaka mingine 25 kwa maana ya 2025/2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu wa maendeleo ambao tunakwenda kuumaliza wa mwaka 2024/2025, tumeweza kuona mambo makubwa ambayo yanaendelea kufanyika, lakini ni Mpango wa miaka 25 ambao toka tumeuanza 2020 kufika 2025/2026 mambo makubwa tumeweza kufanikiwa. Tumeweza kuona kuna maendeleo makubwa katika upande wa umeme japo hatujafikia malengo tuliyojiwekea kwa sababu tulitakiwa tukamilishe tuwe na megawatt 5,000 mpaka kufikia mwakani. Ninaamini tutazifikia kwa sababu zipo mbinu mbalimbali zinaendelea kuwekezwa kuhakikisha kwamba tunafikia japo mpaka sasa tuna takribani zaidi ya megawatt 4,000 za umeme ambazo tumeweza kuzalisha na hasa kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere lenye megawatt 2,115.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kubwa sana kwa Serikali inayoongozwa na Mama yetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini pia na Mawaziri ambao wapo katika sekta mbalimbali ikiwa pamoja na Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati, hongereni sana kwa kukamilisha ujenzi wa Bwawa hilo na sasa kwenye umeme angalau kuna ahueni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia kwa kuendelea kukamilisha miradi mikubwa kama ule Mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma na sasa tunaendelea na ujenzi wa SGR kutoka Dodoma kwenda Tabora, tunaona ujenzi ukiendelea kutoka Mwanza kuja Isaka, Isaka - Tabora lakini pia tunaona harakati zingine kutoka Tabora kwenda Kigoma. Tutakapokamilisha hii SGR uchumi wa nchi yetu utapanuka na utakuwa mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia Serikali kwa kazi nzuri ambayo imefanyika katika usambazaji wa umeme vijijini, sasa karibia 95% ya vijiji vyetu vyote vimepata umeme imebaki asilimia chache kukamilisha na kwa sababu tunaamini Mpango unaokuja unaenda kukamilisha vitongojini. Niiombe Serikali katika mipango yetu tuhakikishe kwamba wananchi wanahitaji hizi huduma kwa haraka na kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia kwa kazi zote zinazofanyika za miradi ya barabara, ninapenda kushauri katika Mpango wetu huu, kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro bado tuna miundombinu ambayo siyo rafiki kwa matumizi ya magari. Niiombe Serikali iharakishe mpango wa kuongeza njia nne kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro, lakini pia njia nne kutoka Morogoro kuja Dodoma, kutoka Dodoma kwenda Tabora kupitia Igunga kwenda mpaka Nzega, mpaka Shinyanga na Mwanza. Ukuaji wa uchumi unaenda sambamba na ukuaji wa miundombinu hasa ya Barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza SGR, lakini tusisahau kuwekeza kwenye ujenzi wa barabara hasa hii njia kubwa ambayo tunapitisha malori makubwa, lakini pia kama tunavyotambua sisi tumezungukwa na Nchi ya Rwanda, Burundi, Congo, Uganda na Zambia. Kwa hiyo lazima tuangalie hili Soko la Afrika tunawezaje kulishika kwa ukaribu. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri katika mipango yako lazima tuwekeze kwenye ujenzi wa miundombinu, lakini pia tuhakikishe kwamba miundombinu hii inakuwa bora na imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kuwaomba Wizara ya Fedha, wazabuni wengi wamepewa kazi mbalimbali katika maeneo mbalimbali tunaomba wawalipe fedha zao kwa wakati ili kazi hizi zisiweze kukwama. Tunaona miradi mbalimbali inatekelezwa na ni mikubwa, lakini Wizara ya Fedha na Mipango wahakikishe fedha zinapatikana kwa wakati ili tusichukue muda mrefu katika kutekeleza mradi ambao tumejiwekea kutekeleza kwa miaka mitatu au miaka miwili tukafanya huo mradi tukautekeleza zaidi ya miaka minne ama sita ni kujirudisha nyuma kimaendeleo. Kwa hiyo niwaombe sana watu wa Wizara ya Fedha wajitahidi katika kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha na tunalipa fedha katika maeneo ambayo tumejiwekea kama sehemu ambayo tunatakiwa kuhakikisha kwamba miradi haikwami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona ujenzi kwenye Sekta ya Kilimo, tunaipongeza Serikali kwa kuwa na nia ya dhati kabisa yakuwekeza fedha kwenye kilimo. Bajeti ya Kilimo imetoka shilingi bilioni 200 na sasa tunazungumza trilioni zaidi ya moja na kidogo. Tunapongeza kazi hii nzuri kwa sababu tunaona ujenzi wa mabwawa, tunaona ujenzi wa skimu za umwagiliaji, lakini tunaona namna ambavyo Wizara na Serikali zina nia ya dhati. Niombe tuwekeze zaidi kwenye kilimo, tuongeze fedha, tujenge mabwawa makubwa kwenye maeneo ambayo kuna mvua za kutosha, ambako tunaweza tukajenga mabwawa tukaweza kuyavuna haya maji, lakini pia tukajenga skimu za umwagiliaji tukawa tunalima mara mbili mpaka mara tatu kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambako ninataka niishauri Wizara ni kwenye upande wa Sekta ya Michezo...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante. Ahsante Mheshimiwa.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na ninaunga mkono hoja. (Makofi)